Mkutano Mkuu
Tunaweza Kuyafanya Mambo Magumu kupitia Yeye
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


10:53

Tunaweza Kuyafanya Mambo Magumu kupitia Yeye

Tunakua katika ufuasi wetu tunapoonyesha imani katika Bwana wakati wa nyakati ngumu.

Wakati wa huduma ya Mwokozi duniani, Alimwona mtu aliyekuwa kipofu. Wanafunzi wa Yesu walimwuliza, “Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu?”

Jibu la Mwokozi la uthabiti, lenye upendo na uaminifu linatuhakikishia sisi kwamba Yeye anajali mahangaiko yetu: “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake: bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”.1

Japo baadhi ya changamoto zinaweza kuja kwa sababu ya kutotii kwa makusudi, tunajua kwamba nyingi za changamoto za maisha hutokana na sababu zingine. Bila kujali vyanzo vya changamoto zetu, vinaweza kuwa fursa nzuri ya kukua.

Familia yetu haijaepushwa na dhiki za maisha. Wakati nakua, nilipendezwa na familia kubwa. Familia kama hizo zilinivutia sana, hasa wakati nilipojiunga na Kanisa katika ujana wangu kupitia mjomba wangu, Sarfo, na mkewe huko Takoradi, Ghana.

Hanna pamoja nami tulipooana, tulitamani kutimiza baraka zetu za kipatriaki, ambazo zilionyesha kwamba tungebarikiwa na watoto wengi. Hata hivyo, kabla ya kuzaliwa kwa mwana wetu wa tatu, iliwekwa dhahiri kimatibabu kwamba Hannah hangeweza kupata mtoto mwingine. Kwa shukrani, ingawa Kenneth alizaliwa katika hali ya kutishia uhai wake na mama yake, alizaliwa salama, na mama yake alipona. Kenneth alianza kushiriki kikamilifu katika maisha ya familia yetu—ikijumuisha kuhudhuria Kanisa, sala za familia za kila siku, kujifunza maandiko, jioni ya nyumbani na shughuli za burudani za kufaa.

Ingawa tulihitaji kubadili matarajio yetu ya familia kubwa, ilikuwa ni shangwe kufanyia mazoezi mafundisho kutoka “Familia: Tangazo Kwa Ulimwengu” pamoja na watoto wetu watatu wapendwa. Kufuata mafundisho hayo kuliongeza maana zaidi katika imani yangu iliyokuwa inakua.

Kama tangazo linavyosema: “Ndoa kati ya mwanamume na mwanamke ni muhimu kwa mpango Wake wa milele. Watoto wana haki ya kuzaliwa ndani ya mikataba ya ndoa, na kulelewa na baba na mama wanaoheshimu viapo vya ndoa kwa uaminifu kamili.”2 Tunapotumia kanuni hizi, tutabarikiwa.

Hata hivyo, wikiendi moja wakati wa huduma yangu kama rais wa kigingi, tulikumbwa na janga ambalo huenda likawa baya kwa wazazi kukutana nalo. Familia yetu ilirejea kutoka kwenye shughuli ya Kanisa na kukusanyika kwa mlo wa mchana. Kisha wavulana wetu watatu wakatoka nje kucheza kwenye ua wetu.

Mke wangu alihisi misukumo iliyojirudia kwamba kuna kitu kinaweza kuwa si sawa. Akaniomba niwaangalie watoto wakati tukiosha vyombo. Nilihisi walikuwa salama kwa vile tungeweza kusikia sauti zao za uchangamfu kutoka kwenye michezo yao.

Wakati sote wawili tulipoenda kuwaangalia wana wetu, kwa mshangao tulimkuta Kenneth wa miezi 18 hajiwezi ndani ya ndoo ya maji, bila kaka zake kujua. Tulimkimbiza hospitali, lakini majaribio yote ya kumfufua hayakufanikiwa.

Tuliumia moyo sana kwamba hatungekuwa na nafasi ya kumlea mtoto wetu wa thamani katika maisha haya. Ingawa tulijua Kenneth angekuwa sehemu ya familia yetu ya milele, nilijikuta nikijiuliza kwa nini Mungu angeruhusu janga hili linitokee wakati nilikuwa nafanya kila niwezalo kukuza wito wangu. Nilikuwa ndio nimerejea nyumbani baada ya kutimiza mojawapo ya wajibu wangu katika kuwahudumia Watakatifu. Kwa nini Mungu hangetazama huduma yangu na kumwokoa mwana wetu na familia yetu kutokana na janga hili? Kadiri nilivyowaza zaidi kuhusu hili, ndivyo uchungu ulivyoongezeka.

Mke wangu kamwe hakunilaumu kwa kutoshughulikia misukumo yake, lakini nilijifunza somo la kubadilisha maisha na nikaweka sheria mbili, zisizovunjwa kamwe:

Sheria ya 1: Sikiliza na uchukue hatua juu ya misukumo ya mke wako.

Sheria ya 2: Kama hauna uhakika wa sababu yoyote, rejea sheria namba 1.

