“Kuona Miujiza ya Mwokozi katika Maisha,” Liahona, Julai 2023.
Miujiza ya Yesu
Kuona Miujiza ya Mwokozi katika Maisha Yetu
Masomo manne kutoka kwa uponyaji wa Mwokozi kwa kipofu.
Kuna nyakati katika maisha yetu tunapotumaini na kuomba kwa ajili ya miujiza. Inaweza kuwa kwa ajili ya mpendwa au kwa ajili ya manufaa yetu wenyewe. Tumaini letu ni kujibiwa maombi yetu, hali mbaya kurekebishwa, nafsi kali kulainishwa na Bwana wa miujiza kutoa suluhisho tunalolihitaji. Pale matokeo yanapokuwa tusichokitarajia au katika ratiba tuliyoiomba, huwa tunajiuliza kwa nini.
Moroni anafundisha “Na ningewashauri ninyi, ndugu zangu wapendwa, kwamba mkumbuke kwamba yeye ndiye yule yule jana, leo, na milele, na kwamba karama hizi zote ambazo nimezungumzia, ambazo ni za kiroho, hazitatolewa mbali, kadiri dunia itakavyokuwepo, kulingana tu na kutoamini kwa watoto wa watu” (Moroni 10:19).
Je, karama hizo na miujiza iliyorekodiwa katika maandika bado yanapatikana katika siku yetu? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuhitimu kupokea baraka hizo? Je, Mwokozi anatambua linaloendelea kwenye maisha yetu na yu radhi kutukomboa kutokana na changamoto zetu?
Ningependa kutumia muujiza wa Mwokozi wa kurejesha uoni kwa kipofu kama msingi wa kujibu maswali haya. (Kwa mfano, ona Mathayo 9:27–31; 12:22–23; Marko 8:22–26; 10:46–52; Yohana 9:1–11.
Tunaweza Kujifunza Nini kuhusu Misheni ya Mwokozi kutoka kwenye Miujiza Yake?
Ili kuelewa athari ya muujiza kwetu na katika maisha yetu, hebu tuanze kwa kutoa maana ya muujiza. Miujiza “ilinuiwa kuwa ushahidi kwa Wayahudi kwamba Yesu alikuwa Kristo. … Mingi ya miujiza pia ilikuwa ishara, ikifundisha … kweli za takatifu. … Miujiza ilikuwa na ni jibu kwa imani na himizo zuri sana la imani. Kamwe haikutendeka pasipo sala, hitaji iliyohisiwa, na imani.”1
Mzee Ronald A. Rasband wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema kwa urahisi na vyema:
“Miujiza ni matendo ya kiungu, madhihirisho na maonyesho ya nguvu ya Mungu isiyo na kikomo na uthibitisho kwamba Yeye ‘ni yule yule jana, leo na hata milele’ [Moroni 10:19]. …
“… Miujiza ni muendelezo wa mpango wa milele wa Mungu; miujiza ni mtitiriko wa maisha kutoka mbinguni kwenda duniani.”2
Hivyo, njia nzuri ya kusoma miujiza ya Mwokozi na kujifunza kutokana nayo ni kwa kukumbuka kwamba kila muujiza huelekeza kwenye kitu kikubwa kuliko tukio lenyewe na kutafuta kweli maalumu kuhusu Mungu na kazi Yake.
Hebu tujadili baadhi ya kweli tunazoweza kujifunza kutoka kwenye miujiza ya Mwokozi ya kurejesha uoni kwa kipofu. Inaweza kugawanywa kwenye masomo manne kama ifuatavyo.
1. Kurejesha Uoni Ilikuwa Ishara ya Masiya
Manabii wa kale walioshuhudia kuhusu kuja kwa Masiya waliongelea miujiza ambayo angeitenda, ikijumuisha kumpa kipofu uoni.
Kwa mfalme Benyamini, malaika mtakatifu alisema kwamba Mwokozi “ataenda miongoni mwa watu, akitenda miujiza mikuu, kama kuponya wagonjwa, kufufua wafu, kusababisha viwete kutembea, vipofu kupata kuona” (Mosia 3:5; ona pia Isaya 35:4–5).3
Hivyo, miujiza ya kurejesha uoni kwa vipofu huthibitisha unabii huo kuhusu ujio wa Mwokozi na huduma Yake kwa watoto wa Mungu.
2. Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
Ukweli huu ulidhihirishwa vyema pale Yesu alipokutana na mwanaume ambaye alikuwa kipofu tangu utoto wake (ona Yohana 9:1–11). Wanafunzi wake walipouliza kama mtu huyo alizaliwa kipofu kwa sababu ya dhambi, Yesu alijibu hapana, “bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake” (mstari wa 3). Kisha kabla ya kurejesha uoni wa mtu huyo, Mwokozi alitamka, “Muda nilipo ulimwenguni, mimi ni nuru ya ulimwengu” (mstari wa 5).
Mzee Bruce R. McConkie (1915–1985) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alielezea: “Kabla ya kufungua macho ya kipofu, kimwili, Yesu aliwakumbusha tamko lake la awali wale waliokuwa wakimsikiliza, ‘Mimi ni nuru ya ulimwengu,’ kama vile kufundisha: ‘Wakati mkumbukapo kwamba nilifungua macho ya kipofu, katika mwili, pia mkumbuke kwamba nimekuja kuleta nuru kwenye macho, kiroho’”4
Tunahitaji kukumbuka jinsi dhambi inavyochukuliwa katika maandiko kama upofu wa kimaadili na kuokolewa kutoka dhambi ni kama kuondolewa kwa upofu huu. Yeye aliye “nuru ya ulimwengu” alikuwa akitumia tukio hili kuashiria kazi kuu aliyoijia duniani kuikamilisha.
