Mafundisho na Maagano 2021
Novemba 1–7. Mafundisho na Maagano 125–128: “Sauti ya Furaha kwa Walio Hai na Wafu”


“Novemba 1–7. Mafundisho na Maagano 125-128: ‘Sauti ya Furaha kwa Walio Hai na Wafu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)

“Novemba 1–7. Mafundisho na Maagano 125–128,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia: 2021

Picha
familia na mababu katika ulimwengu wa roho

Sisi na Wao na Wao na Sisi, na Caitlin Connolly

Novemba 1–7

Mafundisho na Maagano 125–128

“Sauti ya Furaha kwa Walio Hai na Wafu”

Kumbuka kuandika hisia zako unapojifunza Mafundisho na Maagano 125–28 ili kwamba uweze kuzitafakari na kuzishiriki pamoja na wengine.

Andika Misukumo Yako

Mnamo Agosti 1840, Jane Neyman aliyekuwa anaomboleza alimsikiliza Nabii Joseph Smith akizungumza kwenye mazishi ya rafiki yake Seymour Brunson. Cyrus Mwana kijana wa Jane pia alikuwa amefariki hivi karibuni. Kuongezea kwenye maombolezo yake ulikuwa ni ukweli kwamba Cyrus alikuwa kamwe hajabatizwa, na Jane alikuwa na wasiwasi hii itamaanisha nini kwa nafsi yake ya milele. Joseph alijua jinsi Jane alivyokuwa akihisi; alikuwa amejiuliza jambo kama hilo kuhusu mpendwa kaka yake Alvin, ambaye pia alikufa kabla ya kubatizwa. Kwa hiyo Nabii aliamua kushiriki na Jane, na wengine wote mazishini, nini Bwana amefunua kwake kuhusu wale ambao wamekufa bila kupokea ibada za injili—na kile tunachoweza kufanya kuwasaidia.

Mafundisho ya ubatizo kwa ajili ya wafu yaliwasisimua Watakatifu; mawazo yao yaligeuka mara moja kwa wazazi, mababu, na wanafamilia wengine waliofariki. Sasa kulikuwa na matumaini kwa ajili yao! Joseph alishiriki furaha yao, na alitumia lugha ya furaha, na ya shauku kuelezea kile Bwana alichomfundisha kuhusu wokovu wa wafu: “Acheni milima ishangilie kwa shangwe, nanyi mabonde yote lieni kwa sauti; nanyi bahari zote na nchi kavu yatajeni maajabu ya Mfalme wenu wa Milele!” (Mafundisho na Maagano 128:23).

Ona Watakatifu, 1:415–27; “Barua kuhusu Ubatizo kwa ajili ya wafu,” Ufunuo katika Muktadha, 272–76.

Picha
ikoni ya kujifunza binafsi

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Binafsi Maandiko

Mafundisho na Maagano 126

Bwana ananitaka niitunze familia yangu.

Baada ya kurudi nyumbani karibuni kutoka misheni zake kadhaa za Uingereza, Brigham Young alipokea wito mwingine muhimu kutoka kwa Bwana—“kuitunza kwa kipekee familia [yake]” (mstari wa 3), ambayo iliteseka kwa kutokuwepo kwake. Unapotafakari jinsi ushauri huu na mwingine katika sehemu ya 126 unavyokuhusu, fikiria maneno haya kutoka kwa Rais Bonnie L. Oscarson, Rais Mkuu wa wasichana aliyepita:

“Kumbuka kwamba baadhi ya mahitaji makubwa mno yanaweza kuwa yale yaliyo mbele yako. Anzeni huduma katika nyumba zenu wenyewe na katika familia zenu wenyewe. Haya ni mahusiano ambayo yanaweza kuwa ya milele. Hata kama—na labda hususani kama—hali ya familia yako haijakamilika, unaweza kutafuta njia za kutumikia, kuinua, na kuimarisha. Anza pale ulipo, wapende kama walivyo, na jiandae kwa ajili ya familia unayotaka kuwa nayo baadaye” (“Mahitaji mbele Yetu,” Ensign au Liahona, Nov. 2017, 27).

Ona pia “Fanya Matunzo Mahsusi ya Familia Yako,” Ufunuo katika Muktadha, 242–49.

Mafundisho na Maagano 127:2–4

Bwana anajua furaha na huzuni zangu.

