“Je, Wewe Unamtafuta Kristo Kila Siku?,” Liahona, Machi./Aprili 2022
Vijana Wakubwa
Je, Wewe Unamtafuta Kristo Kila Siku?
Uzoefu wangu katika hekalu ulinisaidia kutambua kwamba ninahitaji kutafuta kumpata Kristo kila siku.
Mwandishi anaishi Guatemala.
Nilipokuwa mdogo, nilikuwa nikijiuliza maswali kama “Je! Roho Mtakatifu anazungumza?” “Nitakapokwenda mbinguni, je, nitamwona Mungu?”
Sasa kwa kuwa nimekua kidogo, ninaweza kutazama nyuma na kuona kwamba Baba wa Mbinguni daima alikuwa akiniongoza na kunionyesha ushahidi kwamba Yeye alikuwepo, lakini sikuwa daima nikiweza kuutambua mkono Wake maishani mwangu. Nilibarikiwa kulelewa katika nyumba yenye injili ya Yesu Kristo iliyorejeshwa, lakini niliishi kwa ushuhuda wa watu wengine kwa muda mrefu. Ilikuwa ngumu kwangu kuamini kwamba hakika Mungu alikuwepo.
Siku moja, wakati nilipokuwa na miaka 15, askofu wangu alitangaza safari ya kata kwenda hekaluni. Nilikuwa tayari nimezoea kwenda hekaluni na familia yangu, kwa hivyo sikufikiria hili lilikuwa jambo kubwa. Sikuwahi kuwa na hisia nzuri sana hata hivyo na sikuelewa umuhimu wa maagano na ibada zilizofanywa hekaluni.
Siku ilipofika, niliingia hekaluni na kubadilisha mavazi yangu na kuvaa mavazi yangu meupe. Nilipokuwa nikikipita kioo, niliona taswira yangu nikiwa nimevaa nguo nyeupe na nikiwa na tabasamu usoni. Wakati nikiwasubiri waumini wengine wa kata yangu, nilikuwa kwenye mshangao. Nilikuwa nikitafakari uzuri wa kisima cha ubatizo na michoro wakati ghafla, nilipohisi Roho akigusa moyo wangu kwa upole.
Sitasahau kamwe maneno yaliyokuja akilini mwangu: “Orson, hii ni nyumba ya Bwana. Yeye anakupenda. Anataka ubadilishe maisha yako na ujitahidi kuwa mtu bora kidogo kidogo.”
Nilihisi upendo mwingi katika maneno hayo lakini ghafla nilizidiwa na hatia. Sikuwa nimelichukulia hekalu kwa uzito unaostahili hadi wakati huu. Kwa hivyo nilisema sala moyoni mwangu, nikimwomba Baba wa Mbinguni anisamehe.
Na nilijua Yeye amesikia sala yangu kwa sababu nilihisi amani sana moyoni mwangu.
Siku hiyo, niliimarisha imani yangu na kupokea ushuhuda halisi wa injili ambao niliusubiri kwa hamu. Siku hiyo, niliweza kusema kwa uthabiti kama wale wanafunzi wawili wa Yohana: “Nimemwona Masihi” (ona Yohana 1:41).
Njia Rahisi za Kuunganika
Tangu tukio hili, nimejitahidi kutambua vyema ushawishi wa Baba wa Mbinguni katika maisha yangu kwa kumtafuta Yesu Kristo kila siku. Ingawa ulimwengu unaweza kufanya iwe ngumu kuisikia sauti ya Mwokozi wakati mwingine, ninajua sasa kwamba Yeye ni halisi na kwamba Yuko pamoja nami.
Wengi wetu tuna siku ambazo tunahisi kuwa karibu zaidi na mbingu kuliko kawaida. Tunazo pia siku ngumu wakati tunapohangaika kuhisi ushawishi Wake licha ya kujaribu kwa juhudi zote au siku zenye shughuli nyingi ambapo hatuwezi kupata muda wa kutosha kumtafuta Yeye. Lakini ninajua kwamba ikiwa tuna hamu ya dhati ya kumtafuta, tutauona mkono Wake katika maisha yetu.
Wakati unapohisi umetengenishwa na Mwokozi, jiulize, Je, mimi ninajitahidi kumpata Masihi kila siku?
Tunapotafuta kuwa kama Mitume wa zamani, tukiacha nyavu zetu (ona Mathayo 4:20) na majukumu mengine na masilahi kwa muda mfupi ili kumgeukia Yeye, tutampata.
Kuna vyanzo vyenye nguvu za kiroho ambavyo vinaweza kutusaidia. Nabii Alma alitukumbusha “kwamba kupitia kwa vitu vilivyo vidogo na rahisi vitu vikubwa hutendeka” (Alma 37:6). Matendo madogo madogo ya imani na mazoea ya kiroho tunayofanya kila siku yanaweza kutusaidia kuongeza uwezo wetu wa kumtambua Bwana katika maisha yetu.
Baadhi ya zana hizi za kiroho zinaweza kuwa vitu kama:
-
Kuomba kwa Imani.
-
Kujifunza maandiko kwa kukusudia na kwa kumaanisha
-
Kuwahudumia wengine bila ubinafsi
-
Kushiriki ushuhuda wako kwa rafiki
-
Kusikiliza nyimbo za kanisa au muziki wa kiroho
-
Kuhudhuria maadarasa ya kanisa ya chuo
-
Kuitakasa siku ya Sabato
-
Kufunga
-
Kuhudhuria hekaluni mara kwa mara
Vitu vingi vinaweza kutusaidia kumpata Yesu Kristo, lakini muhimu ni kuendelea kumtafuta. Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Tunapotafuta kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, jitihada zetu za kumsikiliza Yeye zinatakiwa ziwe za dhati zaidi. Inachukua juhudi za hiari na za dhati kujaza maisha yetu ya kila siku kwa maneno Yake, mafundisho Yake na kweli Zake.” 1
Je, Wewe Umemwona Yeye Leo?
Hata ikiwa hupokei majibu yote unayotafuta kwa sasa, endelea! Mtafute tu Kristo na uchague kumwamini Yeye. Ikiwa utajaribu kumtafuta kila siku kupitia matendo madogo madogo, ninajua kuwa utakuja kuhisi kumbatio Lake kutoka mbinguni. Ninajua hii ni kweli kwa sababu nimewahi kulihisi hilo.
Baba wa Mbinguni anatambua juhudi zetu. Hajali sana juu ya ukubwa wa vitu tunavyofanya ili kujenga roho zetu ikiwa tunaweza kusema kila siku kwa uimara na uhakika: “Leo nimemwona Masihi!”
Ni maombi yangu kwamba tuweze kumjua na kumpenda Mwokozi wetu kila siku. Kwamba tutafanya kama Moroni alivyopendekeza na “kumtafuta huyu Yesu” (Etheri 12:41). Acha mimi na wewe tumwone, mwisho wa kila siku, yule ambaye Musa na manabii wengine waliandika juu yake: Yesu wa Nazareti. Katika kumtafuta Kristo, tutauona mkono wa Mungu katika maisha yetu. Na kadiri tunavyomtafuta Kristo kila siku, ndivyo tutakavyomwona zaidi na kuweza kuitambua sauti Yake, ikituongoza na kutuelekeza katika maisha yetu yote.