Acha Tushiriki Ufahamu Wetu juu ya Mwokozi
Kutoka kwenye hotuba ya mkutano wa Wanawake wa Chuo Kikuu cha Brigham Young, “Ufahamu wa Mwokozi,” iliyotolewa Mei 5, 2017.
Wetu ni ujumbe wa amani, na ninyi ni wajumbe mnaohubiri ujumbe huu. Mnaweza kufanya hili kupitia njia mpya na za kuvutia za teknolojia.
Sisi ni Kanisa la Yesu Kristo, lililoanzishwa katika siku za mwisho. Katika njia sawa na ile ambayo Bwana aliwaamuru wanafunzi Wake wa kale, tumeamriwa katika siku za mwisho “enendeni ulimwenguni kote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe” (Marko 16:15).
Nabii wa kale Nefi alifupisha kwa maneno dhahiri misheni hii na ujumbe na madhumuni yake: “Tunazungumza kuhusu Kristo, tunafurahia katika Kristo, tunahubiri kuhusu Kristo, tunatoa unabii kumhusu Kristo, na tunaandika kulingana na unabii wetu, ili watoto wetu wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao” (2 Nefi 25:26).
Katika kitabu cha Mosia, tunasoma jinsi nabii wa kale wa Kitabu cha Mormoni Mfalme Benjamin alivyowakusanya watu wake kutoka nchi yote katika eneo la hekalu, akifanya mnara ujengwe, na akawafundisha Alipowafundisha, aliwatolea pia unabii juu ya siku yetu: “Na zaidi ya hayo, ninakuambia, kwamba wakati unakaribia ambako ufahamu wa Mwokozi utapenya kila taifa, kabila, lugha, na watu” (Mosia 3:20).
“Ufahamu juu ya Mwokozi”
Mojawapo ya zawadi ya thamani inayofaa kuthaminiwa ndani ya familia zetu na kuwapatia wengine ni “ufahamu juu ya Mwokozi,” au juu ya Yesu Kristo.
Kwa ufunguzi wa kipindi cha mwongozo wa Mungu cha utimilifu wa nyakati ilikuja elimu juu ya wanadamu wote na mfumuko wa maendeleo ya kiteknolojia. Ilileta pamoja nayo mapinduzi ya viwanda na zana za mawasiliano, ikiruhusu unabii wa Mfalme Benjamin kutimizwa.
Kama mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, aliyeitwa kama shahidi maalumu “wa jina la Kristo ulimwenguni kote” (M&M 107:23) nikiwa na kazi maalumu kote katika Mambo ya Umma na Kamati ya Huduma za Mawasiliano, Ninaweza kuzingatia kwenye utimiaji wa unabii huu—kwamba “ufahamu juu ya Mwokozi” unasambaa ulimwenguni kote—kwa kutumia teknolojia za hivi karibuni zinazopatikana kwetu.
“Kote katika Kila Taifa, Kabila, Lugha, na Watu”
Kihistoria, maendeleo katika uchapaji na ugunduzi wa redio na TV yamewezesha ujumbe wa Urejesho kwenda kote ulimwenguni. Tunapata mifano mingi ya hili, baadhi ya hiyo iko katika kumbukumbu zetu.
Ndani ya miaka kumi ya Ono la kwanza, na mwezi mmoja kabla ya Kanisa kuanzishwa, nakala 5,000 za Kitabu cha Mormoni zilichapishwa. Tangu hapo, Zaidi ya nakala milioni 175 zimekwisha kuchapishwa.
Jumapili yoyote asubuhi, unaweza kusikiliza au kuangalia matangazo ya Muziki na Neno Simulizi, ambayo inakaribia tangazo lake la 5,000. Matangazo ya kwanza yalitokea mubashara kwenye redio mnamo 1929. Matangazo ya kwanza ya mkutano mkuu kwenye TV yalifanyika mnamo 1949.
