Nira Yake ni Laini na Mzigo Wake ni Mwepesi
Acha tukumbuke kwamba kila mtu hapa duniani ni mtoto wa Mungu na Yeye humpenda kila mmoja.
Hadithi inasimuliwa kuhusu mwanamume anayeitwa Jack ambaye alikuwa na mbwa mpendwa wa kuwinda ndege aliyeitwa Cassie. Jack alijivunia sana kuhusu Cassie na mara nyingi alijisifu kuhusu ujuzi wa mbwa huyu. Kuthibitisha hili, Jack aliwaalika baadhi ya marafiki kumtazama Cassie akiwa mawindoni. Baada ya kufika kwenye klabu ya uwindaji, Jack alimruhusu Cassie kuzunguka zunguka huku yeye akiingia ndani kujisajili.
Ulipofika muda wa kuanza, Jack alikuwa na shauku ya kuonyesha ustadi wa ajabu wa Cassie. Walakini, Cassie alionyesha tabia isiyo ya kawaida. Hakutii amri yoyote ya Jack kama ambavyo amekuwa akifanya kwa hiari. Alichotaka kufanya ni kubaki kando yake tu.
Jack alikanganyikiwa na kuaibika na akiwa na hasira dhidi ya Cassie; punde alipendekeza waondoke. Cassie hakuweza hata kuruka kuingia nyuma ya gari, na kwa hivyo Jack alimnyanyua pasipo subira na kumsukuma kwenye kibanda cha mbwa. Alikasirika wakati wale waliokuwa pamoja naye walipodhihaki tabia ya mbwa wake wakielekea nyumbani. Jack hakuelewa kwa nini Cassie alikuwa hatii. Alikuwa amefunzwa vizuri, na nia yake yote hapo awali ilikuwa kumpendeza na kumtumikia.
Baada ya kufika nyumbani, Jack alianza kumchunguza Cassie kama alikuwa na majeraha, michubuko au kupe kama kawaida yake. Alipouweka mkono wake kifuani, alihisi kitu kimelowa na kukuta mkono wake ukiwa na damu. Kwa aibu na hofu yake, aligundua kwamba Cassie alikuwa na jeraha refu na pana kwenye mfupa wake wa kifua. Alikuta lingine kwenye mguu wake wa mbele wa kulia, pia kwenye mfupa.
Jack alimbeba Cassie mikononi mwake na kuanza kulia. Aibu yake kwa jinsi alivyomhukumu na kumtendea vibaya ilikuwa kubwa. Cassie alikuwa akitenda kinyume na tabia yake siku hiyo kwa sababu alikuwa na majeraha. Tabia yake ilikuwa imechochewa na maumivu yake, mateso yake na majeraha yake. Haikuwa na uhusiano wowote na ukosefu wa hamu ya kumtii Jack au ukosefu wa upendo kwake.1
Nilisikia hadithi hii miaka mingi iliyopita na sijawahi kuisahau. Je, tuna watu wangapi waliojeruhiwa kati yetu? Ni mara ngapi tunawahukumu wengine kulingana na mwonekano na matendo yao ya nje au ukosefu wa matendo, wakati, ikiwa tungeelewa kikamilifu, badala yake tungeonesha huruma na hamu ya kusaidia badala ya kuwaongezea mizigo kwa hukumu yetu?
Nimekuwa na hatia ya hili mara nyingi katika maisha yangu, lakini Bwana amenifundisha kwa subira kupitia uzoefu binafsi na kadiri nilivyosikiliza uzoefu wa maisha ya wengine wengi. Nimekuja kufahamu kikamilifu zaidi mfano wa Mwokozi wetu mpendwa wakati Alipotumia muda Wake mwingi kuwahudumia wengine kwa upendo.
Uzoefu wa maisha wa binti yangu mdogo umejumuisha changamoto za afya ya kihisia tangu alipokuwa msichana mdogo. Kumekuwa na nyakati nyingi katika maisha yake wakati alipohisi hangeweza kuendelea mbele. Tutashukuru milele kwa malaika wa kidunia ambao wamekuwepo katika nyakati hizo: wakikaa pamoja naye; wakimsikiliza; wakilia naye; na kushiriki pamoja karama za kipekee, ufahamu wa kiroho, na uhusiano wa pamoja wa upendo. Katika hali kama hizo za upendo, mizigo imeondolewa pande zote mbili.
Mzee Joseph B. Wirthlin, akinukuu 1 Wakorintho, alisema, “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.”2
Aliendelea:
“Ujumbe wa Paulo kwa kundi hili jipya la Watakatifu ulikuwa rahisi na wa moja kwa moja: Hakuna unachofanya kinacholeta tofauti kubwa kama huna hisani. Unaweza kunena kwa lugha, kuwa na karama ya unabii, kuelewa siri zote, na kuwa na maarifa yote; hata ukiwa na imani ya kuhamisha milima, pasipo hisani haitakufaidia kitu.
“‘Hisani ni upendo msafi wa Kristo’ (Moroni 7:47). Mwokozi alionyesha kwa matendo upendo huo.”3
Katika Yohana tunasoma, “Kwa hili watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”4
Mahubiri mengi yametolewa na viongozi wetu wa Kanisa kuhusu hisani, umoja, upendo, wema, huruma, msamaha na rehema. Ninaamini Mwokozi anatualika kuishi kwa njia ya juu zaidi, takatifu zaidi4—njia Yake ya upendo ambapo wote wanaweza kuhisi kweli ni wa thamani na wanahitajika.
