Mkutano Mkuu
Mipangilio ya Ufuasi
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Mipangilio ya Ufuasi

Kujifunza kuhusu Kristo na njia Zake kunatuongoza sisi kumjua na kumpenda Yeye.

Mpangilio wa Imani

Asubuhi hii watoto wetu wawili na wajukuu watatu huko Amerika Kaskazini, na karibu nusu ya ulimwengu waliona uangavu wa jua likichomoza kwa ufahari upande wa mashariki. Watoto watatu wengine na wajukuu saba huko Afrika, na nusu nyingine ya ulimwengu waliona giza taratibu likiwanyemelea wakati jua lilipokuwa linazama upande wa magharibi.

Uwepo huu usiokuwa na mwisho wa mchana na usiku ni kumbusho moja la kila siku la ukweli ambao unatawala maisha yetu ambao hatuwezi kuubadili. Tunapoheshimu na kuoanisha kile tunachofanya na kweli hizi za milele, tunapata amani na maelewano ya ndani. Tusipofanya hivyo, hatutulii, na mambo hayafanyiki kama vile tunavyotarajia.

Mchana na usiku ni mfano mmoja wa mipangilio ambayo Mungu amempa kila mtu ambaye amewahi kuishi duniani, wa mambo jinsi yalivyo. Huu ni ukweli mtupu wa uwepo wa binadamu kwamba hatuwezi kwenda kinyume nao kufuatia matakwa yetu na kuuepuka. Ninakumbushwa juu ya hili kila wakati ninaposafiri kwa ndege kutoka Afrika kuja kwenye mkutano mkuu, narekebisha saa ya mwili kurudi nyuma kwa saa 10 katika siku moja.

Tunapokuwa makini kutazama, tunaona kwamba Baba wa Mbinguni ametupa ushahidi wa kutosha wa kweli za kutawala maisha yetu ili tumjue Yeye na kupata baraka za amani na furaha.

Kupitia Nabii Joseph Smith, Roho wa Bwana anathibitisha: “Na tena, nitatoa kwenu utaratibu katika mambo yote, ili msidanganyike; kwani Shetani amezagaa katika nchi, na anaenda akiwadanganya mataifa.”1

Korihori mpinga Kristo alianguka kwa udanganyifu kama huo, kutokuamini kuwepo kwa Mungu na kuja kwa Kristo. Kwake nabii Alma alishuhudia: “Vitu vyote vinaonyesha kwamba kuna Mungu; ndiyo, hata dunia, na vitu vyote vilivyo juu yake, ndiyo, na mwendo wake, ndiyo, na pia sayari zote ambazo huenda kwa utaratibu wao zinashuhudia kwamba kuna Muumba Mkuu.”2

Wakati Korihori aliposisitiza kuonyeshwa ishara kabla ya yeye kuamini, Alma alimfanya kuwa bubu. Alipokuwa amenyenyekezwa na mateso yake, Korihori alikiri wazi wazi kuwa alikuwa amedanganywa na iblisi.

Hatuhitaji kudanganywa. Muujiza wa maisha ya akili siku zote unacheza mbele yetu. Na mtazamo kwa ufupi na tafakari juu ya maajabu ya mbinguni yaliyopambwa na nyota zisizo na idadi na galaksi huchochea roho ya moyo uaminio kutangaza, “Mungu wangu, jinsi Ulivyo mkuu!”3

Ndio, Mungu Baba yetu wa Mbinguni yu hai, na Yeye hujidhirihisha Mwenyewe kwetu wakati wote katika njia nyingi.

Mpangilio wa Unyenyekevu

Lakini ili kukiri, kuamini, na kudumu katika Mungu, mioyo yetu inahitaji kupokea Roho wa kweli. Alma alifundisha kwamba imani inatanguliwa na unyenyekevu.4 Mormoni aliongezea kwamba haiwezekani kwa mtu yeyote ambaye si “mpole na mnyenyekevu moyoni” kuwa na imani na tumaini na kumpokea Roho wa Mungu.5 Mfalme Benyamini alitangaza kwamba mtu yeyote atoaye kipaumbele kwa ufukufu wa ulimwengu ni “adui wa Mungu.”6

Kwa kujiweka chini ya ubatizo ili kutimiza haki yote, ingawa Yeye alikuwa mwenye haki na mtakatifu, Yesu Kristo alionyesha kwamba unyenyekevu mbele ya Mungu ni sifa ya msingi ya wafuasi Wake.7

Wafuasi wote wapya wanatakiwa kuonyesha unyenyekevu mbele za Mungu kupitia ibada ya ubatizo. Kwa hiyo “wale wote wenye kunyenyekea wenyewe mbele za Mungu, na kutamani kubatizwa, na wakija na mioyo iliyovunjika na roho zilizopondeka … wapokelewe kwa ubatizo katika kanisa lake.”8

Unyenyekevu huelekeza moyo wa mwanafunzi kuelekea kwenye toba na utiifu. Roho wa Mungu kisha anaweza kuleta ukweli kwenye moyo huo, na ataupata mlango.9

Ni ukosefu wa unyenyekevu ndiyo unaochangia zaidi katika kutimia kwa unabii wa Mtume Paulo katika hizi siku za mwisho.

“Maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye tamaa, wenye kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio safi,

“Wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji, wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema.”10

Mwaliko wa Mwokozi wa kujifunza juu Yake ni mwaliko wa kugeuka kutoka kwenye vishawishi vya malimwengu na kuwa kama Yeye alivyo—mpole na mnyenyekevu wa moyo. Kisha tutaweza kuichukua nira Yake na kugundua kwamba ni nyepesi—kwamba ufuasi si mzigo bali ni shangwe, kama Rais Nelson alivyotufundisha kwa ufasaha sana na kwa kurudia rudia.

Mpangilio wa Upendo

Kujifunza kuhusu Kristo na njia Zake kunatuongoza sisi kumjua na kumpenda Yeye.

Yeye alionyesha kwa mfano kwamba kwa mtazamo wa unyenyekevu kwa kweli inawezekana kumjua na kumpenda Mungu Baba kwa utu wetu wote na kuwapenda wengine kama vile tunavyojipenda wenyewe, bila kuzuia chochote. Huduma Yake ulimwenguni, wakati ambao Yeye aliweka vyote viwili mapenzi Yake na mwili Wake kwenye madhabahu, ilikuwa mpangilio wa matumizi ya kanuni hizi, ambapo juu yake injili Yake ilianzishwa. Kanuni zote mbili ni mwonekano wa nje na ni kuhusu jinsi sisi tunavyohusiana na wengine, sio kutafuta kujiridhisha au utukufu wa kibinafsi.

Kejeli yake ya kimuijiza ni kwamba tunapofokasi juhudi zetu bora juu ya Mungu mwenye upendo na wengine, tunawezeshwa kugundua thamani yetu wenyewe ya kiungu ya kweli, kama wana na mabinti wa Mungu, kwa amani na furaha kamili ambayo jambo hili huleta.

Tunakuwa wamoja na Mungu na wamoja sisi wenyewe kupitia upendo na huduma. Kisha tunaweza kupokea ushahidi wa Roho Mtakatifu wa huo upendo safi, tunda ambalo Lehi huongelea juu yake kama “tunda tamu, zaidi ya yote ambayo nilikuwa nimeonja.”11

Taji ambalo Kristo alipokea kwa kutoa na kufanya yote kwa juhudi Zake ili kuweka mpangilio wa kumpenda Baba na kutupenda sisi ilikuwa ni kupokea nguvu zote, hata yote ambayo Baba anayo, ambayo ndiko kuinuliwa.12

Fursa yetu ya kulea katika nafsi zetu upendo wa kudumu kwa ajili ya Mungu na kwa ajili ya jirani yetu huanzia nyumbani kwa tabia takatifu za kuunganika na Baba kila siku katika maombi binafsi na ya familia katika jina la Mwanawe Mzaliwa wa Pekee, kujifunza pamoja juu Yao kupitia kujifunza maandiko kibinafsi na kama familia, kuishika kitakatifu siku ya Sabato kwa pamoja, na kila mtu kuwa na kibali cha hekaluni, na kukitumia pamoja kila mara kadri tunavyoweza.

Kadri kila mmoja anavyokua katika elimu na upendo wetu kwa Baba na Mwana, tunakua katika kuthaminiana na kupendana. Uwezo wetu wa kupenda na kuwatumikia wengine nje ya nyumba yetu unaimarishwa sana.

Kile tunachofanya nyumbani ndiyo suluhu ya kweli ya ufuasi wa kudumu na wa furaha. Baraka tamu zaidi za injili ya urejesho ambazo mke wangu, Gladys, na mimi tumefurahia katika nyumba yetu zimekuja kutokana na kujifunza kumjua na kumheshimu Mungu nyumbani na kushiriki upendo Wake na wazao wetu.

Mpangilio wa Huduma

Upendo kwa Mungu na huduma kwa mmoja na mwingine iliyolelewa nyumbani na huduma kwa wengine walio nje ya nyumba baada ya muda hukua na kuwa sifa ya hisani.

Hii inaendana na mpangilio wa huduma uliyowekwa wakfu katika ufalme wa Mungu ambao umewekwa mbele yetu na manabii na mitume wa Bwana walio hai. Tunakuwa wamoja pamoja nao.

Kisha ndipo tunapowezeshwa kutazama, kupitia wao, hata kwa Bwana “katika kila wazo,” ili kwamba “tusihofu” wala “kuogopa.”13

Kama vile manabii na mitume wa Bwana walio hai, tunaweza kusonga mbele na “moyo … uliojaa hisani kwa wanadamu wote, na … kwa jamaa ya waaminio, [na] wema [uyapambe] mawazo yetu bila kukoma; … ndipo kujiamini [kwetu] [kutakuwa] imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani … [yatatonatona] juu ya [roho zetu] kama umande utokao mbinguni.”

Pamoja na manabii na mitume wa Bwana walio hai, sisi pia tunaweza kujiunga na mduara wa wema wa imani iliyoimarishwa na huduma iliyowekwa wakfu ambayo kwayo “Roho Mtakatifu ni mwenzi [wetu] daima, na fimbo [yetu] ya kifalme fimbo isiyobadilika ya haki na ukweli; na utawala [wetu] utakuwa utawala usio na mwisho, na usio wa njia ya kulazimisha [utatiririka] [kwetu] milele na milele.”14 Kwani hii ndiyo ahadi ya mpango wa Baba. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha