Mkutano Mkuu
Utumishi Wetu wa Kidunia
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Utumishi Wetu wa Kidunia

Ninashuhudia kwamba baraka kuu za kiroho zimeahidiwa kwa wale wanaoupenda na kutuunza ulimwengu pamoja na wanaume na wanawake wenzao.

Tulipokuwa tukitembelea nchi yetu ya asili ya Ufaransa, mke wangu nami hivi karibuni tulifurahia kuwachukua wajukuu wetu wachache kutembelea bustani nzuri sana iliyo katika mji mdogo wa Giverny. Tulifurahia kuzunguka zunguka kwenye njia zake ili kustaajabia vitalu vya maua mazuri, nyunginyungi maji, na mwangaza ukiangaza vidimbwini.

Picha
Bustani la Givenry

Sehemu hii inayovutia ni matokeo ya shauku ya ubunifu ya mtu mmoja: mchoraji mkuu Claude Monet, ambaye, kwa miaka 40, aliitengeneza vyema na kuilima bustani yake ili kuifanya kuwa eneo lake la kazi ya uchoraji. Monet alizama katika fahari ya asili; kisha, kwa brashi yake ya rangi, aliwasilisha hisia alizohisi kwa michoro ya rangi na mwanga. Kwa miaka mingi, aliunda mkusanyiko wa ajabu wa mamia ya picha za kuchora, zilizochochewa moja kwa moja na bustani yake.

Picha
Mchoro wa Monet wa bustani

Mchoro kutoka Musée d’Orsay, Paris, France / Bridgeman Images

Akina kaka na akina dada, mwingiliano wetu na uzuri wa asili unaotuzunguka unaweza kutoa uzoefu wa kutia moyo na wa kupendeza maishani. Hisia tunazohisi huleta ndani yetu hisia ya kina ya shukrani kwa ajili ya Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, ambaye aliumba dunia hii adhimu—pamoja na milima na vijito vyake, mimea na wanyama—na wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Hawa.1

Kazi ya uumbaji sio mwisho wa yenyewe. Ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa watoto Wake. Kusudi lake ni kuandaa mazingira ambayo wanaume na wanawake wanaweza kujaribiwa, kutumia haki yao ya kujiamulia, kupata furaha na kujifunza na kusonga mbele, ili kwamba siku moja waweze kurudi kwenye uwepo wa Muumba wao na kurithi uzima wa milele.

Uumbaji huu wa ajabu uliandaliwa makusudi kwa faida yetu na ni uthibitisho hai wa upendo ambao Muumba anao kwa watoto Wake. Bwana alitangaza, “Ndiyo, vitu vyote vimeavyo kutoka ardhini … vimefanywa kwa faida na matumizi ya mwanadamu, kwa kuridhisha jicho na kufurahisha moyo.”2

Hata hivyo, zawadi ya kiungu ya Uumbaji haiji bila wajibu na majukumu. Wajibu huu unaelezewa vyema zaidi na dhana ya utumishi. Katika maneno ya injili, neno utumishi hutaja majukumu matakatifu ya kiroho au ya kimwili ya kutunza kitu ambacho ni cha Mungu, ambacho tunawajibikia.3

Kama ilivyofunzwa katika maandiko matakatifu, usimamizi wetu wa kidunia unajumuisha kanuni zifuatazo:

Kanuni ya kwanza: Dunia nzima, ikijumuisha vyote vilivyomo ndani yake, ni vya Mungu.

Muumba amekabidhi rasilimali za dunia na aina zote za uhai kwenye uangalizi wetu, lakini ana umiliki kamili. Alisema, “Mimi, Bwana, nilizitandaza mbingu, na kuijenga dunia, kazi halisi ya mkono wangu; na vitu vyote vilivyomo ni mali yangu.”4 Vyote vilivyo duniani ni vya Mungu, ikijumuisha familia zetu, miili yetu na hata uhai wetu wenyewe.5

Kanuni ya pili: Kama watumishi wa uumbaji wa Mungu, tuna wajibu wa kuviheshimu na kuvitunza.

Kama watoto wa Mungu, tumepokea jukumu la kuwa watumishi, watunzaji na walezi wa uumbaji Wake wa kiungu. Bwana alisema kwamba Yeye alimfanya “kila mtu awajibike, kama msimamizi juu ya baraka za kidunia, ambazo nimezifanya na kuzitayarisha kwa ajili ya viumbe vyangu.”6

Baba yetu wa Mbinguni anaturuhusu kutumia rasilimali za dunia kulingana na hiari yetu wenyewe. Hata hivyo uhuru wetu haupaswi kutafsiriwa kama kibali cha kutumia utajiri wa ulimwengu huu bila hekima au kizuizi. Bwana alitoa onyo hili: “Na imempendeza Mungu kwamba ametoa vitu hivi vyote kwa mwanadamu; kwani ni kwa sababu hii vilifanywa ili vitumiwe, kwa hekima, siyo ufujaji, wala siyo kwa kutumia nguvu.”7

