2022
Bwana Alikuwa pamoja na Yusufu
Machi 2022


“Bwana Alikuwa pamoja na Yusufu,” Liahona, Machi./Aprili 2022

Njoo, Unifuate

Mwanzo 37–41

Bwana Alikuwa pamoja na Yusufu

Tunapozunguka kupitia hali nzuri na mbaya za maisha, tunaweza kujifunza mengi kutokana na mfano wa nabii wa kale Yusufu.

Yusufu wa Misri akielezea ndoto za Farao

Yusufu akielezea ndoto za Farao, na Jean Adrien Guignet, Musée des Beaux-Arts, Rouen, France / Bridgeman Images

Miaka kadhaa iliyopita, familia yetu ilifurahi tulipogundua kwamba mke wangu, Terri, alikuwa anatarajia mtoto wetu wa nne. Walakini, miezi kadhaa katika ujauzito ule, tuligundua kwamba Terri alikuwa na uwezekano wa kuwa na hali ya hatari kiafya. Chaguo salama zaidi lilikuwa ni yeye kulazwa hospitalini, ambapo angeweza kupata uangalizi wa muda wote. Aliwekwa kwenye mapumziko kitandani katika jitihada za kuendeleza ujauzito ule kadiri iwezekanavyo.

Huu ukawa wakati wa giza na mgumu kwa familia yetu, hasa kwa Terri. Alijihisi mpweke sana. Na nilikuwa na changamoto ya kuwatunza watoto wadogo watatu wakati nikifanya kazi katika taaluma yangu na pia nikitumikia kama askofu. Maisha yalionekana kuwa ya vurugu na magumu.

Katika upweke wake, Terri alipata faraja kwenye maneno ya wimbo mzuri wa kanisa:

Ninahitaji uwepo wako kila saa inayopita.

Je! ni nini isipokuwa neema yako iwezayo kuharibu nguvu ya mshawishi?

Nani, kama wewe, mwongozaji na mtulizaji wangu anaweza kuwa?

Kwenye mawingu na mwangaza wa jua, Bwana, kaa nami! 1

Bwana Alikuwa pamoja na Sisi

Mwishowe, upasuaji wa dharura ulihitajika ili kumzaa mtoto wetu Jace. Lakini wote wawili mama na mwana walikuwa salama kwa sababu Terri alikuwa tayari hospitalini. Tulihisi ulinzi wa Bwana katika maisha yetu.

Jace alizaliwa wiki nne kabla na kuwekwa katika chumba cha utunzaji wa watoto njiti. Tulirudi nyumbani bila mtoto wetu. Katika mwezi uliofuata, tulifanya safari za kila siku kwenda hospitalini. Maisha yalionekana kuzunguka kwa kiwango cha chini.

Tena, hata hivyo, tulishuhudia mkono wa Bwana. Jace aliendelea hadi mahali ambapo tuliweza kumleta nyumbani, hatua ya juu wakati tulipoungana kama familia.

Kisha tuligundua kuwa Jace alikuwa na sagittal synostosis, hali ambayo mifupa katika fuvu la kichwa kabla ya kukomaa huungana pamoja. Matokeo yake ni kwamba kichwa cha mtoto hakiwezi kukua. Matibabu pekee ilikuwa kuondoa kwa upasuaji sehemu kubwa ya fuvu la kichwa cha Jace wakati alipokuwa na miezi mitatu tu. Tulivumilia changamoto hii kupitia maombi na baraka za ukuhani. Tena tukauona mkono wa Bwana katika maisha yetu. Sala zilijibiwa. Baraka zilitimizwa. Upasuaji ulikuwa wenye mafanikio. Hatimaye maisha yalikuwa mazuri tena.

Safari yenye changamoto iliyoje! Lakini Bwana alitufundisha masomo mengi katika hii safari. Tunajua alikuwa pamoja nasi kipindi tupo njiani.