Mashitaka ya uongo na vitisho vya kukamatwa vilimlazimisha tena Joseph Smith kujificha katika mwezi wa Agosti 1842. Na bado maneno aliyoyaandika kwa Watakatifu muda huu (sasa Mafundisho na Maagano 127) yamejaa matumaini na furaha. Ni nini mistari ya 2–4 inakufundisha kuhusu Mungu? Kuhusu jinsi unavyoweza kukabiliana na majaribu binafsi?

Fikiria kuandika jinsi Bwana anavyokuondoa katika “maji ya kina kirefu” cha maisha yako.

Mafundisho na Maagano 127:5; 128:1.

“Chochote kile unachokiandika duniani kitaandikwa mbinguni.”

Unaposoma Mafundisho na Maagano 127:5–8; 128:1–8, tafuta sababu kwa nini Bwana alimpa Joseph Smith maelekezo mahususi kuhusu kuandika ubatizo kwa ajili ya wafu. Hii inakufundisha nini kuhusu Bwana na kazi Yake?

Picha
kijana akiwa na kadi zenye majina ya familia

Kufanya huduma za hekaluni kwa ajili ya mababu zetu kunaunganisha mioyo yetu kwao.

Mafundisho na Maagano 128:5–25

Wokovu wa mababu zangu ni muhimu kwa wokovu wangu.

Ni wazi kutoka kile Mungu alichokifunua kupitia Joseph Smith kwa nini mababu zetu ambao hawakubatizwa katika maisha haya wanahitaji msaada wetu kwa ajili ya wokovu wao. Lakini kwa nini unafikiri wokovu wa mababu zetu ni “muhimu na lazima kwa wokovu wetu”? (Ona Mafundisho na Maagano 128:15–18; msisitizo umeongezwa).

Mstari wa 5 unafundisha kwamba ibada za ubatizo kwa ajili ya wafu ilikuwa “imeandaliwa kabla ya kuwekwa kwa msingi wa ulimwengu.” Ukweli huu unakufundisha nini kuhusu Mungu na mpango Wake? Je, ujumbe wa Rais Henry B. Eyring “Kukusanya Familia ya Mungu” unaongeza nini kwenye uelewa wako? (Ensign au Liahona, Mei 2017, 19–22).

Joseph Smith alitumia misemo kama “nguvu ya kuunganisha,” “kiungo unganishi,” na “muungano kamili” wakati anafundisha kuhusu ibada za ukuhani na ubatizo kwa ajili ya wafu. Tafuta misemo hii na ile inayofanana na hii unaposoma Mafundisho na Maagano 128:5–25. Ni baadhi ya vitu gani ambavyo, kupitia kwa Yesu Kristo, vinaweza kufungwa pamoja kwa sababu ya ibada za ukuhani kwa ajili ya wafu? Kwa nini “ujasiri” ni neno zuri kuelezea mafundisho ya wokovu kwa ajili ya wafu? (Ona mistari ya 9–11).

Nini kinakuvutia kuhusu maneno ya Joseph Smith katika mistari ya 19–25? Ni kwa jinsi gani mistari hii inaathiri unavyohisi kuhusu huduma za hekaluni kwa ajili ya mababu zako? kuhusu Yesu Kristo? Unahisi kuvutiwa kufanya nini? (Ona FamilySearch.org/discovery kwa mawazo).

Ona pia 1 Wakorintho 15:29; Dale G. Renland, “Historia ya Familia na Kazi ya Hekalu: Kuunganisha na Kuponya,” Ensign au Liahona, Mei 2018, 46–49: video za “A sacrifice of Time” na “Their hearts Are Bound to You,” ChurchofJesusChrist.org.

Picha
ikoni ya kujifunza kifamilia

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Maandiko Kifamilia na Jioni ya Nyumbani

Mafundisho na Maagano 126.Kusoma ushauri huu kwa Brigham Young kunaweza kuvutia familia yako kuzungumza kuhusu jinsi mnavyoweza kutumia muda zaidi “kushughulikiana vizuri” (mstari wa 3) nyinyi kwa nyinyi.

Mafundisho na Maagano 128:15–18.Ni zipi baadhi ya baraka za kuokoa na kukamilisha za kazi ya historia ya familia? Unaweza kupata baadhi ya mawazo katika video “The Promised Blessings of Family History” (ChurchofJesusChrist.org) au katika wimbo kuhusu historia ya familia, kama vile “Family History—I Am Doing It” (Kitabu cha nyimbo za Watoto, 94).

