Maandiko Matakatifu
Alma 10


Mlango wa 10

Lehi ni wa uzao wa Manase—Amuleki anaelezea jinsi malaika alivyomwamuru kwamba amhudumie Alma—Sala za watu wenye haki zinawaokoa watu—Mawakili na Waamuzi wasio wenye haki wanaanza kupanga maangamizo ya watu. Karibia mwaka 82 K.K.

1 Sasa haya ndiyo maneno ambayo Amuleki aliwahubiria watu ambao walikuwa katika nchi ya Amoniha, akisema:

2 Mimi ni Amuleki; mimi ni mwana wa Gidona, ambaye alikuwa mwana wa Ishmaeli, ambaye alikuwa uzao wa Aminadi; na alikuwa ni huyo Aminadi ambaye alitafsiri maandiko ambayo yalikuwa kwenye ukuta wa hekalu, ambayo yaliandikwa kwa kidole cha Mungu.

3 Na Aminadi alikuwa uzao wa Nefi, ambaye alikuwa ni mwana wa Lehi, ambaye alitoka nchi ya Yerusalemu, ambaye alikuwa uzao wa Manase, ambaye alikuwa mwana wa Yusufu aliyeuzwa Misri kwa mikono ya kaka zake.

4 Na tazama, mimi pia sio mtu aliye na heshima ndogo miongoni mwa wote ambao wananijua; ndiyo, na tazama, nina jamaa na marafiki wengi, na pia nimepokea utajiri mwingi kutokana na bidii ya mikono yangu.

5 Walakini, hata baada ya haya yote, sijaelewa sana kuhusu njia za Bwana, na siri zake na nguvu zake za ajabu. Nilisema kuwa sikuwahi kujua mengi kuhusu vitu hivi; lakini tazama, nimekosea, kwani nimeona siri zake nyingi na nguvu zake za ajabu; ndiyo, hata katika kuhifadhiwa kwa maisha ya watu hawa.

6 Walakini, nilishupaza moyo wangu, kwani niliitwa mara nyingi lakini sikusikia; kwa hivyo nilijua kuhusu vitu hivi, lakini nisingeweza kuvifahamu; kwa hivyo nikaendelea kumuasi Mungu, katika uovu wa moyo wangu, hadi siku ya nne ya mwezi huu wa saba, ambao uko katika mwaka wa kumi wa utawala wa waamuzi.

7 Nilipokuwa nikisafiri kumuona mmoja wa jamaa yangu wa karibu, tazama malaika wa Bwana alinitokea na kuniambia: Amuleki, rudi nyumbani kwako, kwani utamlisha nabii wa Bwana; ndiyo, mtu mtakatifu, ambaye amechaguliwa na Mungu; kwani amefunga siku nyingi kwa sababu ya dhambi za watu hawa, na ana njaa, na utamkaribisha katika nyumba yako na utamlisha, na atakubariki wewe na nyumba yako; na baraka ya Bwana itakuwa juu yako na nyumba yako.

8 Na ikawa kwamba nilitii sauti ya malaika, na nikarudi nyumbani kwangu. Na nilipokuwa nikienda hapo nilimpata mtu ambaye malaika alikuwa ameniambia: Wewe utampokea katika nyumba yako—na tazama ni huyu mtu ambaye amekuwa akiwazungumzia kuhusu vitu vya Mungu.

9 Na malaika aliniambia kuwa yeye ni mtu mtakatifu; kwa hivyo najua kwamba yeye ni mtu mtakatifu kwa sababu ilisemwa na malaika wa Mungu.

10 Na tena, najua kwamba vitu ambavyo ameshuhudia ni vya kweli; kwani tazama nawaambia, jinsi vile Bwana anavyoishi, hata hivyo amemtuma malaika wake kufanya vitu hivi vidhihirishwe kwangu; na amefanya haya wakati huyu Alma alipoishi katika nyumba yangu.

11 Kwani tazama, ameibariki nyumba yangu, amenibariki, na wanawake wangu, na watoto wangu, na baba yangu na jamaa yangu; ndiyo, ameibariki jamaa yangu yote, na baraka za Bwana zimekaa juu yetu kulingana na maneno ambayo alizungumza.

12 Na sasa, Amuleki alipokuwa amezungumza maneno haya watu walianza kustaajabu, wakiona kwamba kulikuwa na shahidi zaidi ya mmoja ambaye alishuhudia kuhusu vitu ambavyo walishutumiwa, na pia kuhusu vitu ambavyo vitakuja, kulingana na roho ya unabii iliyokuwa ndani yao.

13 Walakini, kulikuwa na wengine miongoni mwao ambao walitaka kuwauliza maswali, ili wawanase katika maneno yao kwa mitego, ili wapate ushuhuda dhidi yao, ili wawapeleke mbele ya waamuzi wao ili wahukumiwe kulingana na sheria, na ili wauawe au kutiwa gerezani, kulingana na makosa ambayo wangewasingizia au kushuhudia kinyume chao.