Yusufu Alikuwa na Hali Zake Nzuri na Mbaya

Yusufu akiuzwa Misri

Yusufu akiuzwa Misri, na William Brassey Hole, © Look And Learn / Bridgeman Images

Tunapojifunza maisha ya Yusufu katika Agano la Kale, tunaona kwamba maisha yake, pia, yalikuwa safari kutoka kwenye hali nzuri hadi mbaya na kurudi tena kwenye hali nzuri ya maisha. Na tunajifunza kuwa Bwana alikuwa pamoja naye kila wakati, katika hali nzuri na mbaya.

Kanzu ambayo Yakobo alimpa Yusufu ilikuwa ishara nzuri ya upendo wa Yakobo kwa Yusufu. Lakini pia ilitumika kama ukumbusho wenye kuudhi kwa ndugu za Yusufu juu ya uhusiano kati ya Yusufu na baba yake.

Wakati kaka zake walipokwenda kulisha mifugo ya baba yao, Yakobo alimtuma Yusufu aende kuwaangalia. Yusufu alienda kama alivyoombwa. Walakini, inaonekana alipotea njiani. Kwa hivyo Bwana alimtuma mtu kumpa Yusufu maelekezo ili aweze kuwapata ndugu zake (ona Mwanzo 37:15–17).

Wakati kaka zake Yusufu walipopanga njama ya kumuua, inaonekana zaidi kama bahati nasibu kwamba msafara ulitokea tu kupita njia ile kwenda Misri. Badala ya kumuua Yusufu, au kumwacha afe shimoni, ndugu zake walimuuza kwa ule msafara. (Ona Mwanzo 37:25-28.)

Mwongozo wa Bwana ulionekana dhahiri kwa mara nyingine wakati msafara nao ulipomuuza Yusufu kwa Potifa, nahodha wa walinzi wa Farao. Hata akiwa kama mtumwa, Yusufu aligeuza kila tukio kuwa kitu fulani kizuri. Potifa alimfanya Yusufu kuwa msimamizi juu ya nyumba yake. Aliweka yote aliyokuwa nayo mikononi mwa Yusufu. (Ona Mwanzo 39:4.) Yusufu alikuwa amesafiri kutoka sehemu ya bondeni kwenda kilimani. Sasa alikuwa akifurahia fursa na mazuri ya nyumba ya Potifa.

Walakini, hatua hii ya kuwa juu haikudumu kwa muda mrefu. Wakati Yusufu alipokimbia ushawishi usiofaa wa mke wa Potifa, mwanamke huyu alimshtaki kwa uasherati. Ingawa mashtaka yake yalikuwa ya uwongo, Yusufu angeweza kuuawa kwa urahisi. Inashangaza kwamba, badala yake, aliwekwa tu gerezani. Mkono wa Bwana ulimlinda Yusufu tena.

Imani Iliyotukuka

Ikiwa ungekuwa wewe ndiye uliyetupwa gerezani bila haki, ungefanya nini? Kama kuna mtu yeyote ambaye alikuwa na sababu ya kuvunjika moyo na kuwa na uchungu, alikuwa Yusufu. Kuporomoshwa kwa uovu kutoka hali ya kuwa juu kwenda kuwa chini kungeweza kwa urahisi kumfanya afikiri, “Je, kuna faida gani ya kujaribu kumtumikia Mungu? Anachofanya ni kuniadhibu tu.” Lakini Yusufu hakukasirika au kumlaumu Bwana, na hakukata tamaa. Imani yake iliyotukuka haikuyumba kamwe.

Na hata katika siku za giza za kifungo, Bwana hakumwacha Yusufu. Kwanza, Bwana alitoa fursa kwa Yusufu kutafsiri ndoto za mnyweshaji na mwokaji mikate (ona Mwanzo 40). Halafu, miaka michache baadaye, wakati hilo lilipotoa fursa ya kutafsiri ndoto ya Farao, Yusufu alikubali kuwa uwezo wa kufanya hivyo ulitoka kwa Mungu (ona Mwanzo 41:16). Sio tu kwamba Farao alimrudisha Yusufu, lakini pia “alimfanya awe mkuu juu ya nchi yote ya Misri” (Mwanzo 41:43). Baada ya Yusufu kuteseka na kuhangaika kwa miaka mingi, Mungu alimwezesha Yusufu kuwa mtu mwenye ushawishi katika nchi, wa pili kutoka kwa Farao—hatua nyingine ya kileleni katika maisha ya Yusufu.

