Njoo, Unifuate
Julai 15–21: “Uwezo wa Neno la Mungu.” Alma 30–31


“Julai 15–21: ‘Uwezo wa Neno la Mungu.’ Alma 30–31,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Julai 15–21. Alma 30–31,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: 2024 (2023)

Alma akimfundisha Korihori

Vitu Vyote Vinashuhudia Kuwa Kuna Mungu (Alma na Korihori), na Walter Rane

Julai 15–21: “Uwezo wa Neno la Mungu”

Alma 30–31

Maelezo katika Alma 30–31 yanadhihirisha wazi uwezo wa maneno—kwa uovu na kwa wema. “Maneno ya kusifu” na “maneno kwa sauti kubwa” ya mwalimu wa uongo aliyeitwa Korihori yalitishia kuleta “roho nyingi kwenye maangamizo” (Alma 30:31, 47). Vilevile, mafunzo ya Mnefi muasi aliyeitwa Zoramu yalisababisha kundi zima la watu kufanya “makosa makubwa” na “waliharibu njia za Bwana” (Alma 31:9, 11).

Kinyume cha hayo, Alma alikuwa na imani isiyotikisika kwamba neno la Mungu lingekuwa na “maelekezo ya nguvu zaidi kwa akili za watu kuliko upanga au kitu chochote kingine” (Alma 31:5). Maneno ya Alma yalionesha ukweli wa milele na alitegemea nguvu za mbinguni kumzima Korihori (ona Alma 30:39–50), na waliomba baraka za mbinguni juu ya wale walioenda pamoja naye kuwaleta Wazoramu tena kwenye ukweli (ona Alma 31:31–38). Hii ni mifano ya thamani kwa wafuasi wa Kristo leo wakati ambapo jumbe za uongo zimekuwa kawaida. Tunaweza kupata ukweli kwa kutumainia, kama alivyofanya Alma, “uwezo wa neno la Mungu” (Alma 31:5).

Mawazo kwa ajili ya Kujifunza Nyumbani na Kanisani

Alma 30:6–31

ikoni ya seminari
Adui hujaribu kunidanganya kwa mafundisho ya uongo.

Katika Alma 30, Korihori anaitwa “Mpinga-Kristo” (mstari wa 6). Mpinga Kristo ni mtu yeyote au kitu chochote ambacho kwa uwazi au kwa siri ni upinzani kwa Yesu Kristo na injili Yake. Ni mistari ipi katika Alma 30:6–31 inaonesha kwamba Korihori anafanana na maelezo haya? Kujifunza mafundisho ya uongo ya Korihori kunaweza kukusaidia kuyatambua na kuyakataa mafundisho sawa na hayo. Shughuli zifuatazo zinaweza kusaidia katika kujifunza kwako:

  • Ni masomo gani ya vitendo unayafikiria yanayoweza kuboresha uelewa wako kuhusu tofauti kati ya mafundisho ya Mwokozi na uigaji wa uongo wa Shetani? Baadhi ya mifano ni kama chambo kinachotumiwa katika uvuvi, pesa bandia, na matangazo bandia. Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuelewa kama kitu ni bandia? Ni kwa jinsi gani unaweza kuutambua ukweli?

  • Fikiria kutengeneza orodha ya mafundisho ya uongo Korihori aliyoyafundisha katika Alma 30:6–31. Ni mafundisho yapi katika mafundisho yake ya uongo yangeweza kuwavutia watu leo? (Ona Alma 30:12–18, 23–28). Ni madhara gani yanaweza kutokea kutokana na kukubali mawazo kama hayo? Ni jumbe zipi za uogo adui anatumia ili kujaribu kukudanganya leo?

  • Alma alifanya nini ili kukinza mafundisho ya Korihori kwa ukweli? (ona Alma 30:31–54). Ni kwa jinsi gani unaweza kutumia kanuni sawa na hizi katika maisha yako?

Kama Alma, manabii na mitume wa sasa wanatusaidia tujue tofauti kati ya ukweli na uongo wa Shetani. Ni ushauri upi unaupata katika jumbe hizi: Gary E, Stevenson, “Usinidanganye,” (Liahona, Nov. 2019, 00–00); Dallin H. Oaks, “Usidanganyike” (Liahona, Nov. 2004, 00).

Ona pia Mada za Injili, “Tafuta Ukweli na Uepuke Kudanganywa,” Maktaba ya Injili; “Ukweli ni Nini?,” Nyimbo za Dini, na. 156.

Korihori akizungumza na Alma

Korihori anamkabili Alma, na Robert T. Barrett

Alma 30:39–46

Mambo Yote Yanamshuhudia Mungu.

Watu wengi leo wanaamini kwamba hakuna Mungu. Unapata kipi katika Alma 30:39–46 ambacho kinakusaidia ujue kwamba Mungu ni halisi? Ni kipi hutuzuia sisi kutokumjua Yeye? Ni shuhuda zipi zingine ambazo Mungu amekupatia kwamba Yeye yu hai?

Alma 30:56–60

Adui hawasaidii wafuasi wake.

Tunajifunza nini kutoka Alma 30:56–60 kuhusu jinsi ambavyo ibilisi huwatendea wafuasi wake? Tunaweza kufanya nini ili kulinda nyumba yetu dhidi ya ushawishi wake?

Ona pia Alma 36:3.

Alma 31

Neno la Mungu lina uwezo wa kuongoza watu kuwa wenye haki.

Tatizo la Wazoramu kujitenga na Wanefi linaweza kuwa lilionekana kwa baadhi kama lilihitaji suluhisho la kisiasa au kijeshi (ona Alma 31:1–4). Lakini Alma alikuwa amejifunza kuamini “uwezo wa Neno la Mungu” (Alma 31:5). Unajifunza nini kutoka Alma 31:5 kuhusu nguvu za neno la Mungu? (Ona pia Waebrania 4:12; 1 Nefi 15:23–24; 2 Nefi 31:20; Yakobo 2:8; Helamani 3:29–30).

