Mwezi Huu katika Historia ya Kanisa
Machi 1842: Hisani Haishindwi Kamwe
Miaka 180 iliyopita, Muungano wa Usaidizi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ulianzishwa mnamo tarehe 17 Machi 1842. Ulianzishwa ili kwamba wanawake wangeweza kukusanya rasilimali zao na kuunganisha juhudi zao ili kuweza kukimu mahitaji ya watu katika jamii zao. Hii ndiyo maana unaitwa Muungano wa Usaidizi—ulibuniwa ili kutoa msaada kwa wale wenye uhitaji. Muungano wa Usaidizi wa awali ulisaidia katika kugharamia mafunzo ya kitabibu kwa wanawake, kujenga hospitali, kuanzisha huduma za kuasili watoto, kupata haki za wanawake kupiga kura na mengine mengi.
Hivi leo, Muungano wa Usaidizi unaratibu miradi ya huduma, kufanya urafiki na wanawake wengine na kuwasaidia kukuza vyote ujuzi wa maisha na uelewa wa kina wa Yesu Kristo na injili Yake. Kauli mbiu yake ni “Hisani Haishindwi Kamwe.” Akina dada wa Muungano wa Usaidizi hutafuta kufuata mfano wa Yesu na kuonyesha upendo sawa kwa marafiki, majirani na wageni. Muungano wa Usaidizi ni moja ya taasisi kubwa, ya muda mrefu na anuwai ya wanawake ulimwenguni. Kile kilichoanza kama mkusanyiko mdogo katika ghala la matofali mekundu huko Nauvoo, Illinois, sasa kinajumuisha zaidi ya wanawake milioni 7.5 katika nchi 220.
Wakati Nabii Joseph Smith alipoanzisha Muungano wa Usaidizi, alisema ulianzishwa chini ya ukuhani na kwa kufuata mpangilio wa ukuhani. Eliza R. Snow, Rais mkuu wa pili wa Muungano wa Usaidizi, alisema, “muungano hupata mamlaka yake yote na ushawishi kutoka kwenye chanzo hicho.”1 Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi Jean B. Bingham alisema: “Ninataka watu wajue kwamba Muungano wa Usaidizi ni taasisi yenye nguvu, ndiyo, ya kubadili ulimwengu . . . Leo, Muungano wa Usaidizi umejaa wanawake wa kawaida ambao hufanya vitu vya kipekee kadiri wanavyotumia imani katika Mungu na Yesu Kristo.”2
Mnamo 2021, wanawake saba katika Eneo la Kati la Afrika waliitwa kutumikia katika nafasi mpya zilizoundwa za Washauri wa Taasisi wa Kimataifa wa Eneo wa Kanisa. Wanawake walioitwa katika nafasi hii mpya watatoa mafunzo na unasihi kwa viongozi wa Muungano wa Usaidizi, Msingi na Wasichana wa eneo husika, watashiriki katika mabaraza pamoja na wanaume na wanawake wa Kanisa katika maeneo yao husika na watatumikia chini ya uongozi wa Marais wa Eneo ili kuwasaidia wao kufikia malengo yao ya ukuhani.