Seminari na Vyuo
Alika Kujifunza kwa Bidii


“Alika Kujifunza kwa Bidii,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: Kwa Ajili ya Wote Wanaofundisha Nyumbani na Kanisani (2022)

“Alika Kujifunza kwa Bidii,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

Picha
Yesu akimvuta Petro kutoka maji yenye dhoruba

Mkamilishaji wa Imani, na J. Alan Barrett

Alika Kujifunza kwa Bidii

Hakika ilikuwa ya kuvutia sana kumwangalia Mwokozi akitembea juu ya maji. Lakini hiyo haikuwa ya kutosha kwa Petro. Yeye alitaka kufanya kile Mwokozi alichokuwa anafanya, kuwa pale alipo, na kupitia jambo lile yeye mwenyewe. “Niamuru nije kwako juu ya maji,” alisema. Mwokozi alijibu kwa mwaliko rahisi tu: “Njoo.” Kwa hilo, Petro aliruka kutoka kwenye usalama wa chombo na kutuonyesha sisi kwamba ufuasi siyo tukio la kukaa tu (ona Mathayo 14:24–33). Inahitaji imani katika Yesu Kristo na jitihada za bidii. Lakini pia huleta thawabu nyingi za kutembea pamoja na Mwokozi.

“Njooni.” “Njoo uone.” “Njoo, Unifuate.” “Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo” (Mathayo 14:29; Yohana 1:39; Luka 18:22; 10:37). Kutoka mwanzo wa huduma Yake, Mwokozi aliwaalike wafuasi Wake kujionea wao wenyewe kweli, nguvu, na upendo ambao Yeye aliutoa. Alifanya hili kwa sababu hii ndiyo kujifunza inachomaanisha. Sio tu kusikiliza au kusoma; pia ni kubadilika, kutubu, na kuendelea. Maneno ya Mwokozi, kujifunza huja kwa “kwa kujisomea na pia kwa imani” (Mafundisho na Maagano 88:118; msisitizo umeongezwa). Na imani inajumuisha kujitendea sisi wenyewe, siyo tu kutendewa (ona 2 Nefi 2:26).

Tunapofuata mfano wa Mwokozi, tunawaalika wale tunaowafundisha kuuliza, kutafuta, na kubisha—na ndipo wanapata (ona Mathayo 7:7–8). Na tunakubali mwaliko huo sisi wenyewe. Kwa pamoja, kupitia imani yetu katika Kristo na jitihadi ya bidii, tutakuja kujua wenyewe kile inachomaanisha kutembea pamoja na Yeye.

Kualika Kujifunza kwa Bidii

  • Wasaidie wanafunzi kuwajibika kwa kujifunza kwao wenyewe.

  • Wahimize wanafunzi kuja kumjua Mwokozi kwa kujifunza injili kila siku.

  • Waalike wanafunzi kujiandaa kujifunza.

  • Wahimize wanafunzi kushiriki kweli wanazojifunza.

  • Waalike wanafunzi kuishi kile wanachojifunza.

Mwokozi Aliwasaidia Wengine Kuwajibikaji kwa ajili ya Kujifunza Kwao

Kujenga mashua ambayo yangewavusha salama baharini ingekuwa kazi ngumu kwa kila mmoja. Kaka wa Yaredi “alielekezwa daima na mkono wa Bwana” (Etheri 2:6), kupokea maelekezo kuhusu umbo la vyombo hivyo na jinsi ambavyo vingepatiwa hewa. Lakini unagundua nini kuhusu Bwana alivyojibu wakati kaka wa Yaredi alipouliza kuhusu utoaji wa mwanga katika mashua hizo? (ona Etheri 2:22–25). Ni jinsi gani kaka wa Yaredi alibarikiwa kwa mwaliko wa kuitumia imani yake katika njia hii? (ona Etheri 3:1-16).

Inaweza kuonekana kuwa rahisi kuwaambia tu wanafunzi mambo yote unayofikiri wanafunzi wanapaswa kujua. Hata hivyo, Mzee Bednar alishauri: “Kusudio letu halipaswi kuwa ‘Je, niwaambie nini?’ Badala yake, swali la kujiuliza wenyewe ni ‘Ninaweza kuwaalike kufanya nini? Ni maswali gani yenye mwongozo wa kiungu ninaweza kuuliza, kama wako tayari kujibu, yataanza kumwalika Roho Mtakatifu katika maisha yao?’” (evening with a General Authority, Feb. 7, 2020, broadcasts.ChurchofJesusChrist.org).