Mafundisho na Maagano 128:18.Fikiria kutengeneza mkufu wa karatasi wenye majina ya wanafamilia na mababu kwenye kila kiungo kuonyesha jinsi historia ya familia na kazi ya hekaluni vinavyotengeneza “kiungo unganishi” kinachotuunganisha sisi na mababu zetu. Huenda ungeweza kufanya uchunguzi kiasi kwenye FamilySearch.org kutafuta wanafamilia wa ziada na kuona jinsi gani urefu wa mnyororo wako unavyokua.

Mafundisho na Maagano 128:19–23.Pengine wanafamilia wangeweza kupekua mistari hii kwa ajili ya maneno ambayo yanaonyesha shangwe ya Joseph Smith kuhusu injili ya Yesu Kristo na wokovu wa wafu. Wanafamilia wangeweza kushiriki uzoefu ambao umewafanya washangilie kuhusu kazi hii pia—au mngeweza kutafuta uzoefu kama huo pamoja kwenye FamilySearch.org/discovery.

Kwa mawazo zaidi kwa ajili ya kuwafundisha watoto, ona muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Msingi.

Wimbo uliopendekezwa: “Family History—I Am Doing It,” Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 94.

Picha
ikoni ya sauti za urejesho

Sauti za Urejesho

Ubatizo kwa ajili ya Wafu, “Somo Jipya na la Kitukufu”

Picha
mchoro wa kisima cha ubatizo katika Hekalu la Nauvoo

Mchoro huu unaonyesha kisima cha ubatizo cha Hekalu la Nauvoo kikiwa juu ya ng’ombe kumi na mbili.

Phebe na Wilford Woodruff

Phebe Woodruff alikuwa akiishi karibu na Nauvoo wakati Joseph Smith alipoanza kufundisha kuhusu ubatizo kwa ajili ya wafu. Aliandika kuhusu hilo kwa mume wake, Wilford, ambaye alikuwa akihudumu misheni Uingereza:

“Kaka Joseph … amejifunza kwa ufunuo kwamba wale katika kanisa hili wanaweza kubatizwa kwa ajili ya jamaa zao wowote waliokufa na hawakuwa na fursa ya kuisikia injili hii, hata kwa ajili ya watoto wao, wazazi, kaka, dada, mababu, wajomba, na mashangazi. … Mara tu wanapobatizwa kwa ajili ya marafiki zao wanafunguliwa kutoka kifungoni na wanaweza kuwadai katika ufufuko na kuwaleta kwenye ufalme wa selestia—mafundisho haya yamepokelewa kwa uchangamfu na kanisa na wanasonga mbele kwa wingi, baadhi wanakwenda kubatizwa karibu mara 16 … katika siku moja.”1

Wilford Woodruff baadaye alisema juu ya kanuni hii: “Mara tu niliposikia juu ya hilo roho yangu iliruka kwa furaha. … Nilisonga mbele na nilibatizwa kwa ajili ya jamaa zangu wote waliokufa nilioweza kuwafikiria. … Nilihisi kusema haleluya wakati ufunuo huu ulipokuja ukitufunulia juu ya ubatizo kwa ajili ya wafu. Nilijisikia kwamba tulikuwa na haki ya kushangilia katika baraka za Mbingu.”2

Vilate Kimball

Kama Dada Woodruff, Vilate Kimball alisikia kuhusu ubatizo kwa ajili ya wafu wakati mume wake, Heber, alipokuwa mbali akihubiri injili. Alimwandikia:

