“Je! Niondoke?,” Liahona, Machi./Aprili 2022
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho: Wanawake wa Imani
Je! Niondoke?
Baada ya kukwazwa wakati wa shughuli ya Muungano wa Usaidizi, nilikuwa na uamuzi wa kufanya.
Muda mfupi baada ya kujiunga na Kanisa, kiongozi wa Muungano wa Usaidizi alikuwa akifanya utani kuhusu hali za kuchekesha. Ghafla alianza kunitania mbele ya kila mtu. Sikufurahishwa na nikaruhusu kukwazika.
Wazo langu la kwanza lilikuwa ni kutokurudi tena katika kata ile. Nilifungua maandiko yangu, kujaribu kutafuta faraja. Nilipokuwa nasoma, nilikutana na mstari ambao Yesu aliwauliza wale waliokwazwa na mafundisho Yake, “Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka?” (Yohana 6:67).
Mara moja, nilijijibu akilini, “Hapana, sitaondoka!”
Nilimpigia rais wa Muungano wa Usaidizi, ambaye alipendekeza nimpigie simu dada ambaye alifanya mzaha kuhusu mimi. Nilimpigia simu na kumwelezea hisia zangu. Tulihitimisha kuwa ucheshi ni mzuri lakini kwamba hatupaswi kufanya mzaha juu ya mtu ambaye hatumjui mbele ya kikundi cha watu. Tulizungumza pia juu ya kuwa waangalifu kwa waumini wapya katika kata.
Niliendelea kuhudhuria kata hiyo wakati nilipokuwa nikiishi katika mji huo. Nilipitia mengi mazuri kufuatia uongofu wangu kwenye injili.
Katika safari yangu binafsi ya kushinda makwazo, nilipata maneno haya ya msaada kutoka kwa viongozi wetu wa Kanisa:
“Kama mtu akisema au kufanya jambo ambalo tunafikiria ni la kukwaza, jukumu letu la kwanza ni kukataa kukwazika na kisha tuwasiliane kwa faragha, kwa uaminifu, na moja kwa moja na mhusika huyo.” 1
“Ninakuahidi, unapochagua kutokwazika … , utahisi upendo [wa Mwokozi] na uthibitisho Wake.” 2
Ninashukuru nilichagua kutoacha Kanisa kwa sababu ya maoni yasiyofaa. Na ninashukuru kuwa muumini wa Kanisa lililorejeshwa, ambapo ninapata nguvu ya kuwa mwaminifu na kuendelea kwenye njia ya ufuasi. Ninashukuru kwa ajili ya ushauri wa manabii na mitume, ambao hutufundisha jinsi ya kushirikiana na kaka na dada zetu katika injili.
Ninaweza kuendelea kuwa mwaninifu na kuchagua kutotaka kukwazika. Ninaweza kufokasi kwenye juhudi zangu mwenyewe za kuwa kama Kristo na kuhisi upendo na uthibitisho wa Mwokozi.
Je! Niondoke? Hapana. Ninao ushuhuda kwamba hili ni Kanisa la Yesu Kristo lililorejeshwa duniani leo na kwamba linayo “maneno ya uzima wa milele” (Yohana 6:68).