Seminari na Vyuo
Fundisha kwa Roho


“Fundisha kwa Roho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: Kwa Ajili ya Wote Wanaofundisha Nyumbani na Kanisani (2022)

“Fundisha kwa Roho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

Picha
Mwokozi katika nyika ya Yudea

Kama vile Mwokozi alipotenga muda ili kujiandaa kiroho kwa Huduma Yake, sisi tunapaswa kujiandaa wenyewe kufundisha kwa Roho.

Fundisha kwa Roho

Mwokozi alipomwamuru Joseph Smith na Sidney Rigdon kuhubiri injili Yake, Yeye aliwaahidi, “Roho Mtakatifu angetolewa katika kutoa ushuhuda kwa vitu vyote mtakavyosema” (Mafundisho na Maagano 100:8; ona pia Mafundisho na Maagano 42:15–17; 50:17–22). Ahadi hiyo hiyo inatumika kwa wote wanaofundisha injili ikijumuisha wewe. Unapofundisha injili ya Yesu Kristo, unaweza kuwa na Roho Mtakatifu ili kukuongoza wewe na kushuhudia juu ya ukweli kwenye akili na mioyo ya wale unaowafundisha (ona Mafundisho na Maagano 8:2). Hauko peke yako wakati unapofundisha, kwani “sio wewe unayezungumza, bali ni Roho Mtakatifu” (Marko 13:11).

Roho Mtakatifu ni Mwalimu wa kweli. Hakuna mwalimu mwenye mwili wa kufa, hata kama ana ujuzi na uzoefu kiasi gani, anaweza kuchukua nafasi Yake katika kushuhudia juu ya ukweli, kushuhudia juu ya Yesu Kristo, na kuibadilisha mioyo. Lakini walimu wote wanaweza kuwa vyombo katika kuwasaidia watoto wa Mungu kujifunza kwa Roho.

Fundisha kwa njia ya Roho

  • Jiandae mwenyewe Kiroho.

  • Daima uwe tayari kujibu misukumo ya kiroho kuhusu mahitaji ya wanafunzi.

  • Tengeneza mazingira na fursa kwa ajili ya wanafunzi kufundishwa na Roho Mtakatifu.

  • Wasaidie wanafunzi kutafuta, kutambua na kutenda juu ya ufunuo binafsi.

  • Shuhudia kila mara, na kuwaalika wanafunzi kushiriki hisia zao, uzoefu wao na shuhuda zao.

Mwokozi Yeye Mwenyewe Alijiandaa Kiroho ili Kufundisha

Ili kujianda kwa ajili ya huduma Yake, Mwokozi alitumia siku 40 nyikani “ili kuwa na Mungu” (Tafsiri ya Joseph Smith, Mathayo 4:1 [katika Mathayo 4:1, tanbihi b]). Lakini maandalizi Yake ya kiroho yalianza kitambo kabla. Shetani alipomjaribu, Yeye alikuwa mwenye uwezo wa kutoa “maneno ya uzima” ambayo alikuwa ameyaweka kwenye hazina kwa ajili ya “saa ile” ambapo atayahitaji (Mafundisho na Maagano 84:85). Fikiria kuhusu jitihada zako mwenyewe za kujiandaa kiroho ili kufundisha. Je, unajifunza nini kutoka kwa Mathayo 4:1–11 kuhusu jinsi unavyoweza kufuata mfano wa Mwokozi katika maandalizi yako ya kiroho?

Roho ni mwalimu halisi na chanzo cha kweli cha uongofu. Ufundishaji injili wenye nguvu hauhitaji tu kuandaa somo lakini pia kujiandaa mwenyewe kiroho kabla hujaanza kufundisha. Kama umejiandaa kiroho, utakuwa mwenye kuweza vyema kusikiliza na kufuata mwongozo wa Roho unapofundisha. Njia ya kumwalika Roho Mtakatifu katika ufundishaji wako ni kumwalika Yeye katika maisha yako. Hii inajumuisha kujitahidi kufuata mfano wa Mwokozi na kuishi injili Yake kwa moyo wako wote. Na kwa kuwa hakuna ye yote kati yetu anayefanya hili kiukamilifu, inamaanisha pia kutubu kila siku.

