Mkutano Mkuu
Kusogea Karibu Zaidi na Mwokozi
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


15:4

Kusogea Karibu Zaidi na Mwokozi

Tukitafuta kumjua na kumpenda Mwokozi, tunajitenga na ulimwengu kupitia maagano na Mungu, kuwa wa kipekee, si wa kawaida na tunakuwa maalumu pasipo kujitenga na wengine wanaoamini tofauti na sisi.

Wapendwa kaka zangu na dada zangu, jioni hii ninazungumza na wafuasi wanyenyekevu na waliojitolea kumfuata Yesu Kristo. Ninapoona mema ya maisha na imani yenu katika Mwokozi wetu hapa katika nchi hii na katika mataifa mengine kote ulimwenguni, ninawapenda nyote zaidi.

Kuelekea mwisho wa huduma Yake, wanafunzi wa Yesu walimwomba awaeleze “ishara ya ujio [Wake wa Pili], na mwisho wa dunia.”1

Yesu aliwaambia hali ambazo zingeutangulia wakati wa kurudi Kwake na alihitimisha kwa kutamka kwamba, “Mtakapoona mambo haya, [mtajua] kwamba [wakati] umekaribia.”2

Katika mkutano mkuu uliopita, nilisikiliza kwa makini maneno ya Rais Henry B. Eyring: “Kila mmoja wetu,” yeye alisema, “popote tulipo, anajua kwamba tunaishi katika nyakati za hatari zaidi. … Mtu yeyote aliye na macho ya kuona ishara za nyakati na masikio ya kusikia maneno ya manabii anajua kwamba hiyo ni kweli.”3

Mwokozi aliwasifu wafuasi Wake mashujaa: “Heri macho yenu, kwa kuwa yanaona: na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.”4 Hebu baraka hii iwe yetu wakati tunaposikiliza kwa makini maneno ya Bwana kupitia manabii Wake pamoja na wengine katika mkutano huu.

Ngano na Magugu

Bwana alifafanua kwamba katika wakati huu wa mwisho kabla ya kurudi Kwake, “ngano” ambayo aliielezea kama “watoto wa ufalme,”5 ingekua bega kwa bega na “magugu” au wale ambao hawampendi Mungu na hawashiki amri Zake. Wote “wangekua kwa pamoja,”6 bega kwa bega.

Huu utakuwa ulimwengu wetu hadi Mwokozi atakaporudi, ukiwa na mengi yaliyo mema na mengi ambayo ni mabaya kila kona.7

Unaweza wakati mwingine usihisi kuwa matunda ya ngano imara yaliyokomaa. Kuwa mvumilivu kwako wewe mwenyewe. Bwana alisema kwamba ngano ingejumuisha majani laini yanayochipuka.8 Sisi sote ni Watakatifu Wake wa Siku za Mwisho na ingawa bado hatujawa yote tunayotaka kuwa, tuko makini katika hamu yetu ya kuwa wafuasi Wake wa kweli.

Tuimarishe Imani Yetu katika Yesu Kristo

Tunatambua kwamba kadiri uovu unavyoongezeka katika ulimwengu, kunusurika kwetu kiroho na kunusurika kiroho kwa wale tunao wapenda, kutahitaji kwamba tulee, tuwekee ulinzi na tuimarishe mizizi ya imani yetu katika Yesu Kristo. Mtume Paulo alitushauri tuwe na mizizi,9 wenye shina na wenye kujengwa10 katika upendo wetu kwa Mwokozi na dhamira yetu ya kumfuata Yeye. Leo, na siku zilizo mbele yetu zinahitaji juhudi yenye fokasi zaidi na yenye umakini, kujilinda dhidi ya ukengeufu na kutokujali.11

