Je, Bado Uko Radhi
Kuwa kwetu radhi kumfuata Yesu Kristo kunaenda sawa sawa na kiwango cha muda tunaotoa kuwa katika mahali patakatifu.
Jumapili moja, wakati nikijiandaa kupokea sakramenti baada ya wiki kadhaa za majukumu ya mkutano wa kigingi, wazo la kuvutia lilipita mawazoni mwangu.
Wakati kuhani alipoanza kutoa baraka ya mkate, maneno niliyoyasikia mara nyingi hapo kabla yalipita kwa nguvu kwenye mawazo na moyo wangu. “Na kushuhudia kwako, Ee Mungu, Baba wa Milele, kwamba wako radhi kujichukulia juu yao jina la Mwanao, na daima kumkumbuka na kushika amri zake ambazo amewapa, ili Roho wake apate kuwa pamoja nao.”1 Je, ni mara ngapi tumeshuhudia kwa Mungu kwamba tuko radhi?
Nilipotafakari umuhimu wa maneno hayo matakatifu, neno radhi lilinivutia sana kuliko hapo kabla. Mafuriko ya uzoefu mzuri na mtakatifu yalijaza mawazo na moyo wangu kwa upendo na shukrani kwa dhabihu ya upatanisho ya Mwokozi na jukumu lake muhimu katika mpango wa Baba wa ukombozi kwa ajili yangu na familia yangu. Kisha nilisikia na kuhisi kupenya kwa maneno ya sala ya maji: “Kwamba washuhudie kwako … kwamba daima wamkumbuke.”2 Nilielewa dhahiri katika wasaa ule kwamba kushika maagano yangu lazima kuwe zaidi ya kusudi jema.
Kupokea sakramenti si ibada ya kale ya dini ikionesha ukubali wetu tu. Ni ukumbusho wenye nguvu wa uhalisia wa Upatanisho usio na mwisho wa Kristo na hitaji la daima kumkumbuka Yeye na kushika amri Zake. Utayari wa kufokasi kwa Mwokozi ni muhimu sana ni kiini cha ujumbe wa maandiko yanayonukuliwa sana Kanisani: sala za sakramenti. Kuelewa ukweli wa kile ambacho Baba wa Mbinguni anampa kila mmoja wetu kwa hiari kupitia Mwana Wake wa Pekee kunapaswa kuamsha juhudi zetu za dhati za daima kuwa radhi kama malipo.
Je, msingi wetu wa kiroho umejengwa imara juu ya Yesu Kristo?
Ikiwa msingi wetu wa kiroho hauko imara au hauna kina, tunaweza kugeuzwa kukita utayari wetu kwenye kujiuliza ikiwa kuna faida kijamii au la au kiwango cha usumbufu binafsi. Na kama tutakumbatia mtazamo kwamba Kanisa linaundwa na sera za kizamani au sera za kijamii ambazo si sahihi kisiasa, mazuio binafsi yasiyo na uhalisia na masharti ya muda, basi hitimisho letu kuhusu kuwa radhi litakuwa dhaifu vilevile. Hatupaswi kutarajia kanuni ya kuwa radhi ipate mashiko chanya kwa washawishi wa mitandao ya kijamii au wapenzi wa TikTok. Kanuni za wanadamu mara chache sana zinakubaliana na ukweli mtakatifu.
Kanisa ni mahala pa kukusanyika kwa watu wasio wakamilifu wanaompenda Mungu na ambao wako radhi kumfuata Bwana Yesu Kristo. Kuwa radhi huko kumekita mizizi kwenye uhalisia kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Ukweli huu mtakatifu unaweza kujulikana tu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Kwa hiyo, kuwa kwetu radhi kunaenda sawa sawa na kiwango cha muda tunaotoa kuwa katika mahali patakatifu ambapo ushawishi wa Roho Mtakatifu unapatikana.