Maswali ya Kutafakari: Inamaanisha nini kwako wewe kujiandaa mwenyewe kiroho ili kufundisha? Unahisi ushawishi wa kufanya nini ili kuboresha namna unavyojiandaa kiroho? Ni kwa jinsi gani unafikiri maandalizi ya kiroho yanaweza kufanya tofauti katika ufundishaji wako?

Kutoka kwenye maandiko: Ezra 7:10; Luka 6:12; Alma 17:2–3, 9; Mafundisho na Maagano 11:21; 42:13–14

Mwokozi Daima Alikuwa Tayari Kujibu juu ya Mahitaji ya Wengine

Yairo, mtawala wa sinagogi, alianguka miguuni pa Yesu, akimwomba amsaidie binti yake aliyekuwa mahututi. Yesu na wanafunzi Wake walikuwa wakitembea kwa shida kupitia mitaa iliyojaa watu kuekea nyumbani kwa Yairo wakati ghafla Yesu aliposimama. “Nani aliyenigusa?” Aliwauliza. Lilionekana kama swali la kizushi—katika umati mkubwa wa watu, ni nani ambaye hakuwa Anamgusa? Lakini Yesu alitambua kwamba katika umati ule, kuna mtu amemwendea akiwa na hitaji maalumu akiwa na imani ya kupokea uponyaji ambao Yeye alitoa. Bado kungekuwa na muda wa kumtembelea binti Yairo. Lakini kwanza akasema na yule mwanamke ambaye alikuwa amegusa mavazi Yake, “Binti, imani yako imekuponya; enenda zako na amani” (ona Luka 8:41–48).

Kama mwalimu, unaweza wakati mwingine kujikuta mwenyewe katika haraka za kukamilisha kitu fulani ulichojiandaa kufundisha. Wakati hicho chawezekana kuwa muhimu, uwe na uhakika kuwa katika hiyo haraka yako, wewe pasipo kukusudia unapita hitaji muhimu la mtu unayemfundisha. Katika ziada ya mwongozo wa kiroho uliotafuta ulipokuwa ukijiandaa kufundisha, tafuta pia kuongozwa na Roho wakati ukiwa unafundisha. Jaribu kuwa mwenye ufahamu wa mahitaji, maswali, na mapendeleo ya wanafunzi. Roho Mtakatifu anaweza kukusaidia kutambua jinsi mwanafunzi anavyopokea au kuelewa kitu ulichofundisha. Yeye anaweza kukupa msukumo, nyakati zingine, wa kubadilisha mipango yako. Kwa mfano, unaweza kuvutiwa kutumia muda zaidi kuliko ulivyokusudia juu ya mada au kuacha baadhi ya majadiliano kwa ajili ya baadae katika kupendelea kitu ambacho kina umuhimu zaidi kwa wanafunzi sasa.

Maswali ya Kutafakari: Ni lini ulihisi kwamba mzazi au mwalimu mwingine alijua juu ya mahitaji yako kama mwanafunzi? Je, wale unaowafundisha wanajua kwamba wewe unavutiwa zaidi katika kujifunza kwao kuliko kukamilisha somo? Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasiliana nao vyema kuhusu kuvutiwa kwako?

Kutoka kwenye Maandiko: 1 Petro 3:15; Alma 32:1–9; 40:1; 41:1; 42:1

Mwokozi Alitoa Fursa kwa Watu ili Wafundishwe na Roho Mtakatifu

Ilikuwa vigumu kwa wengi katika wakati wa Yesu kuelewa Yeye alikuwa nani hasa, lakini kulikuwa na maoni mengi. “Wengine wanasema wewe ni Yohana Mbatizaji,” Wanafunzi Wake waliarifu, “wengine, Elia; na wengine, Yeremia, au mmoja wa manabii.” Lakini kisha Yesu akauliza swali ambalo liliwaalika wanafunzi Wake kuweka kando maoni ya watu wengine na kutazama ndani ya mioyo yao wenyewe: “Ninyi mwasema Mimi ni nani? Yeye aliwataka kutafuta majibu siyo kutoka “nyama na damu” bali moja kwa moja kutoka kwa “Baba yangu aliye mbinguni. Ili kuwa aina hii ya ushuhuda—ufunuo binafsi kutoka kwa Roho Mtakatifu—ambao ulimwezesha Petro kutamka, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (ona Mathayo 16:13–17).