“Rais Smith amefungua somo jipya na tukufu … ambalo limesababisha uamsho mkubwa katika Kanisa. Ambalo ni, kubatizwa kwa ajili ya wafu. Paulo analizungumzia, katika Wakorintho wa kwanza mlango wa 15 mstari wa 29. Joseph amepokea maelezo yake kamili zaidi kwa Ufunuo. … Ni fursa ya Kanisa hili kubatizwa kwa ajili ya ndugu zao wote ambao walifariki kabla ya injili hii kuja; hata kurudi nyuma mpaka kwa Babu na Bibi zao wakuu. … Kwa kufanya hivyo, tunatenda kama mawakala kwa ajili yao; na kuwapa wao fursa ya kujitokeza katika ufufuo wa kwanza. Anasema watakuwa na Injili iliyohubiriwa kwao … lakini hakuna kitu kama roho kubatizwa. … Tangu utaratibu huu umekuwa ukihubiriwa hapa, maji yamekuwa yakiendelea kusumbuliwa. Wakati wa mkutano mkuu kulikuwa wakati mwingine kuanzia Wazee nane mpaka kumi katika mto kwa wakati mmoja wakibatiza. … Ninataka kubatizwa kwa ajili ya Mama yangu. Niliazimia kungoja mpaka utakaporudi nyumbani, lakini mara ya mwisho Joseph alipozungumza juu ya swala hili, alishauri kila mtu kuwa tayari na kutenda, na kuwakomboa marafiki zao kutoka kifungoni haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo nafikiri napaswa kusonga mbele wiki hii, kwa vile kuna idadi ya majirani wanaosonga mbele. Baadhi tayari wamebatizwa mara kadhaa zaidi. … Hivyo unaona kuna nafasi kwa ajili ya wote. Je, haya si mafundisho tukufu?”3

Phebe Chase

Mara baada ya kisima cha ubatizo kukamilika katika Hekalu la Nauvoo, ubatizo kwa ajili ya wafu ulifanywa mle badala ya mtoni. Phebe Chase, mkaazi wa Nauvoo, alimwandikia mama yake kuhusu hekalu, akielezea kisima cha ubatizo kama mahali ambapo “tunaweza kubatizwa kwa ajili ya wafu wetu na kuwa wakombozi juu ya Mlima Sayuni.” Aliendelea kuelezea kwamba katika kisima hiki, “nimebatizwa kwa ajili ya mpendwa baba yangu na marafiki zangu wote waliokufa. … Sasa nataka kujua majina ya baba na mama yako ili kwamba niwaweke huru, kwani natamani kuwafariji Wafu. … Bwana amezungumza tena na kurejesha utaratibu wa kale.”4

Sally Randall

Katika kuwaandikia marafiki zake na familia kuhusu ubatizo wa wafu, Sally Randall alikumbuka kufariki kwa mwanae George:

“Aah muda gani wa majaribu ambao ulikuwa kwangu na inaonekana bado kwamba siwezi kupatanishwa nao, lakini … baba yake amebatizwa kwa ajili yake na imekuwa jambo tukufu kwamba tunaamini na kupokea utimilifu wa injili kama inavyohubiriwa sasa na tunaweza kubatizwa kwa ajili ya marafiki zetu wote waliofariki na kuwaokoa kwa kadiri ya tunavyoweza kupata ufahamu kuwahusu.

“Ninataka ungeniandikia majina stahiki ya wote tunaohusiana nao ambao ni wafu kurudi nyuma kwa mababu na mabibi kwa kiasi chochote. Ninakusudia kufanya kile ninachoweza kuwaokoa marafiki zangu na ningekuwa na furaha kuu kama baadhi yenu mngekuja na kunisaidia kwani ni kazi kubwa kwa mmoja kuifanya peke yake. … Nategemea utafikiri haya ni mafundisho ya ajabu lakini utayaona kuwa ya kweli.”5

Muhtasari

  1. Barua ya Phebe Woodruff kwa Wilford Woodruff, Okt. 6, 1840, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake; matamshi na tahajia vimebadilishwa.

  2. “Maoni,” ya Wilford Woodruff, Deseret News, Mei 27, 1857, 91; tahajia imeboreshwa.

  3. Barua ya Vilate Kimball kwenda kwa Heber C. Kimball, Okt. 11, 1840, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake; tahajia na alama za uandishi vimeboreshwa.

  4. Barua ya Phebe Chase, isiyo na tarehe, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake; tahajia na alama za uandishi vimeboreshwa. Wakati Watakatifu kwa mara ya kwanza walipoanza kufanya ubatizo kwa ajili ya wafu, watu binafsi wakati mwingine walibatizwa kwa niaba ya mababu wa jinsia zote. Baadae ilifunuliwa kwamba wanaume wanapaswa kubatizwa kwa ajili ya wanaume na wanawake kwa ajili ya wanawake.

  5. Barua ya Sally Randall, Apr. 21,1844, Maktaba ya Historia ya Kanisa, Jiji la Salt Lake; tahajia na alama za uandishi vimebboreshwa.

Picha
kisima cha ubatizo katika Hekalu la Ogden Utah

Kisima cha ubatizo katika Hekalu la Ogden Utah kipo juu ya migongo ya ng’ombe kumi na wawili.

Chapisha