SAUTI ZA WAUMINI
Kujifunza Maandiko na Mawazo Yangu juu ya Wezi
“Wewe ungelipaswa kuwa mwaminifu; na yeye angelikunyooshea mkono wake na kukutegemeza dhidi ya mishale ya moto ya adui”.1
Hivi karibuni nilikuwa nikipanga kuhama kutoka Mtaa wa Mtwivila na kuingia katika nyumba mpya huko Ikonongo nyumba chache kutoka nilikokuwa nikiishi katika nchi yangu ya Tanzania. Siku chache tu baada ya kulipa kodi yangu ya nyumba ya mwezi wa kwanza, nilianza kusikia hadithi kuhusu wezi. Mama mmoja mlango unaofuata kutoka wangu alinieleza kuhusu jinsi simu yake ya mkononi ilivyoibiwa siku chache zilizopita. Hadithi hizo zilinifanya nisijisikie vizuri na nilifikiria pengine halikuwa wazo zuri kwa mimi kuhamia. Mawazo ya woga yaliendelea kusikika akilini mwangu, kwa kiasi ambacho yalivuruga na kuharibu kujisomea kwangu maandiko kila siku.
Baada ya kukabiliana na hili kwa siku kadhaa, nilichagua kushikilia ratiba yangu na kuendelea kujisomea kwangu Maandiko na Maagano. Wakati nikisoma sehemu ya tatu, akili yangu ilinasa kwenye msatari wa 7 na 8 ambapo Bwana alimwonya Joseph Smith baada ya kumpatia Martin Harris zile kurasa 116 za muswada. Na hatimaye kurasa zile zikapotezwa. Tunajua kwamba Joseph Smith kwa sehemu kubwa alikuwa akitegemea sana msaada wa huyu rafikiye Martin Harris, na kwa sababu hiyo alikuwa na shauku kubwa ya kukidhi maombi ya rafikiye. Kwa sababu hiyo, Bwana alimwambia Joseph Smith: “Kwani Tazama, haungepaswa kumwogopa mwanadamu Zaidi kuliko Mungu . . .
Wewe ungelipaswa kuwa mwaminifu; na Yeye angelikunyoshea mkono wake na kukutegemeza dhidi ya mishale ya moto ya adui; na yeye angelikuwa pamoja na wewe katika wakati wote wa matatizo.”2
Hakikisho hilo liliyeyusha woga wangu wote na nikatambua kwamba nimepoteza muda wangu mwingi wa thamani nikijaribu kufikiria kuhusu kitu wezi wanachoweza kunifanyia mimi niwapo katika makazi mapya badala ya kutumaini katika kitu ambacho Bwana anaweza kukifanya kwa ajili yangu mimi. Wazo la wazi kabisa lilinijia kwamba ninachohitaji kufanya ni kutimiza sehemu yangu katika kufunga madirisha na mlango usiku, na kisha nishike amri za Mungu na Yeye angenipatia amani na ulinzi katika makazi yangu mapya.
Ninafurahi kwamba nilichagua kujisomea maandiko yangu. Suluhisho la mashaka yangu lilikuwa hapo likinisubiri: kufanyia kazi mwaliko wa Nabii wa kujisomea maandiko kila siku. Ninashukuru sana kwa wenza wa Roho Mtakatifu ambaye aliangaza akili yangu ili kuelewa ule ukweli wa thamani kutoka katika Mafundisho na Maagano.
Hatimaye nilihamia, na yote yamekuwa mema kadiri ninavyoendelea kutimiza sehemu yangu na kuacha Bwana afanye Yake. Amani, utulivu na faraja ambayo naipokea kutokana na kujisomea kwangu maandiko kila siku inanifanya niendelee kusonga mbele na kuongeza imani yangu kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Yesu Kristo.
Magreth Ayo Nyambita ni muumini wa Kanisa tawi la Mwanza katika Tanzania.