Mkutano Mkuu
Urithi wa Uhimizaji
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


14:29

Urithi wa Uhimizaji

Ninawahimiza muendelee kujitahidi kuhitimu kurudi kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, nina shukrani kukusanyika pamoja nanyi katika mkutano huu mkuu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Tumehisi imani yenu na upendo wenu popote mlipo. Tumejengwa na mafundisho yenye mwongozo, shuhuda za nguvu sana na muziki adhimu.

Ninawahimiza muendelee kujitahidi kuhitimu kurudi kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Popote mlipo katika njia ya agano, mtapata pambano dhidi ya majaribu ya kimwili ya duniani au upinzani wa Shetani.

Kama vile mama yangu alivyoniambia nilipolalamika juu ya jinsi jambo lilivyokuwa gumu, “Oh, Hal, bila shaka, ni gumu. Inapaswa kuwa hivyo. Maisha ni mtihani.”

Angesema hivyo kwa upole, hata kwa tabasamu, kwa sababu alijua mambo mawili. Bila kujali pambano, kile kilichokuwa muhimu sana ili kufika nyumbani kuwa na Baba yake wa Mbinguni. Na alijua angeweza kufanya hivyo kupitia imani katika Mwokozi wake.

Alihisi Yeye alikuwa karibu naye. Katika zile siku alipojua yu karibu kufariki, alizungumza nami kuhusu Mwokozi akiwa kitandani katika chumba chake cha kulala. Kulikuwa na mlango kwenda kwenye chumba kingine karibu na kitanda chake. Alitabasamu na kutazama mlango ule alipokuwa akiongea kwa upole juu ya kumwona Mwokozi karibuni. Bado nakumbuka nikitazama ule mlango na kuwazia chumba kilicho nyuma yake.

Sasa yu katika ulimwengu wa roho. Aliweza kukita macho yake kwenye tuzo aliyoitaka kupitia licha ya miaka mingi ya majaribu ya kimwili na kibinafsi.

Urithi wa uhimizaji aliotuachia unaelezwa vyema katika Moroni 7, ambapo Mormoni anawahimiza mwanawe Moroni na watu wake. Ni urithi wa uhimizaji kwa uzao kama ilivyokuwa wa mama yangu kwa familia yake. Mormoni alirithisha urithi wa uhimizaji kwa wote ambao walikuwa na dhamira ya kuhitimu, kupitia mitihani yote ya duniani, kwa ajili ya uzima wa milele.

Mormoni alianza katika mistari ya kwanza ya Moroni 7 na ushuhuda wa Yesu Kristo, wa malaika, na wa Roho ya Kristo, ambao huturuhusu kujua mema na maovu na kwa hiyo tuweze kuchagua jema.

Humweka Yesu Kristo kwanza, na vivyo hivyo wale wote wafanikiwao katika kutoa uhimizaji kwa wale wapambanao kupanda juu kwenye njia ya kwenda nyumbani kwao mbinguni.

“Kwani hakuna atakayeokoka, kulingana na maneno ya Kristo, isipokuwa awe na imani katika jina lake; kwani, ikiwa hivi vitu vimekoma, basi imani imekoma pia; na kutisha ni hali ya mtu, kwani ni kama hakujakuwepo na ukombozi uliofanywa.

“Lakini tazama, ndugu zangu wapendwa, ninaweza kuona vitu vyema zaidi kwenu, kwani ninaona kwamba mna imani katika Kristo kwa sababu ya uvumilivu wenu; kwani kama hamna imani ndani yake hamfai kuhesabiwa miongoni mwa watu wa kanisa lake.”1

Mormoni aliona unyenyekevu kama ushahidi wa nguvu za imani yao. Aliona kwamba wao walihisi kumtegemea Mwokozi. Aliwahimiza kwa kutambua imani hiyo. Mormoni aliendelea kuwahimiza wao kwa kuwasaidia kuona kwamba imani na unyenyekevu wao ungejenga uhakika wao na kujiamini kwao kwa ufanisi katika pambano lao.

“Na tena, ndugu zangu wapendwa, ninataka kuwazungumzia kuhusu tumaini. Inawezekanaje kwamba mtafikia imani, isipokuwa muwe na tumaini?

“Na ni kitu gani mtakachotumainia? Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake kulingana na ile ahadi.

“Kwa hivyo, ikiwa mtu ana imani lazima ahitaji kuwa na tumaini; kwani bila imani hakuwezi kuwepo na tumaini lolote.

“Na tena, tazama ninawaambia kwamba hawezi kuwa na imani na tumaini, isipokuwa awe mnyenyekevu, na mpole katika moyo.”2

Mormoni kisha anawahimiza wao kwa kuwashuhudia kuwa walikuwa kwenye njia ya kupokea kipawa cha mioyo yao kujawa na upendo safi wa Kristo. Anafuma pamoja kwa ajili yao muingiliano wa imani katika Yesu Kristo, unyenyekevu, upole, Roho Mtakatifu, na tumaini thabiti la kupata zawadi ya uzima wa milele. Anawahimiza kwa njia hii:

“Kwani hakuna yeyote anayekubaliwa mbele ya Mungu, isipokuwa yule aliye myenyekevu na mpole katika moyo; na kukiri kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Yesu ni Kristo, lazima awe na hisani; kwani kama hana hisani yeye si kitu; kwa hivyo lazima awe na hisani.”3

Nikitazana nyuma, sasa naona jinsi kipawa cha hisani—upendo safi wa Kristo—kilimuimarisha, kilimwongoza, kilimhimili na kilimbadilisha mama yangu katika pambano katika njia yake kurudi nyumbani.

