Uwe Mkweli kwa Mungu na Kazi Yake
Sote tunahitaji kutafuta ushuhuda wetu wenyewe wa Yesu Kristo, kudhibiti tamaa zetu, kutubu dhambi zetu na kuwa wakweli kwa Mungu na kazi Yake.
Mnamo Oktoba iliyopita, nilipewa kazi, pamoja na Rais M. Russell Ballard na Mzee Jeffrey R. Holland, kutembelea Uingereza, ambapo sote watatu tulihudumu kama wamisionari vijana. Tulikuwa na fursa ya kufundisha na kushuhudia, pamoja na kurejelea historia ya awali ya Kanisa katika Visiwa vya Uingereza ambapo babu wa babu wa babu yangu Heber C. Kimball na washirika wake walikuwa wamisionari wa kwanza.1
Rais Russell M. Nelson, anatutania kuhusu jukumu hili ukizingatia kwamba haikuwa kawaida kuwapa jukumu Mitume watatu kutembelea eneo ambalo walihudumu kama wamisionari katika ujana wao. Alikiri kwamba wote wanataka kutumwa kwenye misheni yao ya awali. Kwa tabasamu pana usoni mwake, alieleza kwa ufupi utangulizi kwamba ikiwa kuna kundi lingine la Mitume watatu waliohudumu katika misheni moja zaidi ya miaka 60 iliyopita, basi wao pia wanaweza kupokea jukumu kama hilo.
Katika kujitayarisha na jukumu hilo, nilisoma tena Maisha ya Heber C. Kimball, yaliyoandikwa na mjukuu wake, Orson F. Whitney, ambaye baadaye aliitwa kwenye utume. Juzuu hiyo nilipewa na mama yangu mpendwa nilipokuwa na umri wa karibu miaka 7. Tulikuwa tukijiandaa kuhudhuria kuwekwa wakfu Mnara wa This Is the Place mnamo Julai 24, 1947, na Rais George Albert Smith.2 Mama alitaka nijue zaidi kuhusu babu yangu, Heber C. Kimball.
Kitabu hiki kina taarifa ya kina inayohusishwa na Rais Kimball ambayo ina umuhimu kwa siku zetu. Kabla ya kushiriki taarifa hiyo, acha nitoe maelezo mafupi.
Wakati Nabii Joseph Smith alipokuwa amefungwa katika Jela ya Liberty, Mitume Brigham Young na Heber C. Kimball walikuwa na jukumu, kwenye hali mbaya ya kuogofya sana, la kusimamia uhamishwaji wa Watakatifu kutoka Missouri. Uhamisho ulihitajika kwa sehemu kubwa kutokana na agizo la kuangamiza lililotolewa na Gavana Lilburn W. Boggs.3
Takriban miaka 30 baadaye Heber C. Kimball, akiwa kwenye Urais wa Kwanza, akirejelea kuhusu historia hii kwa kizazi kipya, alifundisha, “Hebu niwaambieni, kwamba wengi wenu mtauona wakati ambapo mtakuwa na shida zote, majaribu na mateso ambayo mnaweza kumudu, na nafasi nyingi za kuonyesha kwamba ninyi ni waaminifu kwa Mungu na kazi Yake.”4
Heber aliendelea: “Ili kukabiliana na matatizo yanayokuja, itakuwa muhimu kwenu wenyewe kuwa na ufahamu wa ukweli wa kazi hii. Shida zitakuwa na sifa ambazo mwanaume au mwanamke ambaye hana ufahamu huu binafsi au ushahidi ataanguka. Ikiwa bado hujapokea ushuhuda, ishi kwa haki, na mwite Bwana na usiache mpaka uufikie. Usipofanya hutasimama. … Wakati utakuja ambapo hakuna mwanamume wala mwanamke atakayeweza kustahimili kwa mwanga wa kuazimwa. Kila mmoja atapaswa kuongozwa na nuru ndani yake mwenyewe. … Ikiwa hauko nayo hutasimama; hivyo utafuteni ushuhuda wa Yesu na shikamana nao, ili wakati wa majaribu utakapokuja msijikwae na kuanguka.”5
Kila mmoja wetu anahitaji ushuhuda wa kazi ya Mungu6 na jukumu kuu la Yesu Kristo. Ile Sehemu ya 76 ya Mafundisho na Maagano inahusu daraja tatu za utukufu na inalinganisha utukufu wa selestia na jua. Kisha inalinganisha ufalme wa terestria na mwezi.7
Inafurahisha kwamba jua lina nuru yake yenyewe, lakini mwezi ni nuru iliyoakisiwa au “nuru iliyoazimwa.” Ukizungumzia ufalme wa terestria, Mstari wa 79 unasema, “Hawa ndiyo wale ambao si majasiri katika ushuhuda wa Yesu.” Hatuwezi kupata ufalme wa selestia na kuishi na Mungu Baba kwenye nuru ya kuazima; tunahitaji ushuhuda wetu wenyewe wa Yesu na injili Yake.