Cha kufurahisha, mnamo 1966, Rais David O. Mckay (1873–1970) alianza kuzungumzia juu ya mambo yajayo: “Uvumbuzi fiche kwa nguvu kama hii, aidha kwa baraka au maangamizo ya binadamu, kwa kuweka uwajibikaji wa mwanadamu katika kuudhibiti ugunduzi huu mkubwa kabisa kuliko ilivyowahi kuwekwa katika mikono ya mwanadamu. … Kipindi hiki ni cha huzuni na hatari zisizo na mipaka, vile vile uwezekano usioelezeka.”1
Mnamo 1974, Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) alielezea ono lake la siku zijazo: “Bwana ameubariki ulimwengu na setilaiti … nyingi. Zimewekwa juu angani, zikipokea na kurusha mawimbi ya matangazo katika kila kona ya uso wa dunia. … Kwa hakika setilaiti hizi ni mwanzo tu wa kile kilichotunzwa kwa ajili ya matangazo ya baadaye ya ulimwengu wote. … Ninaamini kwamba Bwana ana shauku ya kuweka mikononi mwetu uvumbuzi ambao sisi watu wa kawaida tumepata taabu kuona kwa kiwango kidogo sana.”2
Kwa maendeleo ya kiteknolojia katika mawasiliano na vyombo vya habari sasa vikija kwa juu kwa ukubwa karibu sana na mtandao, inaonekana kwamba tumeshuhudia katika maisha yetu uhalisia wa utimilifu wa unabii wa Mfalme Benjamin, Rais Mckay, na Rais Kimball.
Pia kuna mfumo wa kueleweka wa kuchukua teknolojia hizi ili kujenga ufalme wa Bwana duniani. Ningependa kushiriki nanyi mifano ya hili.
LDS.org na Mormon.org
Mnamo 1996, Kanisa lilianza rasmi matumizi ya mtandao kama chombo cha kupokea na kutuma ujumbe na cha mawasiliano. Tangu hapo, karibia mitandao 260 inayodhaminiwa na Kanisa imeanzishwa, ikijumuisha maeneo yanayopatikana karibia katika kila nchi ambapo waumini wa Kanisa wanaishi, katika lugha zao za asili.
Ninaelezea mifano miwili ya tovuti hizi. Kwanza ni LDS.org, iliyoanzishwa mnamo 1996, ambayo leo inapokea zaidi ya watembeleaji wanaokadiriwa zaidi ya milioni 1 kila wiki. Waumini wengi hupata hapa mtaala wa kufundishia na mahubiri ya mkutano mkuu uliopita. Pili ni Mormon.org, tovuti iliyotengenezwa kuitambulisha injili kwa majirani na marafiki zetu ambao siyo waumini wa Kanisa. Eneo hili hupokea zaidi ya watembeleaji wa kipekee zaidi ya milioni 16 kwa mwaka.
Programu-tumizi Tamba ya kwenye simu
Ni kweli, teknolojia zinaziduliwa katika mwendo kasi kali sana, ikihitaji juhudi kubwa na rasilimali kuendelea kuitumia. Kwa uvumbuzi wa simu za mkononi za kisasa ilikuja nguvu ya kufanya kazi na kupata kiasi kikubwa cha data ndani ya kifaa cha kisasa cha mkononi. Nyingi ya data hizi zimepangiliwa katika mfumo wa matumizi ya simu ya mkononi, au “programu-tumizi tamba.” Programu-tumizi tamba ya kwanza iliyodhaminiwa na Kanisa ilitolewa mwaka 2007.
Mifano imejaa ya manufaa yetu ya matumizi ya programu-tumizi tamba ya simu ya mkononi katika kusambaza “ufahamu wetu juu ya Mwokozi.” Sitaelezea undani wa programu-tumizi tamba nyingi ambazo zinapatikana kwenye ncha ya vidole vyako, lakini hii ni baadhi ya mifano ya programu-tumizi tamba ambazo zinafahamika kwako:
-
Gospel Library
-
Mormon Channel
-
LDS Tools
-
LDS Music
-
Family Tree
Hizi zimekuwa zikitumika mara mamilioni kwa wiki na mamilioni ya watumiaji.
