2022
Unyenyekevu ni nini, Hasa?
Machi 2022


“Unyenyekevu ni nini, Hasa?,” Liahona, Machi./Aprili 2022

Unyenyekevu, ni Nini Hasa?

Tunapopanua uelewa wetu juu ya unyenyekevu, tunakuza uwezo wetu wa kuwa wanyenyekevu hata katika hali zisizotarajiwa.

mtu aliyevaa hedifoni

Kwa sababu ya matukio ya kipekee ambayo nimeyapitia, nimekuwa nikifikiria juu ya maana ya unyenyekevu. Hivi ndivyo Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, anavyoufafanua:

“Kuabudu mara nyingi hujumuisha vitendo, lakini kuabudu kwa kweli daima huhusisha tabia fulani ya akili.

“Tabia ya kuabudu huamsha hisia za ndani kabisa za utii, kusujudu na heshima. Kuabudu hujumuisha upendo na unyenyekevu katika hali ya ibada ambayo huzileta roho zetu karibu na Mungu.” 1

Kipi kinakuja akilini unapofikiria juu ya unyenyekevu? Je, Matukio yafuatayo yangezingatiwa kuwa ya unyenyekevu au yasiyo ya unyenyekevu katika mkutano wa sakramenti?

  1. Mtoto anachora kwenye kitabu chake cha kuchorea.

  2. Kijana anapitisha sakramenti akiwa amevaa hedifoni.

  3. Mtu anaruka na kupunga mikono yake kwa fujo.

  4. Msichana anacheza mchezo kwenye simu yake.

  5. Mmisionari anapiga kelele bila mpangilio.

  6. Mwanamke anaketi kwenye korido siku zote, kamwe haingii kanisani.

  7. Mwanamume amelala kwenye godoro kwenye njia ya kuingia kanisani.

  8. Kikundi cha waumini wakifanya ishara na kelele nyingi.

  9. Kijana wa kike ameketi chini ya kiti chake.

  10. Mwanamke akitembeatembea nyuma ya kanisa.

Wengi wetu tutakubali kwamba mmisionari anayepiga kelele katika mkutano wa sakramenti ni mtovu wa unyenyekevu kuliko watoto wanaochora picha ili kuwa na jambo la kufanya. Lakini acha tuchukue muda kupitia upya mawazo yetu juu ya unyenyekevu kwa kutembea kupitia mipangilio hii 10 ya matukio ya kweli—ambayo mimi binafsi nimeyaona katika mikutano ya Kanisa.

  1. Mtoto akichora kanisani. Mazoea haya ni ya kawaida na yanakubaliwa kwa urahisi na karibu waumini wote. Tunajua kwamba hili kwa kawaida sio kukosa unyenyekevu isipokuwa tujiruhusu wenyewe lituondolee umakini.

  2. Mtu anapitisha sakramenti wakati akisikiliza muziki kwenye hedifoni. Hii itakuwa siyo sahihi katika hali nyingi. Lakini niruhusu nishiriki “sehemu iliyobakia ya hadithi.” Nilimjua mtu ambaye alikuwa na ushuhuda wenye nguvu na ametumikia misheni na alikubali miito anuwai. Katika miaka ya hivi karibuni, hata hivyo, aligundulika kuwa na shida ya mawazo kuchanganyikana na msimamo wake. Kuvaa hedifoni kunamruhusu asikie muziki laini, wenye amani na husaidia kuzuia sauti za kila wakati akilini mwake. Anaweza kumhisi Roho na kuwatumikia wengine kwa unyenyekevu kwa msaada wa hedifoni zake.

  3. Kijana anayeruka na kupunga mikono yake hovyo. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Kaka huyu mwenye ulemavu anafurahi kila wakati anapomwona askofu akiwa ameketi mbele. Anaelezea shauku yake kwa kupunga mikono yake na kuruka.

    Children attend primary. One has a service dog and another is in a wheelchair.
  4. Msichana akicheza mchezo kwenye simu yake. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Dada huyu anapambana na wasiwasi wake wa kijamii kwa kucheza kimya kimya kwenye simu yake. Kwa kweli, ana uwezo mzuri wa kusikiliza kwa unyenyekevu na kupokea ujumbe wa mzungumzaji kwa sababu wasiwasi wake umeelekezwa mahali pengine.

