Kuelewa Uislamu
Kwa mema au mabaya, kiukweli hakuna siku inapita ambapo Uislamu na Waislamu hawapo kwenye vichwa vya habari. Ya kueleweka, wasio-Waislamu wengi—ikijumuisha Watakatifu wa Siku za Mwisho—wanataka kujua, hata kuhusika. Je, tuna chochote kinachofanana na jirani zetu Waislamu? Tunaweza kuishi na kufanya kazi pamoja?
Kwanza, baadhi ya historia ya nyuma inaweza kuwa ya manufaa:
Mnamo 610 AD mfanya biashara Muarabu wa umri wa kati aliyeitwa Muhammad alipanda milima juu ya mji wa kwao wa Mecca kutafakari na kuomba kuhusu mkanganyiko wa dini uliomzunguka. Baadaye alisema kuwa alipokea ono likimuita kama nabii kwa watu wake. Tukio hili linaanzisha mwanzo wa dini inayojulikana kama Uislamu (uiss-LAAM), neno ambalo humaanisha “kujinyenyekeza” (kwa Mungu). Anayeamini katika Uislamu anaitwa Muislamu (MUIS-lamu), ikimaanisha “mnyenyekevu.”
Baada ya hapo, Muhammad alisema alipokea mafunuo mengi mpaka kifo chake karibu miaka 25 baadaye. Kwanza alishiriki mafunuo hayo na wakazi wa mji wake, akionya juu ya hukumu za kiungu zinazokuja; akiwashauri waliomsikiliza kutubu na kuwajali wajane, yatima, na maskini; na kuhubiri ufufuko wa wafu wote ulimwenguni na hukumu ya mwisho ya Mungu.
Hata hivyo, dhihaka na mateso ambayo kwayo yeye na wafuasi wake waliwekwa chini yake yalikuwa makali kiasi kwamba walilazimika kukimbia kwenda mji wa Medina, ulio takriban siku nne za kuendesha farasi kuelekea kaskazini.
Huko, jukumu la Mohammad lilibadilika sana.1 Kutoka kuwa mhubiri na muonyaji pekee, akaja kuwa mtoa sheria, hakimu, na kiongozi wa kisiasa kwa muda, wa mji muhimu wa Kiarabu wa Rasi ya Kiarabu. Uanzilishi huu wa mwanzo wa jamii ya waaminio uliupa Uislamu utambulisho wa kidini ulikuwa na mizizi katika sheria na haki ambavyo vimebaki kati ya sifa zinazovutia na kufuatwa sana.
Vikundi vikuu viwili vilijitokeza kati ya wafuasi wa Muhammad baada ya kifo chake mnamo 632 B.K, wakigawanyika kwanza juu ya swali la nani awe mrithi wake kama kiongozi wa jamii ya Kiislamu.2 Kikubwa kati ya hivi kimekuja kuitwa Wasuni (kinadai kufuata sunna, au sheria za kimila za Muhammad na ni rahisi kwa kiasi fulani katika mambo ya urithi ). Kingine, ambacho kilikua kutokana na mkwe wa kiume wa Muhammad, aliyeitwa Ali, kiliitwa shi’at ‘Ali (kikundi kidogo cha ‘Ali) na sasa kinajulikana zaidi kama Washi’a. Tofauti na Wasuni, Washi’a (wakijulikana kama Waislamu wa Shi’i) wanaamini kwamba haki ya kumrithi Muhammad kama viongozi wa jamii kwa utaratibu ni ya ndugu mwanaume wa karibu wa Nabii Muhammad, ‘Ali, na warithi wake.
Licha ya kutokukubaliana huku, ulimwengu wa Kiislamu umekuwa na umoja, tukiongelea upande wa kidini, kuliko mataifa ya Kikristo. Zaidi, kwa karne kadhaa baada ya kama 800 BK, ustaarabu wa Kiislamu ulikuwa haipingiki kuwa ndio ulioendelea ulimwenguni katika nyanja za sayansi, dawa, hisabati, na falsafa.
Vyanzo vya Mafundisho na Desturi za Kiislamu.
