Kwa Moyo Wote
Tunapaswa kuwa wafuasi wa Yesu ambao tuna shangwe na tumetoa moyo wote katika safari yetu ya ufuasi.
Wakati mwingine, inasaidia kujua nini cha kutarajia.
Karibu na mwisho wa huduma Yake, Yesu aliwaambia Mitume Wake kwamba nyakati ngumu zingekuja. Lakini pia alisema, “Angalieni msifadhaike.”1 Ndiyo, angeondoka, lakini asingewaacha peke yao.2 Angemtuma Roho Wake kuwasaidia kukumbuka, kusimama imara na kupata amani. Mwokozi anatimiza ahadi yake ya kuwa pamoja na wafuasi Wake, lakini lazima tuendelee kumtazama Yeye ili atusaidie kutambua na kufurahia uwepo Wake.
Siku zote wafuasi wa Kristo wamekutana na nyakati ngumu.
Rafiki yangu mpendwa alinitumia makala ya zamani kutoka kwenye Nebraska Advertiser, gazeti la Magharibi ya kati ya Marekani, la tarehe 9 Julai, 1857. Ilisomeka: “Leo mapema asubuhi kundi la Wamormoni lilipita katika safari yao ya kwenda Salt Lake. Wanawake (sio dhaifu sana kwa hakika) wakikokota mikokoteni kama wanyama, [mwanamke] mmoja alianguka chini kwenye tope hili jeusi, ikasababisha msafara kusimama kidogo, watoto wadogo walijikokota wakiwa wamevalia mavazi ya [ajabu] ya kigeni wakionekana wenye ari kama mama zao.”3
Nimemfikiria sana huyu mwanamke aliyelowa tope. Kwa nini alikuwa akivuta peke yake? Je alikuwa mjane? Ni nini kilichompa nguvu ya ndani, ujasiri, ustahimilivu wa kusafiri safari hiyo ya kuumiza kupitia kwenye tope, akivuta mali yake yote kwa mkokoteni hadi kwenye jangwa lisilojulikana—nyakati fulani akidhihakiwa na watazamaji?4
Rais Joseph F. Smith alizungumza kuhusu nguvu ya ndani ya wanawake hawa waanzilishi, akisema: “Je, ungeweza kumgeuza mmoja wa wanawake hawa kutoka kwenye dhamira zao katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho? Je, ungeweza kutia kiza akili zao kuhusu misheni ya Nabii Joseph Smith? Je, ungeweza kuwapofusha kuhusu misheni takatifu ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu? La, kamwe katika ulimwengu huu usingeweza kufanya hivyo. Kwa nini? Kwa sababu walijua. Mungu alifunua kwao, na walielewa, na hakuna nguvu yoyote duniani ambayo ingeweza kuwageuza kutoka kwenye kile walichojua kuwa ukweli.”5
Akina kaka na akina dada, kuwa wanaume na wanawake kama hao ni mwito wa siku zetu—wafuasi tunaopambana ili kupata nguvu ya kuendelea kuvuta tunapoitwa kutembea nyikani, wafuasi wenye dhamira iliyofunuliwa kwetu na Mungu, wafuasi wa Yesu tulio na furaha na kwa moyo wote tukisonga katika safari yetu binafsi ya ufuasi. Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunaamini na tunaweza kukua katika kweli tatu muhimu.
Kwanza, Tunaweza Kushika Maagano Yetu, Hata Wakati Si Rahisi
Wakati imani yako, familia yako au kesho yako vinapopata changamoto—wakati unapojiuliza kwa nini maisha ni magumu sana wakati unafanya uwezavyo kuishi injili—kumbuka kwamba Bwana alituambia tutegemee taabu. Taabu ni sehemu ya mpango na haimaanishi kuwa umeachwa; taabu ni sehemu ya kile inachomaanisha kuwa Wake.6 Kwani hata Yeye alikuwa “mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko.”7
Ninajifunza kwamba Baba wa Mbinguni anavutiwa zaidi na ukuaji wangu kama mfuasi wa Yesu Kristo kuliko kuishi kwangu kwa kuridhika. Huenda sitaki iwe hivyo siku zote—lakini ndivyo ilivyo!
Kuishi kwa urahisi hakuleti nguvu. Nguvu tunazohitaji kustahimili joto la siku yetu ni nguvu za Bwana na nguvu Zake hutiririka kupitia maagano yetu pamoja Naye.8 Kuendelea kuonyesha imani yetu tunapokabiliana na upepo mkali—kujitahidi kwa dhati kila siku kufanya kile tulichoagana na Mwokozi kuwa tungefanya, hata na hasa tunapokuwa tumechoka, tuna wasiwasi na tunapambana na maswali na masuala yanayosumbua—humaanisha kupokea hatua kwa hatua nuru Yake, nguvu Zake, upendo Wake, Roho Wake, amani Yake.
Kiini cha kuenenda kwenye njia ya agano ni kumkaribia Mwokozi. Yeye ndiye kiini, wala si maendeleo yetu yenye ukamilifu. Haya si mashindano ya mbio, na hatupaswi kulinganisha safari yetu na ya wengine. Hata tunapojikwaa, Yeye yupo.
