“Njia Yetu Wenyewe Kwenda Emau,” Liahona, Julai 2023.
Njoo, Unifuate
Njia Yetu Wenyewe kwenda Emau
Shughuli tano rahisi znazoweza kutusaidia kujua kwamba Mwokozi daima yu karibu.
Baba yangu alifariki kwa ajili ya kansa nilipokuwa na umri wa miaka 4. Nimekua huku nikijiuliza kwa nini afe. Nilimhoji Mungu na kuuliza kwa nini maisha hayana usawa. Miaka kumi baadaye, nilipokuwa na miaka 14, nilikutana na wamisionari. Walipokuwa wakitufundisha, mama yangu alihisi kwamba walikuwa wanafundisha ukweli na kwamba tunapaswa kusikiliza. Tulipojiunga na Kanisa, injili ya Yesu Kristo na uelewa wa mpango wa wokovu ulikuja kwenye maisha yangu kwenye kipindi nilichokuwa nauhitaji sana.
Baadaye, nilipounganishwa na wazazi wangu hekaluni, mama yangu alininong’oneza, “Ninahisi uwepo wa baba yako.” Nilipokuwa nafikiria baraka ya kuunganishwa, nilijua kwamba Bwana aliijua familia yetu na kwamba amekuwa pamoja nasi mara kwa mara, hata kama hatujui.
Umewahi kujiuliza kama Mwokozi anakujua? Je, anajua mapambano na mahangaiko yako? Je, angesema nini kwako kama ungetembea na kuongea Naye?
Alitembea pamoja Nao
Siku tatu baada ya kifo cha Yesu Kristo, wawili wa wanafunzi wake walikuwa wanatembea kuelekea kijiji cha Emau, ambacho kipo maili saba (12 km) kutoka Yerusalemu. Walimezwa na mawazo yao na hofu, wakati mgeni alipojiunga pamoja nao.
Mgeni akawauliza, “Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakasimama wamekunja nyuso zao.”
Wanafunzi wakaongelea matukio ya hivi karibuni “mambo ya Yesu wa Nazareti.” Waliamini kwamba Yesu alikuja kuikomboa Israeli, lakini ameshitakiwa na kusulubiwa pasipo haki. Pia wakasema kwamba wale waliomjua Kristo walikuwa wakisema amefufuka kutoka wafu.
Mgeni akawaambia walikuwa na “mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii.” Alirejelea kile ambacho maandiko yalifundisha na jinsi Kristo alivyotimiza unabii. Hii iliwapa furaha wanafunzi wale.
Walipofika Emau, wanafunzi walimuomba yule mgeni “kaa pamoja nasi.” Wakati wa chakula cha usiku yule mgeni alibariki mkate na kuuvunja. Ghafla wanafunzi walitambua kwamba mgeni yule hakuwa mgeni kabisa lakini Mwokozi Mwenyewe! (Ona Luka 24:13–32.)
Yeye Hukaa Nasi
Tunaweza kujiuliza kwa nini wale wanafunzi wawili hawakujua kwamba Mwokozi alikuwa akitembea nao. Na bado ni mara ngapi huwa tunashindwa kuelewa kwamba anatembea pamoja nasi? Mara nyingi tumefokasi kwenye changamoto, na hata shangwe, katika maisha yetu ya kila siku kwamba hatuoni kwamba Mwokozi yuko upande wetu.
Tunaweza tusione jinsi anavyokaa nasi, kutupigania, kufanya kazi pamoja nasi na kulia pamoja nasi. Hata katika nyakati zetu za huzuni kubwa, tunaweza kumhisi pamoja nasi na kusikia maneno yake: “Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu” (Zaburi 46:10, msisitizo umeongezwa; ona pia Mafundisho na Maagano 101:16).
Njia Yetu Binafsi
Kila mmoja wetu ana sehemu anahitaji kufika katika maisha haya. Nyakati zingine katika maisha yetu, tunaweza kukumbwa na ugonjwa au kupambana na udhaifu wetu wenyewe. Tunaweza kuwa na matatizo ya kifedha au changamoto zitokanazo na mafanikio, utajiri au kiburi.
Tunaposafiri njia yetu kwenda Emau, hatuhitaji kamwe kutembea peke yetu. Tunaweza kumwomba Mwokozi kuwa pamoja nasi. Hizi ni shughuli tano rahisi ambazo zitatusaidia kusonga karibu Naye.
1. Sali Kila Siku
Sala inapaswa iwe kitu cha kwanza katika maisha yetu ya kila siku. Inaweza kutusaidia kupokea wenza na mwongozo wa Baba wa Mbinguni. Tunaweza kuomba nguvu za kumfuata Mwana Wake na kwa ajili ya nguvu ya Roho, hasa katika nyakati ambapo mawazo yetu huweza kutuongoza kwenye dhambi.
