“Kuhudumu kwa Hisani,” Liahona,, Julai 2023
Kanuni za Kuhudumu
Kuhudumu kwa Hisani
Tunaweza kuleta tofauti kubwa kwa kuonyesha upendo katika njia za asili.
Mfano wa Hisani
Tabitha (pia anajulikana kama Dorkasi) alikuwa ni mwanafunzi wa Yesu Kristo aliyeishi Jopa. Alijulikana kama mwanamke “aliyejaa matendo mema na sadaka alizozitoa” (Matendo ya Mitume 9:36). Alipendwa kwa sababu alifanya mengi kuwapenda wengine. Kama Mwokozi, alitoa maisha yake kwenye kutumikia. Alikuwa na ujuzi na talanta ambazo alizitumia kuleta tofauti.
Mojawapo ya ujuzi huo ilikuwa ni kutengeneza nguo, angalau baadhi ya hizo ziliwaendea wajane wenye mahitaji. Kwa wale waliopokea zawadi zake, alikuwa ametumwa na Mungu. Wakati Petro alipomtembelea baada ya kifo chake, “wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao”.(Matendo ya Mitume 9:39). Petro aliguswa sana kiasi kwamba alimfufua kutoka wafu, na kupelekea wengi kuamini katika Mwokozi (Matendo ya Mitume9:40–42).
Kuhudumu kwa Hisani
Hisani ni upendo ambao Yesu anao kwa ajili yetu na upendo ambao anategemea sisi tuwe nao kila mmoja kwa mwingine. Ni kumpenda jirani yetu kama tunavyojipenda wenyewe (ona Mathayo 22:37–39), tukiwatendea kwa huruma, subira na neema kama ambayo tungependa kwa ajili yetu wenyewe (ona Mathayo 7:12). Ni kuwatumikia wao, kama Tabitha, tukitumia karama na talanta tulizopewa.
Tunaweza kuleta tofauti kubwa kwa kuonyesha upendo wetu katika njia ambazo ni za asili kwetu—hata kama kile tunachokifanya ni chepesi. Kama una kipawa cha kushona, hiyo inaweza kuwa njia ya kuhudumu, lakini labda uko vizuri katika kukata nyasi kwa mashine kuliko kushona. Au huenda kipawa chako ni kujua jinsi ya kusikiliza kwa dhati na kuwepo pale kama rafiki wa dhati.
Kukuza Hisani
Tunawezaje kukuza sifa kama ya Kristo ya hisani?
-
Hisani ni kipawa ambacho Baba wa Mbinguni hukiweka juu ya wale wote ambao ni wafuasi wa Yesu Kristo. “Ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu” (Moroni 7:48).
-
Mormoni alifundisha kile Hisani inamaanisha: “Na hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi, haifikirii mabaya, na haifurahii uovu lakini hufurahi katika ukweli, huvumilia vitu vyote, huamini vitu vyote, hutumaini vitu vyote, hustahamili vitu vyote (Moroni 7:45). Hizi sio njia tu za kusimulia pale unapokuwa umejazwa na upendo, pia ni sifa zinazohusiana ambazo zitachangia kwenye ongezeko la uwezo wa kupenda kadiri tunavyozikuza.
-
Huruma huja kwa kuhisi jinsi wengine wahisivyo.1 Tunapotafuta kuwaelewa wengine, tunaipa hisani fursa kubwa ya kukua. Fanya mazoezi ya kuuliza maswali katika njia yenye msaada na ya upendo, na kisha sikiliza kwa subira na uelewa.
-
Fanyia kazi hisani. Toa muda wako na nyenzo zingine, ikijumuisha msamaha wako, kwa wale wanaouhitaji. Rais Thomas S. Monson (1927–2018) alifundisha: “Msamaha unapaswa uambatane na upendo. … Lawama huacha vidonda kuwa wazi. Msamaha pekee ndio huponya.”2