Ili kunusurika kiroho katika siku za mwisho, watu unaowafundisha wanahitaji ushahidi wa kiroho juu ya ukweli. Huwezi kuwapatia wewe, lakini unaweza kuwaalika, kuwatia moyo, kuwashawishi, na kuwafundisha kuutafuta. Unaweza kuweka wazi—kupitia mawazo yako na vitendo—jinsi gani Roho Mtakatifu alivyo muhimu katika kujifunza injili. Zingatia, kwa mfano, mazingira ya kujifunza unayotengeneza na kuhimiza. Kitu rahisi kama upangaji wa viti katika chumba au njia unayoamkiana na kuongea na wanafunzi inaweka toni ya kiroho kwa ajili ya uzoefu watakaopata wanafunzi. Unaweza pia kuwaalika wanafunzi kujiandaa wenyewe kiroho ili kujifunza, kama vile wewe unavyojiandaa kufundisha. Waombe wawajibike kwa ajili ya roho wanayemleta darasani. Na wewe unaweza kutoa fursa kwao kuhisi Roho akishuhudia juu ya Yesu Kristo na injili Yake. Ushuhuda huo utakuja kuwa “mwamba” kwao, na “milango ya kuzimu haitawashinda [wao]” (Mathayo 16:18).

Maswali ya Kutafakari: Je, umegundua nini ambacho kinachangia mazingira ya kiroho kwa ajili ya kujifunza injili? Ni nini kinavuruga? Ni kitu gani kinawasaidia watu unaowafundisha kujifunza kutokana na Roho? Fikiria kuhusu mazingira ambamo wewe karibia mara nyingi unafundisha. Unahisi vipi unapokuwa hapo? Ni kwa jinsi gani unaweza kwa tija zaidi kumwalika Roho awepo hapo?

Kutoka kwenye Maandiko: Luka 24:31–32; Yohana 14:26; 16:13–15; Moroni 10:4–5; Mafundisho na Maagano 42:16–17; 50:13–24

Picha
wamisionari wakifundisha familia

Tunapofundisha, tunaweza kuwaalika wanafunzi kutafuta ushuhuda wao wa kiroho juu ya ukweli.

Mwokozi Aliwasaidia Wengine Kutafuta, Kutambua, na Kufanyia Kazi Ufunuo Binafsi

Bwana anataka kuwasiliana na sisi—na anataka tujue kwamba Yeye anawasiliana na sisi. Katika mwaka 1829, mwalimu wa shule mwenye umri wa miaka 22 aliyeitwa Oliver Cowdery alikuwa anajifunza kuhusu mafundisho thabiti, ya kusisimua kwamba mtu ye yote anaweza kupokea ufunuo binafsi. Lakini alikuwa na maswali sawasawa na yale wengi wetu tumejiuliza: “Je, Bwana hakika anajaribi kuongea na mimi? Je, ninawezaje kujua kile Yeye anachosema? Ili kujibu maswali haya, Yesu Kristo alimwalika Oliver Cowdery kufikiria nyuma wakati alikuwa na maswali ya udadisi wa kiroho. “Sikusema amani akilini mwako kuhusiana na jambo hili?” Yeye aliuliza (ona Mafundisho na Maagano 6:21 -24. Baadae, Yeye alimfundisha Oliver kuhusu njia nyingine Roho anavyoweza kusema naye (ona Mafundisho na Maagano 8:2–3; 9:7–9; ona pia Mafundisho na Maagano 11:12–14).

Kuishi katika ulimwengu ambao mara nyingi hautambui mambo ya kiroho, sisi sote tunahitaji msaada wa kutambua sauti ya Roho. Yawezekana tumewahi kumsikia Roho pasipo sisi kutambua. Na sisi sote tunaweza kujifunza zaidi kuhusu jinsi ya kumtafuta Roho, kutambua ushawishi Wake, na kufanyia kazi misukumo Yake anayotupatia. Unapofundisha, wasaidie wanafunzi kugundua njia ambazo Roho anaweza kuwasiliana—na jinsi ambavyo Yeye amewasiliana nao. Moja ya zawadi kubwa zaidi unayoweza kutoa kama mwalimu ni kuwasaidia wale unaowafundisha kuendelea katika safari hii ya utafutaji wa ufunuo binafsi.