Tunaishi katika ulimwengu ambamo maovu yanazidi8 na mioyo hugeuka mbali na Mungu kwa sababu ya maagizo ya wanadamu.9 Mojawapo ya mifano katika maandiko juu ya dukuduku la Heber C. Kimball kuhusu kutafuta ushuhuda wa kazi ya Mungu na Yesu Kristo umeelezwa katika ushauri wa Alma kwa wanawe watatu—Helamani, Shibloni, na Koriantoni.10 Wawili wa wanawe walikuwa wakweli kwa Mungu na Kazi Yake. Lakini mwana mmoja alikuwa amefanya maamuzi mabaya. Kwangu mimi umuhimu mkuu wa ushauri wa Alma ni kwamba alikuwa akiutoa kama baba kwa manufaa ya watoto wake mwenyewe.
Wasiwasi wa kwanza wa Alma, kama wa Heber C. Kimball, ulikuwa kwamba kila mmoja apate kuwa na ushuhuda wa Yesu Kristo na kuwa mkweli kwa Mungu na kazi Yake.
Katika mafundisho ya dhati ya Alma kwa mwanawe Helamani, anatoa ahadi kwamba wale ambao “wanaweka tumaini lao kwa Mungu watasaidiwa katika majaribio yao, na shida zao, na mateso yao, na watainuliwa juu katika siku ya mwisho.”11
Ingawa Alma alikuwa amepokea udhihirisho ambapo aliona malaika, hili ni nadra. Misukumo itolewayo na Roho Mtakatifu ni ya kina zaidi. Hisia hizi zinaweza kuwa sawa na muhimu kama kumuona malaika. Rais Joseph Fielding Smith alifundisha: “Misukumo kwenye nafsi ambayo hutoka kwa Roho Mtakatifu ni muhimu zaidi kuliko ono. Roho anapozungumza na roho, matokeo yake kwenye nafsi ni vigumu kuyafuta.”12
Hii inatuelekeza kwenye ushauri wake Alma kwa mwanawe wa pili, Shibloni. Shibloni alikuwa mwadilifu kama alivyokuwa kaka yake Helamani. Ushauri ninaotaka kusisitiza ni Alma 38:12, ambao kwa sehemu unasoma hivi, “Uone kwamba ujifunze kuzuia tamaa zako zote, ili uweze kujazwa na upendo.”
Kuzuia ni neno la kuvutia. Tunapopanda farasi, tunatumia hatamu kumuongoza. Kisawe kizuri kinaweza kuwa kuelekeza, kudhibiti au kuzuia. Agano la Kale linatuambia kwamba tulishangilia kwa shangwe tuliposikia tungekuwa na miili ya nyama na mifupa.13 Mwili si mwovu—ni mzuri na ni muhimu—lakini baadhi ya shauku zisipotumiwa ipasavyo na kwa udhibiti, zinaweza kututenganisha na Mungu na kazi Yake na kuathiri vibaya ushuhuda wetu.
Hebu tuzungumze kuhusu hususan hisia mbili —kwanza, hasira na pili, kutamani.14 Inashangaza kwamba zote mbili zikiachwa bila kuzuiliwa au kudhibitiwa zinaweza kusababisha maumivu makubwa ya moyo, kupunguza ushawishi wa Roho, na kututenganisha na Mungu na kazi Yake. Adui huchukua kila fursa kujaza maisha yetu na picha za vurugu na uasherati.
Katika baadhi ya familia, si nadra kwa mume au mke mwenye hasira kumpiga mwenzi au mtoto. Mnamo Julai, nilishiriki katika Kongamano la Wabunge wa Vyama Vyote vya Uingereza huko London.15 Unyanyasaji kwa wanawake na vijana uliangaziwa kama tatizo kubwa duniani kote. Mbali na vurugu, wengine wamejihusisha na unyanyasaji wa kimaneno. Tangazo kuhusu familia linatuambia “wale wanaowanyanyasa wenzi wao au watoto … siku moja watawajibika mbele za Mungu.”16
Rais Nelson kwa dhati alisisitiza hili asubuhi ya jana.17 Tafadhali weka akilini mwako kwamba bila kujali kama wazazi wako walikunyanyasa au la, hutamnyanyasa kimwili au kimaneno au kihisia mwenzi wako au watoto wako.