Tumeamriwa kuwapenda wengine,6 si kuwahukumu.7 Hebu tuutue mzigo huo mzito; hatupaswi kuubeba.8 Badala yake, tunaweza kuichukua nira ya Mwokozi ya upendo na huruma.
“Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; …
“Kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”9
Mwokozi haruhusu dhambi lakini hutupatia upendo Wake na hutupatia msamaha tunapotubu. Kwa mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, Yeye alisema, “Wala Mimi sikuhukumu; Enenda zako wala usitende dhambi tena.”10 Wale Aliowagusa walihisi upendo Wake, na upendo huo uliwaponya na kuwabadili. Upendo Wake uliwatia msukumo kutaka kubadili maisha yao. Kuishi kwa Njia Yake kunaleta shangwe na amani, na Yeye aliwaalika wengine kufuata njia hiyo ya kuishi kwa upole, wema, na upendo.
Mzee Gary E. Stevenson alisema, “Tunapokabiliana na upepo na dhoruba za maisha, magonjwa na majeraha, Bwana—Mchungaji wetu, Mlezi wetu—ataturutubisha kwa upendo na ukarimu. Ataponya mioyo yetu na kuzirejesha nafsi zetu.”11 Kama wafuasi wa Yesu Kristo, je, hatupaswi kufanya vivyo hivyo?
Mwokozi anatuamuru tujifunze Kwake12 na kufanya mambo ambayo tumemwona akifanya.13 Yeye ni mfano halisi wa hisani, upendo safi. Tunapozidi kujifunza kufanya kile Anachotuamuru—si kwa ajili ya wajibu au hata kwa ajili ya baraka ambazo tunaweza kupokea bali kwa upendo halisi Kwake na kwa Baba yetu wa Mbinguni14—upendo Wake utatiririka kupitia kwetu na kufanya yote anayotutaka tufanye si tu yawezekane bali hatimaye yawe rahisi na mepesi zaidi15 na ya shangwe zaidi kuliko tunavyoweza kufikiri. Itahitaji mazoezi; inaweza kuchukua miaka, kama ilivyokuwa kwangu, lakini tunapotamani tu hata kuwa na upendo kama nguvu yetu ya kuleta hamasa, Yeye anaweza kuchukua hamu hiyo,16 mbegu hiyo, na hatimaye kuigeuza kuwa mti mzuri, uliojaa matunda matamu zaidi.17
Tunaimba katika mojawapo ya nyimbo zetu tunazozipenda, “Mimi ni nani kumhukumu mwingine wakati nami si mkamilifu? Mioyo iliyo kimya huficha masononeko mengi yasiyoonekana kwa macho.”18 Nani kati yetu anaweza kuwa na huzuni iliyofichika? Kijana anayeonekana kuwa mwasi, watoto waliobakia baada ya talaka, mama au baba asiye na mwenzi, wale walio na matatizo ya afya ya kimwili au ya kiakili, wale wanaotilia shaka imani yao, wale wanaopitia ubaguzi wa rangi au tamaduni, wale wanaohisi upweke, wale wanaotamani ndoa, wale walio na uraibu; na wengine wengi wanaoshughulika na aina mbalimbali za uzoefu wa maisha—hata wale ambao maisha yao yanaonekana kuwa makamilifu kwa nje.
Hakuna hata mmoja wetu aliye na maisha makamilifu wala familia yenye ukamilifu; Hata mimi sina. Tunapojaribu kuwahurumia wengine ambao pia wanapitia matatizo na kutokamilika, inaweza kuwasaidia wahisi kwamba hawako peke yao katika matatizo yao. Kila mmoja anahitaji kuhisi kwa dhati kuwa wao wamejumuishwa na wanahitajika kwenye mwili wa Kristo.19 Shauku kuu ya Shetani ni kuwagawa watoto wa Mungu, na amefanikiwa sana, lakini kuna nguvu kubwa katika umoja.20 Yahitajika kiasi gani kutembea tukiwa tumeshikana mikono katika safari hii ya maisha yenye changamoto nyingi!
Nabii wetu, Rais Russell M. Nelson, alisema, “Unyanyasaji wowote au ubaguzi juu ya mwingine kwa sababu ya utaifa, rangi, mtazamo wa kijinsia, jinsia, shahada za elimu, utamaduni au utambulisho mwingine ni chukizo kwa Muumba wetu! Unyanyasaji kama huo unatufanya tuishi chini ya kimo chetu kama wana na mabinti Zake wa agano!”21
Wakati Rais Nelson akiwaalika wote kuingia na kubaki kwenye njia ya agano inayoelekeza kwa Mwokozi wetu na Baba yetu wa Mbinguni, pia alitoa ushauri ufuatao: “Ikiwa marafiki na familia … wamejitenga na Kanisa, endelea kuwapenda. Si juu yako kuhukumu uchaguzi wa mwingine zaidi ya wewe unavyostahili kukosolewa kwa kubakia mwaminifu.”22
Marafiki, hebu tukumbuke kwamba kila mtu hapa duniani ni mtoto wa Mungu23 na Yeye anampenda kila mmoja.24 Je, kuna watu kwenye njia yako ambao umehisi kutaka kuwahukumu? Ikiwa ndivyo, kumbuka kwamba hizi ni fursa nzuri sana kwetu kufanyia kazi kupenda kama vile Mwokozi anavyopenda.25 Tunapofuata mfano Wake tunaweza kufungwa nira pamoja na Yeye na kusaidia kukuza hisia ya upendo na kujali katika mioyo ya watoto wote wa Baba yetu.
“Sisi twampenda Yeye, kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.”26 Tunapojawa na Upendo wa Mwokozi, nira Yake inaweza kuwa laini na mzigo Wake unaweza kuwa mwepesi.27 Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.