“Tusiogope,” Liahona, Julai 2023.
Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Tusiogope
Najua tutakuwa na furaha tunaposhiriki injili pamoja na watu wengi tuwezavyo.
Wengi wa marafiki zangu na wanafunzi wenza ambao si waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wangeniuliza mara kwa mara kuhusu Kanisa. Baada ya muda, nilichoka kujibu maswali yaleyale tena na tena, hivyo nilitafuta suluhisho.
Napenda kutengeneza video za mtandaoni ili kuwaburudisha watu. Ninafanya video za muziki, video za taarifa na vichekesho. Siku moja nilipokuwa nikiwaza nini ningefanya kwa ajili ya video yangu ijayo, niliamua kutengeneza video ambayo ilijibu maswali kuhusu Kanisa.
Nilichukua kamera yangu. Kisha, bila kuandika kile nilichokuwa naenda kusema lakini nikikumbuka maandiko muhimu niliyohitaji kuyataja, niliandaa video. Sikujua nini kingetokea. Nilisukumwa tu kutengeneza video. “Nikiongozwa na Roho, wala sikujua kimbele vitu ambavyo ningefanya” (1 Nefi 4:6).
Bila hofu ya ni marafiki wangapi, wanadarasa na ndugu—waumini wa Kanisa au la—watajibuje, niliipakia video hiyo mtandaoni.
Wiki chache baada ya kupakia video hiyo, nilianza kupokea mrejesho kwenye akaunti zangu za mitandao ya kijamii. Watu ambao hata sikuwajua walianza kutoa maoni na kunishukuru kwa ajili ya video. Kwa sababu ya video yangu, mtu mmoja alianza kuhudhuria mazungumzo ya wamisionari. Baadaye, mtu huyo aliamua kubatizwa.
Tangu nimetengeneza video, watu ninaowajua ambao si waumini wa Kanisa huonekana kunipenda vile vile kama awali—na huenda zaidi. Baadhi yao wameachana hata na kulikosoa Kanisa. Wengine wameacha kuuliza maswali yale yale kuhusu Kanisa kwa sababu sasa wanayo majibu.
Tusiogope kutenda kile ambacho Bwana ametuamuru. Amesema, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe,” (Marko 16:15).
Ninawaahidi kwamba hatutaona aibu kwa kumtii Yeye.