Maandiko Matakatifu
Alma 8


Mlango wa 8

Alma anahubiri na kubatiza katika Meleki—Anakataliwa katika Amoniha na kuondoka—Malaika anamwamuru arudi na kuhubiria watu toba—Anapokelewa na Amuleki, na wao wawili wanahubiri katika Amoniha. Karibia mwaka 82 K.K.

1 Na sasa ikawa kwamba Alma alirudi kutoka nchi ya Gideoni, baada ya kuwafundisha watu wa Gideoni vitu vingi ambavyo haviwezi kuandikwa, baada ya kuimarisha mpangilio wa kanisa, kulingana na vile alivyokuwa amefanya katika nchi ya Zarahemla, ndiyo, alirejea katika nyumba yake Zarahemla kujipumzisha kutokana na ile kazi aliyokuwa ametenda.

2 Na hivyo mwaka wa tisa wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi ulikwisha.

3 Na ikawa kwamba katika mwanzo wa mwaka wa kumi wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi, kwamba Alma aliondoka kutoka huko na kusafiri katika nchi ya Meleki, magharibi kando mwa mto Sidoni, magharibi kando mwa mipaka ya nyika.

4 Na akaanza kuwafundisha watu katika nchi ya Meleki kulingana na mpango mtakatifu wa Mungu, ambao alikuwa ameitwa kwake; na akaanza kufundisha watu kote katika nchi ya Meleki.

5 Na ikawa kwamba watu walimjia kutoka mipaka yote ya nchi ambayo ilikuwa kando ya nyika. Na wakabatizwa kote katika nchi;

6 Kwa hivyo baada ya kukamilisha kazi yake katika Meleki aliondoka huko, na akasafiri muda wa siku tatu kaskazini mwa nchi ya Meleki; na akafika katika mji ulioitwa Amoniha.

7 Sasa ilikuwa ni desturi ya watu wa Nefi kuita nchi zao, na miji yao, na vijiji vyao, ndiyo, na hata vijiji vyao vyote vidogo, kwa jina la yule ambaye aliimiliki kwanza; na ilikuwa hivyo katika nchi ya Amoniha.

8 Na ikawa kwamba baada ya Alma kuwasili katika mji wa Amoniha alianza kuwahubiria neno la Mungu.

9 Sasa Shetani alikuwa amekamata mioyo ya watu wa mji wa Amoniha; kwa hivyo hawakusikiliza maneno ya Alma.

10 Walakini Alma alitia bidii sana katika roho, akipambana na Mungu katika sala kuu, ili awateremshie watu waliokuwa katika mji Roho wake; kwamba akubali kwamba awabatize katika toba.

11 Walakini, walishupaza mioyo yao, na kumwaambia: Tazama, tunajua kwamba wewe ni Alma; na tunajua kwamba wewe ni kuhani mkuu wa kanisa ambalo wewe umeanzisha katika sehemu nyingi za nchi, kulingana na mila zako; na sisi sio washirika wa kanisa lako, na hatuamini mila za kishenzi kama hizo.

12 Na sasa tunajua kwamba kwa sababu sisi sio washirika wa kanisa lako tunajua kwamba huna mamlaka juu yetu; na wewe umemkabidhi Nefiha kiti cha hukumu; kwa hivyo wewe si mwamuzi mkuu juu yetu.

13 Sasa baada ya watu kunena haya, na kuyapinga maneno yake yote, na kumfanyia mzaha, na kumtemea mate, na kumsababisha kwamba atupwe nje ya mji wao, aliondoka hapo na akafunga safari yake akielekea mji ambao uliitwa Haruni.

14 Na ikawa kwamba alipokuwa akisafiri huko, na kuzidiwa sana na huzuni, na kupambana na mateso mengi na kusononeka sana katika nafsi, kwa sababu ya uovu wa watu ambao walikuwa katika mji wa Amoniha, ikawa kwamba wakati ambao Alma alikuwa amezidiwa na huzuni, tazama malaika wa Bwana alimtokea, na kusema:

15 Heri wewe, Alma; kwa hivyo, inua kichwa chako na ufurahi, kwani una sababu kubwa ya kufurahi; kwani umekuwa mwaminifu katika kutii amri za Mungu tangu ule wakati ambao ulipokea ujumbe wako mara ya kwanza kutoka kwake. Tazama, Mimi ndimi yule niliyewaletea.

