“Kuuona Uso wa Mungu kwa Maadui zetu,” Liahona, Machi./Aprili 2022
Kuuona Uso wa Mungu kwa Maadui Zetu
Masomo haya kuhusu kushinda migogoro kutoka katika kitabu cha Mwanzo yanaweza kutoa mfano kwa ajili ya maisha yetu wenyewe.
Kama mpatanishi wa migogoro, nimekusanya hekima nyingi kuhusu jinsi ya kubadili mgogoro na kualika mapatano kutoka katika kuangalia mfano na mafundisho ya Yesu Kristo katika Agano Jipya. Walakini, Agano Jipya sio kitabu pekee cha maandiko ambacho kimeniongoza katika kipindi chote cha taaluma yangu. Agano la Kale lina utambuzi mwingi wa kustaajabisha unaoweza kutusaidia tunapojikuta tumekwama katika migogoro ya uharibifu.
Je, mgogoro wa uharibifu ni nini? Ni wakati kukosa kwetu uwezo wa kutatua matatizo kwa kushirikiana na wengine kunapotuongoza kwenye kuwaumiza wengine au sisi wenyewe.
Pamoja na mgogoro wa uharibifu huja hofu ya maumivu katika kutarajia na kama matokeo ya mgogoro, hofu ya kutopendwa au kuonekana jinsi tunavyotaka tuonwe, na hofu ya kushindwa kupata suluhisho kwa matatizo yanayotukabili. Tunaporuhusu woga huo utushike, hatuhisi tena kuwa na nyenzo za kutatua matatizo tunayokabiliana nayo na mara nyingi tunapata hisia za kukata tamaa, aibu au kukosa msaada.
Aina hiyo ya mgogoro huwa hatari kwa watu wengi, hii ndiyo sababu tunaishia kutumia mipangilio ya migogoro isiyosaidia kama vile kujiepusha, kukubaliana au ushindani kama njia ya kujaribu kumaliza mgogoro. Kwa bahati mbaya, katika mgogoro wa uharibifu, hakuna suluhisho hata moja kati ya hayo ambalo litafanya kazi vizuri.
Ndio, yatupasa tuepuke mabishano (ona 3 Nefi 11:29). Lakini hatupaswi kamwe kuwaepuka, kuwakatia tamaa, au kuwashambulia watu ambao tuna mgogoro nao. Badala yake, tunahitaji kujifunza jinsi ya kuwapenda watu ambao tuna mgogoro nao. Inahitaji uonyeshaji wa hisani, upendo safi wa Kristo, kwa maadui zetu (ona Moroni 7:47).
Yesu alifundisha kwamba kuwapenda wale wanaokupenda wewe ni rahisi. Alisema pia, “Lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, watendeeni mema wale wanaowachukia” (Mathayo 5:44). Mwokozi anatutaka sisi tupende kama Yeye anavyopenda na kuwa wakamilifu kama Yeye alivyo (ona Yohana 13:34; 3 Nefi 12:48). Hii inaweza kumaanisha kuwa tayari kuwapenda wengine hata wakati upendo kama huo unapoonekana kuwa hatari. Tunaweza kusita kwa sababu kiuhalisia tunaepuka hatari. Lakini kuamua kuwapenda wale ambao wanaweza kutuumiza kunaturuhusu sisi kufukuza hofu ya zamani na kuwa tuliojawa na hisani.
Aina hii ya upendo huitaji kutokuwa na hofu mbele ya migogoro. Unatupatia wito tuwe wawazi kwa watu ambao tuna mgogoro nao kwa njia ambayo “huvumilia, hufadhili, … hautafuti mambo yake, hautakabari, haufurahii udhalimu; … huvumilia yote, huamini yote, hutumaini yote, hustahimili yote. … Upendo haupungui neno wakati wowote” (1 Wakorintho 13:4–5, 7–8). Hisani inaonyesha upendo wa aina hii bila dhamana kwamba watu wa upande mwingine wa mgogoro watafanya vivyo hivyo.