14 Sasa ilikuwa ni wale watu ambao walijaribu kuwaangamiza, ambao walikuwa ni mawakili, ambao waliajiriwa au kuchaguliwa na watu kutekeleza sheria wakati wao wa hukumu, au katika hukumu ya makosa ya watu mbele ya waamuzi.

15 Sasa hawa mawakili walikuwa na elimu ya udanganyifu na ujanja wa watu; na hii ni kuwawezesha wawe na ustadi katika kazi yao.

16 Na ikawa kwamba walianza kumuuliza Amuleki maswali, ili wamfanye achanganye maneno yake, au kukanusha maneno ambayo angezungumza.

17 Sasa hawakujua kwamba Amuleki angeweza kujua mipango yao. Lakini ikawa kwamba walipoanza kumuuliza maswali, alihisi mawazo yao, na akawaambia: Ee ninyi kizazi kiovu na kibaya, ninyi mawakili na wanafiki, kwani mnajenga msingi wa ibilisi; kwani mnaweka mitego ya kunasa walio watakatifu wa Mungu.

18 Mnapanga mipango ya kuchafua njia za wenye haki, na kuteremsha ghadhabu ya Mungu juu ya vichwa vyenu, hata kwa maangamizo ya watu hawa.

19 Ndiyo, si ni Mosia, ambaye alikuwa mfalme wetu wa mwisho, aliyesema alipokaribia kutoa ufalme, na hakuwa na yeyote angestahili kupewa, na akasababisha kwamba watu hawa watawaliwe kwa sauti ya watu—ndiyo, alisema kwamba kama wakati utafika ambao sauti ya watu itachagua uovu, yaani, wakati ukifika ambao watu hawa wataanguka katika dhambi, watakuwa tayari kuangamizwa.

20 Na sasa ninawaambia kwamba Bwana anahukumu maovu yenu vyema; na anawalilia watu hawa vyema, kwa sauti ya malaika wake: Tubuni ninyi, tubuni, kwani ufalme wa mbinguni u karibu.

21 Ndiyo, kwa wema analia, kwa sauti ya malaika wake kwamba: Mimi nitashuka chini miongoni mwa watu wangu, na usawa na haki mikononi mwangu.

22 Ndiyo, na ninawaambia kwamba kama sio sala za wenye haki, walio katika nchi hii sasa, kwamba mngekuwa mmetembelewa kwa maangamizo kamili; lakini haingekuwa kwa mafuriko, kama watu katika siku za Nuhu, lakini ingekuwa kwa njaa, na kwa tauni, na kwa upanga.

23 Lakini ni kwa sala za wale wenye haki kwamba mmeachiliwa; sasa kwa hivyo, kama mtawafukuza wale wenye haki kutoka miongoni mwenu basi Bwana hatauzuia mkono wake; lakini katika ghadhabu yake atawateremkia; kisha mtapigwa kwa njaa, na kwa tauni, na kwa upanga; na wakati u karibu msipotubu.

24 Na sasa ikawa kwamba watu walimkasirikia Amuleki zaidi, na wakalia, na kusema: Huyu mtu anadharau sheria zetu ambazo ni za haki, na mawakili wetu wenye busara ambao tumewachagua.

25 Lakini Amuleki aliwanyoshea mkono wake, na kusema kwa nguvu: Ee ninyi kizazi kiovu, mbona Shetani ameingia katika mioyo yenu jinsi hii? Kwa nini mnajitoa kwake na kumruhusu awe na uwezo juu yenu, kufunga macho yenu, kwamba hamfahamu maneno ambayo yamezungumzwa, kulingana na ukweli wao?

26 Kwani tazama, nimezungumza kinyume cha sheria yenu? Ninyi hamfahamu; mnasema kwamba nimezungumza kinyume cha sheria yenu; lakini sikufanya hivyo, lakini nimeisifu sheria yenu, ambayo inawahukumu.

27 Na sasa tazama, nawaambia, kwamba msingi wa maangamizo ya watu hawa umeanza kujengwa na mawakili wenu na waamuzi wenu ambao hawana haki.

28 Na sasa ikawa kwamba baada ya Amuleki kuzungumza maneno haya watu walipaza sauti yao dhidhi yake, na kusema: Sasa tunajua kwamba huyu mtu ni mtoto wa ibilisi, kwani ametudanganya; kwani ameishutumu sheria yetu. Na sasa anasema kwamba hajaishutumu.

29 Na tena, amewashutumu mawakili wetu, na waamuzi wetu.

30 Na ikawa kwamba mawakili waliweka vitu hivi katika mioyo yao ili wavikumbuke dhidi yake.

31 Na kulikuwa na mmoja miongoni mwao ambaye jina lake lilikuwa Zeezromu. Sasa yeye alikuwa wa mbele kumshtaki Amuleki na Alma, yeye akiwa mwenye ujuzi mwingi miongoni mwao, na alikuwa na shughuli nyingi miongoni mwa watu.

32 Sasa lengo la mawakili hawa lilikuwa ni kupata faida; na walipata faida kulingana na kazi yao.