16 Na tazama, nimetumwa kukuamuru kwamba urudi katika mji wa Amoniha, na uwahubirie tena watu wa mji huo; ndiyo, uwahubirie. Ndiyo, uwaambie, wasipotubu Bwana Mungu atawaangamiza.

17 Kwani tazama, wanapanga kwa wakati huu jinsi ya kuangamiza uhuru wa watu wako, (kwani hivyo ndivyo asemavyo Bwana) ambayo ni kinyume cha maagizo, na hukumu, na amri ambazo amewapatia watu wake.

18 Sasa ikawa kwamba baada ya Alma kupokea ujumbe wake kutoka kwa malaika wa Bwana alirudi kwa haraka katika nchi ya Amoniha. Na akaingia katika mji kwa njia nyingine, ndiyo, kwa njia iliyo kusini mwa mji wa Amoniha.

19 Na alipoingia mjini alikuwa na njaa, na akamwambia mtu fulani: Waweza kumpatia mtumishi mnyenyekevu wa Mungu kitu cha kula?

20 Na yule mtu akamwambia: Mimi ni Mnefi, na ninajua kwamba wewe ni nabii mtakatifu wa Mungu, kwani wewe ndiye yule mtu ambaye malaika alisema katika ono: Wewe utampokea. Kwa hivyo, njoo na mimi katika nyumba yangu na nitakupatia chakula changu; na ninajua kwamba wewe utakuwa baraka kwangu mimi na nyumba yangu.

21 Na ikawa kwamba yule mtu alimkaribisha katika nyumba yake; na yule mtu aliitwa Amuleki; na akaleta mkate na nyama na kumpakulia Alma.

22 Na ikawa kwamba Alma alikula mkate na kushiba; na akambariki Amuleki na nyumba yake, na akamshukuru Mungu.

23 Na baada ya kula na kushiba akamwambia Amuleki: Mimi ni Alma, na mimi ni kuhani mkuu wa kanisa la Mungu kote nchini.

24 Na tazama, nimeitwa kuhubiri neno la Mungu miongoni mwa watu hawa wote, kulingana na roho ya ufunuo na unabii; na nilikuwa katika nchi hii na hawakunipokea, lakini walinifukuza na karibu niiache nchi hii milele.

25 Lakini tazama, nimeamuriwa kwamba nirudi tena na niwatolee watu hawa unabii, ndiyo, na kuwashuhudia dhidi ya maovu yao.

26 Na sasa, Amuleki, kwa sababu umenilisha na kunipokea, umebarikiwa; kwani nilikuwa mwenye njaa, kwa kufunga siku nyingi.

27 Na Alma akaishi siku nyingi na Amuleki kabla ya kuanza kuwahubiria watu.

28 Na ikawa kwamba watu waliendelea kuwa wabaya zaidi katika uovu wao.

29 Na neno likamjia Alma, likisema: Nenda; na pia umwambie mtumishi wangu Amuleki, nenda mbele na uwatolee watu hawa unabii, uwaambie—Tubuni, kwani hivyo ndivyo asemavyo Bwana, msipotubu nitawatembelea watu hawa kwa ghadhabu yangu; ndiyo, na sitabadilisha ghadhabu yangu kali kutoka kwao.

30 Na Alma akaenda, pamoja na Amuleki, miongoni mwa watu, kuwatangazia neno la Mungu; na walijazwa na Roho Mtakatifu.

31 Na wakapewa uwezo, hata ikawa kwamba haingewezekana wao kufungwa katika magereza; wala mtu yeyote kuweza kuwaua; walakini hawakutumia uwezo wao hadi walipofungwa kwa kamba na kutupwa gerezani. Sasa, haya yalifanywa ili Bwana adhihirishe uwezo wake ndani yao.

32 Na ikawa kwamba walienda na wakaanza kuhubiria watu na kuwatolea unabii, kulingana na roho na uwezo ambao Bwana alikuwa amewapatia.