Lakini pamoja na ongezeko la ushawishi wa kiulimwengu unaotuzunguka, hatupaswi kuogopa. Bwana kamwe hatawaacha watu Wake wa agano. Kuna nguvu ya fidia ya karama za kiroho na mwongozo wa kiungu kwa wenye haki.12 Nyongeza hii ya baraka ya nguvu ya kiroho, hata hivyo, haitulii juu yetu kwa sababu tu sisi ni sehemu ya kizazi hiki. Inakuja tunapoimarisha imani yetu kwa Bwana Yesu Kristo na kushika amri Zake, pale tunapokuja kumjua na kumpenda Yeye. “Na uzima wa milele ndio huu,” Yesu alisali, “kwamba wakujue wewe Mungu wa pekee wa kweli na Yesu Kristo uliyemtuma.”13

Kama tunavyojua vyema, kuwa na imani katika Yesu Kristo na kuwa mfuasi wa kweli ni uamuzi wa zaidi ya mara moja—zaidi ya tukio la mara moja. Ni mchakato mtakatifu, endelevu ambao unakua na kutanuka kupitia majira ya maisha yetu, ukiendelea hadi tutakapopiga magoti miguuni Pake.

Kukiwa na ngano ikikua miongoni mwa magugu duniani, ni kwa jinsi gani tunaweza kuongeza na kuimarisha msimamo wetu kwa Mwokozi katika siku zilizo mbele?

Hapa kuna mawazo matatu:

Tujikite katika Maisha ya Yesu

Kwanza, tunaweza kujikita kikamilifu kwenye maisha ya Yesu, mafundisho Yake, ukuu Wake, nguvu Zake na dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Mwokozi alisema, “Nitegemeeni katika kila wazo.”14 Mtume Yohana anatukumbusha, “Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza.”15 Tunapoelewa vyema upendo Wake, tunampenda Yeye hata zaidi na, kwa uhalisia kabisa, tunafuata vyema mfano Wake wa kupenda na kuwajali wale walio karibu nasi. Kwa kila hatua ya haki kumwelekea Yeye, tunamwona Yeye kwa uwazi zaidi.16 Tunamwabudu na kujaribu kwa njia zetu ndogo kumwiga Yeye.17

Tufanye Maagano na Bwana

Pili, tunapomjua na kumpenda vyema zaidi Mwokozi, tutamani hata zaidi kumwahidi Yeye utii na uaminifu wetu. Tunafanya maagano na Yeye. Tunaanza na ahadi zetu wakati wa ubatizo na tunathibitisha ahadi hizi na nyinginezo tunapotubu kila siku, kuomba msamaha na kwa shauku tunapotazamia kupokea sakramenti kila wiki. Tunaahidi “daima kumkumbuka yeye na kushika amri zake.”18

Tunapokuwa tayari, tunakumbatia ibada na maagano ya hekaluni. Tukihisi ushawishi wa milele katika nyakati takatifu za ukimya katika nyumba ya Bwana, kwa furaha tunafanya maagano na Mungu na kuimarisha uamuzi wetu wa kuyashika.

Kufanya na kushika maagano kunaruhusu upendo wa Mwokozi kuzama ndani kwa kina katika mioyo yetu. Katika Liahona, ya mwezi huu, Rais Russell M. Nelson alisema: “Maagano [yetu] yatatuongoza kuwa karibu zaidi na Yeye. … Mungu hataacha uhusiano Wake na wale waliojenga makubaliano kama haya na Yeye.”19 Na kama Rais Nelson alivyosema kwa uzuri asubuhi ya leo, “Kwa uwekaji wakfu wa kila hekalu jipya, ongezeko la nguvu za kiungu huja ulimwenguni ili kutuimarisha na kupinga juhudi zinazoongezeka za adui.”20

Je, tunaweza kuona kwa nini Bwana amemwelekeza nabii Wake kuleta mahekalu matatifu karibu zaidi na sisi na kuturuhusu kuwa ndani ya nyumba Yake mara nyingi zaidi?