Zingatia jinsi unavyoweza kuwaalika wanafunzi kuchukua jukumu la kujifunza wenyewe. Kwa mfano, ungeweza kuwaalika kuuliza maswali yao wenyewe, kutafuta majibu, kutafakari, na kushiriki au kuandika mawazo na hisia zao. Wanapofanya hivyo, wataimarisha imani yao, watagundua ukweli katika maneno ya Mungu, na watapata uzoefu wao wenyewe katika kweli hizi. Tunapowajibika kwa ajili ya kujifunza kwetu sisi wenyewe, tunaweza kusema, kama Joseph Smith alivyofanya, “Nimejua mimi mwenyewe” (Joseph Smith—Historia 1:20).

Maswali ya Kutafakari: Kwa nini ni muhimu kwa wanafunzi kujishughulisha kuliko kukaa tuli katika kujifunza kwao? Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia kuwajibika kwa ajili ya kujifunza kwao? Je, ni kwa namna gani walimu walikusaidia wewe kufanya hivi? Ni mifano gani kutoka katika maandiko unayofikiria ya watu walioalikwa kujifunza wenyewe? Mifano hii inaathiri vipi jinsi wewe unavyofundisha?

Kutoka katika Maandiko: 1 Nefi 11; Mafundisho na Maagano 9:7–8; 58:26–28; 88:118–125; Joseph Smith—Historia 1:11–20

Mwokozi Alihimiza Wengine Kuja Kumjua Yeye kwa Kujifunza Neno Lake

Wakati ulipofika wa Mwokozi kuunda rasmi Kanisa Lake katika siku za mwisho, aliwaambia watumishi Wake, “Tegemeeni mambo ambayo yameandikwa” (Mafundisho na Maagano 18:3). Ndiyo, Kitabu cha Mormoni, ambacho walikuwa wamekaribia kumaliza kukitafsiri, kilikuwa na maelekezo yenye msaada kwa ajili ya kazi, ikijumuisha jinsi ya kubatiza, jinsi ya kuhudumia sakramenti, na maelezo mengine muhimu. Lakini Mwokozi pia alitaka watumishi Wake kuona mafunuo Yake kama fursa ya kumsikia Yeye na kuja kumjua Yeye kwa kina zaidi. Katika ufunuo huo huo, Yeye aliwaambia, “Ni sauti yangu ndiyo inenayo [maneno hayo] kwenu; … kwa hiyo, mnaweza kushuhudia kwamba mmesikia sauti yangu na mnayajua maneno yangu” (Mafundisho na Maagano 18:35–36).

Fikiria kuhusu watu unaowafundisha. Wanaonaje kuhusu kujifunza maandiko? Kwa sababu hiyo, wewe unaonaje? Je, ni zaidi ya kazi ya siku moja? Unapojifunza maandiko, je, unahisi Mwokozi anasema nawe moja kwa moja? Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Ni wapi tunaweza kwenda kumsikiliza Yeye? Tunaweza kwenda kwenye maandiko. … Kuzama kila siku kwenye neno la Mungu ni muhimu kwa uhai wa kiroho, hasa katika siku hizi za ongezeko la mabadiliko ya ghafla. Tunaposherehekea katika maneno ya Kristo kila siku, maneno ya Kristo yatatuambia jinsi ya kukabiliana na ugumu ambao hatukutegemea kuukabili” (“Msikilize Yeye,” Liahona, Mei 2020, 89). Unapofundisha, wahimize wanafunzi kujisomea maandiko kwa lengo la kumpata Mwokozi—siyo tu kupata mistari au kweli kuhusu Yeye bali kumpata Yeye. Kusikiliza sauti ya Bwana kila siku katika maandiko ni ya msingi kwa bidii ya maisha yote, kujifunza injili kwa uhuru.

Maswali ya Kutafakari: Zingatia tabia zako mwenyewe za kujifunza maandiko. Jinsi gani kujifunza neno la Mungu kumeimarisha uhusiano wako na Yeye? Unaweza kufanya nini ili kuboresha kujifunza kwako? Ni kwa jinsi gani utawashawishi wengine kujifunza neno la Mungu kwa bidii na kila siku? Ni baraka zipi watapokea wanapofanya hivyo?

Kutoka kwenye Maandiko: Yoshua 1:8; 2 Timotheo 3:15–17; 2 Nefi 32:3; Yakobo 2:8; 4:6; Mafundisho na Maagano 33:16

Mwokozi Aliwaalika Wengine Kujiandaa Kujifunza

Hata mbegu bora zaidi haziwezi kukua kwenye ardhi ngumu, yenye mawe au miiba. Vivyo hivyo, mafundisho ya thamani kubwa na yenye kuhamasisha imani hayawezi kubadili moyo ambao haujaandaliwa kuyapokea. Hiyo ni sehemu ya ujumbe wa mfano wa Mwokozi kuhusu mpanzi, mbegu, na udongo wa hali tofauti tofauti. Ni katika “udongo mzuri”—moyo ambao umelainishwa na kuondolewa mawe ya kiroho na miiba—ndimo neno la Mungu hutoa matunda yenye kuleta uhai (ona Mathayo 13:1–9, 18–23).

