“Kila Mmoja Anahitaji Injili,” Liahona, Julai 2023.
Kila Mmoja Anahitaji Injili
Nilikuwa nimepanga kutumikia misheni, lakini baada ya chuo nilidhani sihitaji kutumikia—mpaka nilipopata kazi ya kushughulikia wasichana walionyanyaswa. Kisha niliona kwamba kila mmoja anahitaji injili.
Nilipokuwa shule ya msingi, siwezi kukumbuka ni mara ngapi walimu wangu waliuliza nani miongoni mwetu watataka kutumikia misheni. Katika akili yangu ya kitoto daima nilijibu ningetumikia.
Mama yangu alinionyesha jinsi kukusanya Israeli ilivyokuwa muhimu kwa kuwasaidia wamisionari kufundisha na kushiriki injili. Siku moja nilijiunga naye kutafuta nyumba ya dada mmoja kwenye kata ambaye hakuwa amehudhuria kanisani kwa muda sasa. Karibu tupotee kwa sababu hatukujua hasa alipokuwa anaishi. Badala ya kukerwa, mama yangu kwa bidii alitafuta nyumba ya dada huyo. Kama mwanamke katika mfano wa sarafu iliyopotea (ona Luka 15:8–10), alimpata dada yule na kushangilia.
Jinsi mama yangu alivyojitoa kwa dhati kwenye kazi ya Bwana, sio tu kwa kushiriki injili lakini pia katika miito mingine ya Kanisa, ilinisaidia kutambua kwamba kila mmoja lazima amtumikie Bwana, hata katika njia ndogo ndogo.
Kadiri miaka ilivyosonga, nilihitimu seminari, nikapokea medali yangu ya Wasichana, nikahitimu chuo na kuanza kazi. Kidogo kidogo, hisia ya kuwa mmisionari ikaanza kuwa si kipaumbele tena. Japo bado nilikuwa nahudhuria kikamilifu na kukuza miito yangu ya Kanisa, nilijiambia, “Ni SAWA kutotumikia misheni kwa sababu siyo jukumu langu. Mimi ni dada, na ninaweza kumtumikia Bwana katika njia zingine nyingi.”
Kilichobadilisha Mawazo Yangu
Nilipokuwa na miaka 22, nilikuwa na fursa ya kufanya kazi kwenye kituo ambapo niliwahudumia wasichana waliopitia unyanyasaji na kutengwa. Nilihisi huruma kwa ajili yao. Niliona jinsi unyanyasaji ulivyovunja mioyo yao na kuharibu upendo wao juu yao wenyewe. Baadhi yao walijaribu kujiua. Baadhi yao hawakutaka kumwamini mtu yeyote. Wengi wao hawakuwa na tumaini katika maisha na hawakuhisi upendo wa Mwokozi.
Mara kwa mara nilijiuliza, “Je, unyanyasaji huu hauwezi kuzuiliwa? Vipi kama wanyanyasaji wangepokea injili? Vipi kama wazazi wao wangekuwa waumini wa Kanisa kabla ya wasichana hawa kuzaliwa?” Nilitambua kwamba wasichana hawa wasingepitia majaribu haya kama wazazi wao na wanyanyasaji wangepokea na kuiishi injili.
Nikitafakari maswali haya na kufanya kazi katika kituo hicho kulinisaidia kuona kwamba watu wote wanahitaji injili. Kama vile jeshi la Helamani katika Kitabu cha Mormoni walipigana kulinda imani yao na familia zao, Bwana anahitaji wamisionari kushiriki injili Yake na kulinda ufalme Wake.
Uzoefu nilioupata kwa wasichana kwenye kituo ulinishawishi nitembee kwenye njia ambayo Bwana alitaka mimi niipitie. Niliamua ninahitaji kujiunga na jeshi la umisionari la Bwana. Bwana aliiona hamu hii na niliitwa kutumikia Misheni ya Cauayan Ufilipino.
Kutumikia Misheni
Kwenye misheni yangu, niliona watu wakibadilika walipokuwa wakijifunza injili. Niliwafundisha watu ambao hawakujua jinsi ya kusamehe, ambao walivuta sigara na kunywa pombe, wenye kiburi, wasiojua kusali. Kwa sababu ya injili, waliachana na njia zao za kale ili kustahili kwa kile Mungu alichokiahidi: uzima wa milele.
Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, nilijifunza kwamba kila mtu anaweza kuanza upya au kurejea kwenye njia nyembamba na iliyosonga kama wakitubu. Injili ya Yesu Kristo itatusaidia kubadilika na kusonga mbele kuelekea ukamilifu na kuwa wenye kustahili baraka kuu ambazo Baba wa Mbinguni ameziandaa kwa ajili yetu. Mabadiliko haya yanaweza kuwa kutoka kwenye huzuni hadi kwenye furaha, machafuko hadi kwenye amani, hasira hadi kwenye msamaha, udhaifu hadi kwenye uimara, chuki hadi kwenye upendo.
Ninahisi kubarikiwa kwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Injili ya Yesu Kristo hunisaidia kuelewa ustahili wangu kama binti wa wazazi wa mbinguni, hata katika hali mbaya. Baba yetu wa Mbinguni daima hunifariji kupitia Roho Mtakatifu. Maandiko ni dira yangu ninapokuwa nimekanganyikiwa na kuhitajika kufanya maamuzi.
Mimi pamoja na familia yangu tunajitahidi kuvumilia mpaka mwisho kwa uaminifu. Nina shukrani kwa kuolewa na mwanaume anayeshikilia ukuhani na ana ushuhuda imara wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Maagano yangu pamoja na Bwana sio tu kwa ajili yangu lakini kwa ajili ya familia yangu na ufalme Wake.
Mwandishi anaishi Ufilipino