2021
Kuonyesha Upendo Wetu kwa Bwana Kupitia Huduma
Septemba/ Oktoba 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA UKUHANI

Kuonyesha Upendo Wetu kwa Bwana Kupitia Huduma

Upendo wetu kwa Bwana huonyeshwa kupitia upendo wetu na huduma yetu kwa majirani zetu.

Biblia inatueleza kwenye Kitabu cha Mathayo kwamba mwanasheria alimuuliza Yesu swali la kumjaribu. Alimwuliza ni ipi ilikuwa amri kuu katika torati. Yesu alijibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza” (Mathayo 22:37–38).

Upendo kwa Mungu humaanisha upendo kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye Yesu Kristo. La kuvutia ni kwamba, Yesu alisema mahususi kwamba tunapaswa kuwapenda Wao “kwa mioyo [yetu] yote”. Moyo ndio hazina ya hisia za mwanadamu na ni dhahiri kwamba Bwana anataka upendo wetu utokee moyoni; utokee ndani. Anajua kwamba wakati mwingine tunaelezea upendo wetu kwa maneno na matendo, lakini hakusema kwamba tumpende Yeye kwa maneno yetu yote bali kwa moyo wetu wote. Njia mojawapo tunayoonyesha upendo kwa Bwana ni kwa kushika amri Zake. Alisema, “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15).

Baba yetu wa Mbinguni ameonyesha upendo Wake kwetu kwa kumtoa Mwanaye wa Pekee kama dhabihu. Kama watoto Wake, Yeye hataki tuonyeshe upendo wetu kwa ajili Yake kwa kutoa dhabihu kama alivyofanya Yeye. Bali, Anatutaka tuwe tayari kufanya kile ambacho Yeye anatuamuru. Kile Anachotuamuru sisi tufanye ni kufuata mfano wa Mwanaye Yesu kristo, kutii amri Zake na kuwapenda na kuwahudumia majirani zetu. Mzee Jeffrey R. Holland alifundisha, “Kwa hiyo tunao majirani wa kuwabariki, watoto wa kuwalinda, maskini wa kuwainua . . .

Tuna mabaya ya kusahihisha . . . na mazuri ya kufanya. Kwa ufupi, tuna maisha ya ufuasi wa dhati ya kutoa katika kuonyesha upendo wetu kwa Bwana.”1

Katika hubiri lake, Mzee Holland anatuomba kila mmoja wetu kupata taswira tukiwa mbele ya kiti cha hukumu, tukijaribu kujibu swali la Bwana: ‘Je, ulinipenda?’ Katika mtiririko huo huo, najaribu kufikiria mazungumzo ya Yesu akiwa na Simoni Petro kama vile yuko pamoja nami: ‘Je, wanipenda? Je, wanipenda hata wakati unapopitia majaribu? Je, wanipenda kwa kuwapenda na kuwahudumia wengine?’

Katika Mathayo 25, tunajifunza kwamba wakati Mwana wa mtu atakapokuja katika utukufu wake, Atawaweka kondoo mkono wake wa kuume kwa sababu ya matendo yao yote mema Kwake. Kisha wenye haki watamwuliza ni lini walifanya mambo haya yote na Yeye atajibu, “kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.”2 Upendo wetu kwa Bwana hudhihirishwa katika upendo na huduma kwa majirani zetu.

Mzee Gerrit W. Gong alisema kwamba “wadogo hawa” ni kila mmoja wetu.3 Kwa hakika, kuna wale wanaotuzunguka ambao huonekana kuwa wadogo wa wadogo: hawa ni watoto wadogo ambao hawawezi kujilinda, wazee ambao wamepoteza uwezo wao wa kujihudumia wenyewe, marafiki na wanafamilia ambao kwa namna moja au nyingine hawawezi kukidhi mahitaji yao ya kiroho, kimwili na wanahitaji msaada wetu.

Tunapompenda Mungu ambaye hatumwoni kwa macho yetu ya kibinadamu, tunatafuta fursa za kuwapenda na kuwatendea mema majirani zetu tunaowaona. Ninashuhudia kwamba mimi binafsi nimebarikiwa na kupata shangwe kila siku wakati ninapomfikia “mmoja wa wadogo hawa”.

Wakati mwingine, matendo ya kawaida kama ujumbe mfupi wa kupongeza, neno la kutia moyo, na kumsikiliza mtu mwenye mahitaji huleta tofauti.

Hivi karibuni kaka mmoja ambaye nilikutana naye nilipokuwa nikihudumu kama rais wa kigingi miaka kadhaa iliyopita alinitumia barua pepe. Aliandika: “Kila neno lako limenisaidia kurudi kwenye njia na pia kunipatia mawazo mapya ambayo yameniletea miujiza na baraka kubwa na kunifanya kuwa mtu mwema kuliko nilivyokuwa mwanzo. Asante kwa upendo wako na kujali kwako katika kumuimarisha kaka wa kawaida kama mimi . . . Upendo ulionionyesha umenisaidia kujifunza na kuendelea kujifunza. Mimi sasa ni mshiriki wa Urais wa Akidi ya Wazee, mwenye nia na niliyejitolea kwenye kazi katika kitengo changu; mimi ni mume mtarajiwa mwenye upendo ambaye [karibuni] nitaunganishwa katika hekalu Takatifu mbele ya Baba yangu wa Mbinguni.”

Nina shukrani kwa baraka nyingi za thamani nilizopokea mimi binafsi na katika familia yangu kupitia matendo madogo tulivu ya huduma kwa majirani zetu. Basi kila mmoja wetu na aitikie wito wa kumpenda Mungu na Mwanaye Yesu Kristo kwa mioyo yetu yote kwa kushika amri Zake na kutafuta fursa za kuwapenda na kuwahudumia wengine.

Eustache Ilunga alitajwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2018. Yeye na mkewe, Mamie, ni wazazi wa watoto wanne. Mzee na Dada Ilunga wanaishi Kinshasa, katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Muhtasari

  1. Jeffrey R. Holland, “The First Great Commandment”, Liahona, Nov. 2012, 84–85.

  2. Mathayo 25:40.

  3. Gerrit W. Gong, “Room in the Inn”, Liahona, May 2021, 25.