Tunapoingia ndani ya hekalu, tunaachiliwa huru kwa muda kutoka kwenye ushawishi wa ulimwengu unaokusanyika dhidi yetu wakati tunapojifunza juu ya kusudi la maisha yetu na vipawa vya milele vinavyotolewa kwetu kupitia Mwokozi wetu, Yesu Kristo.

Tulinde Kipawa cha Roho Mtakatifu

Mwisho, wazo langu la tatu: katika jtihada hii takatifu, tunathamini, kulinda na kutetea kipawa cha Roho Mtakatifu. Wote wawili Rais M. Russell Ballard mapema leo na Elder Kevin W. Pearson dakika chache tu zilizopita wamezungumza juu ya onyo la kinabii la Rais Nelson ambalo nitalirudia tena: “Haitawezekana kunusurika kiroho bila ushawishi wenye mwongozo, maelekezo, faraja na endelevu wa Roho Mtakatifu.”21 Ni zawadi ipitayo kifani. Tunafanya vyema kadiri tuwezavyo ili kulinda uzoefu wetu wa kila siku ili Roho Mtakatifu aweze kubaki pamoja nasi. Sisi ni nuru kwa ulimwengu na inapobidi, kwa hiari yetu tunachagua kuwa tofauti na wengine. Rais Dallin H. Oaks hivi karibuni aliwauliza vijana wakubwa: “Je, mnathubutu kuwa tofauti?’ … Muhimu [hasa] … ni chaguzi mnazofanya katika maisha yenu binafsi. … Je, mnasonga mbele dhidi ya upinzani wa ulimwengu?”22

Tuchague Kuwa Tofauti na Ulimwengu

Katika posti ya hivi karibuni katika mtandao wa kijamii, niliwaomba wafuasi wenzangu kushiriki chaguzi walizofanya ambazo ziliwahitaji wao kuwa tofauti na ulimwengu. Nilipokea mamia ya majibu.23 Haya ni baadhi ya machache tu.

Amanda: Mimi ni muuguzi ninayefanya kazi katika gereza katika eneo langu. Ninajaribu kuwashughulikia wafungwa kama ambavyo Kristo angefanya.

Raheli: Mimi ni mwimbaji wa opera na mara kwa mara inatazamiwa kwamba nitavaa tu vazi lolote nitakalopewa, bila kujali maadili. [Kwa sababu mimi nimepokea endaumenti,] niliwajulisha [ wasimamizi] kwamba vazi lingehitajika kuwa la [heshima]. Hawakufurahi … lakini kwa shingo upande wakafanya marekebisho. Nisingebadilisha amani ambayo inakuja kutokana na kusimama kama shahidi wa Kristo wakati wote.

Chriss: Mimi ni mlevi (katika hatua za kupona), mwenye kustahili kwenda hekaluni, muumini wa Kanisa. Mimi siyo mkimya kuhusu uzoefu wangu wa uraibu na kupata ushuhuda juu ya Upatanisho [wa Yesu Kristo].

Lauren: Nilikuwa nikiandika mchezo wa uigizaji pamoja na wanadarasa wenzangu katika ya shule ya upili. Walitaka tabia yangu ya utulivu, ya staha ghafla iwe ya mlipuko wa matusi. Waliendelea kunishinikiza, lakini nilikataa, nikashikilia msimamo wangu.

Adam: Watu wengi hawaniamini ninaposema ninatii sheria ya usafi wa kimwili na kuchagua kujizuia kutokana na ponografia. Hawaelewi umuhimu wa shangwe na amani ya akili ninayopata.

Ella: Baba yangu ni mshiriki wa jumuiya ya LGBTQ. Daima najaribu kuweka hisia za watu wengine katika mawazo yangu wakati nikisimama kama shahidi wa Kristo na kuwa mkweli kwa kile ninachoamini.

Andrade: Niliamua kuendelea kwenda kanisani wakati familia yangu ilipoamua kutokwenda.