Ingawa uzoefu ulikuwa wa kuumiza sana, na bado tunaomboleza, mzigo wetu mzito hatimaye ulikuwa mwepesi.3 Mimi pamoja na mke wangu tulijifunza masomo mahususi kutokana na msiba wetu. Tulihisi kuunganika na kufungwa na maagano yetu ya hekaluni; tunajua kwamba tunaweza kumrejesha Kenneth kama wetu katika ulimwengu ujao kwa sababu alizaliwa katika agano. Pia tulipata uzoefu unaohitajika wa kuwahudumia wengine na kuwahurumia kwa machungu yao. Ninashuhudia kwamba machungu yetu yametoweka kadiri tunavyoonyesha imani katika Bwana. Uzoefu wetu unaendelea kuwa mgumu, lakini tumejifunza pamoja na Mtume Paulo kwamba “tunayaweza mambo yote katika yeye [atutiaye nguvu]” kama tutafokasi Kwake.4

Rais Russell M. Nelson alifundisha: “Wakati fokasi ya maisha yetu iko katika mpango wa Mungu wa wokovu … na Yesu Kristo na injili Yake, tunaweza kuhisi furaha bila kujali nini kinatokea—au kutotokea—katika maisha yetu.” Aliongezea, “Furaha huja kutoka Kwake na kwa sababu Yake.”5

Tunaweza kujipa moyo na kujawa na amani katika nyakati zetu ngumu. Upendo tunaohisi kwa sababu ya Mwokozi na Upatanisho Wake huwa nyenzo yenye nguvu kwetu katika nyakati zetu za majaribu. “Yale yasiyo haki [na magumu] kuhusu maisha yanaweza kufanywa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.”6 Yeye aliamuru, “Ulimwenguni mnayo dhiki: lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”7 Yeye anaweza kutusaidia kuvumilia uchungu wowote, ugonjwa na majaribu tunayokabiliana nayo katika maisha.

Kuna hadithi nyingi za kimaandiko za viongozi wakuu na wenye heshima, kama Yeremia, Ayubu, Joseph Smith na Nefi, ambao hawakuachwa kutokana na mahangaiko na changamoto za duniani. Walikuwa watu ambao walijifunza kumtii Bwana hata katika mazingira magumu.8

Katika zile siku mbaya katika Jela ya Liberty, Joseph Smith alilia kwa sauti, “Ee Mungu, uko wapi? Na ni wapi lilipo hema lifichalo mahali pako pa kujificha?”9 Bwana alimfunza Jospeh kuvumilia vyema10 na aliahidi kwamba kama angefanya hivyo, mambo haya yote yangempatia uzoefu na yangekuwa kwa manufaa yake.11

Nikiangazia uzoefu wangu mwenyewe, ninatambua kwamba nimejifunza baadhi ya masomo yangu bora katika wakati wa nyakati zangu ngumu, nyakati ambazo ziliniondoa kwenye mazingira yangu ya faraja. Magumu niliyokumbana nayo kama kijana, wakati nikijifunza kuhusu Kanisa kupitia seminari, kama mwongofu mpya, na kama mmisionari na changamoto nilizokabiliana nazo katika elimu yangu, katika kujitahidi kukuza wito wangu na katika kulea familia yameniandaa kwa ajili ya siku za baadaye. Kadiri ninavyojibu kwa furaha katika mazingira magumu kwa imani katika Bwana, ndiyo zaidi ninakua katika ufuasi.

Mambo magumu katika maisha yetu yanapaswa kuja pasipo mshangao mara tunapoingia katika njia iliyosonga na nyembamba.12 Yesu Kristo alijifunza “kutii kwa mateso hayo yaliyompata.”13 Tunapomfuata Yeye, hasa katika nyakati zetu ngumu, tunaweza kukua zaidi kama Yeye.

Moja ya maagano tunayofanya na Bwana hekaluni ni kuishi sheria ya dhabihu. Dhabihu siku zote imekuwa sehemu ya injili ya Yesu Kristo. Ni ukumbusho wa dhabihu ya upatanisho mkuu wa Yesu Kristo kwa ajili ya wale wote ambao wamewahi kuishi au watakaoishi ulimwenguni.

Wamisionari wa Mzee Morrison

Ninajua kwamba Bwana siku zote hulipia tamaa zetu za haki. Unakumbuka watoto wengi nilioahidiwa katika baraka yangu ya patriaki? Hiyo baraka inatimizwa. Mimi pamoja na mke wangu tulitumikia pamoja na wamisionari mamia kadhaa, kutoka zaidi ya nchi 25, katika Misheni ya Ghana Cape Coast. Wao ni wa thamani kwetu kwa vile walikuwa kihalisia watoto wetu wenyewe.

Ninashuhudia kwamba tunakua katika ufuasi wetu tunapoonyesha imani katika Bwana wakati wa nyakati ngumu. Tunapofanya hivyo, Yeye atatuimarisha na kutusaidia kubeba mizigo yetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.