Maaandalizi ya kiroho ni muhimu—kwako wewe na kwa watu unaowafundisha. Hivyo tunaiandaaje mioyo yetu ili iwe “ardhi nzuri” kwa ajili ya neno la Mungu? Fikiria kanuni hizi zifuatazo za maandalizi, ambazo unaweza kuzitumia katika maisha yako na kuzihimiza katika maisha ya wale unaowafundisha. Omba ili kujua kile Bwana anachotaka wewe ujifunze. Ishi katika namna ambayo inayoalika uwepo Wake katika maisha yako. Tubu kila siku. Kuza hamu yako ya kujifunza kwa kuuliza maswali ya dhati. Jisomee neno la Mungu kwa imani kwamba atakuongoza kwenye majibu ya maswali yako. Fungua moyo wako kwa lo lote atakalokufundisha.

Wanafunzi wanapojiandaa kujifunza katika njia hii, watakuwa na macho ya kiroho ya kuona na masikio ya kusikia kile Bwana angetaka wao wajue (ona Mathayo 13:16).

Maswali ya Kutafakari: Unafanya nini wewe ili kujiandaa mwenyewe kujifunza? Ni kwa jinsi gani maandalizi yako huathiri namna unavyoona, kusikia, na kuelewa neno la Mungu? Unawezaje kuwashawishi wengine kujiandaa kujifunza? Kuna tofauti gani inayoweza kufanya katika jinsi wanavyopokea kweli za injili?

Kutoka kwenye Maandiko: Enoshi 1:1–8; Alma 16:16–17; 32:6, 27–43; 3 Nefi 17:3

Picha
mtoto akisoma maandiko darasani

Wanafunzi wanafaidika kutokana na fursa za kushiriki na wengine kile wanachojifunza.

Mwokozi Aliwahimiza Wengine Kushiriki Kweli Walizokuwa Wakijifunza

“Mimi si mwepesi wa kusema,” Henoko alimlalamikia Bwana alipomwita kuhubiri injili. Lakini lugha ya kushawishi haijawahi kuwa sifa kwa mtumishi wa Bwana. Badala yake, Bwana alimwahidi Henoko kwamba kama angekuwa na imani ya kutosha kufungua kinywa chake, maneno yangetoka. “Nitakupa maneno,” Yeye alisema (Musa 6:31–32). Henoko aliitumia imani yake, naye Bwana alinena kupitia kwake, kwa maneno yenye nguvu ambayo yalisababisha watu kutetemeka (ona Musa 6:47). Kwa hakika, yalisababisha nchi kutetemeka yenyewe. Milima kukimbia, mito iligeuzwa uelekeo wake, na mataifa waliwaogopa watu wa Mungu, “neno la Henoko lilikuwa na nguvu sana, na lugha ambayo Mungu alimpa ilikuwa yenye nguvu kubwa” (Musa 7:13).

Bwana anataka sisi sote—sio tu manabii Wake—tuwe na nguvu ya kunena neno Lake. Yeye anataka hivyo kwa sisi sote, ikijumuisha watu unaowafundisha (ona Mafundisho na Maagano 1:20–21). Maneno yetu yawezekana yasihamishe milima au kuchepusha uelekeo wa mito, lakini yanaweza kubadili mioyo. Hiyo ndiyo kwa nini ni muhimu kuwapatia wanafunzi fursa kushiriki wao kwa wao kile wanchojifunza kuhusu Mwokozi na injili Yake. Kufanya hili kutawasaidia wao kufanya kweli wanazofundishwa kuwa zinawahusu na kuweza kuzielezea. Inaweza pia kuwasaidia kupata kujiamini katika uwezo wao wa kushiriki kweli katika mazingira mengine.

Maswali ya Kutafakari: Fikiria kuhusu wakati ulioongelea kuhusu ukweli wa injili na mtu mwingine. Umejifunza nini kutokana na uzoefu huo? Ni lini ulikuwa mwenye shukrani kwamba mtu amekuwa jasiri kushiriki mawazo na imani zao? Ni kwa jinsi gani watu unaowafundisha wananufaika kutokana na fursa ya kuzungumza kuhusu mambo wanayojifunza? Je,ni fursa gani unaweza kutengeneza kwa ajili yao?

