Mkutano Mkuu
Aliinuliwa Juu ya Msalaba
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


13:6

Aliinuliwa Juu ya Msalaba

Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo mtu lazima wakati mwingine abebe mzigona kwenda mahali ambako dhabihu inahitajika na mateso hayaepukiki.

Miaka mingi iliyopita, kufuatia mjadala wa shule ya wahitimu juu ya historia ya kidini ya Amerika, mwanafunzi mwenzangu aliniuliza, “Kwa nini Watakatifu wa Siku za Mwisho hawajaasili msalaba ambao Wakristo wengine wanautumia kama alama ya imani yao?”

Kwa vile maswali kama haya kuhusu msalaba mara nyingi ni swali kuhusu dhamira yetu kwa Kristo, mara moja nilimwambia kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linazingatia dhabihu ya upatanisho ya Yesu Kristo kuwa kiini, msingi muhimu, fundisho kuu na onyesho kuu la upendo wa kiungu katika mpango mkuu wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa watoto Wake.1 Nilielezea kwamba neema ya kuokoa iliyo katika tendo hilo ilikuwa muhimu na ilitolewa kama zawadi kwa ulimwengu wote kwa familia nzima ya mwanadamu kuanzia kwa Adamu na Hawa hadi mwisho wa ulimwengu.2 Nilimnukuu Nabii Joseph Smith, aliyesema, “Vitu … vyote vihusianavyo na dini yetu ni viambatisho tu” kwenye Upatanisho wa Yesu Kristo.3

Kisha nilimsomea kile alichoandika Nefi miaka 600 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu: “Na … malaika akanizungumzia … , akisema: Angalia! Na nikaangalia na nikamwona Mwanakondoo wa Mungu, … [ambaye] aliinuliwa juu ya msalaba na kuuawa kwa dhambi za ulimwengu.”4

Nikiwa na bidii yangu ya “kupenda, kushiriki na kualika” kwa kiwango cha juu, niliendelea kusoma! Kwa Wanefi katika Bara ya Amerika Mwokozi aliyefufuka alisema, “Baba yangu alinituma ili nipate kuinuliwa juu kwenye msalaba; … kwamba ningeleta watu wote kwangu, … na kwa sababu hii nimeinuliwa juu.”5

Nilikuwa nakaribia kumnukuu Mtume Paulo ndipo niligundua kwamba macho ya rafiki yangu yalianza kuangaza angaza. Akiangalia kwa haraka kwenye saa yake ya mkononi ilionekana kumkumbusha kwamba alihitajika kuwa mahali fulani—popote—na akaondoka mbio kwenda kwenye ahadi yake ya uongo. Maongezi yetu yakaishia hivyo.

Asubuhi hii, miaka 50 baadaye, nimedhamiria kumalizia maelezo yale—hata kama kila mmoja wenu ataanza kuangalia saa yake ya mkononi. Ninapojaribu kuelezea kwa nini sisi kwa ujumla hatutumii alama ya msalaba, ningependa kuweka wazi heshima yetu ya kina na matamanio ya dhati kwa imani iliyojaa dhamira na maisha ya kujitoa ya wale wanaofanya hivyo.

Sababu moja ambayo sisi hatutilii mkazo msalaba kama alama inatokana na vyanzo vyetu vya Kibiblia. Kwa sababu kusulubiwa ilikuwa moja ya njia kali sana za kuua za utawala wa Kirumi, wafuasi wengi wa mwanzoni wa Yesu walichagua kutoangazia aina hiyo ya kikatili ya mateso. Maana iletwayo na kifo cha Kristo kwa hakika ilikuwa kitovu cha imani yao, lakini kwa takribani miaka mia tatu walitafuta kufikisha utambulisho wao wa injili kupitia njia zingine.6

Mnamo karne ya nne na ya tano, msalaba ulikuwa unatambulishwa kama alama ya Ukristo wa pamoja, lakini dini yetu haipo kwenye “Ukristo wa pamoja” Sisi si Wakatoliki au Waprotestanti, sisi, badala yake, ni wa kanisa lililorejeshwa, kanisa lililorejeshwa la Agano Jipya. Hivyo, asili na mamlaka yetu hurudi nyuma kabla ya wakati wa mabaraza, kanuni za imani na sanaa ya matumizi ya alama.7 Katika hali hii, kutokuwepo kwa alama ambayo ilichelewa kuja katika matumizi ya kawaida bado ni ushahidi mwingine kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni urejesho wa kweli wa kuanza kwa Ukristo.

