“Moto wa Kutakasa wa Mateso,” Liahona, Machi./Aprili 2022
Moto wa kutakasa wa Mateso
Ninaomba kwamba kila mmoja wetu atasogea karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Mwokozi kupitia dhiki zetu binafsi.
Dhiki katika maisha haipaswi kutushangaza. Iwe inatokana na dhambi zetu wenyewe na makosa au kitu kingine, dhiki ni ukweli wa maisha katika mwili wenye kufa. Watu wengine wanafikiria wanapaswa kuepukwa na dhiki yoyote ikiwa watashika amri za Mungu, lakini ni “katika kalibu ya masumbuko”(Isaya 48:10; 1 Nefi 20:10) ndimo tunachaguliwa. Hata Mwokozi hakuepushwa:
“Na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata;
“Naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii” (Waebrania 5:8–9).
Kwa wale miongoni mwetu ambao tunawajibika, ugumu mara nyingi ni jambo muhimu sana la hatimaye “kufanywa wakamilifu.” Ni kitu kinachofanya maisha kuwa zaidi ya jaribio rahisi lenye chaguzi nyingi. Mungu havutiwi tu na kile tunachofanya au tusichofanya bali katika kile sisi tunachokuwa. 1 Ikiwa tuko radhi, Yeye atatufundisha kutenda kama Yeye anavyotenda badala ya kutendewa tu na nguvu nyingine (ona 2 Nefi 2:14–16). Lazima tujifunze kuwa waadilifu katika hali zote au, kama Rais Brigham Young (1801–77) alivyosema, hata “gizani.” 2
Ninaamini kuwa changamoto ya kushinda na kukua kutokana na dhiki ilitupendeza wakati Mungu alipowasilisha mpango Wake wa ukombozi katika ulimwengu ule wa kabla ya kuzaliwa. Tunapaswa kuikabili changamoto hiyo sasa tukijua kwamba Baba yetu wa Mbinguni atatutegemeza. Lakini ni muhimu sana tumgeukie Yeye. Bila Mungu, uzoefu wa kiza wa mateso na dhiki utajaribu kutuvunja moyo, kutukatisha tamaa na hata kuleta huzuni.
Kwa msaada wa kiungu, hatimaye faraja inachukua nafasi ya maumivu, amani inachukua nafasi ya msukosuko, na tumaini huchukua nafasi ya huzuni. Mungu atabadili jaribu kuwa baraka na, kwa maneno ya Isaya, “atatoa … taji ya maua badala ya majivu” (Isaya 61:3). Ahadi yake sio kutuepusha na migogoro bali kutuhifadhi na kutufariji katika shida zetu na kuziweka wakfu kwa faida yetu (ona 2 Nefi 2:2; 4:19–26; Yakobo 3:1).
Wakati Baba yetu wa Mbinguni hatalazimisha msaada na baraka Zake juu yetu, Atatenda kupitia rehema na neema ya Mwanaye Mpendwa na nguvu ya Roho Mtakatifu ili kututegemeza pale tunapomtafuta. Tunapata mifano mingi ya msaada huo ikituzunguka na katika kumbukumbu za maandiko.
Mifano ya Agano la Kale
Katika Agano la Kale tunamwona Ibrahimu mtiifu kwa subira akisubiri kwa miaka mingi kwa ajili ya ahadi za Mungu kwake za—nchi ya urithi na uzao wa haki—zitimizwe. Kupitia njaa, vitisho kwa maisha yake, huzuni, na majaribu, Ibrahimu aliendelea kumtumaini na kumtumikia Mungu na alilipwa kwa kutegemezwa na Yeye. Sasa tunamheshimu Ibrahimu kama “baba wa waaminifu.” 3
Mjukuu wa Ibrahimu, Yakobo alikimbia kutoka nyumbani, akiwa peke yake na inaonekana wazi akiwa na vitu vichache zaidi ya nguo zake, ili kutoroka vitisho vya kuuawa vya kaka yake, Esau. Kwa miaka 20 iliyofuata, Yakobo alimtumikia mjomba wake, Labani. Japokuwa Labani alimpa Yakobo makazi salama na hatimaye binti zake wawili katika ndoa, alimfanyia kwa unafiki mkubwa, akibadilisha malipo yake na makubaliano yao mara nyingi kila wakati Yakobo alipoonekana kuwa mbele (ona Mwanzo 31:41).
Hatimaye walipoenda njia tofauti, Yakobo alimlalamikia mkwewe, “Kama Mungu wa baba yangu … hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu” (Mwanzo 31:42). Badala yake, Mungu akiwa pamoja naye, Yakobo alirudi nyumbani akiwa amebadilishwa kutoka mkimbizi asiye na pesa kuwa mume na baba wa familia kubwa. Alikuwa na idadi kubwa ya watumishi na alibarikiwa sana kwa utajiri wa wakati huo—kondoo, ng’ombe, na ngamia (ona Mwanzo 32).
