Mkutano Mkuu
Mfuate Yesu Kristo kwa Hatua za Imani
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Mfuate Yesu Kristo kwa Hatua za Imani

Kristo anaweza kutusaidia leo kuweza kupita nyakati zetu ngumu. Yeye alifanya hivyo kwa wale waanzilishi wa mwanzoni, na anafanya hivyo sasa kwa kila mmoja wetu.

Asanteni, kwaya, kwa kuimba “Imani katika kila Hatua.” Muziki na maneno ya wimbo huo yaliandikwa mwaka 1996 na Kaka Newell Dayley1 katika maandalizi ya kusherehekea kumbukizi ya mwaka wa 150 wa kuwasili kwa waanzilishi wa mwanzoni kabisa kwenye hili Bonde la Salt Lake mnamo mwaka 1847.

Ingawa wimbo huu uliandikwa katika maandalizi kwa ajili ya sherehe hizo, ujumbe wake unagusa ulimwengu wote.

Daima nimekuwa nikipendezwa na kibwagizo:

Kwa imani katika kila hatua, tunamfuata Kristo, Bwana;

Na tukijawa na matumaini kupitia upendo wake msafi, tunaimba kwa sauti moja.2

Akina kaka na akina dada, ninashuhudia kwamba tunapomfuata Yesu Kristo kwa hatua za imani, kuna matumaini. Kuna matumaini katika Yesu Kristo. Kuna matumaini kwa ajili ya wote katika maisha haya. Kuna matumaini ya kushinda makosa yetu, huzuni yetu, mapambano yetu, majaribu yetu na matatizo yetu. Kuna matumaini katika toba na kusamehewa na katika kuwasamehe wengine. Ninashuhudia kwamba kuna matumaini na amani katika Kristo. Yeye anaweza kutusaidia leo kuweza kupita nyakati zetu ngumu. Yeye alifanya hivyo kwa wale waanzilishi wa mwanzoni, na atafanya hivyo sasa kwa kila mmoja wetu.

Mwaka huu ni kumbukizi ya miaka 175 ya kuwasili kwa waanzilishi wa mwanzo wa Kanisa kwenye Bonde la Salt Lake, kumbukizi ambalo limenifanya mimi kuwafikiria mababu zangu, ambao baadhi yao walitembea kutoka Nauvoo hadi Bonde hili la Salt Lake. Ninao mababu wa wazazi wangu ambao walitembea kwenye nyanda katika ujana wao. Henry Ballard alikuwa na umri wa miaka 20;3 Margaret McNeil alikuwa na miaka 13;4 na Joseph F. Smith, ambaye baadaye alikuja kuwa Rais wa sita wa Kanisa, alikuwa na miaka 9 tu alipofika katika hili Bonde la Salt Lake.5

Walikabiliana na kupungukiwa kwa kila aina wakiwa njiani, mfano msimu wa baridi, magonjwa, na upungufu wa mavazi ya kutosha na chakula. Kwa mfano, wakati Henry Ballard aliingia katika Bonde la Salt Lake, alifurahia kuona “Nchi ya Ahadi” lakini aliishi kwa hofu kwamba mtu angemuona kwa sababu nguo alizokuwa amevalia zilikuwa zimechanika hata hazingeficha mwili wake kabisa. Alijificha kwenye vichaka siku nzima mpaka giza kuingia. Kisha alikwenda kwenye nyumba na kuomba nguo ili kwamba angeweza kuendelea na safari yake na kuwatafuta wazazi wake. Alimshukuru Mungu kwamba alikuwa amefika katika nyumba ya siku za usoni salama.6

Mababu wa babu yake walimfuata Yesu Kristo kwa hatua za imani kote katika kila majaribu yao. Nina shukrani kwao kwa kutokata tamaa kamwe. Hatua zao za imani zimenibariki mimi na vizazi vilivyofuata, kama vile tu hatua zenu za imani leo zitakavyobariki wazao wenu.