Rais Russell M. Nelson aliwahi kusema: “Kama wafadhiliwa wa Uumbaji wa kiungu, tutafanya nini? Tunapaswa kuutunza ulimwengu, kuwa watumishi wenye hekima juu yake na kuuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo.”8

Zaidi ya kuwa hitaji la kisayansi au la kisiasa, utunzaji wa ulimwengu na mazingira yetu ya asili ni jukumu takatifu ambalo Mungu ametukabidhi, ambalo linapaswa kutujaza hisia ya kina ya wajibu na unyenyekevu. Pia ni sehemu muhimu ya ufuasi wetu. Tunawezaje kumheshimu na kumpenda Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo bila kuheshimu na kupenda uumbaji Wao?

Kuna mambo mengi ambayo tunaweza kufanya—kwa pamoja na kibinafsi—ili kuwa watumishi wazuri. Kwa kuzingatia hali zetu za kibinafsi, kila mmoja wetu anaweza kutumia rasilimali nyingi za ulimwengu kwa heshima na busara zaidi. Tunaweza kuunga mkono jitihada za jumuiya za kutunza ulimwengu. Tunaweza kufuata mitindo ya maisha ya kibinafsi na tabia zinazoheshimu uumbaji wa Mungu na kufanya maeneo yetu wenyewe ya kuishi kuwa safi, mazuri zaidi, na yenye kuinua zaidi.9

Usimamizi wetu juu ya uumbaji wa Mungu pia unajumuisha, katika kilele chake, wajibu mtakatifu wa kuwapenda, kuwaheshimu na kuwajali wanadamu wote ambao tunashiriki nao ulimwengu huu. Wao ni wana na mabinti wa Mungu, dada zetu na kaka zetu, na furaha yao ya milele ndiyo kusudi hasa la kazi ya uumbaji.

Mwandishi Antoine de Saint-Exupéry alisimulia yafuatayo: Siku moja, alipokuwa akisafiri kwa garimoshi, alijikuta ameketi katikati ya kundi la wakimbizi. Akiwa ameguswa sana na hali ya kukosa tumaini aliyoiona usoni mwa mtoto mchanga, alisema kwa mshangao, “Wakati kwa mabadiliko waridi mpya huoota katika bustani, watunza bustani wote hufurahi. Wao hulitenga waridi, hulitunza, hulilea. Lakini hakuna mtunza bustani kwa ajili ya watu.”10

Kaka na dada zangu, hatupaswi kuwa watunza bustani wa wanaume na wanawake wenzetu? Je, sisi si walinzi wa ndugu zetu? Yesu alituamuru tuwapende jirani zetu kama nafsi zetu.11 Kutoka kinywani Mwake, neno jirani halimaanishi tu ukaribu wa kijiografia; linaashiria ukaribu wa moyo. Linajumuisha wakaaji wote wa sayari hii— iwe wanaishi karibu nasi au katika nchi ya mbali, bila kujali asili yao, historia yao, au hali zao.

Kama wafuasi wa Kristo, tuna wajibu maalumu la kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya amani na upatano miongoni mwa mataifa yote ya ulimwengu. Ni lazima tufanye yote tuwezayo kulinda na kuleta faraja na ahueni kwa wanyonge, wahitaji na wale wote wanaoteseka au waliokandamizwa. Zaidi ya yote, zawadi kuu ya upendo tunayoweza kuwapa wenzetu ni kushiriki nao furaha ya injili na kuwaalika kuja kwa Mwokozi wao kupitia maagano na ibada takatifu.

Kanuni ya tatu: Tunaalikwa kushiriki katika kazi ya uumbaji.

Mchakato wa kiungu wa uumbaji bado haujakamilika. Kila siku, uumbaji wa Mungu unaendelea kukua, kupanuka na kuongezeka. Jambo zuri zaidi ni kwamba Baba yetu wa Mbinguni anatupatia mwaliko wa kushiriki katika kazi Yake ya uumbaji.

Tunashiriki katika kazi ya uumbaji pale tunapoilima ardhi au kuongeza miundo yetu wenyewe kwenye dunia hii—ilimradi tuonyeshe heshima kwa uumbaji wa Mungu. Michango yetu inaweza kuonyeshwa kupitia uundaji wa kazi za sanaa, usanifu, muziki, fasihi na utamaduni, ambavyo hupamba sayari yetu, kuhuisha hisia zetu na kuangaza maisha yetu. Pia tunachangia kupitia uvumbuzi wa kisayansi na kitabibu unaohifadhi dunia na uhai juu yake. Rais Thomas S. Monson alifanyia muhtasari dhana hii kwa maneno haya mazuri: “Mungu aliacha dunia bila kukamilika ili mwanadamu aoneshe ujuzi wake … ili mwanadamu apate kujua shangwe na utukufu wa uumbaji.”12

