Mkutano Mkuu
Ujasiri wa Kutangaza Ukweli
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


11:26

Ujasiri wa Kutangaza Ukweli

Mara tunapojifunza ukweli, Bwana anatupa nafasi ya kufanya kile ambacho Yeye angefanya kama angekuwepo hapa leo.

Mnamo mwaka 1982, nilikuwa namaliza shahada yangu ya miaka miwili kwenye topografia katika shule ya ufundi.

Mwishoni mwa mwaka, mwanadarasa alinialika kuwa na mazungumzo naye. Nakumbuka kwamba tuliwaacha wanadarasa wengine na kwenda katika eneo pembezoni mwa uwanja wa michezo. Tulipofika pale, alizungumza nami kuhusu imani yake katika dini, na si tu kwamba alinionyesha kitabu, bali alinipa kitabu. Kusema kweli, sikumbuki maneno yote aliyozungumza, lakini nakumbuka muda ule vizuri na jinsi nilivyohisi wakati aliposema, “Napenda kutoa ushuhuda wangu kwako kwamba kitabu hiki ni cha kweli na kwamba injili ya Yesu Kristo imerejeshwa.”

Baada ya mazungumzo yetu, nilienda nyumbani, nikafungua kurasa chache za kitabu na kukiweka kwenye rafu. Kwa sababu tulikuwa mwishoni mwa mwaka na ulikuwa mwaka wangu wa mwisho wa shahada yangu ya topografia, sikuweka sana umakini kwenye kitabu, wala kwa mwanadarasa mwenzangu aliyeshiriki nami kitabu. Jina la kitabu unaweza kuwa tayari umeshatabiri. Ndiyo, kilikuwa Kitabu cha Mormoni.

Miezi mitano baadaye, wamisionari walikuja nyumbani kwangu; walikuwa wanaondoka wakati nilipokuwa narudi kutoka kazini. Niliwakaribisha warejee ndani. Tuliketi katika sebule mbele ya nyumba yangu na walinifundisha.

Katika kutafuta kwangu ukweli, niliwauliza ni kanisa lipi lilikuwa la kweli na ni vipi ningeweza kulipata. Wamisionari walinifundisha kwamba ningeweza kupata jibu lile mimi mwenyewe. Nikiwa na matarajio na hamu kubwa, nilikubali changamoto yao kusoma sura kadhaa kutoka Kitabu cha Mormoni. Nilisali kwa moyo wa dhati na kusudi halisi (ona Moroni 10:4–5). Jibu kwa swali langu lilikuwa wazi na siku kadhaa baadaye—kwa uhakika zaidi Mei 1, 1983—nilibatizwa na kuthibitishwa kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Leo, ninapofikiria kuhusu mlolongo wa matukio yaliyotokea, naona kwa uhakika ni muhimu kiasi gani ujasiri wa mwanadarasa mwenzangu ulikuwa wakati alipotoa ushuhuda kuhusu ukweli uliorejeshwa na kunipa ushahidi wa kushikika wa Urejesho wa injili ya Yesu Kristo, hata Kitabu cha Mormoni. Kitendo kile cha kawaida, lakini chenye umuhimu sana kwangu, kilijenga muunganiko kati yangu na wamisionari pale nilipokutana nao.

Ukweli ulikuwa umewasilishwa kwangu na baada ya ubatizo wangu, nikawa mfuasi wa Yesu Kristo. Wakati wa miaka iliyofuata, na kwa msaada wa watu maalumu kama vile viongozi, walimu, marafiki na pia kupitia kusoma kwangu binafsi, nilijifunza kwamba nilipoamua kuwa mfuasi wa Yesu Kristo, nilikubali jukumu si tu la kutetea ukweli, bali pia la kuutangaza.