  5. Mmisionari anapiga kelele bila mpangilio. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Wakati nilipokuwa katika kituo cha mafunzo ya umisionari, mmisionari katika kanda yangu alikuwa na tatizo kwenye mfumo wa neva. Mara kwa mara, angepiga kelele darasani, kwenye chumba cha chakula, na kwenye mikutano ya Kanisa. Kelele yake haikuonekana kukosa unyenyekevu; tuliona haraka kuwa alikuwa tayari kuhudumu, akiwa na ari ya kushiriki injili, na aliyejawa na Roho.

  6. Mwanamke anaketi kwenye korido siku zote, kamwe haingii kanisani. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Wakati nilipokuwa nikifanya kazi ya Kanisa huko Jijini Salt Lake, dada mmoja aliiandikia ofisi yetu ya huduma kwa watu wenye ulemavu kuhusu uzoefu wake juu ya maradhi ya msongo wa mawazo kwa sababu ya utumishi wake jeshini. Kwa sababu mwito wa simu ya mkononi au kelele nyingine ya ghafla inaweza kuchochea kumbukumbu za nyuma, kamwe hakuwahi kukaa ndani ya kanisa ili asije akamuumiza mtu yeyote bila kukusudia.

  7. Mwanamume amelala kwenye godoro kwenye njia. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Wakati nilipohamia kwenye kata mpya, nilishangaa kumwona kaka kwenye kitanda cha hospitali chenye magurudumu ndani ya kanisa. Mtu huyu alikuwa mwenye ulemavu mwingi na aliweza kuhudhuria kanisani kwa njia hii tu. Niligundua haraka hii ilikuwa kawaida kwa kata hii, na nikazoea hilo haraka. Kuwepo kwake pale haikuwa kukosa unyenyekevu bali, kwa kweli, ilikuwa kinyume kabisa. Hata hivyo, je, Mwokozi hakumponya mtu ambaye alikuwa ameshushwa kitandani na rafiki zake ndani ya nyumba iliyojaa watu? (ona Luka 5:18–20).

  8. Kikundi cha waumini wakipiga kelele nyingi na ishara nyingi. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Mikutano ya Viziwi inaweza kuwa “yenye kelele” kwa wahudhuriaji wanaosikia. Kwa jamii ya viziwi, si kukosa unyenyekevu kwa mtu kupiga kelele, kucheka, au kukohoa kwa sauti kubwa, lakini inachukuliwa kuwa si unyenyekevu kwa washiriki kujihusisha na vitu vya kidunia wakati wa mkutano wa sakramenti.

  9. Kijana wa kike ameketi chini ya viti. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Nilipokuwa kijana, mmoja wa wasichana wa rika langu kila wakati alikuwa akikaa chini ya kiti chake darasani. Dada huyu kijana alikuwa amekulia katika nyumba nyingi za malezi na alihisi salama tu katika eneo lililofungwa. Tangu wakati huo, nimetambua kuwa hatuwezi kutarajia kwamba wanafunzi watajifunza wanapokuwa katika hali ya kupigana, kuruka, au ya kutulia. Wanafunzi lazima wahisi salama ikiwa wanatakiwa kujifunza na, muhimu zaidi, wahisi upendo wa Mwokozi.

  10. Mwanamke anayetembea huku na huko kwenye ukumbi. Sehemu iliyobakia ya hadithi: Hii, kwa kweli, ni mimi. Nimepambana na wasiwasi kwa zaidi ya muongo mmoja, nikipitia hali ya wasiwasi mkali na maswala mengine ya kiafya. Katika nyakati hizi, njia pekee ninayoweza kuhudhuria kanisani ni ikiwa tu ninaweza kutembea tembea. Kutembea tembea au kucheza na kijiti cha kujifurahisha mikononi mwangu wakati mwingine ndiyo njia pekee ambayo ninaweza kuwa makini kwa wazungumzaji na kumhisi Roho. 

Shetani hutumia ukweli kwamba hatujui kila wakati hadithi iliyobakia, kwamba hatujui kila wakati ni changamoto gani kaka na dada zetu wanakabiliana nazo kila siku. Anataka tusahau kwamba waumini wengi wanafanya bidii yao ya juu kabisa, licha ya vile inavyoweza kuonekana kwa wengine. Matukio niliyoorodhesha hapo juu yanaweza kuwa nadra, lakini yanawakilisha mapambano mengi binafsi ambayo waumini wenzetu wanayapitia katika mahudhurio yao ya kanisani.

