Mlango wa 27
Bwana anamwamuru Amoni awaongoze watu wa Anti-Nefi-Lehi kwenye usalama—Wakati anakutana na Alma, shangwe ya Amoni inapunguza nguvu zake—Wanefi wanagawia wa Anti-Nefi-Lehi nchi ya Yershoni—Wanaitwa watu wa Amoni. Karibia mwaka 90–77 K.K.
1 Sasa ikawa kwamba wakati wale Walamani ambao walikuwa wameanzisha vita na Wanefi walipata, baada ya kujaribu mara nyingi kuwaangamiza, kwamba ilikuwa ni bure kutazamia kuwaangamiza, walirudi tena kwa nchi ya Nefi.
2 Na ikawa kwamba Waamaleki, kwa sababu ya hasara yao, walikasirika kupita kiasi. Na walipoona kwamba hawangelipiza kisasi kwa Wanefi, walianza kuwavuruga watu kuwa na hasira dhidi ya ndugu zao, watu wa Anti-Nefi-Lehi; kwa hivyo walianza tena kuwaangamiza.
3 Sasa hawa watu walikataa tena kutwaa silaha zao, na wakavumilia wenyewe wauawe vile maadui wao walivyotaka.
4 Sasa Amoni na ndugu zake walipoona hii kazi ya mauaji baina ya wale ambao waliwapenda sana, na kati ya wale waliowapenda—kwani walikuwa wanatendewa kama kwamba ni malaika waliotumwa kutoka kwa Mungu kuwaokoa kutoka kwa maangamizo yasiyo na mwisho—kwa hivyo, Amoni na ndugu zake walipoona kazi hii kubwa ya mauaji, walivurugwa na huruma, na wakamwambia mfalme:
5 Acha tukusanye pamoja hawa watu wa Bwana, na acha sisi tuteremke kwenye nchi ya Zarahemla mahali pa ndugu zetu Wanefi, na tutoroke kutoka mikono ya maadui wetu, ili tusiuawe.
6 Lakini mfalme aliwambia: Tazama, Wanefi watatuangamiza, kwa sababu ya mauaji mengi na dhambi ambazo tumetenda dhidi yao.
7 Na Amoni akasema: Nitaenda kuuliza kutoka kwa Bwana, na ikiwa atatuambia, nendeni mahali ndugu zenu wapo, je, utaenda?
8 Na mfalme akamwambia: Ndiyo, ikiwa Bwana atatuambia twende, tutaenda chini kwenye ndugu zetu, na tutakuwa watumwa wao hadi tutakapowalipa mauaji mengi na dhambi ambazo tumetenda dhidi yao.
9 Lakini Amoni aliwaambia: Ni kinyume cha sheria ya ndugu zetu, ambayo ilianzishwa na baba yangu, kwamba kusiwe na watumwa baina yao; kwa hivyo acha twende chini na kutegemea juu ya rehema ya ndugu zetu.
10 Lakini mfalme aliwambia: Mwulize Bwana, na ikiwa atatuambia twende, tutaenda; la sivyo tutaangamia hapa nchini.
11 Na ikawa kwamba Amoni akaenda na kumwuliza Bwana, na Bwana akamwambia:
12 Toa hawa watu kutoka nchi hii, ili wasiangamie; kwani Shetani ameshikilia mioyo ya Waamaleki, ambao wanawavuruga Walamani kukasirika dhidi ya ndugu zao kuwaua; kwa hivyo nendeni ninyi nje ya nchi hii; na heri kwa watu hawa wa kizazi hiki, kwani nitawahifadhi.
13 Na sasa ikawa kwamba Amoni alienda na kumwambia mfalme maneno yote ambayo Bwana alikuwa amemwambia.
14 Na wakakusanya pamoja watu wao wote, ndiyo, watu wote wa Bwana, na walikusanya mifugo yao yote na makundi, na kutoka katika nchi, na kwenda kwenye nyika ambayo ilitenganisha nchi ya Nefi kutoka kwa nchi ya Zarahemla, na ilikuwa juu karibu na mpaka wa nchi.
15 Na ikawa kwamba Amoni aliwaambia: Tazama, mimi na ndugu zangu tutaenda mbele kwenye nchi ya Zarahemla, na mtabaki hapa mpaka tutakaporudi; na tutajaribu mioyo ya ndugu zetu, kama watakubali mje kwa nchi yao.
16 Na ikawa kwamba wakati Amoni alipokuwa anaenda mbele nchini, ndiyo yeye na ndugu zake walikutana na Alma, juu mahali ambapo palikuwa pame zungumzwa; na tazama, huu ulikuwa mkutano wa furaha.