Tunapokubali kuamini katika ukweli, kuufuata na tunapofanya jitihada kuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo, hatupokei cheti chenye dhamana kwamba hatutafanya makosa, kwamba hatutakosolewa, kwamba hatutajaribiwa kujitenga na ukweli au hata kwamba hatutapata maumivu. Lakini ufahamu wa ukweli hufundisha kwamba tunapoingia njia iliyo nyembamba na iliyosonga ambayo itatupeleka kurudi kwenye uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni, patakuwepo daima njia ya kukwepa matatizo haya (ona 1 Wakorintho 10:13); patakuwepo daima uwezekano wa kutilia shaka mashaka yetu kabla ya kutilia shaka imani yetu (ona Dieter F. Uchtdorf, “Njoo, Ujiunge Nasi,” Liahona, Nov. 2013, 21); na mwisho, tuna hakikisho kuwa kamwe hatutakuwa peke yetu nyakati za mateso, kwani Mungu huwatembelea watu Wake katikati ya mateso yao (ona Mosia 24:14).

Mara tunapojifunza ukweli, Bwana anatupa nafasi ya kufanya kile ambacho Yeye angefanya kama angekuwepo hapa leo. Hakika, Alituonyesha kwa mafundisho Yake nini tunapaswa kufanya: “Nanyi mtaenenda mbele katika nguvu ya Roho wangu, mkihubiri injili yangu, wawili wawili, katika jina langu, mkipaza sauti zenu kama kwa sauti ya tarumbeta, mkilitangaza neno langu kama vile malaika wa Mungu” (Mafundisho na Maagano 42:6). Fursa ya kazi ya umisionari katika ujana wetu ni ya kipekee!

Tafadhali, wavulana, msiahirishe maandalizi yenu ya kumtumikia Bwana kama wamisionari. Wakati unapokabiliana na hali ya kusababisha maamuzi ya kwenda kutumikia misheni kuwa magumu—kama vile kusitisha masomo yako kwa muda, kusema kwaheri kwa rafiki yako wa kike ambaye huna uhakika kama mtaendelea kuwa marafiki tena au hata kuacha kazi nzuri—kumbuka mfano wa Mwokozi. Wakati wa huduma Yake, Yeye vilevile alikabiliwa na magumu, ikijumuisha kukosolewa, kuteswa na hatimaye kikombe kichungu cha dhabihu Yake ya upatanisho. Na bado katika hali zote Yeye alitafuta kufanya mapenzi ya Baba Yake na kumpa Yeye utukufu. (Ona Yohana 5:30; 6:38–39; 3 Nefi 11:11; Mafundisho na Maagano 19:18–19.)

Wasichana, mnakaribishwa sana, ikiwa mtataka, kufanya kazi katika shamba la Bwana na mnapojitayarisha kuhudumu kama wamisionari, hamtaondolewa kwenye changamoto kama hizo.

Kwa wale wote wanaoamua kumtumikia Yeye, ninawaahidi kwamba miezi 24 au 18 ya huduma itapita kama ambavyo ingepita ikiwa ungebaki nyumbani, lakini fursa zinazowasubiri wavulana na wasichana wa Kanisa hili katika misheni ni za kipekee. Fursa ya kumwakilisha Mwokozi Yesu Kristo na Kanisa Lake haiwezi kupuuzwa. Kushiriki katika sala zisizohesabika, kukuza na kutoa ushuhuda wako mara nyingi kutwa nzima, masaa mengi ya kusoma maandiko na kukutana na watu ambao usingeweza kukutana nao kama ungebaki nyumbani ni uzoefu usioelezeka. Kiwango hichohicho cha uzoefu kimewekwa kwa ajili ya vijana ambao Bwana huwaita kutumikia katika misheni za huduma. Mnakaribishwa sana na ni wa muhimu. Tafadhali msipunguze umuhimu wa misheni za huduma, kwani misheni za huduma pia zinatoa uzoefu usioelezeka. “Thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu” (Mafundisho na Maagano 18:10), ikijumuisha thamani ya nafsi yako.

