“Kwa Ajili ya Viongozi—Kuwasaidia Walimu Wafanikiwe,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: Kwa Ajili ya Wote Wanaofundisha Nyumbani na Kanisani (2022)
“Kwa ajili ya Viongozi—Kuwasaidia Walimu Wafanikiwe,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi
Kwa ajili ya Viongozi—Kuwasaidia Walimu Wafanikiwe
Kuchangamana na mtu mmoja mmoja
Mara nyingi njia bora ya kukidhi mahitaji ya kipekee ya walimu ni kuchangamana na mtu mmoja mmoja. Kwa mfano, kama kiongozi, ungeweza kuwa na majadiliano ya muda mfupi na mwalimu kabla au baada ya darasa ili kujadili kanuni za Kufundisha Katika Njia ya Mwokozi. Ungeweza kujiandaa kwa majadiliano haya kwa kumwangalia mwalimu akifundisha. Tafuta kuelewa vyema nguvu ya mwalimu na gundua jinsi unavyoweza kumpatia msaada.
Kujenga juu ya nguvu za mwalimu ni muhimu kama ilivyo kutambua fursa za kuboresha. Ni ya msaada kuanza majadiliano na walimu kwa kuwaomba wao wenyewe wafikirie kile kinachoenda vyema na wapi wanadhani maboresho yanaweza kufanyika.
Unapokutana na walimu, fikiria njia za kuwaimarisha na kuwatia moyo kwa ukarimu na shukrani kwa ajili ya huduma wanayoitoa.
Mikutano ya Baraza la Walimu
Kila kata inapaswa kuwa na mikutano ya baraza la walimu kila robo ya mwaka ambapo walimu wanaweza kushauriana pamoja kuhusu kanuni za kufundisha kama Kristo. Mikutano ya baraza la walimu inaweza pia kufanyika kwa ajili ya wazazi (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 13.5, ChurchofJesusChrist.org).
Ni Wakati Gani Mikutano Hii Inapaswa Kufanyika?
Mikutano ya baraza la walimu inafanyika wakati wa darasa la dakika 50 katika ratiba ya Jumapili.
-
Walimu wa Ukuhani, Muungano wa Usaidizi, na Wasichana wanaweza kuhudhuria mojawapo ya Jumapili ya kwanza au ya tatu, kama itakavyoamuliwa na viongozi wenyeji.
-
Walimu wa Shule ya Jumapili wanaweza kuhudhuria mojawapo ya Jumapili ya pili au ya nne, kama itakavyoamuliwa na viongozi wenyeji.
-
Walimu wa Watoto wanaweza kuhudhuria Jumapili yoyote, kama itakavyoamuliwa na urais wa Watoto na wa Shule ya Jumapili katika kata. Ikiwa itapendekezwa, Walimu wa Darasa la Watoto wanaweza kukutana tofauti na walimu wengine ili washauriane kuhusu mahitaji ya kipekee ya watoto wanaowafundisha. Hii inaweza kutokea wakati wa dakika 20 za muda wa kuimba, kabla au baada ya mikutano ya kila Jumapili, au katika siku nyingine ya wiki. Zaidi ya mkutano mmoja wa baraza la walimu inaweza kufanyika katika robo mwaka kwa ajili ya walimu wa Watoto, ili kwamba wote wasikose madarasa ya Watoto katika wiki hiyo. (Kumbuka: Kama itakavyohitajika, urais wa Darasa la Watoto huwateua walimu mbadala, huunganisha madarasa, au kufanya mipango mingine ili kuwaruhusu walimu wa Watoto kuhudhuria mikutano ya baraza la walimu.)
-
Mikutano ya baraza la walimu kwa ajili ya wazazi inaweza kufanyika Jumapili yoyote, kama itakavyoamuliwa na baraza la kata.
Ni Nani Anapaswa Kuhudhuria?
Kila mtu anayefundisha akidi au darasa katika kata anapaswa kuhudhuria, pamoja na angalau mmoja wa viongozi wa ukuhani au kikundi walio na wajibu juu ya akidi au madarasa hayo. Kama itabidi, washiriki wanaweza kugawanywa katika vikundi kulingana na mahitaji ya wale ambao wanawafundisha. Kwa mfano, walimu wa vijana au watoto wanaweza kunufaika kwa kukutana peke yao mara kadhaa ili kujadili maswala ambayo ni mahususi ya kuwafundisha vijana au watoto.
Kwa ajili ya mikutano ya baraza la walimu kwa ajili ya wazazi, baraza la kata linaamua kama linawaalika wazazi mahususi au kuweka mahudhurio wazi kwa yeyote anayetaka kushiriki.
