Sehemu ya 89
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Kirtland, Ohio, 27Â Februari 1833. Kama matokeo ya viongozi wa awali kutumia tumbaku katika mikutano yao, Nabii aliongozwa kutafakari juu ya jambo hili; matokeo yake, alimwuliza Bwana kuhusiana na jambo hilo. Ufunuo huu, unaojulikana kama Neno la Hekima, ulikuwa ndiyo jibu.
1–9, Matumizi ya mvinyo, vinywaji vikali, tumbaku, na vinywaji vya moto vinakatazwa; 10–17, Majani, matunda, nyama, na nafaka vimewekwa kwa matumizi ya wanadamu na ya wanyama; 18–21, Utii kwa sheria ya injili, pamoja na Neno la Hekima, huleta baraka za kimwili na kiroho.
1 Neno la Hekima, kwa manufaa ya baraza la makuhani wakuu, waliokusanyika Kirtland, na kanisa, na pia watakatifu katika Sayuni—
2 Kwa kutuma salamu; siyo kwa amri au kwa lazima, ila kwa ufunuo na neno la hekima, ambalo huonyesha mpango na mapenzi ya Mungu katika wokovu wa kimwili wa watakatifu wote katika siku za mwisho—
3 Limetolewa kwa kanuni yenye ahadi, na kuchukuliwa kwa kiwango cha wadhaifu na wadhaifu zaidi ya watakatifu wote, ambao ni au wanaweza kuitwa watakatifu.
4 Tazama, amini, hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwenu: Kwa sababu ya uovu na njama ambazo zipo na zitaendelea kuwepo katika mioyo ya watu wenye kula njama katika siku za mwisho, nimewaonya, na ninawaonya mapema, kwa kuwapa ninyi hili neno la hekima kwa ufunuo—
5 Kwamba ikiwa mtu yeyote anakunywa divai au kinywaji kikali miongoni mwenu, tazama hivyo siyo vyema, wala haifai machoni pa Baba yenu, isipokuwa tu katika kukusanyika kwenu pamoja kutoa sakramenti mbele zake.
6 Na, tazama, hii yapasa kuwa divai, ndiyo, divai halisi ya tunda la mizabibu, mliyotengeneza ninyi wenyewe.
7 Na, tena, vinywaji vikali siyo kwa ajili ya tumbo, ila kwa kuosha miili yenu.
8 Na tena, tumbaku siyo kwa ajili ya mwili, wala kwa tumbo, na siyo nzuri kwa mwanadamu, bali ni dawa kwa ajili ya majeraha na ngʼombe wote wagonjwa, itumiwe kwa kipimo na ujuzi.
9 Na tena, vinywaji vya moto siyo kwa ajili ya mwili au tumbo.
10 Na tena, amini ninawaambia, majani yote ya mimea Mungu ameiweka kwa ajili ya maumbile, sura, na kwa matumizi ya mwanadamu—
11 Kila mmea katika majira yake, na kila tunda katika majira yake; vyote hivi vitumiwe kwa busara na kwa shukrani.
12 Ndiyo, pia nyama ya wanyama na ya ndege wa angani, Mimi, Bwana, nimeviweka kwa matumizi ya wanadamu kwa shukrani; hata hivyo vitumike kwa uangalifu;
13 Na yapendeza kwangu ikiwa havitatumiwa, isipokuwa tu nyakati za baridi, au katika baridi, au njaa.
14 Nafaka zote zimewekwa kwa ajili ya matumizi ya mwanadamu na wanyama, kuwa chakula cha kutegemewa, siyo tu kwa mwanadamu bali hata kwa wanyama wa mashambani, na ndege wa angani, na wanyama wote wa porini wale watembeao au watambaao juu ya dunia;
15 Na hivi Mungu amevitengeneza kwa matumizi ya mwanadamu tu katika nyakati za ukame na njaa kali.
16 Nafaka zote ni nzuri kwa chakula cha mwanadamu; pia kama vile uzao wa mizabibu; ule utoao matunda, iwe katika ardhi au juu ya ardhi—
17 Hata hivyo, ngano kwa mwanadamu, na mahindi kwa ngʼombe, na mtama kwa farasi, na uwele kwa ndege na kwa nguruwe, na kwa wanyama wote wa mashamba, na shayiri ni kwa wanyama wote watumikao, na kwa vinywaji laini, kama vile nafaka nyinginezo.
18 Na watakatifu wote ambao wanakumbuka kushika na kutenda maneno haya, wakitembea katika utii kwa amri hizi, watapata afya mwilini mwao na mafuta mifupani mwao;
19 Na watapata hekima na hazina kubwa ya maarifa, hata hazina zilizofichika;
20 Na watakimbia na wasichoke, na watatembea wala hawatazimia.
21 Na Mimi, Bwana, ninatoa ahadi kwao, kwamba malaika mwangamizaji atawapita, kama wana wa Israeli, na hatawaua. Amina.