Katika mfano wa Yesu wa talanta, wakati bwana aliporudi kutoka katika safari yake, aliwasifu na kuwapa thawabu watumishi wawili waliokuza na kuzidisha talanta zao. Kinyume chake, alimwita mtumishi aliyeficha talanta yake ya pekee ardhini “hafai kitu,” na alichukua hata kile alichokuwa amepokea.13

Vivyo hivyo, kazi yetu kama watumishi wa uumbaji wa duniani haihusu tu na kuvilinda au kuvihifadhi. Bwana anatarajia sisi kufanya kazi kwa bidii, tukiongozwa na Roho Wake Mtakatifu, kukuza, kuimarisha na kuboresha rasilimali Yeye alizotukabidhi—si kwa manufaa yetu tu bali kuwabariki wengine.

Miongoni mwa mafanikio yote ya mwanadamu, hakuna kinachoweza kulinganishwa na uzoefu wa kuwa waumbaji wenza pamoja na Mungu katika kuleta uhai au katika kumsaidia mtoto kujifunza, kukua, na kustawi—iwe kama wazazi, walimu, viongozi au katika jukumu lingine lolote. Hakuna utumishi ulio mtakatifu zaidi, unaotosheleza zaidi, lakini pia unaotuhitaji zaidi, kuliko ule wa kushirikiana na Muumba wetu katika kuleta miili ya nyama kwa watoto Wake wa kiroho na kisha kuwasaidia kufikia uwezo wao wa kiungu.

Jukumu la uumbaji wenza hutumika kama ukumbusho wa kila mara kwamba uhai na mwili wa kila mtu ni vitakatifu, kwamba si mali ya mwingine ila Mungu, na kwamba ametufanya kuwa walinzi ili kuviheshimu, kuvilinda na kuvitunza. Amri za Mungu, zinazotawala uwezo wa uumbaji na uanzishwaji wa familia za milele, hutuongoza katika usimamizi huu mtakatifu, ambao ni wa muhimu sana kwa mpango Wake.

Kaka na dada zangu, tunapaswa kutambua kwamba yote ni ya kiroho kwa Bwana—ikiwa ni pamoja na mambo ya muda ya maisha yetu. Ninashuhudia kwamba baraka kuu za kiroho zimeahidiwa kwa wale wanaoupenda na kutuunza ulimwengu pamoja na wanaume na wanawake wenzao. Unapokuwa mwaminifu katika usimamizi huu mtakatifu na kuheshimu maagano yako ya milele, utakua katika ujuzi wa Mungu na Mwanawe, Yesu Kristo, na utahisi upendo Wao na ushawishi Wao kwa wingi zaidi katika maisha yako. Haya yote yatakutayarisha kukaa Nao na kupokea nguvu za ziada za uumbaji14 katika maisha yajayo.

Mwishoni mwa maisha haya ya duniani, Bwana atatutaka sisi kutoa hesabu kwa ajili ya utumishi wetu mtakatifu, ikijumuisha jinsi tulivyoujali uumbaji Wake. Ninaomba kwamba basi tutasikia maneno Yake ya upendo yakinong’onezwa mioyoni mwetu: “Vema, mtumishi mwema na mwaminifu: umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakufanya kuwa mtawala juu ya mambo mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako.”15 Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Mihtasari

  1. Dunia na vitu vyote vilivyo juu yake (isipokuwa Adamu na Hawa) viliumbwa na Yesu Kristo chini ya uongozi wa Baba; Adamu na Hawa, wazazi wetu wa kwanza, waliumbwa na Mungu Baba (ona Yohana 1:1–3; Musa 2:1, 26–27).

  2. Mafundisho na Maagano 59:18.

  3. Ona Spencer W. Kimball, “Welfare Services: The Gospel in Action,” Ensign, Nov. 1977, 76–79.

  4. Mafundisho na Maagano 104:14.

  5. Ona Spencer W. Kimball, “Welfare Services,” 76–79.

  6. Mafundisho na Maagano 104:13.

  7. Mafundisho na Maagano 59:20.

  8. Russell M. Nelson, “Uumbaji,” Liahona, Julai 2000, 104.

  9. Ona Gospel Topics, “Environmental Stewardship and Conservation,” topics.ChurchofJesusChrist.org.

  10. Antoine de Saint-Exupéry, Terre des Hommes (1939), 214; ona pia Wind, Sand and Stars (1939) katika Airman’s Odyssey (1984), 206.

  11. Ona Marko 12:31.

  12. Thomas S. Monson, “In Quest of the Abundant Life,” Ensign, Mar. 1988, 2.2.

  13. Ona Mathayo 25:14–30.

  14. Ona David A. Bednar na Susan K. Bednar, “Moral Purity” (Brigham Young University–Idaho devotional, Jan. 7, 2003), byui.edu.

  15. Mathayo 25:21.

Chapisha