Mitandao ya Kijamii
Kwa tafsiri, mitandao ya kijamii ni teknolojia inayopatanishwa na kompyuta inayoruhusu watu na mashirika kuangalia, kutengeneza, na kushiriki taarifa, mawazo, na aina zingine za kujieleza kupitia jamii zisizo banaya na mfumo mtandao.
Kuanzia karibia mwakani 2010, Kanisa lilianza kukubali kwa dhati azimio la matumizi ya mitandao ya kijamii ili kufanikisha kusambaza “ufahamu juu ya Mwokozi.” Hiki ni kipindi cha kukimbia haraka na cha mabadiliko makubwa kidigitali. Ni kama hakiwezi kufananishwa na chochote katika kasi ya kubadilika.
Sifa moja ya kuonekana ya mitandao ya kijamii ni kwamba punde tu mtu anapohisi kupata ufahamu au kuridhika na jukwaa moja, nyingine mpya, kubwa, au inayoonekana nzuri au nzuri zaidi hutokea.
Kwa ufupi nitaelezea majukwaa matano ya mitandao ya kijamii ambayo Kanisa linatumia kama njia za mawasiliano:
1. Facebook ina watumiaji zaidi ya bilioni 2 ulimwenguni kote. Hapa, watumiaji hutengeneza mtandao wao wenyewe wa kijamii wa marafiki waliounganishwa.
2. Instagram ni mtandao wa kijamii ambao hujikita kwenye picha na video.
3. Pinterest ni kama ubao wa kweli wa habari. Hapa picha za kuonekana zinazoitwa “pins” hupachikwa kwenye ubao. Hizi zaweza kuwa vifungu vyenye ushawishi au taswira za picha za kuleta ushawishi bora.
4. Twitter ni mtandao wa kijamii unaowawezesha watumiaji kutuma na kusoma jumbe za herufi 280 zinazoitwa “tweets.”
5. Snapchat hujumuisha picha na video fupi ambayo hupotea aidha baada ya muda mfupi au ndani ya saa 24.
Kitaasisi, tunatumia haya maeneo ya mitandao ya kijamii katika njia zenye nguvu.
Unaweza kujikumbusha ujumbe mzuri wa mkutano juu ya mfadhaiko ambao Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitoa miaka michache iliyopita.3 Kutoka katika hutuba hii, kipande cha video kilitengenezwa ambacho kilitazamwa zaidi ya mara milioni mbili kwenye Facebook tu, na maelfu ya kupenda, kushiriki, na maoni chanya.4
Mnamo Agosti 2016, Rais Dieter F. Uchtdorf aliweka video kwenye Instagram, akifundisha kanuni za injili kwa mjukuu wake Erik katika—unaweza kubashiri—chumba cha rubani kwenye ndege!5 Bandiko la Instagram la Rais Uchtdorf lilifurahiwa na maelfu, na maoni mengi chanya yaliambatana nalo.
Kanisa pia lilichapisha kwenye akaunti yake ya Instagramu mnamo Novemba 2017 video ya Mzee Dallin H. Oaks na Mzee M. Russell Ballard wakijibu maswali ya wasishana wazima kuhusu kina dada kutumikia misheni. Posti hii ilitazamwa zaidi ya mara 112,000.
Kwenye Pinterest, mtu anaweza kupata mamia ya pins kutoka LDS.org na hata zaidi kutoka watu binafsi, zikiwapa wengine mwongozo.