Neno waanzilishi ni vyote viwili jina na kitendo. Kama jina linaweza kumaanisha mtu aliye miongoni mwa wale wa kwanza kugundua au kukaa katika eneo jipya. Kama kitendo, linaweza kumaanisha kufungua au kutayarisha njia kwa ajili ya wengine kufuata.7

Ninapofikiria kuhusu waanzilishi ambao wametayarisha njia kwa ajili ya wengine, kwanza ninamfikiria Nabii Joseph Smith. Joseph alikuwa mwanzilishi kwa sababu hatua zake za imani zilimwongozo kwenye kijisitu cha miti ambako alipiga magoti katika sala na akafungua njia kwa ajili yetu sisi kuwa na injili timilifu ya Yesu Kristo. Imani ya Joseph ya “kumwomba Mungu”8 katika asubuhi ile ya majira ya kuchipua ya mwaka 1820 ilifungua njia kwa ajili ya Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo ambao unajumuisha manabii na mitume kuitwa kuhudumu duniani kwa mara nyingine tena.9 Ninajua Joseph Smith ni nabii wa Mungu. Ninajua hatua zake zilizojaa imani zilimwongoza kupiga magoti katika uwepo wa Mungu Baba na Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo.

Hatua za imani za Nabii Joseph zilimwezesha yeye kuwa chombo cha Bwana katika kukileta Kitabu cha Mormoni, ambacho ni ushuhuda mwingine wa Yesu Kristo na neema Yake ya kulipia dhambi.

Kupitia imani na ustahimilivu wa Joseph Smith katika makabiliano na magumu na upinzani wa ajabu, yeye aliweza kuwa chombo mikononi mwa Bwana katika kulianzisha Kanisa la Yesu Kristo kwa mara nyingine tena ulimwenguni.

Wakati wa mkutano mkuu uliopita, nilizungumza kuhusu jinsi huduma yangu ya umisionari ilivyonibariki. Nilibarikiwa nilipokuwa nikifundisha kuhusu mpango wa wokovu ulio mtukufu wa Baba wa Mbinguni, Ono la Kwanza la Joseph Smith, na kutafsiri kwake Kitabu cha Mormoni. Mafundisho haya yaliyorejeshwa yameongoza hatua zangu za imani katika kuwafundisha wale waliokuwa tayari kuusikiliza ujumbe wa Urejesho wa injili.

Wamisionari wetu wa leo ni waanzilishi wa siku za sasa kwa sababu wao wanashiriki ujumbe huu mtukufu na watu kote ulimwenguni, hivyo wakifungua njia kwa ajili ya watoto wa Baba yetu wa Mbinguni kumjua Yeye na Mwanawe Yesu Kristo. Kuikubali injili ya Yesu Kristo kunafungua njia kwa kila mmoja kujiandaa kwa ajili ya na kupokea ibada na baraka za Kanisa na hekalu.

Mkutano uliopita, Rais Russell M. Nelson alisisitiza tena “kwamba Bwana anamtaka kila kijana wa kiume, mwenye kustahili, anayeweza ajiandae kwa ajili ya misheni na kuhudumu misheni” na kwamba “misheni pia ni fursa yenye nguvu, lakini ni ya hiari” kwa “wakina dada vijana na wanaojiweza.”10

Wapendwa wavulana na wasichana, hatua zenu za imani zitakusaidieni kufuata mwaliko wa Bwana wa kuhudumu misheni—kuwa waanzilishi katika siku hizi za sasa—kwa kufungua njia kwa ajili ya watoto wa Mungu ili kuipata njia na kubakia kwenye njia ya agano yenye kuwaongoza kurudi kwenye uwepo Wake mtukufu.

Rais Nelson amekuwa mwanzilishi katika Kanisa. Kama Mtume yeye amesafiri nchi nyingi na kufungua nchi hizo kwa ajili ya kuhubiriwa kwa injili. Muda mfupi baada ya kuwa nabii na Rais wa Kanisa, yeye alituomba sisi tuongeze uwezo wetu wa kiroho ili kupokea ufunuo.11 Anaendelea kutufundisha kuimarisha shuhuda zetu. Katika ibada ya vijana wakubwa, yeye alisema:

“Ninakusihini msimamie shuhuda zenu. Lifanyieni kazi hilo. Limilikini hilo. Lishughulikieni hilo. Lileeni hilo ili likue. …

“[Kisha] angalieni miujiza inayotokea katika maisha yenu.”12

Anatufundisha sisi jinsi ya kuwa wenye kujitegemea zaidi kiroho. Yeye amesema kwamba “katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila ushawishi wa kudumu wenye kuongoza, kuelekeza, kufariji wa Roho Mtakatifu.”13

Ninashuhudia kwamba Rais Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu hapa duniani leo.

Mwokozi wetu, Yesu Kristo ndiye mwanzilishi mkuu katika kuandaa njia. Ndiyo, Yeye ni “njia”14 kwa ajili ya kukamilisha mpango wa wokovu ili tuweze kutubu na, kupitia imani katika Yeye, turudi kwa Baba Yetu wa Mbinguni.

