Maandiko Matakatifu
Mosia 28


Mlango wa 28

Wana wa Mosia wanaenda kuwahubiria Walamani—Akitumia yale mawe mawili ya mwonaji, Mosia anatafsiri mabamba ya Kiyaredi. Karibia mwaka 92 K.K.

1 Sasa ikawa kwamba baada ya wana wa Mosia kufanya vitu hivi vyote, walichukua kikundi kidogo na kurejea kwa baba yao, mfalme, na wakataka waruhusiwe, wao pamoja na wale ambao walikuwa wamewateua, kwamba waende hadi katika nchi ya Nefi ili wahubiri vitu vile ambavyo walikuwa wamesikia, na ili wawapatie ndugu zao, Walamani, neno la Mungu—

2 Ili pengine wawafahamishe kuhusu Bwana Mungu wao, na kuwasadikisha kuhusu maovu ya baba zao; na ili pengine waponye chuki yao kwa Wanefi, ili pia wawezeshwe kumsherehekea Bwana Mungu wao, ili wawe marafiki wao kwa wao, kwamba kusiwe na mabishano katika nchi yote ambayo Bwana Mungu wao alikuwa amewapatia.

3 Sasa walitamani kwamba wokovu utangaziwe kila kiumbe, kwani hawangevumilia kwamba nafsi ya mwanadamu yeyote iangamie; ndiyo, hata mafikira kwamba kuna nafsi yoyote itakayopata kuteswa kwa milele iliwafanya kutetemeka na kutikisika.

4 Na hivyo ndivyo Roho wa Bwana alivyowatendea, kwani wao ndiyo waliokuwa wenye dhambi mbaya mno. Na Bwana katika rehema yake aliona kwamba inafaa awaachilie; walakini waliteseka sana katika nafsi zao kwa sababu ya maovu yao, wakiteseka sana na kuogopa kwamba watatengwa milele.

5 Na ikawa kwamba walimsihi baba yao kwa siku nyingi ili waende katika nchi ya Nefi.

6 Na mfalme Mosia akaenda kumwuliza Bwana ili ajue kama atawaruhusu wanawe waende kuhubiria neno miongoni mwa Walamani.

7 Na Bwana akamwaambia Mosia: Waruhusu waende, kwani wengi wataamini maneno yao, na watapokea uzima wa milele; na nitawakomboa wana wako kutoka mikono ya Walamani.

8 Na ikawa kwamba Mosia aliwaruhusu waende na kutenda kulingana na haja yao.

9 Na wakasafiri nyikani ili wahubiri neno miongoni mwa Walamani; na nitatoa historia ya matendo yao hapo baadaye.

10 Sasa mfalme Mosia hakuwa na yeyote wa kumkabidhi ufalme wake, kwani hakukuwa na yeyote miongoni mwa wanawe aliyekubali ufalme.

11 Kwa hivyo alichukua kumbukumbu ambazo zilikuwa zimechorwa katika mabamba ya shaba nyeupe, na pia mabamba ya Nefi, na vitu vyote alivyokuwa ameweka na kuhifadhi kulingana na amri za Mungu, baada ya kutafsiri na kusababisha kuandikwa kumbukumbu ambazo zilikuwa kwenye mabamba ya dhahabu ambayo yalikuwa yamegunduliwa na watu wa Limhi, na ambayo alipewa kwa mkono wa Limhi;

12 Na alifanya hivi kwa sababu ya wasiwasi mkuu wa watu wake; kwani walitamani sana kujua kuhusu wale watu ambao walikuwa wameangamizwa.

13 Na sasa alizitafsiri kwa kuyatumia yale mawe mawili ambayo yalikuwa yamefungiliwa katika ile mizingo miwili ya pinde.

14 Sasa hivi vilikuwa vimetayarishwa tangu mwanzo, na vilipitishwa kutoka kizazi hadi kizazi, kwa lengo la kutafsiri lugha;

15 Na vimewekwa na kuhifadhiwa kwa mkono wa Bwana, ili afichulie kila kiumbe ambacho kitamiliki nchi maovu na machukizo ya watu wake;

16 Na yeyote aliye na vitu hivi anaitwa mwonaji, kama zile nyakati za kale.

17 Sasa baada ya Mosia kumaliza kutafsiri maandishi haya, tazama, yalieleza historia ya watu ambao waliangamizwa, kutoka ule wakati walioangamizwa hadi ule wakati ule mnara mkuu uliojengwa, ule wakati ambao Bwana alichanganya lugha ya watu na wakatawanywa kote usoni mwa ulimwengu, ndiyo, na hata kutoka wakati huo kurudi nyuma hadi uumbaji wa Adamu.

18 Sasa historia hii iliwafanya watu wa Mosia kuomboleza sana, ndiyo, walijazwa na hofu; walakini iliwapa ufahamu mwingi, ambao uliwafurahisha.

19 Na historia hii itaandikwa hapo baadaye; kwani tazama, ni muhimu watu wote kujua vitu ambavyo vimeandikwa katika historia hii.

20 Na sasa, kama vile nilivyowaambia, kwamba baada ya mfalme Mosia kutenda vitu hivi, alichukua yale mabamba ya shaba nyeupe, na vitu vyote ambavyo alikuwa ameweka, na kumkabidhi Alma, ambaye alikuwa ni mwana wa Alma; ndiyo, maandishi yote, na pia vitafsiri, na kumpatia yeye, na akamwamuru kwamba aviweke na avihifadhi, na pia aweke maandishi ya wale watu, na kuvipitisha kutoka kizazi hadi kizazi, hata kama vile vilikuwa vimepitishwa tangu ule wakati Lehi alipoondoka Yerusalemu.