Baada ya kurudi kutoka kwenye huduma yako, pengine rafiki yako wa kike au wa kiume hakusubirii tena, lakini utakuwa umejifunza vizuri zaidi namna bora ya kufanya urafiki. Masomo yako ya taaluma yatakuwa na maana zaidi yakibeba maono uliyokuwa nayo kuhusu kujiandaa vya kutosha kwa ajili ya sehemu ya kazi na hatimaye, utakuwa na uhakika kamili wa kuwa na ujasiri wa kutangaza injili ya amani, ukishuhudia kuhusu ukweli uliorejeshwa.

Kwa wale kati yenu ambao ni wanandoa na mko katika hatua tofauti tofauti za maisha, ninyi ni muhimu katika kazi ya Bwana. Jiandaeni wenyewe. Ishini maisha yenye afya, mkitafuta kujitegemea kimwili na kiroho, kwa sababu fursa za kufanya kile ambacho Bwana angefanya kwa ajili ya watoto wake hazina ukomo kwenye kundi moja la umri. Uzoefu wa kupendeza ambao mimi na mke wangu tumeupata miaka ya karibuni umekuja wakati tukitumikia sambamba na wamisionari wanandoa maalumu, wakitumikia katika sehemu maalumu na katika kuwahudumia watu maalumu.

Uzoefu nilioupata mwishoni mwa shahada yangu ya topografia ulinifundisha kwamba daima tunatetea ukweli wakati tunapoutangaza na kwamba kuutetea ukweli ni jambo hai. Utetezi wa ukweli haupaswi kufanywa kwa kutumia nguvu bali kwa nia ya kweli ya kupenda, kushiriki na kuwaalika watu tunaowashuhudia ukweli, tukifikiria tu ustawi wa kimwili na kiroho wa watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo (ona Mosia 2:41).

Katika mkutano mkuu wa Oktoba 2021, Rais Russell M. Nelson, nabii wetu mpendwa, alifundisha kwamba kinyume na wengi wanavyofikiri, hakika kuna kile tunachoita sahihi na si sahihi. Hakika kuna ukweli halisi—ukweli wa milele. (Ona “Ukweli Halisi, Mafundisho Halisi na Ufunuo Halisi,” Liahona, Nov. 2021, 6.)

Maandiko matakatifu yanatufundisha, “ukweli ni maarifa ya mambo kama yalivyo, na kama yalivyokuwa, na kama yatakavyokuwa” (Mafundisho na Maagano 93:24).

Maarifa ya ukweli hayatufanyi sisi kuwa bora kuliko watu wengine, bali hutufundisha nini tunapaswa kufanya ili kurudi kuishi katika uwepo wa Mungu.

Kadiri unavyosonga mbele kwa uimara katika Kristo na kwa ujasiri si tu katika kuutangaza ukweli bali kuuishi, utapata amani na faraja wakati wa misukosuko ambayo utakumbana nayo katika siku hizi.

Changamoto za maisha zinaweza kutuangusha chini, lakini tambua kwamba tunapokuwa na imani katika Yesu Kristo, “maumivu [yetu] yatakuwa kwa muda mfupi” (Mafundisho na Maagano 121:7) katika mpango mkuu wa milele. Tafadhali usiweke kikomo cha muda kwa matatizo yako na changamoto zako. Mtumaini Baba wa Mbinguni na usikate tamaa, kwani tukikata tamaa, kamwe hatutajua jinsi ambavyo mwisho wa safari yetu ungekuwa katika ufalme wa Mungu.

Shikilia katika ukweli, ukijifunza kutoka katika vyanzo vya ukweli:

Ninatoa ushuhuda wangu juu ya Yesu Kristo na kwamba hili ni Kanisa Lake. Tunaye nabii aliye hai, na daima tutahisi huru pale tunapotangaza ukweli kwa ujasiri. Katika jina la Yesu Kristo, amina.