Na mwisho, kutoka kwa Sherry: Tulikuwa tukihudhuria hafla nyumbani kwa gavana. Walianza kugawa glasi za shampeni kwa ajili ya “kugonga.” Mimi nilisisitza kunywa maji, ingawa wafanyakazi walisema ingekuwa chukizo. Tuligonga glasi na gavana, na mimi niliinua glasi yangu ya maji juu! Gavana hakuchukizwa.

Rais Nelson alisema, “Ndiyo, unaishi ulimwenguni, lakini una viwango tofauti sana na vya ulimwengu ili kukusaidia kuepuka mawaa ya dunia.”24

Anastasia, mama kijana huko Ukrane alikuwa hospitali akiwa punde tu amejifungua mtoto wa kiume wakati mabomu yalipoanza kupigwa huko Kyiv Februari hii iliyopita. Muuguzi alifungua mlango wa chumba cha hospitali na kusema kwa sauti ya dharura, “Mchukue mtoto wako, mfunike blanketi na nenda naye ukumbini—sasa!”

Baadaye, Anastasia alitoa maoni:

“Sikudhani siku zangu za mwanzo za kuwa mama zingekuwa ngumu hivyo, … lakini … ninafokasi juu ya … baraka na miujiza niliyoiona. …

“Sasa hivi, … yawezekana ikaonekana kama haiwezekani kuwasamehe wale waliosababisha maangamizo na maumivu … , lakini kama mfuasi wa Kristo, nina imani kwamba nitaweza [kusamehe]. …

“Sijui yote ambayo yatatokea siku zijazo … lakini ninajua kwamba kushika maagano yetu kutamruhusu Roho kuwa pamoja nasi daima, … akituruhusu kuhisi shangwe na tumaini … hata katika nyakati ngumu.”25

Ahadi ya Uzima wa Milele na Utukufu wa Selestia

Kaka zangu na dada zangu, nimebarikiwa kupokea kwa wingi upendo wa Mwokozi wetu mpendwa, Yesu Kristo. Ninajua yu hai na anaongoza kazi Yake takatifu. Sina maneno yaliyokamilika kuelezea upendo wangu Kwake.

Sisi sote ni “watoto wa agano” tukisambaa kote ulimwenguni katika mataifa na tamaduni katika kila bara, kwa idadi ya mamilioni, tunapongojea kurudi kwa ufukufu kwa Bwana na Mwokozi wetu. Tuking’ara kama nuru kwa wengine wanaotuzunguka, kwa uangalifu tunarekebisha matamanio, mawazo, chaguzi na matendo yetu. Tukitafuta kwa moyo wetu wote kumjua na kumpenda Mwokozi, tunajitenga na ulimwengu kupitia maagano na Mungu, tukiwa wa kipekee, si wa kawaida na tukiwa maalumu, pale tunapomheshimu Yeye na mafundisho Yake pasipo kujitenga na wengine wanaoamini tofauti na sisi

Ni safari ya kuvutia kuwa ngano miongoni mwa magugu, wakati mwingine tukitiwa hofu kwa kuvunjika moyo lakini daima tukitulizwa kwa utulivu wenye ukomavu na hakikisho wa imani yetu. Unaporuhusu upendo wako kwa Mwokozi na upendo Wake kwako uzame kwa kina ndani ya moyo wako, ninakuahidi ongezeko la kujiamini, amani na shangwe katika kukabiliana na changamoto za maisha yako. Na Mwokozi anatuahidi: “Kwa hiyo, ni lazima niwakusanye watu wangu pamoja, kulingana na mfano wa ngano na magugu, ili ngano ipate kuhifadhiwa ghalani ili kumiliki uzima wa milele, na kuvikwa taji la utukufu wa selestia.”26 Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mathayo 24:3.

  2. Mathayo 24:33.

  3. Henry B. Eyring, “Imara katika Dhoruba,” Liahona, Mei 2022.

  4. Mathayo 13:16; msisitizo umeongezwa.

  5. Mathayo 13:38.

  6. Mathayo 13:30.

  7. Mzee Neal A. Maxwell alisema: “Waumini wa Kanisa wataishi katika hali hii ya ngano na magugu hadi Milenia. Baadhi ya magugu hujifanya kuwa ngano” (“Becometh as a Child,” Ensign, Mei 1996, 68).