Ninaamini Shetani angependa tuamini kwamba ibada yetu imezuiliwa kwa mahangaiko, utofauti au udhaifu wa wengine. Kwa kweli, nimegundua kuwa ni katika nyakati hizi hasa za kuonekana kuwa usumbufu ndio nimefundishwa zaidi juu ya upendo wa Mwokozi wangu.

Yale Niliyojifunza juu ya Unyenyekevu

mwanamke akitumia lugha ya alama

1. Unyenyekevu ni uchaguzi na ujuzi.

Ni juu yangu mimi kuhisi unyenyekevu. Mara nyingi sihisi unyenyekevu kwa sababu ninaruhusu upotevu wa umakini. Ninapojenga nidhamu yangu ya kiroho na kuifundisha roho yangu kuzingatia kile kilicho muhimu zaidi, nina uwezo bora wa kuchukua jukumu kamili kwa uhusiano wangu na Baba yangu wa Mbinguni.

2. Unyenyekevu haufanani kwa wote.

Rafiki wa familia ambaye alikuwa gerezani kwa miaka 17 alimkaribisha Roho ndani ya chumba chake kwa kujenga mifano tata ya mahekalu kwa kutumia karatasi. Unyenyekevu unaweza kuwepo katika hali yoyote ikiwa tunamkaribisha Roho.

3. Unyenyekevu unaweza kuhimizwa lakini ni uchaguzi wa mtu binafsi.

Unyenyekevu huja kupitia msimamo wa ndani wa kukuza “tabia ya kuabudu.” Unaweza kuwapo pale tu kwa dhati tunapohisi na kuonyesha upendo wetu kwa Bwana na kwa waumini wengine. Baba yangu aliwahi kuniambia kwamba tunapokubali uwajibikaji kwa unyenyekevu wetu, mtazamo wetu hubadilika kutoka “Unaharibu kuabudu kwangu hapa!” kuwa “Uko sawa. Unakaribishwa hapa. Hauharibu unyenyekevu wangu kwa sababu ninachagua kuwa mnyenyekevu.” Kisha tunatambua kuwa vitendo vya wengine sio lazima viingie katika njia ya uhusiano wetu binafsi na Mwokozi na Baba yetu wa Mbinguni. Hakika, kuchukua jukumu binafsi kwa unyenyekevu wetu wenyewe haimaanishi kwamba tunapaswa kupuuza jinsi tabia zetu zinavyoweza kuathiri uzoefu wa wengine. Jitihada zetu kwenye unyenyekevu binafsi zinaweza kuwa ongezeko la upendo wetu kwao kama kaka na dada zetu.

Huduma ya Mwokozi

Katika mfano mzuri wa utumishi, Mwokozi alikuwa na huruma kwa mtu aliyekuwa na jeshi la mapepo wachafu. Ingawa mtu huyo alikuwa akipiga kelele na alitembea bila nguo, Yesu hakukataa kumponya. Ilikuwa baada ya kuponywa ndipo mtu huyu aliweza kukaa “miguuni pa Yesu, akiwa amevaa nguo, na akiwa na akili timamu,” akiomba kwamba aweze kubaki na Bwana. (Ona Luka 8:27–39; ona pia Marko 5:1–20.)

Vivyo hivyo, Yesu hakumwambia kijana mwenye pepo mchafu aache kujigandisha, kutoa povu na kusaga meno kabla ya kumponya (ona Marko 9:17–27). Aliona hali hizi kama uzoefu katika mwili wenye kufa, sio kasoro za kiroho. Walikuwa ni Mafarisayo tu ambao Yeye aliwafukuza kwa kuwa kujipa kwao haki binafsi na kiburi vilizuia uponyaji.

Wakati mimi na wewe tunapopanua ufafanuzi wetu juu ya unyenyekevu, tutaweza kufundisha na kuhudumu katika njia ya Mwokozi. Tutakumbuka thamani ya kila nafsi mbele za Mungu (ona Mafundisho na Maagano 18:10). Tutaweza kuwa wanyenyekevu hata katika hali zisizotarajiwa.

Pengine unyenyekevu machoni pa Bwana hauhusiani kabisa na kukaa kimya na kuzungumza kwa upole na unahusu zaidi utulivu wa akili zetu na ulaini wa mioyo yetu.

Mwandishi anaishi Texas, Marekani.

Muhtasari

  1. Dallin H. Oaks, Wasafi Moyoni (1988), 125.