Mafunuo yanayodaiwa na Muhammad yalikusanywa katika kitabu kilichoitwa Kurani (kutoka kitenzi cha Kiarabu qara’a, “kusoma” au “kukariri”) ndani ya muongo mmoja au miwili ya kifo chake. Kikiwa na sura 114, Kurani siyo hadithi kuhusu Muhammad. Karibu sawa na Mafundisho na Maagano, siyo simulizi kabisa; Waislamu wanaichukulia kama neno (na maneno) ya Mungu yaliyotolewa moja kwa moja kwa Muhammad.3
Wakristo wanaoisoma watapata dhamira zinazokaribiana. Inaongelea, kwa mfano, juu ya uumbaji wa Mungu wa ulimwengu katika siku saba, kuwaweka Kwake Adamu na Hawa ndani ya Bustani ya Edeni, kujaribiwa kwao na shetani, anguko lao, na wito wa mstari wa kufuatia manabii (wengi wao ambao huonekana katika Biblia). Manabii hawa wameelezewa ndani ya Kurani kama waislamu, wakiwa wameweka mapenzi yao kwa Mungu.
Ibrahimu, aliyeelezewa kama rafiki ya Mungu, mtu muhimu katika maandishi.4 (Miongoni mwa mambo mengine, inaaminiwa kuwa alipokea mafunuo ambayo aliyandika lakini tangu hapo yamepotea.5) Musa, Farao, na Kutoka kwa wana wa Israeli Misri pia huchukua nafasi.
Cha kushangaza, Mariamu, mama wa Yesu, anatajwa mara 34 ndani ya Kurani, ikilinganishwa na mara 19 ndani ya Agano Jipya. (Yeye, kwa kweli, ndiye mwanamke pekee aliyetajwa ndani ya Kurani.)
Mojawapo ya kiitikio cha daima cha Kurani ni fundisho la tawhid (taw-HEED), neno ambalo linaweza kutafsiriwa kama “imani kwamba kuna Mungu mmoja” au, kiuhalisia zaidi, kama “kufanya moja.” Inawakilisha moja ya kanuni kuu ya Uislamu: kwamba kuna kiumbe mmoja wa kipekee mtakatifu kabisa. “Hazai, wala hajazaliwa,” inatangaza Kurani, “na hakuna kama yeye.”6 Kinachofuata kutoka katika hili hakika ni tofauti muhimu kati ya Uislamu na Ukristo: Waislamu hawaamini katika uungu wa Yesu Kristo au Roho Mtakatifu. Pia inaonyesha kwamba, wakati watu wote ni viumbe sawa vya Mungu, kulingana na mafundisho ya Kiislamu sisi siyo watoto Wake.
Bado Waislamu huamini Yesu kuwa alikuwa nabii wa Mungu asiye na dhambi, aliyezaliwa na bikira na aliyekusudiwa kutimiza jukumu kuu katika matukio ya siku za mwisho. Ametajwa mara nyingi na kwa unyenyekevu ndani ya Kurani.
Mafundisho na Desturi za Msingi za Kiislamu
Kile kinachoitwa “Nguzo Tano za Uislamu”—kimefanyiwa muhtasari siyo ndani ya Kurani bali katika kauli iliyohusishwa kiutamaduni na Muhammad—na kuanzisha baadhi ya mafundisho ya msingi ya Kiislamu:
1. Ushuhuda
Kama Uislamu ni imani ya ulimwengu, ni shahada (sha-HAD-ah), “ungamo la imani,” au “ushuhuda.” Neno hurejea kanuni ya Kiarabu ambayo, tafsiri yake ni kama ifuatavyo: “Ninashuhudia kwamba hakuna mungu bali Mungu [Allah] na kwamba Muhammad ni Mjumbe wa Mungu.” Shahada ni njia ya kuingia kwenye Uislamu. Kuikariri kwa imani ya dhati ni kuwa Muislamu.
Neno la Kiarabu linganifu na neno Mungu ni Allah. Ufupisho wa maneno al- na ilah (“mungu”), siyo jina sahihi bali cheo, na linakaribia kuwa na uhusiano na neno la Kiebrania Elohimu.