Kwa mfano, wengi hushirikiana na wengine maneno ya manabii—wale waliopita na waliopo. Pin moja kati ya mafundisho ya Rais Thomas S. Monson inasomeka, “Mambo mengi katika maisha yetu hutegemea mtazamo wetu.”6
Tweet ambayo Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alishiriki mwaka jana wakati wa asubuhi ya Pasaka, iliangaliwa mara 210,000. Mzee Bednar alionyesha kwamba ujumbe mfupi, rahisi, “Hayupo hapa, kwani amefufuka” (Mathayo 28:6), unaweza kuwa na matokeo makubwa na ya kudumu.
snapchat
Hatimaye, picha na maneno yakishiriki mojawapo ya Ujumbe wa Urais wa Kwanza wa Rais Monson hivi karibuni ulitokea kwenye Snapchat.
Hatari Zinazohusishwa Nazo
Sasa, baada ya kuunga mkono wema wote wa teknolojia hizi mpya na kuonyesha matumizi yake sahihi, nafikiri pia ni muhimu kujadili baadhi ya hatari zinazohusishwa nazo.
Tunapaswa kuwa makini na muda unaoweza kutumiwa kwenye mitandao ya kijamii au matumizi ya programu-tumizi tamba. Matumizi ya mitandao ya kijamii pia hubeba hatari ya kupunguza muingiliano wa uso-kwa-uso, ambayo inaweza kukomesha maendeleo ya ujuzi wa kijamii ya vijana wetu wengi.
Majanga yanayohusishwa na maudhui yasiyofaa hayawezi kupuuzwa. Kuna ongezeko la mlipuko ya uraibu wa ponografia katika jamii, ambao huathiri vibaya na husumbua hata waumini wa Kanisa na familia.
Hatimaye, ninatoa hatari mbili za ziada zinazoungana, ambazo nyavu zake hurushwa kwa kila mtu, ikijumuisha wasichana na wakina mama na wake wa kimilenia. Ninazipa hatari hizi majina ya “ulimbwende” na “ulinganishaji unaodhoofisha.” Nafikiri njia nzuri ya kuzielezea hizi hatari mbili ni kutoa baadhi ya mifano.
Kwa ujumla, picha zinazowekwa kwenye mitandao ya kijamii hujaribu kuelezea maisha katika ubora wake na mara nyingi hata katika njia zisizo halisi. Mara nyingi zimejaa taswira nzuri za mapambo ya nyumbani, maeneo mazuri ya matembezi, na maandalizi nakshi ya chakula. Hatari, hata hivyo, ni kwamba watu wengi wanakatishwa tamaa kwamba wanaonekana hawaendani na ulimbwende wa kweli.
Akivutiwa na pin ya “chapati ya kumimina” ya siku ya kuzaliwa, mpwa wangu karibuni aliweka jaribio lake kama hilo. Badala ya kuruhusu hili kuleta shinikizo isiyofaa, yeye aliamua kushawishi wengine kwa kuweka (sawa) “kushindwa kwake Pinterest” (tazama picha ya keki ya kimiminwa).
Kwa matumaini, tunaweza kujifunza kupata ucheshi zaidi na kupunguza kukata tamaa wakati tunapokabiliana na picha zinazoweza kuonyesha ulimbwende na ambao mara nyingi husababisha ulinganishi unaodhoofisha.
Hii inavyoonekana siyo tu dalili ya siku zetu bali, kwa kulinganisha maneno kutoka kwa Paulo, ilikuwako pia katika nyakati zilizopita: “Bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao … na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili” (2 Wakorintho 10:12).