Upendo unaturuhusu kuwaona kaka na dada zetu ambao tuna mgogoro nao kwa uwazi sana kwamba mahitaji na matamanio yao ni muhimu kwetu kama yalivyo yetu, bila kujali jinsi wanavyotuona. Tutafanya chochote kinachohitajika ili kupata masuluhisho ambayo yanakidhi mahitaji yao na pia yetu.
Hadithi mbili kutoka Agano la Kale ni mifano mizuri ya upendo huu.
Esau na Yakobo
Katika Mwanzo 25, tunakutana na mgogoro wa kifamilia kati ya ndugu wawili, Esau na Yakobo, wana wa Isaka. Esau aliuza urithi wake kwa Yakobo kwa bakuli moja la chakula (ona Mwanzo 25:30–31). Baadaye, kufuatia ushauri wa mama yake, Yakobo alijifanya yeye kuwa Esau ili apate baraka ya mwisho ya Isaka (ona Mwanzo 27:6–29).
Esau alimchukia Yakobo na akaapa kumuua ndugu yake. Yakobo alikimbia kwenda kuishi na mjomba wake, Labani. (Ona Mwanzo 27:41–45.) Mwishowe Yakobo aliingia matatizoni na mjomba wake na hivyo kulazimika kurudi nyumbani (ona Mwanzo 31). Yakobo alijua hiyo ilimaanisha kukabiliana na Esau, ambaye alikuwa na jeshi kubwa. Alihofia maisha yake na ya familia yake (ona Mwanzo 32:7–8).
Siku ambayo walipaswa kukutana, Yakobo alituma makundi mengi ya mbuzi, ngamia, ng’ombe, kondoo na punda kama sadaka ya amani. Kisha alisujudu mara saba alipomkaribia kaka yake. Esau alijibu kwa njia ambayo Yakobo hakutarajia. Esau alilia, akamkumbatia kaka yake, na kumwambia hakukuwa na haja ya sadaka ya amani.
Yakobo aliguswa na upendo wa Esau na akajibu:
“ Sivyo; kama nimekubalika machoni pako tafadhali upokee zawadi yangu mkononi mwangu: iwapo nimeona uso wako kama kuona uso wa Mungu, ukapendezwa nami.
“Pokea, tafadhali, mbaraka wangu, ulioletewa, kwa sababu Mungu amenineemesha, na kwa sababu ninavyo hivi vyote. Akamshurutisha, naye akapokea” (Mwanzo 33:10–11).
Vipengele Vitatu Vinahitajika ili Kuishi kwa Amani
Yakobo alijumuisha mpangilio wa upendo hapa ambao nimeona kuwa njia yenye tija zaidi ili kualika mapatano na wale ambao tumewakosea au ambao wametukosea.
Zaburi 85:10 inaelezea masharti ya mapatano: “Fadhili na kweli zimekutana, Haki na amani zimehusiana.” Kitendo cha Yakobo na Esau cha kufanya amani kinakidhi masharti yanayopatikana katika Zaburi.
Ilihitaji ujasiri kwa Yakobo na Esau kuutambua ukweli kwamba hawakuwa maadui—walikuwa ndugu. Ilihitaji fadhili kusameheana. Ilihitaji haki—aina ya haki ambayo inasahihisha kile ambacho sisi au wengine wamekosea—kwa Yakobo kumpa Esau sehemu ya kile ambacho alikuwa amebarikiwa nacho. Wakati vitu vyote vitatu vilipokuwepo, viliwaruhusu kuishi kwa amani.
Tunaweza kufuata mpangilio huo katika maisha yetu wenyewe.
Tunapokwama katika migogoro ya uharibifu, hofu yetu ya mgogoro na hofu yetu juu ya wengine inaweza kutupooza au kutufanya tutende kwa njia ambazo hufanya mambo kuwa mabaya zaidi, sio bora. Mara nyingi tunahalalisha kwamba chochote tunachoweza kufanya ili kurudisha nyuma mzunguko wa uharibifu hakitafanya kazi. Tunakuwa wenye wasiwasi kuwa wengine hawawezi kubadilika.