Mungu Anayakusudia kwa Faida Yetu

Yusufu hatimaye alikutana na kaka zake tena, wale ambao walikuwa wamefanya njama dhidi yake na kumuuza utumwani. Angeweza kuwa na hasira. Angeweza kuwalaumu wao kwa “ukosefu wa haki wa kukasirisha” waliomfanyia. 2

Lakini Yusufu aligundua kuwa heka heka za maisha yake zilisimamiwa na Bwana. Kauli yake kwa kaka zake inatoa ufahamu juu ya uelewa huo:

“Nanyi kweli mlinikusudia mabaya, bali Mungu aliyakusudia kuwa mema, ili itokee kuokoa taifa kubwa, kama ilivyo leo.

“Basi sasa msiogope; mimi nitawalisha na watoto wenu. Akawafariji, na kusema nao vema” (Mwanzo 50:20–21).

Tunapozunguka kupitia hali nzuri na mbaya za maisha, ni ukumbusho mzuri kiasi gani, kwamba Mungu anayakusudia kwa faida yetu. Bwana alielezea kanuni hiyo hiyo kwa Joseph wa siku za mwisho:

“Kama wewe umeitwa kupita kwenye taabu; …

“Kama wewe utashtakiwa kwa namna zote za shutuma za uongo; kama adui zako wataanguka juu yako; kama watakuondoa wewe kutoka kwenye jumuiya ya baba yako na mama … nawe utaburuzwa kwenda gerezani, …

“… Fahamu wewe, mwanangu, kwamba mambo haya yote yatakupa wewe uzoefu, na yatakuwa kwa faida yako” (Mafundisho na Maagano 122:5–7).

Daima Kumekuwapo Ugumu

Wakati mimi na Terri tulipokuwa tukipitia changamoto zetu, tulipata faraja katika kauli hii kutoka kwa nabii wa Mungu:

“Ninataka mjue kuwa daima kumekuwako na ugumu katika maisha ya mwili wenye kufa, na daima utakuwapo. Lakini kujua kile tunachojua, na kuishi vile tunavyopaswa kuishi, kwa kweli hakuna mahali, hakuna kisingizio, cha kukata tamaa na kuvunjika moyo. …

“… Natumaini hamtaamini kwamba magumu yote ya ulimwengu yamejumuishwa katika muongo wenu, au kwamba mambo hayajawahi kuwa mabaya zaidi kama yalivyo kwako wewe binafsi, au kwamba hayatakuja kuwa bora kamwe. Ninawahakikishia kuwa mambo yamekuwa mabaya na yatakuwa daima mazuri. Daima yanakuwa—hususani tunapoishi na kuipenda injili ya Yesu Kristo na kuipa nafasi ya kustawi katika maisha yetu.” 3

Kutoka katika hadithi ya Yusufu na kutoka katika matukio mabaya katika ulimwengu unaotuzunguka, ni rahisi kuona kwamba mambo mabaya yanawatokea watu wema. Kuishi kwa haki hakumaanishi kwamba tutaepuka changamoto na huzuni katika maisha yetu. Walakini, kama vile Bwana alivyokuwa pamoja na Yusufu katika dhiki yake, Yeye pia atakuwa pamoja na sisi. Majaribu bila shaka yatakuja. Lakini kama tutayapitia kwa dhamira ya kumsikiliza Yeye, Bwana atatuongoza na kututia moyo, kama vile alivyofanya kwa Yusufu.

Muhtasari

  1. Kaa Nami!Wimbo wa Kanisa, na. 166.

  2. Ona Dale G. Renlund, “Ya Kukasirisha Yasiyo Haki,” Liahona, Mei 2021, 41–45.

  3. Howard W. Hunter, “Nanga kwa Nafsi za Wanadamu,” Ensign, Oktoba. 1993, 70.