Kwa kuwa hakuna ukuhani wa Kiislamu, hakuna ibada za ukuhani. Wala hakuna “kanisa” hata moja la Kiislamu. Hivyo kukiri wa shahada, katika fasili ya dhana akilini, ni sawa na ubatizo. Kukosekana kwa sasa kwa muundo wa uongozi rasmi, uliounganika, ulimwenguni kote una hatari zingine. Kwa mfano, hakuna kiongozi wa jumla wa Waislamu ulimwenguni, hakuna anayeongea kwa ajili ya jamii nzima. (Muhammad karibu anatazamwa kiulimwengu kama nabii wa mwisho.) Hii pia inamaanisha kwamba hakuna kanisa ambapo magaidi au “waasi” wanaweza kutengwa.
2. Sala
Wasio Waislamu wengi wanajua utaratibu wa Waislamu wa sala uitwao salat (sa-LAAT), ambao hujumuisha idadi maalumu ya kusujudu kimwili, mara tano kila siku. Kukariri mistari iliyoamuriwa kutoka kwenye Kurani na kugusisha chini paji la uso huonyesha unyenyekevu wa kujiweka chini ya Mungu. Sala ya hiyari zaidi, inayoitwa du’a, inaweza kutolewa muda wowote na haiitaji kusujudu.
Kwa ajili ya sala za mchana siku ya ijumaa, wanaume wa Kiislamu huhitajika na wanawake wa Kiislamu wanashauriwa kusali msikitini (kutoka Kiarabu masjid, au “mahali pa kusujudu”). Hapo, katika makundi yaliyotengwa kijinsia, wanatengeneza mistari, na kusali kama inavyoongozwa na imam wa msikiti (ee-MAAM, kutoka Kiarabu amama, ikimaanisha “mbele ya”), na kusikiliza mahubiri mafupi. Siku za Ijumaa, hata hivyo, siyo sawa kabisa na Sabato; japokuwa “mwisho wa wiki” katika nchi nyingi za Kiislamu hulenga katika yawm al-jum’a (“siku ya kukusanyika”) au Ijumaa, kufanya kazi siku hiyo haichukuliwi kama dhambi.
3. Utoaji Sadaka
Zakat (za-KAAT, ikimaanisha “kile kinachotakasa”) humaanisha kufanya matoleo ya hisani kuwasaidia maskini, na pia kwa misikiti na shughuli zingine za Kiislamu. Kwa ujumla hukadiriwa kuwa asilimia 2.5 ya jumla ya mali ya Muislamu juu ya kiasi fulani cha chini. Katika baadhi ya nchi za Kiislamu, hukusanywa na mashirika ya serikali. Katika nchi zingine, ni kwa hiari.
4. Kufunga
Kila mwaka Waislamu wenye moyo wa dhati huacha kula, kunywa, na mahusiano ya kingono kutoka macheo mpaka machweo wakati wa mwezi unaofuata kuandama kwa mwezi wa Ramadhani. Wao pia mara kwa mara hujitolea kwa ajili ya hisani maalumu kwa masikini na kusoma Kurani kwa kipindi cha mwezi mmoja.7
5. Hija
Waislamu wenye afya na rasilimali za kufanya hivyo wanapaswa kufanya hija Maka angalau mara moja katika maisha yao. (Ziara ya Madina, mji wa pili kwa utakatifu katika Uislamu, hujumuishwa hasa lakini sio lazima.) Kwa Waislamu waaminifu, kufanya hivyo ni tukio lenye mguso wa kina zaidi kiroho, jambo lililo sawa na wewe binafsi kuhudhuria mkutano mkuu au kuingia hekaluni kwa mara ya kwanza.
Baadhi ya Hoja za Sasa
Mambo matatu ya kuzingatiwa kwa wasio-Waislamu wa siku hizi kuhusu Uislamu ni vurugu za kidini; Uislamu, au sheria za shari’a, na Uislamu unavyowatendea wanawake.
Baadhi ya watu wenye siasa kali wametumia neno jihadi kumaanisha kwa kipekee “vita takatifu,” lakini neno hili kwa kweli humaanisha “kazi kwa vitendo,” kinyume na sala na kusoma maandiko “tu”.