Unapojifunza Alma 31, ni kweli zipi zingine za injili unaweza kuzipata ambazo zinatumika kwenye uzoefu wa maisha yako? Kwa mfano:

  • Ni kwa jinsi gani umeona neno la Mungu likiwaongoza watu kufanya vitu vizuri? (ona mstari wa 5).

  • Linganisha mitazamo, hisia, na matendo ya Alma kuwahusu wengine (ona mistari 34–35) na ile ya Wazoramu (ona mistari 17–28). Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwa zaidi kama Alma?

  • Je, ni kipi unakipata katika Alma 31:30–38 ambacho kinaweza kuwasaidia wale wanaohuzunika kwa ajili ya dhambi za wengine?

Alma 31:5–6

Kwa sababu ya Yesu Kristo, mtu yeyote anaweza kubadilika.

Tazama kikundi cha watu wa Alma aliowachukua pamoja naye kufundisha injili kwa Wazoramu (ona Alma 31:6). Je, unajifunza nini kuhusu maisha ya watu hawa katika Mosia 27:8–37; 28:4; Alma 10:1–6; 11:21–25; 15:3–12). Je, ni ujumbe upi ungeweza kuwa pale kwa ajili yako katika uzoefu wao?

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la Liahona na magazeti ya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana.

Mapendekezo kwa ajili ya Kuwafundisha Watoto

Alma 30

Kitabu cha Mormoni kinanionya mimi dhidi ya mafundisho ya uongo.

  • Fikiria kuonesha baadhi ya vitu (kama vile pesa au chakula) na mfano bandia wa vitu hivi. Hii ingaliweza kuongoza kwenye mjadala kuhusu jinsi ya kujua tofauti kati ya vitu ambavyo ni vya kweli na vitu ambavyo ni vya bandia. Kisha ungeweza kuwasaidia watoto wako watambue kutoka katika Alma 30:12–18 uongo au mafundisho ya uongo ambayo Korihori alifundisha kuhusu Mungu. Katika Alma 30:32–35, ni kwa jinsi gani Alma alijibu uongo huu? Tunajifunza nini kutokana na mfano wake?

Alma 30:44

Vitu vyote vinamshuhudia Mungu.

  • Alma alizungumza kuhusu jinsi vitu angani na duniani vinavyoshuhudia kwamba Mungu yu hai. Kama inawezekana, fanya matembezi ya nje pamoja na watoto wako au simameni dirishani wakati mkisoma Alma 30:44. Waombe waoneshe vitu wanavyoviona ambavyo vinawasaidia wajue Mungu ni halisi na kwamba Yeye anawapenda. Wanaweza pia kuchora picha za vitu walivyogundua (ona ukurasa wa shughuli ya wiki hii).

  • Wakati wewe na watoto mnapoimba “My Heavenly Father Loves Me” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 228–29), pitisha mpira au kitu kingine. Mara kwa mara simamisha muziki, muombe mtoto aliyeshikilia kitu ashiriki kitu kimoja ambacho Baba wa Mbinguni aliumba ambacho anashukuru kwa ajili ya kitu hicho.

Watoto wanajifunza kupitia vielelezo. Vielelezo vitawasaidia watoto wako waelewe vyema na kukumbuka kwa muda mrefu kile walichofundishwa. Nyingi kati ya shughuli kwa ajili ya watoto katika muhtasari huu zinapendekeza vielelezo kutumika. Fikiria kutumia vielelezo hivyo hivyo tena baadaye ili kuwasaidia watoto wako wakumbuke kile walichojifunza.

Alma 31:5

Neno la Mungu ni lenye nguvu.

  • Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto wako waelewe kwamba neno la Mungu lina nguvu zaidi kuliko “kitu kingine chochote”? (Alma 31:5). Fikiria kuwaomba watoto wafikirie kitu fulani au mtu mwenye nguvu, au waoneshe picha ya baadhi ya vitu vichache vyenye nguvu. Nini huvifanya viwe na nguvu sana? Someni Alma 31:5 pamoja na waulize watoto wako kile wanachodhani mstari huu humaanisha. Shiriki uzoefu ambapo neno la Mungu lilikuwa na ushawishi wenye nguvu kwako.

Alma 31:8–35

Baba wa Mbinguni husikia sala zangu.

  • Fanya muhtasari wa hadithi ya Alma na Wazoramu, ukitumia mistari kutoka katika Alma 31:8–35 (ona pia “Mlango wa 28: Wazoramu na RameumptomuHadithi za Kitabu cha Mormoni, 78–80). Wasaidie watoto wako watambue mambo Wazoramu waliyoyasema katika sala zao (ona Alma 31:15–18) wakati wakikusaidia kujenga mnara wa Rameumptomu kwa kutumia matofali au mawe. Eleza kwamba hivi sivyo jinsi tunavyopaswa kusali. Wewe na watoto wako mnapozungumza kuhusu jinsi tunavyopaswa kusali, waruhusu waondoe tofali au jiwe moja moja kwa wakati. Labda wangeweza kuweka mojawapo ya mawe kando ya kitanda chao kama ukumbusho wa kusali kila asubuhi na usiku. Wangeweza pia kufurahia kupamba jiwe lao.

Kwa mawazo zaidi, ona toleo la mwezi huu la gazeti la Rafiki.

Mzoramu akisali juu ya Rameumptomu

Mioyo ya Wazoramu “iliinuliwa juu kwenye kujisifu sana, katika kiburi chao” (Alma 31:25).