Ni Nani Huongoza Mikutano Hii?
Baraza la kata, likiwa na usaidizi kutoka kwa urais wa Shule ya Jumapili, husimamia mikutano ya baraza la walimu. Wanashauriana pamoja kuhusu mahitaji ya walimu na wanafunzi kutokana na kile walichokiona katika darasa na katika mikutano. Wanafanya kazi pamoja kuamua ni kanuni gani na desturi zipi kutoka katika Kufundisha katika Njia ya Mwokozi zitakidhi vyema mahitaji waliyoyaona.
Kwa kawaida, mshiriki wa urais wa Shule ya Jumapili, huongoza mikutano ya baraza la walimu. Hata hivyo, washiriki wengine wa kata wanaweza kupangiwa kuongoza mikutano hiyo mara moja moja. Urais wa akidi na kikundi husisitiza pamoja na walimu wao kanuni na desturi zilizojadiliwa katika mkutano.
Ni Nini Kinapaswa Kutendeka katika Mkutano wa Baraza la Walimu?
Mkutano wa baraza la walimu unapaswa kufuata utaratibu huu:
-
Shirikini na mshauriane pamoja. Waalike walimu waelezee uzoefu wa kufundisha wa hivi karibuni, uliza maswali yanayohusiana na kufundisha, na toa mawazo juu ya kushinda changamoto. Sehemu hii ya mkutano inaweza kujumuisha marejeo ya kanuni zilizojadiliwa katika mikutano iliyopita.
-
Jifunzeni pamoja. Waalike walimu kujadili mojawapo ya kanuni zifuatazo zilizowasilishwa katika nyenzo hii: fokasi juu ya Yesu Kristo, wapende wale unaowafundisha, fundisha kupitia Roho, fundisha mafundisho, na alika kujifunza kwa bidii. Kanuni zinaweza kushughulikiwa kwa mpangilio wowote, na isipokuwa ielekezwe vinginevyo na baraza la kata, washiriki katika mkutano wanaweza kuchagua kanuni itakayojadiliwa. Unaweza kutumia mkutano zaidi ya mmoja ili kujadili kanuni moja ikiwa itabidi kufanya hivyo.
-
Panga na ualike. Wasaidie walimu wapange namna watakavyozitumia kanuni walizozijadili. Kama itafaa, mngeweza pia kufanyia mazoezi pamoja ujuzi mlioujadili. Waalike waandike na watende juu ya misukumo yoyote ambayo wanapokea kuhusu jinsi ya kutumia kanuni katika kufundisha kwao—ikiwa ni pamoja na juhudi zao katika kufundisha majumbani mwao. Wahimize waanze kusoma kanuni inayofuata itakayojadiliwa.
Kadiri iwezekanavyo, mikutano ya baraza la walimu inapaswa kuwa mfano wa kanuni ambazo zinajadiliwa.
Kuwaelekeza Walimu Wapya Walioitwa
Kama kiongozi, unalo jukumu la “kukutana na walimu wapya walioitwa” katika kikundi chako na “kuwasaidia wajiandae kwa ajili ya miito yao” (Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 17.3, ChurchofJesusChrist.org). Mikutano hii ni fursa ya kuwatambulisha walimu wapya kwenye miito yao mitakatifu na kuwahamasisha kwa ono la kile inachomaanisha kufundisha katika njia ya Mwokozi. Kama kiongozi, unaweza kuwasaidia walimu wapya wajiandae kutumikia kwa kufanya mambo yafuatayo:
-
Elezea ujasiri kwamba Mwokozi atawasaidia katika wito wao (ona Mafundisho na Maagano 88:78).
-
Wape walimu wapya nakala ya nyenzo hii, na watie moyo watafute njia za kutumia kanuni zake katika kufundisha.
-
Shiriki na walimu wapya kitu chochote kuhusu kikundi chako ambacho kitakuwa msaada kwao kujua.
-
Kadiri inavyohitajika, waambie walimu wapya ni chumba gani watakachotumia kufundisha na somo watakaloanza nalo. Toa taarifa yoyote wanayohitaji kuhusu darasa na washiriki wa darasa.
-
Waelezee walimu wapya kwamba unaweza kuwasaidia katika wito wao. Toa msaada darasani na kwa upatikanaji wa nyenzo kama itahitajika.
-
Jitolee kuangalia darasa la mwalimu mara kwa mara, na toa mrejesho kadiri utakavyoongozwa na Roho.
-
Waalike walimu washiriki katika mikutano ya robo mwaka ya baraza la walimu.