Mzee J. Devn Cornish wa Sabini hivi karibuni ametoa ushauri kwa wakati muafaka pia: “Tunajitesa wenyewe isivyohitajika kwa kushindana na kujilinganisha. Kimakosa tunauhukumu wema wetu kwa vitu tunavyovifanya au tusivyo kuwa navyo na kwa maoni ya wengine. Kama ni lazima kujilinganisha, acheni tujilinganishe tulivyokuwa awali dhidi ya leo—na hata jinsi tunavyotaka kuwa hapo baadaye.”7
Acha nishiriki nanyi mojawapo ya siri za familia yetu, inayopatikana katika picha hii ya familia: (tazama ukurasa ufuatao) iliyopigwa miaka kadhaa iliyopita, kabla ya ujio wa mitandao ya kijamii. Hii ingepigwa leo, kuna uwezekano ingebandikwa, ikiwakilisha familia ya wapendwa wanne, rangi zilizochanganywa, wavulana wenye utii wakifurahia fursa nzuri ya picha ya familia pamoja. Je, ungependa kujua hadithi halisi?
Bado nakumbuka nilipopokea simu kutoka kwa mke wangu. “Gary, uko wapi? Tuko hapa kwenye chumba cha nje cha mpiga picha. Wote tuko tayari kupigwa picha. Haikuwa rahisi kuwavalisha wavulana wote, wote kuwa sawa, na tayari. Je, umekaribia hapa?”
Vema, nilikuwa nimesahau na nilikuwa sijatoka ofisini bado! Nilikuwa nimechelewa nusu saa, na mambo hayakuwa yamekwenda vizuri nilipokuwa sipo, hata kufikia mpaka kwenye fujo.
Nini kilikuwa kimetendeka? Vema, mvulana wangu mkubwa alikuwa akikimbia kwenye uani na akaona mti wa tufaha, akachuma matufaha kadhaa, na akaanza kuyarusha kwa wavulana wengine. Alimpiga mvulana wetu wa tatu mgongoni kwa tufaha na kumfanya aanguke, na hivyo alianza kulia.
Wakati huo, hilo likitendeka, mvulana wangu wa pili, alikaa chini na suruali yake ilipanda kidogo. Watoto wengine walipoona kwamba soksi zake zilikuwa soksi nyeupe za riadha, siyo soksi za kanisani mama yake alizokuwa amemtolea avae. Mke wangu alimuuliza, “kwa nini hukuvaa soksi zako za kanisani?”
Alisema, “Vema, Sizipendi. Zinakwaruza.”
Na wakati anaongea naye, mvulana wetu wa miaka miwili, anakimbia kuzunguka ua, anateleza kwenye kitu na anaanguka, na pua yake inatoka damu. Sasa kuna damu inadondoka kwenye shati yake nyeupe ya kukaba shingo, na inachafuka. Hapa ndipo nilipotokea. Njia pekee ya kuokoa picha ilikuwa ni kugeuza kikaba shingo na kukielekeza nyuma, kuficha madoa ya damu kwenye kamera.
Kilichotokea, wakati mwana wetu mkubwa akikimbia huku na huko na kurusha matufaha, alianguka na kupata doa kubwa la nyasi kwenye goti lake. Hivyo, katika picha, mkono wake umewekwa kwa werevu, kufunika madoa ya nyasi.
Na kwa mvulana wetu wa tatu, vema, tulisubiri kwa dakika 20 ili macho yake yasiwe tena mekundu kwa sababu ya kulia.
Na, ndiyo, madoa ya damu sasa yako nyuma ya shati ya mwana wetu mdogo.
Sasa, mwana wetu wa pili mikono yake imewekwa kwa werevu juu ya soksi zake nyeupe za riadha ili kwamba kila kitu kifanane.
Na kwangu, vema, mimi lawama zote ziko juu yangu kwa sababu ilikuwa ni kufika kwangu kwa kuchelewa kulikokuwa kichocheo cha haya yote.
Hivyo, unapoona picha hii nzuri ya familia yetu na kuomboleza, “Kwa nini tusiweke mambo pamoja na kuwa picha kamilifu ya familia kama ya kwao?” wote mnajua vizuri zaidi!
