“Mungu Anaweza Kutusaidia katika Nyakati Ngumu,” Liahona, Machi./Aprili 2022
Kanuni za Kuhudumu
Mungu Anaweza Kutusaidia katika Nyakati Ngumu
Na tunaweza kutumia kile tunachokipata kutoka kwenye majaribu yetu ili kuwasaidia wengine.
Marcela Endrek, mwenyeji wa Córdoba, Argentina, alikuwa mgonjwa na mwenye huzuni. Jambo hili lilimkatisha sana tamaa. Katikati ya kuhisi kwamba hakuna njia ya kutoka, alisikia hotuba ya mkutano ambayo ilizungumza juu ya maombi. Wazo lilikuja moja kwa moja moyoni mwake la kuomba kwa dhati juu ya matatizo yake.
Alianza kuomba mara kwa mara ili apate nafuu. Kuomba kulimletea amani na faraja ingawaje afya yake haikuimarika. Kwa kweli, hali yake ilizidi kuwa mbaya hadi akashindwa kufanya kazi tena. Sasa alikuwa na msongo wa ziada wa mawazo wa kutokuwa na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Kwa sababu ya ulazima, alianza kuchunguza jinsi anavyoweza kukabiliana na shida zake za kiafya kwa njia nyingine. Alihisi kushawishiwa kufokasi kwenye kubadilisha tabia kadhaa za mlo na alishangaa ni kiasi gani ilimsaidia. Kupona kwake kulivutia sana kiasi kwamba alianza kusoma mambo ya lishe kwa kina.
Wakati fulani baadaye, alikutana na msichana anayeitwa Evelyn akiwa katika hali kama ile aliyokuwa nayo Marcela—mgonjwa, mwenye huzuni, na anayetafuta majibu. Marcela alijiona yeye mwenyewe kwa rafiki yake mpya. Alishiriki baadhi ya yale ambayo alikuwa akijifunza juu ya uchaguzi wa chakula na lishe. Pia alishiriki na Evelyn ushuhuda wake juu ya nguvu ya maombi. Alimwalika Evelyn aombe ili yeye pia aweze kuhisi upendo wa Mungu na kujua kwamba Mungu alikuwa akimfahamu.
Siku chache baadaye, Marcela alifurahi kumuona Evelyn tena. Mabadiliko tayari yalikuwa dhahiri kimwili na kiroho. Evelyn alimjulisha kuwa maisha yake yalikuwa yakibadilika na kwamba angeweza kuhisi upendo wa Mungu kwake.
Kutoka kwenye majaribio na changamoto zake, Marcela alipata vyote huruma na taarifa aliyohitaji ili kuwasaidia wengine.
Tumekombolewa Ili Tuweze Kukomboa
Hadithi ya Yusufu huko Misri ni mfano mwingine wa kile kinachoweza kutokea wakati tunapokuwa tumeamua kumtumaini Mungu katika majaribu yetu: sio tu Yeye anaweza kutukomboa sisi, lakini anaweza kutuweka sisi kutumia uzoefu wetu ili kuwasaidia wengine (ona Mwanzo 37–45).
Yusufu alikuwa amedhamiria kumtumaini Mungu na kushika amri Zake licha ya usaliti, hasara, na kifungo. Kwa sababu ya imani ya Yusufu kwa Mungu na utayari wake wa kuvumilia majaribu yake kwa uvumilivu na bila kinyongo, “Bwana alikuwa pamoja na Yusufu” (Mwanzo 39:21) na kumweka katika nafasi ya kuwabariki wengi (ona Mwanzo 45:5–8).
Kanuni za Kuzingatia
Unapofikiria fursa zako za kuwahudumia wengine, fikiria kanuni hizi zilizoelezewa katika hadithi:
-
Changamoto zetu zinaweza kuwa baraka. Ikiwa “tutaomba kila wakati, na kuwa wenye kuamini” pale tunapopitia changamoto zetu, Baba wa Mbinguni anaweza kuzigeuza kuwa kwa faida yetu (ona Mafundisho na Maagano 90:24; ona pia Warumi 8:28).
-
Changamoto zetu zinaweza kutuandaa sisi. Ikiwa tutakuwa wapole katika majaribu, Mungu anaweza kutumia uzoefu wetu kutufundisha na kutubadilisha (ona Mafundisho na Maagano 112:13).
-
Changamoto zetu zinaweza kuwa fursa za kuhudumu. Ikiwa tuko tayari kumtumaini Yeye, Baba wa Mbinguni atatuweka katika nafasi za kutumia yale tuliyojifunza katika uzoefu wetu ili kuwasaidia wengine (ona Mosia 24:13–14).
Je, Tunaweza Kufanya Nini?
Omba kujua ni kwa jinsi uzoefu wako unaweza kukusaidia kuwabariki wale unaowahudumia. Kisha wafikie.