2018
Duka la Viatu la Abuelo
April 2018


Duka la Viatu la Abuelo

Mwandishi anaishi Utah, Marekani.

“Unajua, sisi tunahitaji kuwa zaidi kama hiki kiatu,” Babu alisema.

“’Samahani’ kila mara si rahisi kusema” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 98).

Abuelos Shoe Shop

Miguel alifungua mlango wa duka la viatu la abuelo (la babu yake). Alihisi harufu ya ngozi ambayo Abuelo alikua akiifanyia kazi. Ilikua ni moja ya harufu alizozipenda zaidi.

“Halo, Abuelo!”

Abuelo alikuwa amepiga magoti na akichora wayo wa mteja kwenye kipande cha karatasi. Hakuinua kichwa. Uwezo wa Abuelo wa kusikia haukuwa mzuri.

Miguel aliketi kwenye ubao wa kufanyia kazi. Alitazama rundo la ngozi zilizokatwa. Alijaribu kufikiria kile Abuelo angetengeneza kwa kutumia kila ngozi, akitumia nyundo yake na chamburo.

Vifaa vilimkumbusha Miguel kitu kingine alichokipenda. Abuelo daima alimpa kipande cha peremende endapo Miguel alimsaidia kusafisha.

Lakini Miguel alikuwa na njaa sasa! Alijua hakupaswa kuchukua zawadi bila kuomba, lakini ilionekana kama Abuelo angekuwa na shughuli kwa muda. “Labda sihitaji kusubiri,” Miguel alifikiria.

Miguel alinyoosha mkono chini ya kaunta kuchukua chupa ya peremende. Ilikuwa imejaa peremende alizozipenda zaidi—tamu na zilizotiwa kiungo zikiwa na unga wa pilipili! Alipoifungua, Miguel alihisi kidogo wasiwasi. Lakini peremende ilionekana kuwa tamu sana. Aliharakisha na kuiweka mdomoni mwake.

Punde kidogo mteja aliondoka. Abuelo alichukua kipande cha ngozi na kukichovya kwenye maji. Hiyo ilisaidia kuifanya ngozi iwe laini na rahisi kuifanyia kazi.

Miguel alitafuna kwa pupa peremende iliyobaki haraka kwa kadri alivyoweza. Kisha akatembea kuelekea kwa Abuelo.

“Halo!” Abuelo alisema kwa tabasamu. “Ninafurahi umekuja kuniona.”

Miguel alimkumbatia Abuelo. Alitumaini Abuelo asingejua amekula kipande cha peremende. Miguel aliondoa woga.

“Inaonekana una kazi nyingi leo,” Miguel alisema, akionyesha kwa kidole rundo la ngozi. “Unahitaji msaada wo wote?”

“Hakika! Unaweza kunisogezea huo uzi?”

Miguel alifikia kipande kirefu cha uzi. Alikivuta kwa nguvu kati ya mikono yake. Kilikuwa kizito kuliko kilivyoonekana.

“Wee, hiyo ni imara.”

Abuelo alicheka kwa chini chini. “Inapaswa kuwa, ili kudumu mpaka uchakavu wa maisha.” Abuelo alivuta uzi kwenye ngozi. Kisha akawa na mtazamo ule kwenye uso wake mtazamo ambao Mamá wakati mwingine huuita mtazamo wa “Abuelo mwenye Busara”

“Unajua, tunahitaji kuwa zaidi kama hiki kiatu,” Abuelo alisema kwa ishara ya kukubali kwa kichwa.

Miguel alitupa jicho kwenye ngozi. “Um. Kweli?

“Ndiyo, kabisa. Tunapaswa kuwa imara. Kwa njia hiyo majaribu ya Shetani hayatatufanya tusambaratike.

Peremende nyekundu ikamulika kwenye akili ya Miguel. Alijua alipaswa kumwambia Abuelo kuhusu peremende.

Abuelo alichukua kiatu cha zamani kutoka kwenye rafu. “Unaona hili tundu kubwa?”

Miguel labda angeweza kuingiza mkono wake kupitia lile tundu. “Ndiyo.”

“Hili mwanzo lilikua tundu dogo ambalo lingeweza kuzibwa kiurahisi. Lakini walisubiri, na sasa itakua vigumu sana kuliziba. Tabia mbaya na chaguzi mbaya ni kama tundu hilo. Ni vizuri zaidi kuzishughulikia mapema.”

Abuelo alikubali tena kwa kichwa, na mtazamo wa Abuelo mwenye busara ulirudi kuwa tabasamu. Waliendelea kuongea wakati Abuelo akifanya kazi. Muda wote, Miguel aliendelea kufikiria kuhusu peremende nyekundu ya kijiti.

Abuelo alipomaliza, Miguel alimsaidia kusafisha. Kisha Abuelo alichukua chupa yake ya peremende.

Hatimaye Miguel hakuweza kuvumilia zaidi. “Nilichukua moja ya peremende zako!” aliropoka.

Abuelo akaweka chupa chini. “Umesemaje?”

Miguel alimwambia kuhusu kuchukua peremende bila kuomba. “Nisamehe, Abuelo! Sitarudia tena, Naahidi!”

Abuelo alimkumbatia Miguel. Miguel alijisikia vizuri sana.

“Asante kwa kuwa mwaminifu. Hilo ni muhimu zaidi kwangu kuliko tu kitu kingine chochote.”

Katika matembezi ya kurudi nyumbani, Miguel alijisikia kama tu moja ya jozi mpya ya viatu vya Abuelo. Imara kama inavyoweza kuwa, na tayari kwa maisha!