Wanasheria na wanafalsafa wa Kiislamu wametofautiana katika uelewa wao juu ya jihadi. Vyanzo vya viwango vya sheria hutoa hoja, kwa mfano, kwamba jeshi la jihadi linalokubalika linapaswa kujilinda na kwamba wapinzani wanapaswa kuonywa kabla na kupewa nafasi kuacha matendo ya kuchokoza. Baadhi ya wanasheria na wanafalsafa wa Kiislamu leo wanatoa hoja kwamba jihadi inaweza kudhihirisha matendo yoyote ya busara yaliyokusudiwa kunufaisha jamii ya Kiislamu au kuboresha ulimwengu kiujumla zaidi. Muhammad anasemekana kutenganisha kati ya “jihadi kubwa” na “jihadi ndogo.” Hiyo ya mwisho, yeye alisema, ni vita. Lakini jihad kubwa ni kupambana na ukiukaji wa haki vile vile upinzani wa mtu binafsi wa kuishi kwa haki.
Ugaidi wa leo wa Uislamu unadai kuwa na mizizi ya kidini, lakini kihoja huakisi malalamiko kijamii, kisiasa, na kiuchumi ambayo yana uhusiano mdogo au yasiyo na uhusiano na dini.8 Zaidi ya hayo, ni muhimu kukumbuka kwamba wengi wa Waislamu ulimwenguni hawaungani na magaidi katika vurugu zao.9
Shari’a ni jambo lingine linalowapa wasiwasi baadhi ya watu wasio Waislamu. Ikitolewa kutoka kwenye Kurani na hadith—ripoti fupi za kile Muhammad na wenzake wa karibu walisema na kufanya ambavyo hutoa mfano wa tabia ya Kiislamu vilevile huongezea na kuelezea vifungu vya Kurani—ni mfumo wa kanuni na taratibu zilizokubaliwa Kiislamu.10 Sheria zinazotawala uvaaji kwa wote wanaume na wanawake (kama vile hijabu, au mtandio) inapatikana katika shari’a; wakati zikishurutishwa na baadhi ya nchi za Kiislamu, zimeachwa kuwa uchaguzi wa mtu binafsi katika nchi zingine. Shari’a pia hushughulikia mambo kama usafi binafsi; muda na yaliyomo katika sala; sheria zinazotawala ndoa, talaka, na mirathi. Hivyo, wakati Waislamu wanapoonyesha katika utafiti kwamba wao wanatamani kutawaliwa na shari’a, wanaweza kuwa au wasiwe wanatoa kauli ya kisiasa. Wanaweza kuwa wanasema tu kwamba wanatamani kuishi maisha halisi ya Kiislamu.
Watu wengi wasio-Waislamu, wanapofikiria kuhusu Uislamu unavyowachukulia wanawake, mara moja hufikiria juu ya ndoa za mitala na mitandio. Lakini uhalisia wa kitamaduni ni chamgamani sana. Vifungu vingi ndani ya Kurani hutangaza wanawake kuwa sawa na wanaume, wakati vingine vikionekana kuwapa nafasi za chini. Hakika kuna baadhi ya mazoea katika nchi nyingi za Kiislamu—mara nyingi yakiwa na mizizi katika utamaduni wa kikabila kabla ya-Uislamu au mila zingine zilizokuwepo kabla—ambazo huonyesha wanawake ni wa kutumikia. Hata hivyo, jinsi Waislamu wanavyochukulia nafasi za wanawake inatofautiana sana toka nchi hadi nchi nyingine na hata miongoni mwa nchi.
Mitazamo ya Watakatifu wa Siku za Mwisho juu ya Uislamu
Licha ya Imani zetu tofauti, ni kwa jinsi gani Watakatifu wa Siku za Mwisho wanaweza kushughulikia kujenga uhusiano na Waislamu?