Katika siku zetu mojawapo ya changamoto kuu ni mabishano na unyanyasaji wa kimaneno yanayohusiana na masuala ya kijamii. Katika visa vingi hasira na lugha ya unyanyasaji imechukua nafasi ya mantiki, majadiliano na ustaarabu. Wengi wameacha maonyo ya Mtume mkuu wa Mwokozi, Petro, ya kutafuta sifa kama za Kristo kama vile kiasi, subira, utauwa, ukarimu, na hisani.18 Pia wameacha sifa ya unyenyekevu kama ya Kristo.
Zaidi ya kudhibiti hasira na kudhibiti tamaa nyinginezo, tunahitaji kuishi maisha safi ya kimaadili kwa kudhibiti mawazo, lugha, na matendo yetu. Tunahitaji kuepuka ponografia, kutathmini usafi wa yale tunayoangalia katika nyumba zetu, na kuepuka kila namna ya mwenendo wenye dhambi.
Hii inatuleta kwenye ushauri wa Alma kwa mwanawe Koriantoni. Tofauti na kaka zake, Helamani na Shibloni, Koriantoni alihusika katika uvunjaji wa maadili.
Kwa sababu Koriantoni alikuwa amejihusisha na uasherati, ilikuwa muhimu kwa Alma kumfundisha kuhusu toba. Alipaswa kumfundisha uzito wa dhambi na kisha jinsi ya kutubu.19
Kwa hivyo, ushauri wa Alma wa namna ya kuzuia ulikuwa ni kudhibiti tamaa, lakini kwa wale ambao wamevunja sheria, kutubu. Rais Nelson aliwapa waumini ushauri wa kina juu ya toba katika mkutano mkuu wa Aprili 2019. Alibainisha wazi kwamba toba ya kila siku ni muhimu kwa maisha yetu. “Toba siyo tukio; ni mchakato. Ni ufunguo kwa furaha na amani ya akili,” alifundisha. “Toba ya kila siku ndiyo njia ya kuelekea usafi, na usafi huleta nguvu.”20 Ikiwa Koriantoni angefanya kile Rais Nelson alishauri, angetubu punde tu alipoanza kuhisi mawazo machafu. Makosa makubwa yasingetokea.
Ushauri wa kuhitimisha ambao Alma aliutoa kwa wanawe ni baadhi ya mafundisho muhimu sana katika maandiko yote. Inahusiana na Upatanisho uliofanywa na Yesu Kristo.
Alma alishuhudia kwamba Kristo angeondoa dhambi.21 Bila Upatanisho wa Mwokozi, kanuni ya milele ya haki ingehitaji kuwepo na adhabu.22 Kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi, rehema inaweza kuwepo kwa wale ambao wametubu, na kuwaruhusu kurudi kwenye uwepo wa Mungu. Tungefanya vyema kutafakari fundisho hili la kupendeza.
Hakuna awezaye kurudi kwa Mungu kwa juhudi zake pekee, sote tunahitaji msaada wa dhabihu ya Mwokozi. Wote wametenda dhambi, na ni kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo pekee ndipo tunaweza kupata rehema na kuishi na Mungu.23
Alma pia alitoa ushauri wa kupendeza kwa Koriantoni kwa ajili yetu sisi sote ambao tunapitia au tutapitia mchakato wa toba, bila kujali kama dhambi ni ndogo au za kutubu kwa muda mrefu kama zile zilizotendwa na Koriantoni. Mstari wa 29 wa Alma 42 unasema, “Na sasa, mwana wangu, nataka kwamba usiache vitu hivi vikusumbue mara nyingine, na ni dhambi zako tu zikusumbue, pamoja na taabu hiyo ambayo itakuleta wewe katika toba.”
Koriantoni alitii ushauri wa Alma na alitubu na kutumikia kwa heshima. Kwasababu ya Upatanisho wa Mwokozi, uponyaji unapatikana kwa wote.
Katika siku za Alma, katika siku za Heber, na kwa hakika katika siku zetu sisi sote tunahitaji kutafuta ushuhuda wetu wenyewe wa Yesu Kristo, kudhibiti tamaa zetu, kutubu dhambi zetu, na kupata amani kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo na kuwa wakweli kwa Mungu na kazi Yake.
Katika ujumbe wa hivi karibuni na pia asubuhi hii, Rais Russell M. Nelson alisema hivi: “Ninawasihi kuchukua jukumu la ushuhuda wenu juu ya Yesu Kristo. Ufanyie kazi. Umiliki. Utunze. Ulee ili kwamba uweze kukua. Kisha tazamia miujiza kutendeka katika maisha yako.”24
Ninashukuru kwamba sasa tutasikia kutoka kwa Rais Nelson. Ninashuhudia kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii kwa ajili ya wakati wetu. Ninapenda na kuthamini msukumo wa kupendeza na mwongozo tunaopokea kupitia yeye.
Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninatoa ushuhuda wangu wa hakika wa uungu wa Mwokozi na uhalisi wa Upatanisho Wake katika jina la Yesu Kristo, amina.