2021
Ina maana gani kumpenda Mungu kwa moyo wako wote?
Septemba/ Oktoba 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Ina maana gani kumpenda Mungu kwa moyo wako wote?

Jibu ni rahisi sana na rahisi kikamilifu. Yesu Kristo alifundisha: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.”

Ina maana gani kupenda kitu au mtu kwa moyo wako wote?

Miaka mingi iliyopita, niliona maana ya upendo kwa wenzi, Keith na Geneva, ambao walionesha kwa mfano upendo wao kwa kila mmoja kwa zaidi ya miaka 56 ya ndoa. Ndoa yaweza kuleta shangwe nyingi. Katika maagano binafsi ya kina ya ndoa, inaweza pia kutoa fursa adhimu ya kutoa msaada kwa kila mwenzi katika kipindi cha magonjwa au jaribu. Kwa Keith na Geneva, upendo wao kwa kila mmoja ulijaribiwa baada ya miaka 27 ya ndoa na watoto sita.

Katika umri wa miaka 52, Geneva alipatikana na matatizo kadhaa ya ubongo na uti wa mgongo (multiple sclerosis [M.S.]), ugonjwa wa kuzorotesha neva ambao ulichukua uwezo wa Geneva wa kukimbia, kudansi na hatimaye hata kutembea au kusimama. Mchongaji mwenye talanta na msanii, alipoteza uwezo wa kutumia mikono yake kuchonga. Kutokana na asili ya uzoroteshaji ya ugonjwa, kiwango cha talaka ni kikubwa kati ya wenzi ambao mmoja wa mwenzi amepatikana na M.S. Geneva kwa ujasiri alipambana na ugonjwa kwa miaka 29. Moja ya sababu za Geneva kuweza kuishi na ugonjwa kwa ujasiri kama huo ilikuwa matunzo endelevu, ya kujitolea ya mume wake, Keith. Keith alimthamini mke wake kipenzi. Alimpenda kwa moyo wake wote. Alifanya mabadiliko katika nyumba yao ili kufanya mambo yawe rahisi kwa Geneva. Alirekebisha ratiba yake ili kukidhi mahitaji ya mkewe. Alisimama pamoja naye kipindi chote cha miadi yake ya dawa na tiba. Alimjali kwa uaminifu na kwa mfano kadiri ugonjwa ulipoendelea katika mwili wake. Aliishi kuyafanya maisha ya mkewe kuwa uzoefu wa shangwe, licha ya kuendelea kwa ugonjwa.

Kamusi ya Urban inatoa maana ya upendo kama “tendo la kujali na kutoa kwa mtu mwingine. Kuwa na mapendeleo bora na ustawi wa mtu fulani kama kipaumbele katika maisha yako.”

Tunapompenda mtu fulani kwa mioyo yetu yote, tunawaweka kuwa kipaumbele katika maisha yetu. Tunawapa muda, nguvu, talanta na rasilimali zetu.

Yesu Kristo alifundisha ukweli huu wa milele:

“Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi.

Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.

Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo.” (Yohana 15:12–14)

Kristo hakika alionesha upendo Wake kwa kila mmoja wetu kwa kuyatoa maisha Yake kwa ajili ya rafiki Zake. Lakini pia alionesha upendo Wake kwetu kwa jinsi Yeye alivyoishi kwa ajili yetu. Alitoa muda Wake ili kujifunza kila moja ya nguvu zetu na udhaifu wetu binafsi, mafanikio yetu na dhambi zetu. Kama Mwalimu Mkuu, Yeye alitupatia maneno Yake na mafundisho Yake ili yatuongoze katika njia za kweli na haki ili kusaidia kutuongoza kila siku ikiwa tutamfuata Yeye. Katika dhabihu Yake kuu ya upatanisho, Yeye kwa hiyari aliyatoa maisha yake ili kwamba tuweze siku moja kufufuka na kupata shangwe ya kutokufa. Yeye pia alijichukulia juu Yake dhambi zetu na maumivu yetu na masumbuko yetu (Ona Alma 7:11–14), kwa ahadi kwamba tunaweza kuwa wasafi mbele za Mungu kwa vigezo vya toba.

Yesu Kristo alikufa kwa ajili yetu na Aliishi kwa ajili yetu. Yeye hakika anatupenda.

Kama malipo, ni jinsi gani tunaonesha upendo wetu Kwake na kwa Baba yetu wa Mbinguni ambaye alimtuma Mwana Wake Mpendwa ili kutuokoa kutokana na kifo na dhambi? Hatutakiwi kufa kwa ajili Yake, lakini tunatakiwa kuishi kwa ajili Yake. Tunafanyaje hilo?

Jibu ni rahisi sana na rahisi kikamilifu. Yesu Kristo alifundisha: “Mkinipenda, mtazishika amri zangu.” (Yohana 14:15)

Kumpenda Mungu kwa mioyo yetu yote, tunatumia muda, nguvu, talanta na rasilimali zetu kutunza amri Zake.

Ninakualika kupata taswira juu ya jinsi unavyotumia muda, nguvu, talanta na rasilimali zako. Je unatumia muda wako kujifunza amri za Mungu ni nini, ili uweze kuzitii?

Ni jinsi gani unatumia nguvu zako? Wakati ni muhimu kufanya kazi na kukimu mahitaji yako na mahitaji ya wale unaowapenda, je unatunza nguvu za kutosha kutii amri za Mungu—mkihudhuria Kanisani mara kwa mara siku ya Sabato na kuwahudumia wanadamu wenzako? Je, unatumia talanta na rasilimali Mungu alizokupa ili kutii amri Zake na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo? Unapofikiria yale yote Mungu aliyofanya kwa ajili yako na upendo Aliokuonesha, ninakusihi kupata taswira ya jinsi unavyoonesha upendo wako Kwake kama malipo.

Kadiri nilivyotazama upendo kati ya Keith na Geneva ukistawi na kuongezeka kwa miaka mingi na majaribu mengi, kwa shauku nilitazamia kuona shangwe kubwa watakayopata wakiwa na miili iliyofufuka na kuendelea katika maisha yao na ndoa yao pamoja kote katika umilele, huru kutokana na ugonjwa na maumivu ya mwili. Walipendana kwa mioyo yao yote.

Wakati kila mmoja wetu binafsi tunaonesha upendo wetu kwa Mungu kwa kutumia muda, nguvu, talanta na rasilimali zetu kutii amri Zake, ninashuhudia kwamba tutakuwa zaidi kama Mungu. Tutajisikia vizuri katika uwepo Wake. Tutakuwa na shangwe kuu katika miili yetu iliyofufuka. Na kupitia toba, sisi, pia, tunaweza kuwa na shangwe ya milele, maisha ya Mungu, na maisha yaliyojaa upendo. Na tuoneshe kuwa tunampenda Mungu kwa mioyo yetu yote kwa kutii amri Zake kwa muda wetu, nguvu, talanta na rasilimali zetu zote.

Katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Matthew L. Carpenter aliitwa kama Sabini Mkuu mwenye Mamlaka mnamo Machi 2018. Amemuoa Michelle (Shelly) Kay Brown; wao ni wazazi wa watoto watano.