Yesu alisema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”15 Ameahidi hatatuacha pasipo mfariji; Yeye atatujia katika majaribu yetu.16 Ametualika sisi “tuje [Kwake] kwa kusudi kamili la moyo, na [Yeye] atatuponya [sisi].”17

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwokozi na Mkombozi wetu, Mwombezi wetu kwa Baba. Baba yetu wa Mbinguni amefungua njia kwetu ya kurudi Kwake kupitia kumfuata Mwanawe Mpendwa, Yesu Kristo, kwa imani katika kila hatua.

Mababu wa wazazi wangu na waanzilishi wengine wa mwanzoni walikabiliwa na vikwazo vingi walipokuwa wakija kwa magari ya kukokotwa, mikokoteni na kutembea kwa miguu kuja Bonde la Salt Lake. Sisi pia tunaweza kukabiliwa na changamoto katika safari zetu binafsi katika maisha yetu. Sisi hatusukumi mikokoteni au kuendesha magari yaliyofunikwa yakikokotwa na farasi au ng’ombe kwenye milima mirefu na kupitia kina kirefu cha theluji; tunajaribu kama wao walivyofanya kushinda majaribu na changamoto za kiroho za siku zetu. Tunazo njia za kutembelea; tuna vilima—na nyakati zingine milima—ya kukwea. Ingawa majaribu ya leo ni tofauti na yale ya waanzilishi wa mwanzo, changamoto zake ni sawa na zetu sisi.

Ni muhimu kumfuata nabii na kuweka miguu yetu ikiwa imepandwa imara kwenye njia ya agano kwa uaminifu kama ilivyokuwa kwa waanzilishi wa mwanzo.

Hebu na tumfuate Yesu Kristo kwa imani katika kila hatua. Tunahitaji kumhudumia Bwana na kuhudumiana sisi wenyewe. Tunahitaji kuimarishana wenyewe kiroho kwa kushika na kuheshimu maagano yetu. Hatupaswi kupoteza hisia za uharaka wa kushika amri. Shetani anajaribu kufifiza ahadi na upendo wetu kwa Mungu na kwa Bwana Yesu Kristo. Tafadhali kumbukeni kwamba kama mtu yeyote atapotea njia, kamwe hatapotea kwa Mwokozi wetu. Kwa baraka ya toba, tunaweza kumgeukia Yeye. Yeye atatusaidia kujifunza, kukua, na kubadilika tunapojitahidi kubaki kwenye njia ya agano.

Na daima tufuate katika hatua za Yesu Kristo na, kwa imani katika kila hatua, fokasi yetu iwe Kwake, tukiendelea kuweka miguu yetu thabiti kwenye njia ya agano, ndiyo maombi yangu ya unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona K. Newell Dayley, “Faith in Every Footstep,” Ensign, Jan. 1997, 15; Liahona, Feb. 1997, 22–23.

  2. Dayley, “Faith in Every Footstep,” Ensign, Jan. 1997, 15; Liahona, Feb. 1997, 23.

  3. Ona Henry Ballard diary, L. Tom Perry Special Collections, Harold B. Lee Library, Brigham Young University, Provo, Utah, archives.lib.byu.edu/repositories/ltpsc/resources/upb_msssc998.

  4. Ona “A ‘Small Glimpse’ into Pioneer Experiences,” Church News, June 15, 1996, thechurchnews.com.

  5. Ona Teachings of Presidents of the Church: Joseph F. Smith (1998), 400.

  6. Ona Douglas O. Crookston, ed., Henry Ballard: The Story of a Courageous Pioneer, 1832–1908 (1994), 14–15.

  7. Ona Merriam-Webster.com Dictionary, “pioneer.”

  8. Yakobo 1:5.

  9. Ona Joseph Smith—Historia ya 1:5–20.

  10. Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6; mkazo wa mwanzo umeondolewa.

  11. Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” Liahona,. Mei 2018, 96.

  12. Russell M. Nelson, “Chaguzi za Milele” (ibada duniani kote kwa vijana, Mei 15, 2022), broadcasts.ChurchofJesusChrist.org.

  13. Russell M. Nelson, “Ufunuo kwa ajili ya Kanisa, Ufunuo kwa ajili ya Maisha Yetu,” 96.

  14. Yohana 14:6.

  15. Yohana 14:6.

  16. Ona Yohana 14:16–18.

  17. 3 Nefi 18:32.

Chapisha