2022
Nipigie Simu Mimi Kwanza
Machi 2022


“Nipigie Simu Mimi Kwanza,” Liahona, Machi./Aprili 2022

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho: Wanawake wa Imani

Nipigie Simu Mimi Kwanza

Nafurahi sikupoteza nafasi ya kumsaidia dada ambaye alinihitaji na ambaye mimi nilimhitaji.

mwanamke mzee na mwanamke kijana wanatembeleana

Wakati nilipokuwa mama kijana wa mtoto wangu wa kwanza, mume wangu alikuwa bado yuko chuoni. Sote tulifanya kazi ya muda ili kukidhi mahitaji yetu.

Nikitarajia siku ya kupumzika kazini, nilikuwa nimepanga kutazama sinema ya zamani kwenye runinga. Hii ilikuwa kabla ya DVD au huduma za utiririshaji.

Sinema hiyo ingeanza wakati mzuri—saa 4:00 asubuhi—wakati mtoto wetu atakuwa amelala. Ilimshirikisha Cary Grant, mmoja wa nyota wa Kimarekani niwapendao katika sinema.

Usiku kabla ya siku yangu iliyotarajiwa ya kupumzika, raisi wa Muungano wa Usaidizi wa kata alipiga simu. Dada katika kata yetu alikuwa amepata kiharusi kidogo na alihitaji uangalizi siku iliyofuata hadi mtoto wake atakaporudi kutoka kazini.

“Ningefanya hili mwenyewe, lakini nina ugeni,” rais wa Muungano wa Usaidizi alisema. Alielezea kwamba hakuwa na mtu mwingine wa kumwomba na alijitolea kumwangalia mtoto wetu wakati mimi nikimtunza dada huyo. Nilikubali kwa shingo upande.

Asubuhi iliyofuata, nilimwacha mtoto wetu na kwenda kumtembelea dada huyo. Jina lake lilikuwa Louise, na nilihisi kumpenda ghafla. Alikuwa na umri wa kutosha kuwa bibi yangu, ambaye alikuwa amefariki karibuni.

Nilimsaidia Louise kuvaa na kisha nikamwandalia kifungua kinywa. Alitulia kwenye kiti na kuwasha runinga. Punde iliwadia saa 4 asubuhi. Alipokuwa akipitia chaneli kwa rimoti, alisema, “Televisheni hii haina chochote cha kutuonyesha.”

Nilisita kisha nikasema, “Kuna sinema ya Cary Grant kwenye chaneli ya 11.”

“Kweli?” Aliuliza. “ Ninampenda Cary Grant!”

Tuliangalia sinema na kuifurahia yote. Baadaye, alinisimulia juu ya maisha yake wakati alipokuwa na umri kama wangu. Aliniambia juu ya mtoto wake, nami nikamwambia kuhusu wangu. Alizungumza juu ya Kanisa na jinsi ambavyo hajahudhuria kwa muda mrefu.

Mwanaye aliporudi, niliahidi kurejea. Nilimwambia rais wa Muungano wa Usaidizi anipigie simu mimi kwanza ikiwa Louise angehitaji mtu.

Wakati fulani katika wiki mbili zilizofuata, Louise alipata kiharusi kingine na akafariki kabla sijapata nafasi ya kumuona tena. Tulikuwa tumekuwa pamoja kwa masaa tisa tu na kuangalia sinema moja, lakini alikuwa rafiki mpendwa. Namfikiria mara nyingi.

Nashukuru sikupoteza nafasi ya kumsaidia dada ambaye alinihitaji—na ambaye mimi nilimhitaji, ingawa sikulitambua hilo.