3. Imani Hutangulia Miujiza
Na Yesu alipokuwa akipita mitaa ya Kapernaumu, vipofu wawili walimwendea, wakisema, “Uturehemu, Mwana wa Daudi.” Kisha akazungumza nao, akisema, “Mnaamini kwamba naweza kufanya hili?” Na wakajibu, “Naam, Bwana.”
Ushahidi wa imani yao kwamba Bwana angeweza kuwasaidia ilikuwa katika kumfuata kwao Mwokozi pasipo kukata tamaa na katika kukubali kwao kwa haraka na kwa wazi kuhusu imani hiyo pale walipoulizwa. Mwokozi aligusa macho yao, akisema, “Kwa kadiri ya imani yenu mpate.” Matokeo yalikuwa ya mara moja: “macho yao yakafunguka” (Mathayo 9:27–31).
Mzee McConkie anasema: “Mara kwa mara katika kufungua macho ya kipofu, Yesu, kama hapa, anajumuisha amri yake aliyoiongea na baadhi ya matendo ya kimwili. Katika hili na matukio mengine aligusa macho ya asiyeona.”
Kwa nini Mwokozi alifanya hilo? “Hakuna hata moja ya haya matendo yasiyo ya kawaida … yana umuhimu kwenye matumizi ya nguvu ya uponyaji,” alielezea Mzee McConkie. Lakini tunajua kwamba imani hutangulia miujiza na hivyo “Lengo la Kristo lilikuwa kuimarisha imani ya mtu kipofu au kiziwi.”5
4. Miujiza Wakati Mwingine Huja Mstari Juu ya Mstari
Huko Bethsaida, watu walimleta mwanaume kipofu kwa Yesu Baada ya kumtoa mtu yule nje ya kijiji, Yesu “akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake.” Uoni wa mtu huyo ulirejeshwa kidogo tu kwa wakati huo, na Mwokozi “akaweka tena mikono yake juu ya macho yake,” na kuleta uponyaji kamili. (Ona Marko 8:22–26.)
Mzee McConkie alitoa kweli ambazo tunaweza kujifunza kutokana na tukio hili:
“Ingeweza kuonekana kwamba mifano mfululizo ya kukutana na Mwokozi ilikuwa na athari ya kuongeza tumaini, uhakika na imani kwa wasio na uoni.
“… Watu wanapaswa kutafuta neema ya uponyaji ya Bwana kwa nguvu zao zote na imani, ingawa hiyo inatosha kwa ajili ya uponyaji wa mdogo tu. … Kisha wanaweza kupata nyongeza ya hakikisho na imani ya kufanywa wakamilifu na wazima kila sehemu Watu pia mara nyingi huponywa magonjwa yao ya kiroho kwa viwango, hatua kwa hatua wanapopatanisha maisha yao na mipango na madhumuni ya Mungu.”6
Kwa kufanya muujiza huu katika hatua mbili tofauti, Bwana alimsaidia yule kipofu kuwa tayari kupokea baraka kamili. Je, tunaweza kuona mfumo huu pia katika utafiti wetu wa miujiza—kitu ambacho tunahitajika kufanya, au kutofanya, kabla ya kuwa tayari kwa ajili ya uingiliaji wa hali ya juu?
Imani ya Kutokuponywa
Ingawa tunaweza kuona umuhimu wa imani katika kuleta miujiza, ni muhimu kutambua kwamba wakati mwingine hata Watakatifu waaminifu sana hawatapokea majibu ya matamanio yao na maombi yao
Mzee David A. Bednar wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitufundisha:
“Haki na imani kwa hakika ni vya msingi katika kuhamisha milima—kama kuhamisha milima hukamilisha madhumuni ya Mungu na ni kulingana na mapenzi Yake. Haki na imani kwa hakika ni vya msingi katika kumponya mgonjwa, kiziwi na kiwete—kama uponyaji huo hukamilisha malengo ya Mungu na ni kulingana na mapenzi Yake. Kwa hivyo, hata kama tuna imani thabiti, milima mingi haitaondolewa. Na si wagonjwa na wenye mapungufu wote wataponywa. Kama upinzani wote ungepunguzwa, kama maradhi yote yangeondolewa, basi malengo ya msingi ya mpango wa Baba yangevurugika.
“Masomo mengi tunayopaswa kujifunza katika maisha haya ya duniani yanaweza kupokelewa tu kupitia vitu tunavyopitia na wakati mwingine vinavyotuumiza. Na Mungu anategemea na kutuamini kukabiliana na dhiki za muda za maisha haya kwa msaada Wake ili tujifunze tunachopaswa kujifunza na hatimaye kuwa kile tunachopaswa kuwa katika umilele.”7
Nataka kuongeza ushuhuda wangu kwenye ushahidi wa manabii wa kale na sasa. Miujiza bado hutokea miongoni mwetu. Mwokozi Yesu Kristo ndiye kiini cha nguvu yote, nuru na faraja. Ninashuhudia kwamba kupitia imani yetu Kwake, tunaweza kuponywa, na kama hatutaponywa, bado tunaweza kupata amani kupitia Mfalme wa Amani, Nuru ya Ulimwengu na Mponyaji wa Waponyaji.