Sababu nyingine ya kutotumia alama ya msalaba iliyopo ni msisitizo wetu juu ya muujiza kamili wa huduma ya Kristo—Ufufuko Wake mtukufu pamoja na mateso na kifo chake cha kidhabihu. Katika kusisitiza uhusiano huo, naonyesha vipande viwili vya sanaa8 ambavyo hutumika kama mwonekano wa nyuma wa ukutani kwa ajili ya Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili katika mikutano yao mitakatifu ya hekaluni kila Alhamisi huko Jijini Salt Lake. Sanaa hizi zinatumika kama ukumbusho endelevu kwetu juu ya fidia ambayo ililipwa na ushindi uliopatikana kupitia Kwake Yeye ambaye sisi ni watumishi Wake.

Kusulubishwa, na Harry Anderson
Kufufuka, na Harry Anderson

Uwakilishi wa wazi zaidi wa sehemu mbili za ushindi wa Kristo ni matumizi yetu ya picha hii ndogo ya Thorvaldsen ya Kristo aliyefufuka akitokea katika utukufu kutoka kaburini akiwa bado na majeraha ya Kusulubiwa Kwake.9

Nembo ya Kanisa

Sababu ya mwisho, tujikumbushe wenyewe kwamba Rais Gordon B. Hinckley aliwahi kusema, “Maisha ya watu wetu lazima [yawe] … alama ya [imani] yetu.”10 mazingatio haya—hasa hili la mwisho—huniongoza kwenye marejeleo ya msingi sana ya maandiko yahusianayo na msalaba. Haihusiani kwa vyovyote na vidani au vito, minara au mabango. Badala yake, inahusiana na uadilifu usiotingishika na maadili thabiti ambayo Wakristo wanapaswa kuyaonyesha kwenye wito ambao Yesu ameutoa kwa kila mmoja wa wafuasi Wake. Katika kila nchi na umri, Yeye amesema kwetu sote, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.”11

Hii inaongelea juu ya misalaba tunayoibeba kuliko ile tunayovaa. Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo mtu lazima wakati mwingine abebe mzigo—wa kwako mwenyewe au wa mtu mwingine—na kwenda mahali ambako dhabihu inahitajika na mateso hayaepukiki. Mkristo wa kweli hawezi kumfuata Mwalimu kwa masuala yale tu ambayo yeye anakubaliana nayo. La hasha. Tunamfuata Yeye kila mahali, ikijumuisha, kama ni muhimu, ndani ya viwanja vilivyojaa machozi na taabu, ambako wakati mwingine yawezekana tukasimama peke yetu.

Ninawajua watu, ndani na nje ya Kanisa, ambao wanamfuata Kristo kwa uaminifu kama huo. Ninawajua watoto wenye ulemavu mkubwa wa kimwili, na ninawajua wazazi ambao wanawatunza. Wakati mwigine ninawaona wakifanya kazi hadi kuchoka kabisa, wakitafuta nguvu, usalama na nyakati chache za furaha ambazo haziji kabisa. Ninawajua watu wazima wengi waseja ambao wanatamani, na wanastahili, mwenza mwenye upendo, ndoa nzuri na nyumba iliyojaa watoto wa kwao wenyewe. Hilo ni tamanio la haki zaidi, lakini mwaka hadi mwaka bahati nzuri kama hiyo bado haitokezei. Ninawajua wale ambao wanapambana na ugonjwa wa afya ya akili wa aina nyingi, ambao wanaomba msaada wanaposali na kutamani na kupambania nchi ya ahadi ya utulivu wa kihisia. Ninawajua wale wanaoishi na umaskini unaodhoofisha lakini, bila kukata tamaa, huomba tu nafasi ya kufanya maisha mazuri kwa ajili ya wapendwa wao na wengine wenye shida wanaowazunguka. Nawajua wengi wanaohangaika na masuala ya utambulisho, jinsi na jinsia. Ninalia kwa ajili yao, na ninalia pamoja nao, nikijua umuhimu wa matokeo ya chaguzi zao yatakavyokuwa.

Hizi ni chache tu ya hali nyingi ngumu tunazoweza kukumbana nazo maishani, ukumbusho wa dhati kwamba kuna gharama kwenye ufuasi. Kwa Arauna, aliyejaribu kumpatia Daudi mafahali ya ng’ombe bure na kuni kwa ajili ya sadaka yake ya kuteketeza, Mfalme Daudi alisema “Hapana; bali hakika nitanunua kwako kwa bei: … [kwani Mimi] [sitamtolea] … Bwana Mungu wangu … kile ambacho hakinigharimu chochote.”12 Na sisi sote, pia, tuseme hivyo.