Kijana Joseph Smith, wakati anamuomba Mungu katika ombi kwa ajili ya jibu, adui alijaribu kumzuia (ona Joseph Smith—Historia ya 1:16). Kama Joseph tunapaswa kuendelea kusali n kuamini kwamba Baba wa Mbinguni kamwe hachoki kutusikiliza. Yeye atatusaidia kuelewa muda Wake na majbu Yake.
2. Sherehekea Maandiko
Mwokozi alionesha mfano kwetu kwa kusoma maandiko. Aliyanukuu mara kwa mara alipofundisha. Kusoma maandiko mara kwa mara hutusaidia kuwa na akili makini, moyo wenye kukubali ambao hutunza maneno ya Mungu na mikono iliyo tayari kutumikia.
Tunapojifunza maandiko, Roho Mtakatifu anaweza kutujaza na hamu ya kutenda mema. Kutanoa uoni wetu kuona kile ambacho macho ya asili hayakioni. Kutatusaidia kusikia vilio vya wahitaji. Tutabarikiwa kufuata mfano wa Mwokozi wa kuwafariji wanaohitaji kufarijiwa (ona Mosia 18:8–9). Kisha tunapokabiliana na shughuli za siku, kamwe hatutatembea peke yetu. Mwokozi atatembea pamoja nasi hatua kwa hatua.
3. Wafuate Manabii Wanaoishi
Tunapaswa kufuata ushauri wa nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, na manabii, waonaji na wafunuzi wengine. Kisha tutagundua kwamba njia yetu kwenda Emau itakuwa salama na angavu. Watatuongoza salama na kutusaidia kujua kwamba Mwokozi yu pamoja nasi.
4. Mwalike Yeye Akae Nawe
Tunapojifunza kuhusu Yesu Kristo na tunapotii amri Zake, tunamwalika Mwokozi kuwa pamoja nasi. Tunajifunza kutambua ushawishi Wake katika maisha yetu.
Wanafunzi wawili wakiwa njiani kwenda Emau walitembea na Mwokozi, wakiongea Naye na kuhisi mioyo yao ikiwaka ndani yao (ona Luka 24:32). Ombi lao Kwake la “Kaa nasi” (Luka 24:29), linapaswa pia kuwa ombi letu.
Wakati wanafunzi walipomtambua Mwokozi, ghafla alitoweka kutoka uwepo wao. Wanafunzi mara moja walirejea Yerusalemu na kushuhudia kwa Mitume kwamba Mwokozi amefufuka. Wakati wakishuhudia, Bwana “alisimama katikati yao” (Luka 24:36). Tunaweza pia kumhisi Yeye wakati akiwa katikati yetu.
5. Fanya Upya Maagano Kila Mara
Ibada na maagano ya injili ya Yesu Kristo vinaweza kubadili asili yetu. Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alisema, “Kuabudu na kutumia kwetu wa kanuni za milele hutuleta karibu na Mungu na kukuza uwezo wetu wa kupenda.”1 Kwa mfano, ubatizo huruhusu Bwana kututakasa. Na kama tu waaminifu na watiifu, maagano na ibada za hekaluni hutuandaa siku moja kuishi kwenye uwepo wa Baba na Mwana.
Sakramenti hutusaidia kukumbuka na kuturuhusu kufanya upya maagano yetu, kutubu na kujaribu tena. Kila tunapopokea sakramenti, tunaashiria utayari wetu wa kujichukulia jina la Yesu Kristo juu yetu, kuweka dhamiri tena ya kumkumbuka Yeye na kushika amri Zake. Kisha tunaahidiwa kwamba Roho Wake daima atakuwa pamoja nasi. (Ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79.) Daima tunapaswa kukumbuka ibada na maagano tuliyofanya.
Mwokozi Atakuwa Karibu
Kwenye njia yetu kwenda Emau, Mwokozi kwa upendo anatualika kuja Kwake na kupata shangwe ndani Yake. Tunaposali kila siku, kusherehekea maandiko, kuwafuata manabii wanaoishi, kumwalika Yeye kukaa nasi na kufanya upya na kuheshimu maagano yetu, Yeye atakuwa karibu nasi. Kisha tutajua, kama wanafunzi njiani kwenda Emau walivyojua, kwamba Yesu Kristo amefufuka na kwamba kweli Yeye anaishi na kutupenda.
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Anatamani kuwa pamoja nasi na kutuongoza salama kwenye njia yetu.