Kutoka kwenye Maandiko: Alma 17:2–3; Moroni 6:4–6; Mafundisho na Maagano 84:85; 88:122; 100:5–8

Mwokozi Aliwaalika Wengine Kuishi Yale Aliyofundisha

“Nuru yenu na iangaze mbele ya watu.” “Wapendeni adui zenu.” “Ombeni, nanyi mtapewa.” “Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba.” Mathayo 5:16, 44; 7:7,13. Baadhi ya mialiko ya wazi, ya kukumbukwa katika huduma nzima ya duniani ya Mwokozi ilisemwa alipokuwa akiwafundisha wafuasi Wake upande wa mlima uangaliao Bahari ya Galilaya. Madhumuni ya Mwokozi ni kubadilisha maisha, kama yalivyofanywa wazi na mwaliko wake wa kufunga: “Basi kila asikiaye haya maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba” (Mathayo 7:24; msisitizo umeongezwa).

Mvua hunyesha na mafuriko kuja na pepo zinavuna katika maisha ya kila mtu. Kujifunza kuhusu injili haitoshi kama wanafunzi inawabidi kuyakabili majaribu watakayokabiliana nayo. Hii ndiyo kwa nini tunapaswa kutokusita kuwaalika wanafunzi kufikiria jinsi wanavyoweza kuishi kile wanachojifunza. Kutokana na kuheshimu haki ya kujiamulia ya watu wengine, mialiko yetu mingi itakuwa ya kawaida: “Je, unahisi kusukumwa kufanya nini?” Mara chache sana mialiko yetu yaweza kuhitaji kuwa mahususi: “Je, utachagua moja ya sifa za Mwokozi ambayo ungependa kuifanyia kazi?” Unapotoa fursa kwa wanafunzi kusikia, kutambua, na kushiriki misukumo kutoka kwa Roho Mtakatifu, Yeye atawafundisha hatua gani binafsi wanahitaji kuchukua. Wasaidie wanafunzi kufikiria baraka ambazo zitafuata wanapotenda juu ya kile wanachojifunza, na wahimize kuendelea hata wakati inapokuwa vigumu. Kuishi ukweli ni njia ya haraka zaidi kuelekea kwenye imani kubwa, ushuhuda, na uongofu. Kama Mwokozi alivyosema kuishi mafundisho ya Baba ndio njia kwetu sisi sote kujua kwa hakika mafundisho ni ya kweli (ona Yohana 7:17).

Maswali ya Kutafakari: Ni lini ulishawishika kutenda kwa sababu ya mwaliko uliopewa na mtu? Je, maisha yako yalibadilikaje kama matokeo yake? Tambua mialiko ambayo imetolewa katika maandiko na viongozi wa Kanisa. Unajifunza nini ambacho kinaweza kukusaidia kuwaalika wengine kutenda? Je, ni kwa njia zipi unaweza kufuatilia mialiko yako?

Kutoka kwenye Mandiko: Luka 10:36–37; Yohana 7:17; Yakobo 1:22; Mosia 4:9–10; Mafundisho na Maagano 43:8–10; 82:10

Baadhi ya Njia za Kutumia Kile Unachojifunza

  • Waombe wengine kuja wakiwa wamejiandaa kushiriki kitu ambacho Roho Mtakatifu amewafundisha, kama vile utambuzi kutoka kwenye kifungu cha maneno katika maandiko.

  • Wape wanafunzi fursa ya kufundisha sehemu ya somo.

  • Wahimize wanafunzi kurejelea video, andiko, au ujumbe kabla ya kukutana.

  • Shinda mtazamo wa wewe kujibu kila swali. Washirikishe wengine katika kutafuta majibu.

  • Kabla ya kushiriki utambuzi wako kuhusu andiko, waombe wanafunzi kushiriki utambuzi wao wenyewe.

  • “Uliza maswali yanayowahitaji wanafunzi kutafuta majibu katika neno la Mungu.

  • Waalike wanafunzi kuuliza maswali yao wenyewe kuhusu kile wanachojifunza.

  • Toa muda kwa wanafunzi wote kutafakari swali kabla kuwataka kushiriki majibu.

  • Fikiria kuwagawa wanafunzi katika makundi madogo madogo, kadiri inavyofaa.

  • Elezea matarajio wazi wazi ili kuwasaidia wanafunzi kukua.

  • Toa mialiko ambayo inawashawishi wanafunzi kujiboresha lakini sio wa kuwazidia. Fuatilia na waalike wanafunzi kushiriki uzoefu wao.

  • Wasaidie wanafunzi kujifunza kutoka kwenye maandiko kwa:

    • Kuwekea alama vifungu vyenye maana, kama wanahitaji.

    • Kualika ufunuo kupitia kutafakari na kwa sala.

    • Kuandika misukumo ya kiroho.

    • Tunza shajara ya kujifunzia.

    • Kuweka malengo ya kutendea kazi kile wanachojifunza.

Chapisha