  8. Ona Mafundisho na Maagano 86:4, 6.

  9. Ona Wakolosai 2:7.

  10. Ona Wakolosai 1:23; ona pia Waefeso 3:17; Neal A. Maxwell, “Grounded, Rooted, Established, and Settled,” (Brigham Young University devotional, Sept. 15, 1981), speeches.byu.edu.

  11. Katika Mathayo 13:22, Yesu aliwatahadharisha wafuasi Wake wasiache shida za ulimwengu na udanganyifu wa mali “kulisonga neno” na hivyo kusimamisha ukuaji wake wa kiroho. Ninapenda kuunganisha kirai “kulisonga neno” na sura ya kwanza ya Yohana, ambapo Yohana anatangaza kuwa neno ni Yesu: “Hapo mwanzo kulikuwako neno naye neno alikuwa Mungu. … Vyote vilifanyika kwa huyo; na pasipo yeye hapakufanyika chochote kilichofanyika” (Yohana 1:1, 3). Imani yetu katika Yesu Kristo, msimamo wetu wa kumfuata Yeye, upendo wetu kwa Mwokozi unaweza kusongwa au kuzuiliwa usikue, pale unapokuwa umenyimwa nuru na lishe ya kiroho (ona Alma 32:37–41).

  12. Ona Neil L. Andersen, “A Compensatory Spiritual Power for the Righteous” (Brigham Young University devotional, Aug. 18, 2015), speeches.byu.edu.

  13. Yohana 17:3.

  14. Mafundisho na Maagano 6:36.

  15. 1 Yohana 4:19.

  16. Mzee David B. Haight alisema:

    “Ni kweli kwamba baadhi hakika wamemwona Mwokozi, lakini mtu anaporejeleaa kwenye kamusi, anajifunza kwamba kuna maana zingine nyingi za neno ona, kama vile kumjua Yeye, kumtambua Yeye na kazi Yake, kuelewa umuhimu Wake au kumuelewa Yeye.

    “Such heavenly enlightenment and blessings are available to each of us” (“Temples and Work Therein,” Ensign, Nov. 1990, 61).

  17. Ona Mosia 5:13.

  18. Mafundisho na Maagano 20:77.

  19. Russell M. Nelson, “Agano lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 5.

  20. Russell M. Nelson, “Ni Kipi cha Kweli?,” Liahona, Nov. 2022, 29.

  21. Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Liahona,. Mei 2018, 96.

  22. Dallin H. Oaks, “Going Forward in the Second Century,” (Brigham Young University devotional, Sept. 13, 2022), speeches.byu.edu. Rais Oaks alisifia kirai “thubutu kuwa tofauti” katika makala ya hivi karibuni katika Deseret Magazine na Mzee Clark G. Gilbert, Kamishna wa Mfumo wa Elimu wa Kanisa, juu ya kulinda utambulisho wa kidini katika elimu ya juu (ona “Dare to Be Different,” Deseret Magazine, Sept. 2022, deseret.com).

  23. Kama ungependa kujifunza kutoka kwa wengine ambao walitoa maoni jinsi ambavyo wamekuwa tofauti kutoka kwenye ulimwengu, unaweza kusoma maoni yao kwenye Facebook (ona Neil L. Andersen, Facebook, Aug. 18, 2022, facebook.com/neill.andersen) au Instagram (ona Neil L. Andersen, Instagram, Aug. 18, 2022, instagram.com/neillandersen).

  24. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (mkutano wa ibada wa vijana ulimwenguni kote, Juni 3, 2018), HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  25. Anastasia Kocheva, “Facing the Conflict in Ukraine; Healing the Conflict in My Heart,” YA Weekly, Mei 2022.

  26. Mafundisho na Maagano 101:65.