“Na hisani huvumilia, na ni karimu, na haina wivu, na haijivuni, haitafuti mambo yake, haifutuki kwa upesi, haifikirii mabaya, na haifurahii uovu lakini hufurahi katika ukweli, huvumilia vitu vyote, huamini vitu vyote, hutumaini vitu vyote, hustahamili vitu vyote.

“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, kama hamna hisani, ninyi si kitu, kwani hisani haikosi kufaulu kamwe. Kwa hivyo, ambatana na hisani, ambayo ni kubwa kuliko yote, kwani vitu vyote lazima vishindwe—

“Lakini hisani ni upendo msafi wa Kristo, na inavumilia milele; na yeyote atakayepatikana nayo katika siku ya mwisho, itakuwa vyema kwake.

“Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo; ili muwe wana wa Mungu; kwamba wakati atakapoonekana tutakuwa kama yeye, kwani tutamwona vile alivyo; ili tuwe na tumaini hili; ili tutakaswe hata vile alivyo mtakatifu.4

Nina shukrani kwa uhimizaji wa mfano na mafundisho ya Mormoni. Nimebarikiwa pia na urithi wa mama yangu. Manabii kutoka Adamu hadi siku ya leo, kupitia kwa mafundisho na kwa mfano, wameniimarisha.

Kutokana na utofauti wa wale ninaowajua kibinafsi na familia zao, nachagua kutotafuta kuthibitisha undani wa mapambano yao au kuongelea juu ya vipawa vyao vikuu hadharani. Lakini bado kile nimekiona kimenihimiza na kunibadilisha kwa wema.

Nikihofia hatari ya kuingilia ufaragha wa mke wangu, nitaongeza ripoti fupi ya uhimizaji wa mke wangu. Ninafanya hivyo kwa makini sana. Yeye ni mtu msiri ambaye hatafuti wala hapendelei sifa.

Tumeoana kwa miaka 60. Ni kwa sababu ya uzoefu huo mimi sasa naelewa maana ya haya maneno ya kiroho: imani, tumaini, upole, uvumilivu, kutotafuta mambo yake mwenyewe, hufurahi katika ukweli, haufurahii uovu, na juu ya yote, hisani.5 Kwa msingi wa uzoefu huo, niweze kutoa ushuhuda kwamba wanadamu wanaweza kutumia mifano hii yote mizuri katika maisha yao ya kila siku wanapoinuka kupitia changamoto za maisha.

Mamilioni yenu mnaosikiliza mnawajua watu kama hao. Wengi wenu mu watu kama hao. Sisi sote tunahitaji mifano ya kuhimiza kama hiyo na marafiki wenye upendo kama hao.

Unapoketi na mtu fulani kama dada mhudumiaji au kaka mhudumiaji wao; unamwakilisha Bwana. Fikiria kile Yeye angefanya au kusema. Angewaalika wao kuja Kwake. Angewahimiza wao. Angetambua na kusifu mwanzo wa mabadiliko watakayohitaji kufanya. Na Yeye angekuwa mfano mkamilifu wao wa kuiga.

Hakuna anayeweza kufanya hivyo kikamilifu bado, lakini kwa kusikiliza mkutano huu, unaweza kujua upo njiani. Mwokozi anajua mapambano yako kwa undani. Yeye anajua uwezo wako mkubwa wa kukua katika imani, tumaini na hisani.

Amri na maagano anayoyatoa kwako si mitihani ya kukudhibiti. Ni vipawa vya kukuinua kuelekea kupokea vipawa vyote vya Mungu na kurejea nyumbani kwa Baba yako wa Mbinguni na Bwana, ambao wanakupenda.

Yesu Kristo alilipia thamani ya dhambi zetu. Tunaweza kudai baraka hiyo ya uzima wa milele kama tutakuwa na imani katika Yeye ya kutosha kutubu na kuwa kama mtoto, msafi na tayari kupokea kipawa kikuu kati vipawa vyote vya Mungu.

Ninaomba kwamba mtapokea mwaliko Wake na kwamba mtautoa kwa wengine wa watoto wa Baba wa Mbinguni.

Ninaomba kwa ajili ya wamisionari wetu kote duniani. Naomba wapate mwongozo wa kumhimiza kila mtu kutaka na kuamini kwamba mwaliko huu ni kutoka kwa Yesu Kristo kupitia watumishi Wake ambao wamejichukulia juu yao jina Lake.

Ninashuhudia kwamba Yeye yu hai na anaongoza Kanisa Lake. Mimi ni shahidi Wake. Rais Russell M. Nelson ni nabii aliye hai wa Mungu kwa ajili ya ulimwengu wote. Ninajua kwamba hilo ni kweli. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.