Yusufu mwana wa Yakobo ni mfano wa kutumiwa wa mtu ambaye alishinda dhiki kila mara kwa kumtumaini Mungu wakati wengine wangehisi wameachwa na Yeye. Kwanza, aliuzwa utumwani na ndugu zake. Halafu, alipoinuka katika wadhifa na heshima katika nyumba ya bwana wake wa Misri, Potifa, Yusufu alishtakiwa kwa uwongo na mke wa Potifa na kufungwa jela licha ya kuwa alikuwa ameikimbia dhambi. Walakini, Yusufu aliendelea kumtumaini Mungu. Hata gerezani alistawishwa lakini alisahaulika na wale aliowasaidia licha ya ahadi zao. (Ona Mwanzo 37; 39–41.) Mwishowe, kama tunavyojua, Yusufu alizawadiwa ofisi ya juu na kuwa njia ya kuokoa familia ya baba yake (na Misri yote) wakati wa baa la njaa.
Kuvumilia kwa subira
Mifano hii na mingine inatuonyesha kuwa dhiki kwa kawaida hushindwa baada ya muda fulani. Kuna haja ya kuvumilia na kustahimili. Bado, Baba yetu wa Mbinguni hutuangalia na kutusaidia katika kipindi chote cha uvumilivu huo—Yeye hasubiri hadi mwisho.
Mzee Neal A. Maxwell (1926–2004) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili aliwahi kusema: “Kwa yenyewe, kwa kweli, kupita kwa muda hakuleti maendeleo ya moja kwa moja. Walakini, kama mwana mpotevu, mara nyingi tunahitaji ‘mchakato wa muda’ ili tuweze kurejea kwenye fahamu zetu za kiroho. (Luka 15:17.) Kukutana tena kunakogusa kwa Yakobo na Esau jangwani, miaka mingi baada ya uadui wa undugu wao, ni mfano mzuri. Ukarimu unaweza kuchukua nafasi ya uhasama. Tafakuri inaweza kuleta utambuzi. Lakini tafakuri na utafutaji huhitaji muda. Matokeo mengi sana ya kiroho yanahitaji kweli okozi zilizochanganywa na muda, kutengeneza suluhisho la uzoefu, ambalo ni dawa bora kwa vitu vingi.” 4
Mzee M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alisema:
“Kumngojea Bwana hakumaanishi kuungojea wakati mzuri. Haupaswi kamwe kuhisi kama uko katika chumba cha kusubiri.
“Kumngojea Bwana kuna maanisha hatua ya tendo. Nimejifunza kwa miaka kadhaa kwamba tumaini letu katika Kristo huongezeka tunapowatumikia wengine. …
“Ukuaji binafsi ambao mtu anaweza kuufikia sasa wakati anapomngojea Bwana na ahadi zake ni jambo la maana sana, takatifu, la mpango Wake kwa kila mmoja wetu.” 5
Kuvumilia kwa subira ni aina ya kumgeukia na kumtumaini Mungu. Katika mistari iliyotangulia ushauri wake wa kumwuliza Mungu ikiwa tunakosa hekima, Yakobo anasema hivi juu ya uvumilivu:
“Hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali;
“Mkifahamu ya kwamba kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.
“Saburi na iwe na kazi kamilifu, mpate kuwa wakamilifu na watimilifu bila [kupungukiwa] na neno.” (Tafsiri ya Joseph Smith, Yakobo 1:2 [katika Yakobo 1:2, tanbihi a]; Yakobo 1:3–4).
Kutakaswa kwa Mateso
Tunapokuwa na msaada wa Baba yetu wa Mbinguni, dhiki zetu na mateso yetu vitatutakasa badala ya kutushinda (ona Mafundisho na Maagano 121:7–8). Tutaibuka viumbe wenye furaha na walio watakatifu zaidi. Katika ufunuo kwa Rais wa wakati huo wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, Thomas B. Marsh, Bwana alisema hivi juu ya Mitume Wake: “Na baada ya majaribu yao, na dhiki nyingi, tazama, mimi, Bwana, nitawatafuta , na ikiwa hawataishupaza mioyo yao, na kuzikaza shingo zao dhidi yangu, wataongolewa, nami nitawaponya ” (Mafundisho na Maagano 112:13).
Tungeweza kusema kwamba katika dhiki tunapata kumjua “Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo, ambaye [Amemtuma]”(Yohana 17:3). Katika dhiki, tunatembea na Wao siku hadi siku. Tukiwa tumenyenyekezwa, tunajifunza kuwategemea Wao “katika kila wazo” (Mafundisho na Maagano 6:36). Wao watatuhudumia sisi katika mchakato wa kuzaliwa upya kiroho. Ninaamini hakuna njia nyingine.
Ninaomba kwamba kila mmoja wetu atasogea karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Mwokozi kupitia dhiki zetu binafsi. Wakati huo huo, na tujifunze kuwahudumia wengine katika dhiki zao kulingana na mpangilio wa Mungu. Ilikuwa kupitia “maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina” kwamba Mwokozi alikuja kujua “jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:11–12). Kwetu sisi, “wakati, kwa wakati huu, sisi wenyewe hatujatundikwa juu ya msalaba wowote, tunapaswa kuwa chini ya miguu ya mtu mwingine—tukiwa tumejaa huruma na kutoa zawadi ya viburudisho vya kiroho” 6