Tutaonesha busara kutumia muda zaidi kwenye mazungumzo yenye maana tukijadili dukuduku zetu na Baba mwenye upendo wa Mbinguni na muda mchache kutafuta mawazo ya sauti zinginezo. Tunaweza pia kuchagua kubadili vyanzo vyetu vya habari vya kila siku kuwa maneno ya Kristo kwenye maandiko na maneno ya kinabii ya manabii Wake walio hai.
Umuhimu tunaoweka kwenye kuitunza kwetu sabato, kulipa zaka kwa uaminifu, kuwa na kibali hai cha hekaluni, kuhudhuria hekaluni na kuheshimu maagano yetu matakatifu ya hekaluni vyote ni viashiria vyenye nguvu vya kuwa kwetu radhi na ushahidi wa msimamo wetu. Je, tuko radhi kuweka mbele juhudi zaidi kwenye kuimarisha imani yetu katika Kristo?
Baba wa Mbinguni anatupenda kwa ukamilifu, lakini upendo huo huja na matarajio makubwa. Yeye anatarajia sisi tuwe radhi kumweka Mwokozi awe kiini hasa cha maisha yetu. Mwokozi ni mfano wetu mkamilifu wa kuwa radhi kujinyenyekeza kwa Baba kwenye mambo yote. Yeye ndiye “njia, kweli na uzima.”3 Yeye alikuwa radhi kulipia dhambi zetu. Yeye yu radhi kuifanya rahisi mizigo yetu, hutuliza hofu zetu, hutupatia nguvu na huleta amani na uelewa kwenye mioyo yetu katika nyakati za mateso na huzuni.
Lakini bado imani katika Yesu Kristo ni uchaguzi. “Ikiwa [sisi] hatuwezi ila kutamani kuamini”4 kwa maneno Yake, tunakuwa na mahala pa kuanzia au pa kurekebisha upya safari yetu ya imani. Maneno Yake, ikiwa yatapandwa ndani ya mioyo yetu kama mbegu na kutunzwa kwa uangalizi mkubwa, yatakuwa na mizizi na imani yetu itakua kwenye hakikisho na kuwa kanuni ya matendo na nguvu. Kitabu cha Mormoni ni nyenzo yetu yenye nguvu ya kukuza na kurejesha imani yetu. Kuwa radhi ni chachu ya imani.
Maisha ya duniani, kwa usanifu mtakatifu, si rahisi na nyakati zingine yanaweza kuchosha. Hata hivyo, “[sisi] tupo, ili [sisi] tuweze kuwa na shangwe”!5 Kufokasi kwa Mwokozi na maagano yetu matakatifu huleta shangwe ya kudumu! Lengo la maisha ya duniani ni kuthibitisha kuwa kwetu radhi. “Jukumu kubwa la maisha [na gharama ya ufuasi] ni kujifunza mapenzi ya Bwana na kisha kuyafanya.”6 Ufuasi wa kweli huongoza kwenye ukamilifu wa shangwe. Je, tuko radhi kulipa gharama ya ufuasi?
Njia ya agano si orodha rahisi ya kuweka vema; ni mchakato wa ukuaji kiroho na kuongeza msimamo kwa Bwana Yesu Kristo. Kiini cha lengo la kila amri, kanuni, agano na ibada ni kujenga imani na tumaini katika Kristo. Ari yetu ya kukita maisha yetu kwa Kristo, kwa hiyo, inapaswa kuwa endelevu—si ya masharti, kutegemea hali au dhaifu. Hatuwezi kumudu kwenda mapumzikoni au kujipa muda wa kutofanyia kazi kuwa kwetu radhi “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote na katika mahali popote.”7 Ufuasi si rahisi, kwa sababu wenza wa Roho Mtakatifu hauna gharama.