Walakini, mfano wa Yakobo pia unatupatia sisi njia ya kutatua aina hiyo ya mgogoro. Yakobo alikabiliana na hofu yake juu ya kaka yake na hofu yake juu ya mgogoro wake na kaka yake. Alikuwa amejikita zaidi juu ya “kujenga mahusiano yao” kuliko “kukuza mapendeleo yake mwenyewe” kwa wakati huo, kwa hivyo alimgeukia kaka yake, akimpa vyote ukweli na haki kwa makosa yoyote aliyoyafanya. Moyo wa Esau, ambao wakati mmoja ulikuwa juu ya kumuua Yakobo, ulilainishwa; fadhila na amani zilimrudia kama malipo. Jakobo alipata njia ya kumpenda adui yake na, kwa kufanya hivyo, akauona “uso wa Mungu” ukimtazama.
Licha ya wasiwasi ambao tunaweza kuhisi katika kuukabili mgogoro kwa njia hii, ni yenye tija zaidi katika kuubadilisha mgogoro huo kuliko kitu kingine chochote. Upendo kama wa Kristo hutengeneza nafasi kwetu kuwaona watu ambao tunapambana nao kwa njia ambayo kimsingi inatubadilisha sisi na wao.
Yusufu na kaka zake
Kizazi kimoja baada ya Yakobo, tunaona mfano mwingine wenye nguvu wa upendo kutoka kwa kijana wa mwisho wa Yakobo, Yusufu.
Yusufu anauzwa utumwani na kaka zake wenye wivu akiwa mdogo. Kama vile Esau, kaka zake Yusufu walihisi kwamba baba yao alikuwa akimpenda zaidi na kwamba Yusufu alikuwa amepata upendeleo zaidi. Yusufu aliteseka sana kwa sababu ya uovu wa ndugu zake kwake. Alitengwa kutoka kwa familia yake kwa miaka kadhaa, akaishia kuwa mtumishi, na akafungwa kwa muda. Mwishowe, Bwana alimsaidia kushinda dhiki yake, na akawa mtawala mwenye nguvu nchini Misri. (Ona Mwanzo 37–45.)
Kaka zake pia waliteseka na, wakati wa njaa, walifika Misri, wakiwa na njaa na walioshindwa. Walipokutana na Yusufu, hawakumtambua na walimwomba msaada.
Yusufu alikuwa na haki zote za kuwatupa ndugu zake gerezani ili haki itendeke. Hicho ndicho walichostahili. Alichagua badala yake kutumia neema—kuwasamehe, na kuwapenda.
“Karibuni kwangu; basi” aliwaambia. “Wakakaribia. Akasema, Mimi ndimi Yusufu ndugu yenu, ambaye mlimuuza kwenda Misri.
“Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku: maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.” (Mwanzo 45:4–5).
Yusufu hakuwasamehe tu kaka zake bali pia aliona kusudi lenye kujenga katika mgogoro wao. Alitambua kuwa mkono wa Mungu ulikuwa katika kila kitu na kwamba licha ya mateso waliyovumilia wote, “Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu” (Mwanzo 45:7).
Tena, mpangilio kama huo unaweza kuwa sehemu ya maisha yetu wakati tunapokiri kwamba maumivu ya mgogoro yanaweza kutuongoza kwenye matokeo ambayo yataimarisha familia na jumuiya zetu ikiwa tutashirikiana kupata suluhisho.
Sisi sote tutapitia migogoro. Itaumiza. Wakati mwingine sana. Mara zote huwa naheshimu maumivu ambayo wengine wanayahisi wakati wanapojumuishwa kwenye mgogoro, hasa na wapendwa wao. Walakini, maumivu hayo na hofu sio lazima yawe mwisho wa hadithi.
Tunaweza kuchagua kuiangalia migogoro na watu ambao tuna migogoro nao kitofauti, kama vile Yusufu alivyofanya. Tunaweza kuchagua kuacha hasira, chuki, na kulaumu na kuwakumbatia maadui zetu.
Tunaweza kuchagua upendo dhidi ya woga na kugundua—kama vile Yakobo, Esau, Yusufu, na kaka zake walivyogundua—kwamba maadui zetu ni kaka na dada zetu. Kwa kujitahidi kupatana nao, sisi pia tunaweza kuuona uso wa Mungu.