Mitandao ya Kijamii na Kazi ya Umisionari
Kama unavyoona, tunahitajika kuwa waangalifu kwa madhara na hatari, ikijumuisha ulimbwende na ulinganishi unaodhoofisha. Ulimwengu kwa kawaida haung’ari kama inavyoonekana kwenye mitandao ya kijamii. Hata hivyo, kuna mengi mazuri ambayo yamekuja na yatakuja kupitia majukwaa haya ya mawasiliano.
Idara ya Misionari ilitoa maelekezo fulani mapya katika mwaka wa 2017 juu ya njia za utendaji mitandao ya kijamii inaweza kutumika katika kazi ya umisionari. Nyenzo nyingi za kidijitali zilizopo kwetu zinaweza kutumika kwa nguvu, urahisi, na kwa njia zenye kuleta matokeo yanayotakiwa.
Kuna matumizi ya aina nyingi kwa utumiaji wa teknolojia katika njia sahihi na za kushawishi. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kufundisha utumiaji sahihi ya teknolojia kwa kizazi kinachochipuka na kuonya na kuzuia utumiaji mbaya na hatari zinazohusiana nazo pia. Hii inapaswa kusaidia kutuhakikishia kwamba manufaa ya teknolojia yatazidi hatari zinazohusiana nazo.
“Ni Wazuri kiasi gani Wajumbe Hawa”
Wakati nilipokuwa Nikitafakari na kuomba kwa kina kuhusu ujumbe huu, Niliamka mapema asubuhi moja nikiwa na wimbo na maneno yake rahisi: “ni wazuri kiasi gani wajumbe hawa ambao hututangazia injili ya amani.”8
Wetu ni ujumbe wa amani, na ninyi ni wajumbe wazuri mnaoutangaza ujumbe huu. Unaweza kufanya hivi kupitia hizi njia mpya, za kupendeza za teknolojia. Tunaishi katika ulimwengu wa kipekee katika utimilifu wa nyakati tukiwa na uwezo wa kuhubiri injili ya amani kiuhalisia kwenye ncha za vidole vyetu.
Tuna maneno ya kinabii ya manabii wa kale, ambayo kwa ukamilifu yanasifia wakati wetu na kutoa uelekeo kwa siku yetu: “Na zaidi ya hayo, ninakuambia, kwamba wakati unakaribia ambako ufahamu juu ya Mwokozi utapenya kila taifa, kabila, lugha, na watu” (Mosia 3:20).
Pia tuna maneno yanayokuja kwetu kupitia ufunuo wa siku za leo, yakiongea nasi na kutupa muongozo kwa ajili ya wakati wetu na mazingira yetu. Ninamnukuu Mzee Bednar: “Ninaamini wakati umefika kwetu kama wafuasi wa Kristo kutumia zana hizi zenye ushawishi kwa usahihi na kwa weledi zaidi kushuhudia juu ya Mungu Baba wa Milele, mpango Wake wa furaha kwa watoto Wake, na Mwanawe, Yesu Kristo, kama Mwokozi wa ulimwengu; kutangaza uhalisia wa Urejesho wa injili katika siku za mwisho; na kutekeleza kazi ya Bwana.”9
Ninamwalika kila mmoja wenu kwa ukamilifu kufikiria nafasi yako ya kuhubiri injili ya amani kama mjumbe mzuri. Acha kila mmoja wetu tufanye sehemu yetu kwa kushiriki na wengine “ufahamu wetu juu ya Mwokozi” kwa kila taifa, kabila, lugha, na watu. Njia nzuri zaidi ya kufanya hili ni hatua moja kwa wakati na katika njia ya kipekee inayofanya kazi kwako na kwa familia yako. Na kila mmoja wetu awe na ujasiri wa kublogu, kupin, kupenda, kushiriki, kubandika, kufanya urafiki, kutweet, kusnap, na kubadilisha katika njia ambayo itamtukuza, kumpa heshima, na kutii mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo na kuleta ufahamu juu ya Mwokozi kwa familia yako, wapendwa wako, na marafiki—ikijumuisha rafiki zako katika mitandao ya kijamii.