Kuwasaidia Waumini Wanaopitia na Talaka
Baba wa Mbinguni atatusaidia kujua vyema jinsi ya kuandaa mazingira salama na yenye makaribisho katika kata zetu na matawi yetu kwa ajili ya wale waliopeana talaka au wanaopitia talaka.
Wanaume wawili katika kata walibakia kuwa waseja karibia kipindi sawa, kila mmoja baada ya miaka kadhaa ya ndoa na wake zao. Wakati mwanaume wa kwanza alipobakia kuwa mseja, kata ilimfikia mara kwa mara, kumpatia chakula na kutafuta njia za kuhakikisha hakuhisi mpweke. Kwa ajili ya mwanaume wa pili, huduma hii haikutokea, na alibakia akihisi ametengwa na asiye sawa na wengine.
Ni nini ilikuwa tofauti kati ya wanaume hawa wawili? Wa kwanza alibakia mjane na wa pili ilikuwa talaka. Pale mwanaume aliyepitia talaka aliposhiriki uzoefu wake pamoja nami, ombi lake lilikuwa rahisi: tunaweza kuwasaidia waumini wa Kanisa kuelewa vyema jinsi ya kuwahudumia wale waliotalikiana na kutambua kwamba bado wana sehemu sawa yenye thamani katika kata na matawi yetu?
Kata nyingi hufanya kazi nzuri ya kuwahudumia wale wanaopitia madhara ya talaka, lakini bado ombi la mwanaume huyu huweza kutuongoza sote kuuliza kama kuna kitu bado tunaweza kufanya vyema. Hitaji hili la kuhisi kukaribishwa na kusaidiwa linahusiana na mwaliko kutoka kwa viongozi wa Kanisa—kuwapenda wote walio ndani ya zizi la Mungu na kuwasaidia kuhisi kukaribishwa na salama katika vigingi vyetu vya Sayuni.1
“Wakati wowote tunapomwinua mtu yeyote kiuhalisia tunatengeneza sehemu ya ulinzi kwa ajili yao.”2 Kata zetu na matawi yetu yanapaswa kuwa miongoni mwa hizo sehemu tunapotafuta kutii amri kuu mbili za kumpenda Mungu na kuwapenda wengine kama tunavyojipenda wenyewe (ona Mathayo 22:37–39). Kanuni zifuatazo zinaweza kutusaidia jinsi ya kuwa msaada borakwa wale katika kata zetu na matawi yetu ambao wamepitia au wanapitia talaka.
Kumbuka Kwamba Talaka Huhusisha Hisia Nyingi
Kwa sababu tunajua fundisho la msingi la ndoa ya milele na nguvu ya agano la kuunganisha katika mpango wa wokovu wa Mungu, talaka inaweza kuwa ya kuvunja moyo. Na bado si kila mtu atahisi katika njia sawa kuhusu talaka yao. Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alifundisha kwamba talaka “ni somo nyeti kwa sababu huhusisha hisia kali kutoka kwa wahusika katika njia tofauti. Baadhi hujiona au huwaona wapendwa wao kama wahanga wa talaka. Wengine hujiona kama wanufaika. Baadhi huona talaka kama kigezo cha ushinde. Wengine huichukulia kama kigezo cha kutoroka ndoa.”3
Badala ya kubashiri jinsi mtu anayepitia talaka huchukulia hali zao, tenga muda kusikiliza pale na kwa vyovyote mtu awapo tayari kushiriki nawe. Fikiria kuuliza, “Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa msaada kwa wakati huu?” au “Kwa njia gani tunaweza kukusaidia kwenye hili na hata baada ya talaka?”
Maswali ya Kuzingatia:
-
Ni kwa jinsi gani watu wanaweza kupitia hisia za tofauti katika vipindi tofauti kila siku, wiki au mwezi? Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa makini na wa msaada katika kila aina ya hisia hizo?