Tunapochukua misalaba yetu na kumfuata Yeye, itakuwa ya kuhuzunisha kabisa kama uzito wa changamoto zetu haukutufanya kuwa wenye huzuni na wasikivu zaidi kwa mizigo iliyobebwa na wengine. Hiki ni moja ya vitendawili vyenye nguvu vya Kusulubiwa kwamba mikono ya Mwokozi ilinyooshwa wazi na kisha kugongelewa misumari, bila kujua lakini kwa usahihi kabisa kuonyesha kwamba kila mwanaume, mwanamke na mtoto katika familia yote ya mwanadamu siyo tu anakaribishwa bali pia anaalikwa katika kumbatio Lake lenye kukomboa na kuinua.13

Kama vile Ufufuko mtukufu uliotokea baada ya Usulubisho wa uchungu, ndivyo baraka za kila aina zinavyomwagwa juu ya wale walio tayari, kama nabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo anavyosema, “kuamini katika Kristo, na kutazama kifo Chake, na kuukubali msalaba Wake.” Wakati mwingine baraka hizi huja mapema na wakati mwingine huja baadaye, lakini hitimisho la kupendeza kwetu tukipita katika njia ya mateso14 ni ahadi kutoka kwa Bwana Mwenyewe kwamba zinakuja. Ili kupata baraka hizo, naomba tumfuate Yeye—bila kushindwa, pasipo kuyumba wala kukimbia, pasipo kutegea katika jukumu, siyo tu wakati misalaba yetu ni mizito na siyo wakati, njia inapozidi kuwa na kiza. Kwa ajili ya nguvu zako, utiifi na upendo, ninatoa shukrani binafsi za dhati. Siku hii ninatoa ushahidi wa kitume wa Yeye “aliyeinuliwa”15 na wa baraka za milele anazozitoa kwa wale “wanaoinuliwa” pamoja Naye, hata Bwana Yesu Kristo, amina.

Mihtasari

  1. Ona Jeffrey R. Holland, Encyclopedia of Mormonism (1992), “Atonement of Jesus Christ,” 1:83.

  2. Amuleki anaongea juu ya Upatanisho wa Kristo kama “dhabihu kuu na ya mwisho” ikiwa “isiyo na mwisho na ya milele” katika kiwango chake (Alma 34:10). Kwa maana “wote wameanguka na kupotea, na lazima waangamie isipokuwa imekuwa kupitia upatanisho huu” (Alma 34:9; ona pia mistari ya 8–12). President John Taylor adds: “In a manner to us incomprehensible and inexplicable, [Jesus] bore the weight of the sins of the whole world; not only of Adam, but of his posterity; and in doing that, opened the kingdom of heaven, not only to all believers and all who obeyed the law of God, but to more than one-half of the human family who die before they come to years of maturity, as well as to [those] who, having died without law, will, through His mediation, be resurrected without law, and be judged without law, and thus participate … in the blessings of His atonement” (An Examination into and an Elucidation of the Great Principle of the Mediation and Atonement of Our Lord and Savior Jesus Christ [1892], 148–49; Teachings of Presidents of the Church: John Taylor [2001], 52–53).

  3. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 49.

  4. 1 Nefi 11:32–33.

  5. 3 Nefi 27:14–15.

  6. Yapo, ndiyo, marejeleo juu ya msalaba katika mafundisho ya Paulo (ona, kwa mfano, 1 Wakorintho 1:17–18; Wagalatia 6:14; Wafilipi 3:18), lakini haya yanaongelea kwa mambo mengine makubwa zaidi kuliko zile boriti mbili zilizopigiliwa misumari kwa pamoja, au alama yoyote ndogo ya jinsi hiyo. Hivyo, Paulo anapoongelea juu ya msalaba, yeye anatumia hatimkato ya kimafundisho ili kuongelea kuhusu ukuu wa Upatanisho, uwanja ambao Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa utayari kabisa huungana naye na kumnukuu.

  7. Early and traditional Christian figures such as Martin Luther’s associate Andreas Karlstadt (1486–1541) were arguing by the late Middle Ages that “the crucifix [on its own] depicted only Christ’s human suffering and neglected to display his resurrection and redemptive [powers]” (in John Hilton III, Considering the Cross: How Calvary Connects Us with Christ [2021], 17).

  8. Harry Anderson, The Crucifixion; Harry Anderson, Mary and the Resurrected Lord.

  9. See Russell M. Nelson, “Kufungua Mbingu kwa ajili ya Msaada,” Liahona, May 2020, 72–74.

  10. Gordon B. Hinckley, “The Symbol of Christ,” Ensign, May 1975, 92.

  11. Mathayo 16:24.

  12. 2 Samweli 24:24.

  13. “Mkono Wake umenyoshwa kwa watu wote watakaotubu na kuamini katika jina Lake” (Alma 19:36; ona pia 2 Nefi 26:33; Alma 5:33).

  14. Via dolorosa is a Latin phrase meaning “a painfully difficult route, passage, or series of experiences” (Merriam-Webster.com Dictionary, “via dolorosa”). It is most often associated with Jesus’s movement from His condemnation at the hand of Pilate to His Crucifixion on Calvary.

  15. Ona 3 Nefi 27:14–15.