Hakika Bwana alifikiria siku yetu pale alipofundisha mfano wa wanawali kumi. Kwa watano wenye busara, Yeye alisema: “wamemchukua Roho Mtakatifu kuwa kiongozi wao na hawajadanganyika,”8 wakati taa za wapumbavu “zinazimika” kwa kukosa mafuta.9 Pengine maneno ya Nefi yanawaelezea vyema waumini hawa wa Kanisa ambao awali walikuwa waaminifu: “Na wengine atawapatanisha na awapatie usalama wa kimwili, kwamba watasema: Yote yako salama Sayuni.”10
Usalama wa kimwili ni kutafuta na kutumaini vitu vya kidunia badala ya Kristo—kwa maneno mengine, kutazama kupitia lenzi ya dunia badala ya lenzi ya kiroho. Roho Mtakatifu hutupatia uwezo wa kuona “vitu kama vilivyo, na … kama vitavyokuwa.”11 “Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu pekee [tunaweza] kujua ukweli wa vitu vyote”12 na kutodanganyika. Tunamweka Kristo kuwa kiini cha maisha yetu na kutamka kuwa kwetu radhi kushika amri Zake si kwa sababu hatuoni bali kwa sababu tunaweza kuona.13
Vipi kuhusu wanawali wapumbavu? Kwa nini hawakuwa radhi kubeba chupa ya mafuta ya kiroho? Je, waliahirisha tu? Pengine walikuwa wa kawaida sana kwa sababu ilikuwa usumbufu au ilionekana si muhimu? Bila kujali sababu, walidanganyika kuhusu jukumu muhimu la Kristo. Huu ni udanganyifu muhimu wa Shetani na sababu ya taa zao za ushuhuda hatimaye kuzimika kwa kukosa mafuta ya kiroho. Mfano huu ni mfanano wa siku zetu. Wengi humwacha Mwokozi na maagano yao muda mrefu kabla ya kuacha Kanisa Lake.
Tunaishi nyakati zisizo na kifani zilizotabiriwa zamani na manabii wa kale, siku ambayo Shetani atavuma “mioyoni mwa watoto wa watu, na [awavuruge] wakasirikie yale ambayo ni mema”14 Wengi wetu tunaishi katika ulimwengu wa mtandaoni uliofurikwa na burudani na kutuma jumbe zilizo kinyume na utambulisho wa kiungu na kuamini katika Kristo.
Ushawishi wa kiroho wenye nguvu zaidi katika maisha ya mtoto ni mfano wa uadilifu wa wazazi na bibi na babu wenye upendo ambao kwa uaminifu hushika maagano yao matakatifu. Wazazi wenye kusudi huwafunza watoto wao imani katika Bwana Yesu Kristo, ili kwamba watoto pia “wajue asili ya kutegemea msamaha wa dhambi zao.”15 Ushikaji wa maagano wa kawaida na usio endelevu huongoza kwenye kujeruhiwa. Hasara ya kiroho mara zote ni kubwa kwa watoto na wajukuu zetu. Wazazi na bibi na babu, je, bado tuko radhi?
Rais Russell M. Nelson ameonya kwamba “Katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila ushawishi wenye mwongozo, maelekezo, faraja na endelevu wa Roho Mtakatifu.”16 Hili ni onyo la wazi na sahihi la kurekebisha taa zetu na kuongeza akiba ya mafuta yetu ya kiroho. Je, bado tuko radhi kuwafuata manabii walio hai? Ni kipi kiwango cha mafuta ya kiroho kwenye taa yako? Ni mabadiliko yapi katika maisha yako binafsi yatakuwezesha kuwa na ushawishi wa Roho Mtakatifu daima?
Leo, kama vile katika siku za Yesu, kutakuwa na wale watakaorudi nyuma, wasio radhi kukubali gharama ya ufuasi. Wakati ukosoaji mkali na wenye chuki unapoelekezwa kwa Kanisa la Mwokozi na kwa wale wanaomfuata, ufuasi wetu utahitaji utayari wetu mkubwa wa kunyoosha na kuimarisha uti wetu wa mgongo wa kiroho na kutowasikiliza.17
Ikiwa msingi wetu wa kiroho umejengwa imara juu ya Yesu Kristo, hatutaanguka na hatupaswi kuogopa.
“Tazama, Bwana anahitaji moyo na akili yenye kukubali; na wenye kukubali na kutii watakula mema ya Sayuni katika siku za mwisho.”18
Na daima tuwe radhi. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.