Kwanza kabisa, tunapaswa kutambua haki za Waislamu za “kuabudu namna, mahali na chochote watakacho” (Makala ya Imani 1:11). Mnamo 1841, Watakatifu wa Siku za Mwisho katika halmashauri ya mji wa Nauvoo ilipitisha sheria juu ya uhuru wa dini ikitoa dhamana ya “uvumilivu huru, na fursa sawa” kwa “Wakatoliki, Wapresbiteri, Wamethodisti, Wabaptisti, Watakatifu wa Siku za Mwisho, Wakweka, Waepiskopo, Wayunivesalisti, Wayunitariani, Wamohammedi [Waislamu], na vikundi na madhehebu mengine yote ya dini.”11
Tunapaswa pia kukumbuka kwamba viongozi wetu wa Kanisa wamekuwa kwa ujumla wakileta mvuto chanya katika ukubali wao wa mwanzilishi wa Uislamu. Mnamo 1855, kwa mfano, wakati ambapo Wakristo wengi walimtuhumu Muhammad kama mpinga kristo, Wazee George A. Smith (1817–75) na Parley P. Pratt (1807–57) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili walitoa mahubiri marefu siyo tu kuonyesha kuvutiwa kwao na taarifa na uelewa mzuri wa historia ya Uislamu bali pia wakimsifu Muhammad mwenyewe. Mzee Smith alisema kwamba Muhammad “bila shaka aliinuliwa na Mungu kwa lengo” kuhubiri dhidi ya kuabudu sanamu, na alielezea huruma kwa Waislamu, ambao, kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, huona ni vigumu “kupata historia ya uaminifu” ikiandikwa kuhusu wao. Akiongea punde tu baadaye, Mzee Pratt alielezea matamanio kwa mafundisho ya Muhammad na kwa maadili na taasisi za jamii ya Kiislamu.12
Kauli rasmi ya hivi karibuni ilikuja mnamo 1978 kutoka kwa Urais wa Kwanza. Inamtaja mahususi Muhammad kati ya “viongozi wa dini wakuu wa ulimwengu,” ikisema kwamba, kama wao, “alipokea kiasi cha nuru ya Mungu. Kweli za kimaadili zilitolewa kwa [viongozi hawa] na Mungu,” aliandika Rais Spencer W. Kimball, N. Eldon Tanner, and Marion G. Romney, “kuelimisha mataifa yote na kuleta hatua kubwa ya uelewa kwa watu.”13Kujenga katika Uwanda Sawa
Wakati Watakatifu wa Siku za Mwisho na Waislamu kwa wazi tunatofautiana katika mambo muhimu—maarufu utambulisho wa kiungu wa Yesu Kristo, nafasi Yake kama Mwokozi, na wito wa manabii wa siku hizi—hata hivyo tuna mambo mengi yanayofanana. Sote tunaamini, kwa mfano, kwamba sote tunawajibika kimaadili mbele za Mungu, kwamba lazima tutafute vyote utu wa haki na jamii nzuri na ya haki, na kwamba tutafufuka na kuletwa mbele ya Mungu kwa hukumu.
Wote Waislamu na Watakatifu wa Siku za Mwisho huamini katika umuhimu wa familia imara na katika amri takatifu ya kuwasaidia maskini na wenye shida na kwamba tunaonyesha imani yetu kupitia matendo ya ufuasi. Inaonekana hakuna sababu kwa nini Watakatifu wa Siku za Mwisho hawawezi kufanya hivyo wao kwa wao na hata, wakati fursa zinapotokea, kwa kushirikiana pamoja katika jamii ambapo, zaidi na zaidi, tunajikuta ni majirani katika ulimwengu unaokua usio na dini. Pamoja, tunaweza kuonyesha kwamba imani ya kidini inaweza kuwa nguvu ya juu kwa mazuri na siyo tu chanzo cha ubishi na hata vurugu, kama baadhi ya wakosoaji wanavyotoa hoja.
Kurani yenyewe inapendekeza njia ya kuishi pamoja kwa amani licha ya tofauti zetu: “Kama Mungu angetaka, angewafanya jamii moja. Lakini alikusudia kuwajaribu katika kile alichowapa. Hivyo, shindaneni katika matendo mazuri. Wote mtarudi kwa Mungu, na atawaambia kuhusiana na mambo ambayo kwayo mlitofautiana.”14