Maswali ya Kutafakari: Kwa nini ni muhimu kujifunza kupokea ufunuo binafsi? Je, kuna mtu ye yote amekusaidia kuelewa jinsi ya kutafuta na kutambua ufunuo? Unawezaje kuwahimiza wale unaowafundisha kutafuta, kutambua na kutenda juu ya ufunuo kutoka kwa Roho Mtakatifu?

Kutoka kwenye Maandiko: Wagalatia 5:22–23; Alma 5:45–47; Mafundisho na Maagano 42:61; 121:33; Joseph Smith—Historia ya 1:8–20

Mwokozi Alitoa Ushuhuda kwa Wale Aliowafundisha

Katika wakati mahususi sana wa kufundisha na kuhudumia, Yesu alitafuta kumfariji rafiki Yake Martha, ambaye kaka yake alikuwa amefariki. Alishiriki naye ushuhuda rahisi juu ya ukweli wa milele: “Ndugu yako atafufuka” (Yohana 11:23). Ushuhuda Wake ulimsukuma Martha naye kutoa ushuhuda wake mwenyewe: “Ninajua kwamba atafufuka katika siku ya mwisho” (Yohana 11:24). Angalia jinsi mpangilio huu unavyorudia katika Yohana 11:25–27. Nini kinachokuvutia kuhusu mfano wa Mwokozi? Kwa nini kushiriki ushuhuda juu ya ukweli wa injili ni sehemu muhimu hivi ya kufundisha?

Ushuhuda wako unaweza kuwa na ushawishi wenye nguvu kwa wale unaowafundisha. Hauhitaji kuwa wa lugha tamu au mrefu. Na hauhitaji kuanza na “Ningependa kutoa ushuhuda wangu.” Kwa urahisi kabisa shiriki kile unachojua kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Ushuhuda juu ya ukweli unakuwa na nguvu zaidi unapokuwa wa moja kwa moja na wa kutoka moyoni. Toa ushuhuda mara kwa mara juu ya Mwokozi, injili Yake, na nguvu Yake katika maisha yako, na wahimize wale unaowafundisha kufanya vivyo hivyo. Na kumbuka kwamba wakati mwingine ushuhuda wenye nguvu zaidi hautolewi na mwalimu bali na mwanafunzi mwenzao.

Maswali ya Kutafakari: Tafuta mifano katika maandiko ambayo inafafanua ushawishi wenye nguvu wa mtu mwenye kutoa ushuhuda. Je, unajifunza nini kutoka katika mifano hiyo? Je, ni lini umebarikiwa kutokana na ushuhuda wa mtu? Ni kwa jinsi gani kushiriki ushuhuda wako kuliwashawishi wale unaowafundisha? Hayo yamekuchawishi kivipi?

Kutoka kwenye Maandiko: Matendo ya Mitume 2:32–38; Mosia 5:1–3; Alma 5:45–48; 18:24–42; 22:12–18; Mafundisho na Maagano 46:13–14; 62:3

Baadhi ya Njia ya Kutumia Kile Unachojifunza

  • Waombe wanafunzi washiriki kile Roho Mtakatifu alichowafundisha walipojifunza neno la Mungu.

  • Jiandae mapema kupokea misukumo ya kiroho wakati ukifundisha.

  • Andika mawazo ya kiroho yanayokujia wakati unapojiandaa.

  • Toa fursa mara chache kwa washiriki wa darasa kukaa kimya huku wakitafakari kile Roho anachowafundisha.

  • Tumia muziki mtakatifu na picha ili kualika ushawishi wa Roho.

  • Sikiliza misukumo unapopanga na unapofundisha, na uwe tayari kurekebisha mipango yako.

  • Toa fursa kwa wanafunzi wote kutoa ushuhuda wao wa kile wanachojifunza.

  • Wasaidie wengine kutambua wakati Roho anapokuwepo.

  • Ishi kweli unazofundisha ili kwamba uweze kuzitolea ushuhuda.

  • Fuata misukumo ya kufundisha katika nyakati zinazojitokeza zenyewe, na zisizopangwa.

Chapisha