17 Sasa shangwe ya Amoni ilikuwa nyingi sana hata ikajaa; ndiyo, alimezwa kwenye shangwe ya Mungu wake, hata akapungukiwa na nguvu; na akainama tena kwenye ardhi.
18 Sasa si hii ilikuwa shangwe kuu? Tazama, hii ni shangwe ambayo hakuna yeyote aipataye isipokuwa tu yule ambaye ametubu na anayetafuta furaha kwa unyenyekevu.
19 Sasa shangwe ya Alma kukutana na ndugu zake kwa kweli ilikuwa kubwa, na pia shangwe ya Haruni, ya Omneri, na Himni; lakini tazama shangwe yao haikuwa ya kushinda nguvu zao.
20 Na sasa ikawa kwamba Alma aliwaongoza ndugu zake kurudi kwa nchi ya Zarahemla; hata kwenye nyumba yake. Na walienda na kumwambia mwamuzi mkuu vitu vyote ambavyo vilitendeka kwao kwenye nchi ya Nefi, miongoni mwa ndugu zao, Walamani.
21 Na ikawa kwamba mwamuzi mkuu alituma tangazo nchini kote, akiuliza maoni ya watu kuhusu kukubaliwa kwa ndugu zao, ambao walikuwa watu wa Anti-Nefi-Lehi.
22 Na ikawa kwamba sauti ya watu ilirudi, ikisema: Tazama, tutaitoa nchi ya Yershoni, ambayo iko mashariki kando ya bahari, ambayo inaungana na nchi ya Neema, ambayo iko kusini mwa nchi ya Neema; na hii nchi ya Yershoni ndiyo nchi ambayo tutawapatia ndugu zetu kwa urithi.
23 Na tazama, tutaweka majeshi yetu katikati ya nchi ya Yershoni na nchi ya Nefi, ili tuwalinde ndugu zetu kwenye nchi ya Yershoni; na hivi tunafanya kwa ajili ya ndugu zetu, kwa sababu ya woga wao wa kuchukua silaha dhidi ya ndugu zao wakihofia kutenda dhambi; na huu woga wao mwingi uliwajia kwa kutubu sana, kwa sababu ya mauaji yao mengi na maovu yao ya kutisha.
24 Na sasa tazama, hivi ndivyo tutawafanyia ndugu zetu, ili warithi nchi ya Yershoni; na tutawakinga kutoka kwa maadui wao na majeshi yetu, kwa masharti kwamba watatoa sehemu ya mazao yao kutusaidia sisi ili tudumishe majeshi yetu.
25 Sasa, ikawa kwamba Amoni alipokuwa amesikia hivi, alirejea kwa watu wa Anti-Nefi-Lehi, na pia akiwa na Alma, kwenye nyika, ambapo walikuwa wamepiga hema zao, na kuwajulisha hivi vitu vyote. Na Alma pia aliwaambia juu ya uongofu wake, na Amoni na Haruni, na ndugu zake.
26 Na ikawa kwamba ilisababisha shangwe nyingi miongoni mwao. Na wakaelekea chini kwenye nchi ya Yershoni, na kumiliki nchi ya Yershoni; na wakaitwa na Wanefi watu wa Amoni; kwa hivyo walitambulika kwa hilo jina siku zote za baadaye.
27 Na walikuwa miongoni mwa watu wa Nefi, na pia wakahesabiwa miongoni mwa watu ambao walikuwa kwenye kanisa la Mungu. Na pia walitambulika kwa juhudi yao kwa Mungu, na pia kwa watu; kwani walikuwa wakamilifu na wa kuaminiwa na wa kusimama wima kwa vitu vyote; na walikuwa imara kwa imani yao ya Kristo, hadi mwisho.
28 Na waliangalia kumwaga damu ya ndugu zao ni machukizo makuu; na hawangeweza kushawishiwa kuchukua silaha dhidi ya ndugu zao; na hawakuona kifo kwa woga wowote, kwa matumaini na maoni yao nikatika Kristo na ufufuo; kwa hivyo, kifo kilimezwa kwao na ushindi wa Kristo juu yake.
29 Kwa hivyo, wangevumilia kifo kwa njia ya kukasirika na kuudhika ambayo ndugu zao waliwapasha, mbele ya kuchukua panga au kitara kuwaua.
30 Na hivyo walikuwa watu wa juhudi na wapendwa, watu ambao walipendwa sana na Bwana.