Pili, Tunaweza Kutenda kwa Imani
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunaelewa kwamba imani katika Yeye inahitaji matendo—hasa katika nyakati ngumu.9
Miaka mingi iliyopita, wazazi wangu waliamua kuweka zulia jipya kwenye nyumba. Usiku kabla ya zulia jipya kufika, mama yangu aliwaomba kaka zangu waondoe samani na kung’oa mazulia ya chumbani ili zulia jipya liweze kuwekwa. Dada yangu Emily, akiwa na miaka 7 wakati huo, alikuwa tayari amelala. Kwa hiyo, akiwa amelala, waliondoa samani zote kutoka chumbani kwake kimya kimya, isipokuwa kitanda, na kisha walichana zulia. Na, kama ambavyo kaka wakubwa hufanya nyakati zingine, waliamua kufanya mchezo wa mzaha. Walitoa vitu vyake vilivyosalia chumbani na kwenye kuta, na kuacha chumba tupu. Kisha wakaandika ujumbe na kuubandika ukutani: “Mpendwa Emily, tumehama. Tutakuandikia siku chache zijazo na kukuambia tulipo. Kwa Upendo, familia yako.”
Asubuhi iliyofuata Emily hakutokeza kupata kiamsha kinywa, kaka zangu walienda kumtazama—walimkuta, akiwa mwenye huzuni na mpweke nyuma ya mlango uliofungwa. Emily baadaye alielezea uzoefu huu: “Nilivunjika moyo. Lakini nini kingetokea kama tu ningefungua mlango? Ningesikia nini? Ningenusa nini? Ningejua kuwa sipo peke yangu. Ningejua kwamba nilipendwa kwa dhati. Wazo hata halikupita akilini mwangu la kufanya jambo kuhusu hali yangu. Nilikata tamaa na kubaki chumbani kwangu nikilia tu. Lakini kama tu ningefungua mlango.”10
Dada yangu alikuwa na dhana kulingana na kile alichokiona, lakini haikuwa taswira ya jinsi mambo yalivyokuwa hasa. Je, si ya kuvutia kwamba sisi, kama Emily, tunaweza kulemewa na huzuni au maumivu au kukatishwa tamaa au wasiwasi au upweke au hasira au kufadhaika kiasi kwamba hatupati wazo la kufanya chochote, kufungua mlango, kutenda kwa imani katika Yesu Kristo?
Maandiko yamejawa na mifano ya wanaume na wanawake, wafuasi wa Kristo, ambao, walipokabiliwa na yasiyowezekana, walitenda tu—waliinuka kwa imani na kutembea.11
Kwa wenye ukoma waliotafuta uponyaji, Kristo alisema, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa, walipokuwa wakienda, walitakasika.”12
Walienda kujionyesha kwa makuhani kana kwamba walikuwa tayari wameponywa, na katika mchakato wa kutenda, waliponywa.
Pia ninataka kusema kama wazo la kuchukua hatua katikati ya maumivu yako haliwezekani, tafadhali acha hatua yako iwe kutafuta usaidizi—kwa rafiki, mwanafamilia, kiongozi wa Kanisa, mtaalamu. Hii inaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea tumaini.
Tatu, Tunaweza Kujitoa kwa Moyo Wote na kuwa Wenye Shangwe katika Uaminifu Wetu13
Nyakati ngumu zinapokuja, ninajaribu kukumbuka kwamba nilichagua kumfuata Kristo kabla sijaja duniani na kwamba changamoto kwenye imani yangu, afya yangu na uvumilivu wangu vyote ni sehemu ya sababu ya mimi kuwa hapa. Na kamwe sipaswi kufikiri kwamba jaribu la leo linatilia shaka upendo wa Mungu kwangu au kuruhusu ligeuze imani yangu Kwake kuwa shaka. Taabu hazimaanishi kuwa mpango una dosari; ni sehemu ya mpango zilizokusudiwa kunisaidia kumtafuta Mungu. Ninakuwa zaidi kama Yeye ninapovumilia kwa subira na kwa tumaini, kama Yeye, katika uchungu, ninaomba kwa bidii zaidi.14
Yesu Kristo alikuwa kielelezo kamili cha kumpenda Baba yetu kwa moyo Wake wote—cha kufanya mapenzi Yake, bila kujali gharama.15 Ninataka kufuata mfano wake kwa kufanya vivyo hivyo.
Ninavutiwa na ufuasi wa moyo wote, nafsi yote ya mjane aliyetoa senti zake mbili katika hazina ya hekalu. Alitoa vyote alivyokuwa navyo.16
Yesu Kristo alitambua wingi wa alivyokuwa navyo wakati wengine waliona tu upungufu wake. Ndivyo ilivyo kwa kila mmoja wetu. Yeye haoni upungufu wetu kama kushindwa bali kama fursa ya kuonyesha imani na kukua.
Hitimisho
Wafuasi wenzangu wa Yesu Kristo, kwa moyo wangu wote, ninachagua kusimama na Bwana. Ninachagua kusimama na watumishi Wake waliochaguliwa—Rais Russell M. Nelson na Mitume wenzake—kwani wanazungumza kwa niaba Yake na ni wasimamizi wa ibada na maagano ambayo huniunganisha mimi kwa Mwokozi.
Ninapojikwaa, nitaendelea kuinuka, nikitegemea neema na nguvu ya kuwezesha ya Yesu Kristo. Nitabaki katika agano langu Naye na kufanyia kazi maswali yangu kwa kujifunza neno la Mungu, kwa imani na kwa usaidizi wa Roho Mtakatifu, ambaye ninatumaini mwongozo wake. Nitamtafuta Roho Wake kila siku kwa kufanya mambo madogo na rahisi.
Hii ndiyo njia yangu ya ufuasi.
Na hadi siku ambayo majeraha ya kila siku ya dunia yatakapoponywa, nitamngoja Bwana na kumtumaini Yeye—wakati Wake, hekima Yake, mpango Wake.17
Nikiwa nimeshikamana nanyi, nataka kusimama Naye milele. Kwa moyo wote. Nikijua kwamba tunapompenda Yesu Kristo kwa mioyo yetu yote, Yeye hutubariki kwa vyote kama malipo.18 Katika jina la Yesu Kristo, amina.