-
Ni kwa jinsi gani ninaweza kuwa msikivu kwenye ufunuo kuhusu jinsi ya kusaidia katika nyakati tofauti?
-
Ni mawazo gani ninayo ambayo ningeweza kuachana nayo ili kutafuta na kutendea kazi ufunuo kuhusu jinsi ya kusaidia?
Fokasi kwenye Kupenda Badala ya Kuhukumu
Katika maswala ya talaka, kwa nadra tutajua mambo yote yaliyopelekea wanandoa kutalikiana—na hatuhitaji kujua. “Talaka inapotokea, wahusika wana jukumu la kusamehe, kuinuana na kusaidia kuliko kulaumiana”;4 hili ni sahihi kwa wanandoa na wale wanaowazunguka. Tunapaswa kuwa makini kwenye kufokasi kuwapenda wengine, kutowahukumu, bila kujali ni mwenza yupi tuna uhusiano mkubwa naye.
Badala ya kufokasi kwenye hukumu, tunaweza kufokasi kwenye upendo na umoja, kama ilivyofundishwa na Dada J. Anette Dennis, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Muungano wa Usaidizi.
“Ni mara ngapi tunawahukumu wengine kulingana na mwonekano na matendo yao ya nje au ukosefu wa matendo, wakati, ikiwa tungeelewa kikamilifu, badala yake tungeonesha huruma na hamu ya kusaidia badala ya kuwaongezea mizigo kwa hukumu yetu? …
Tumeamriwa kuwapenda wengine, si kuwahukumu. Hebu tuutue mzigo huo mzito; hatupaswi kuubeba. Badala yake, tunaweza kuichukua nira ya Mwokozi ya upendo na huruma. …
“… Kila mmoja anahitaji kuhisi kwa dhati kuwa wao wamejumuishwa na wanahitajika kwenye mwili wa Kristo.”5
Maswali ya Kuzingatia:
-
Ninaweza kufanya nini ili kufokasi zaidi kwenye kuwapenda wengine kama Yesu Kristo?
-
Je, kuna njia ambazo namuhukumu mwingine, ikijumuisha kutafuta au kupachikia makosa, ambazo zinaweza kuwa zinanizuia kuweza kutoa msaada unaohitajika?
-
Nitafanye nini ili kuhisi vyema upendo wa Mungu kwa wengine?
Tafuta Njia za Kuwajumuisha
Kupitia talaka, kawaida watu hupoteza urafiki unaotokana na marafiki wa mwenza wake wa zamani au familia. Na nini hutokea pale urafiki uliofanyika wakati wa ndoa, na marafiki hawawezi tena kuwaalikeni nyie mlioachana kwenye shughuli kwa wakati mmoja?
Dada mmoja alishiriki kwamba yeye na mume wake walikuwa na kawaida ya kushiriki usiku wa michezo wa kila wiki pamoja na marafiki wa kata yake. Baada ya talaka, alihuzunishwa pale mialiko ya usiku wa michezo ilipokoma kuja kwa sababu ilikuwa ni wanandoa tu waliohudhuria. Dada mwingine alishiriki kwamba waumini wengi wa kata walidhani kwamba kwa kuwa sasa alikuwa yuko peke yake, hakuwa na muda wa kuhudhuria shughuli pamoja na marafiki kama alivyofanya awali; kwa hivyo, hawakumwalika ili asihisi huzuni kwa kutoweza kuhudhuria. Hata hivyo, hili lilimfanya azidi kuhisi kutengwa zaidi na mpweke sana. Dada huyu alishiriki kwamba ingekuwa vyema kuendelea kualikwa (hata kama asingeweza kujiunga)—ili kujua kwamba wengine walimhitaji awepo pale.
Kila tukio liko tofauti, lakini “sote tunahitaji kuhisi ukarimu wa rafiki na kusikia tangazo thabiti la imani.”6
Maswali ya Kuzingatia
-
Ni maboresho gani naweza kufanya kwenye shughuli ili kuwasaidia waumini ambao wamebakia peke yao wahisi faraja sawa na wanandoa wengine wakati wa kuhudhuria?
-
Ni kwa jinsi gani kata yetu inaweza kutoa fursa za kujumuishwa za ziada kwa shughuli zinazoendana na mahitaji ya waumini waliotalikiana?
-
Ni shughuli gani zinaweza kumsaidia rafiki yangu kutumikia au kuchangia, hasa ujasiri wake unapohitajika kurejeshwa baada ya uhusiano mgumu?
“Kwanza Angalia, Kisha Hudumu”7
Wale wanaopitia talaka wanajirekebisha kwenye mabadiliko ya kipesa, ratiba, hisia, tamaduni za kila siku na mwaka, mipango ya kuishi na zaidi. Hili ni kweli kwa watu wazima na kwa watoto pia, ambao wanaweza kuwa na majukumu ya ziada majumbani mwao.
Mabaraza ya kata au tawi yanaweza kuangalia jinsi ya kumsaidia kila mwanafamilia, ikijumuisha watoto. Kama watu binafsi, pia tuna fursa nyingi za kuona mahitaji na kisha kwa sala kutendea kazi ufunuo binafsi ili kusaidia katika kuyatimiza.
Dada mmoja alibarikiwa pale jirani alipotambua kwamba mume wa dada huyo alizoea kila mwaka kusafisha uwanja kabla ya theluji kudondoka, ikijumuisha kuondoa maji ya ziada kwenye mabomba, na alijitolea kufanya kwa ajili yake na kumuonyesha nini cha kufanya. Baba aliyeachana na mkewe alibarikiwa pale majirani walipotoa mawazo kwa ajili ya malezi salama ya watoto kwenye eneo lake jipya.
Hapa kuna baadhi ya njia zinginezo ambazo waumini wa kata wamewasaidia familia:
-
Viongozi wa kata, vijana na Msingi huweka mifano inayofaa ya ushawishi wa kama baba au mama katika maisha ya watoto kama inavyofaa.
-
Zawadi za Krismasi ziligawiwa, kama ilivyokuwa kwa pesa ili kusaidia na gharama za misheni.
-
Chakula cha ziada kutoka mikutano ya vijana au shughuli kilitumwa nyumbani kwa familia.
-
Waumini wa kata walishiriki shughuli za michezo za watoto.
-
Mabaraza ya walimu yalijadili jinsi ya kuwajali watoto watokao kwenye familia zenye talaka, hasa kwa masomo kuhusu familia au wakati watoto walipohudhuria kata kila wiki pale walipokuwa na mzazi fulani.
-
Wanandoa wazee wamebeba jukumu la kutunza familia ya mzazi mmoja.
Pia tukumbuke kwamba watu binafsi na familia watahitaji muda ili kuendana na hali mpya. Kuwa mkarimu kwa kuruhusu wao kupona na kusonga katika ratiba ya Mungu na ya kwao, na sio ratiba zetu.
Maswali ya Kuzingatia
-
Kwa jinsi gani naweza kuimarisha urafiki uliopo ili kwamba wale wanaopitia talaka wahisi faraja kupokea msaada pale wanapouhitaji, hata kama sio sasa?
-
Yapi ya “mwanzo” yanaweza kuwa magumu kwa familia, kama vile mara ya kwanza watoto hawako pamoja na mzazi kwenye siku kuu? Ninawezaje kutoa msaada wa ziada katika nyakati hizo?
-
Ni nyenzo gani familia itahitaji ambazo naweza kusaidia, au ninawezaje kuwajumuisha wengine wenye ujuzi wa kusaidia?
Kwa sala tunapotafuta kuelewa vyema na kuwahudumia wale waliotalikiana, pamoja na familia zao, tunaweza kuhisi na kushiriki sehemu ya upendo wa Mungu kwa watoto wake wote.