Mkutano Mkuu
Ufuasi wa Kudumu
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


10:23

Ufuasi wa Kudumu

Tunaweza kupata kujiamini na amani ya kiroho tunapokuza tabia za utakatifu na desturi za haki ambazo zinaweza kuendeleza na kuchochea moto wa imani yetu.

Wakati wa majira ya joto yaliyopita, zaidi ya vijana wetu 200,000 kote ulimwenguni walikua katika imani katika mojawapo wa mamia ya vikao vya wiki nzima vya Kwa ajili ya Nguvu kwa Vijana, au mikutano ya KNV. Kutoka katika vizuizi vya kujitenga vya janga la ulimwenguni kote, kwa wengi lilikuwa tendo la imani katika Bwana hata kuhudhuria tu. Wengi wa washiriki vijana walionekana kufuata tao lilelile la juu kuelekea uongofu wa kina. Mwishoni wa wiki yao, nilipendelea kuwauliza, “Ilienda vipi?”

Wao wakati mwingine walisema kitu kama hiki: “Sawa, Jumatatu nilimkasirikia sana mama yangu kwa sababu alinisukuma nije. Na sikumjua yeyote. Na sikujua kama ilikuwa inafaa kwangu. Na nisingepata rafiki yeyote. … Lakini sasa ni Ijumaa, na nataka tu kubaki hapa. Ninataka kumhisi Roho katika maisha yangu. Ninataka kuishi kama hivi.”

Kila mmoja wao ana hadithi yake mwenyewe ya kusimulia ya nyakati za uwazi na vipawa vya kiroho vikiwatakasa na kuwabeba kwenye tao la ukuaji. Mimi pia nilibadilishwa na majira haya ya joto ya KNV kwani nimeona Roho wa Mungu bila kusita akijibu matamanio ya haki ya mioyo binafsi ya umati wa vijana hawa ambao kila mmoja alipata ujasiri wa kumtumaini Yeye katika wiki ya uangalizi Wake.

Kama meli ya chuma inayong’aa ikiwa baharini, tunaishi katika mazingira yaliyo na kutu ya kiroho ambapo misimamo angavu sana lazima idumishwe kwa makini vinginevyo inaweza kukwaruzwa, kisha kupatwa na kutu, na kisha kuvunjika.

Ni Mambo ya Aina gani Tunaweza Kufanya ili Kudumisha Moto wa Misimamo Yetu?

Uzoefu kama mikutano ya KNV, kambi, mikutano ya sakramenti na misheni inaweza kusaidia kuwasha shuhuda zetu, ikitupeleka kupitia tao la ukuaji na ugunduzi wa kiroho hadi sehemu za amani. Lakini ni nini lazima tufanye ili tuendelee kubaki hapo na kuendelea “kusonga mbele tukiwa na imani imara katika Kristo” (2 Nefi 31:20), badala ya kuteleza kurudi nyuma? Lazima tuendelee kufanya mambo yale ambayo yalituleta hapo tangu mwanzo, kama vile kuomba kila mara, kuzama katika maandiko na kuhudumu kwa dhati.

Kwa baadhi yetu, inaweza kuhitaji zoezi la kumtumaini Bwana hata kuhudhuria mkutano wa sakramenti. Lakini tukiwa hapo, ushawishi wa uponyaji wa sakramenti ya Bwana, ujazo wa kanuni za injili na kujali kwa jamii ya kanisa kunaweza kutupeleka nyumbani kwenye uwanda wa juu.

Ni Wapi Nguvu za Kukusanyika Pamoja Zinatoka?

Katika KNV, vijana wetu laki moja na zaidi walikuja kumjua vyema Mwokozi kwa kutumia mbinu rahisi ya kuja pamoja ambapo wawili wao au zaidi walikusanyika katika jina Lake (ona Mathayo 18:20), wakijishughulisha na injili na maandiko, wakiimba pamoja, wakiomba pamoja na kupata amani katika Kristo. Hili ni agizo lenye nguvu kwa ajili ya mwamko wa kiroho.

Kundi hili lililotawanyika la akina kaka na akina dada sasa limeenda nyumbani kubainisha kile inachomaanisha kuendelea “kumtumaini Bwana” (Mithali 3:5; dhima ya vijana ya mwaka 2022) wakati wanaposombwa na makelele ya ulimwengu. Ni kitu kimoja “kumsikiliza Yeye” (Joseph Smith—Histora ya 1:17) katika mahali pa kimya pa kutafakari ukiwa na maandiko yaliyofunguliwa. Lakini ni kitu kingine kabisa kubeba ufuasi wetu katika maisha ya duniani yaliyo na vivuta mawazo vingi, ambapo lazima tujitahidi “kumsikiliza Yeye,” hata kupitia ukungu wa wasiwasi binafsi na ujasiri unaopungua. Na kusiwe na shaka: ni mambo hasa ya kishujaa yaliyoonyeshwa na vijana wetu wakati wanapoweka mioyo yao na akili zao kusimama wima dhidi ya misukosuko mikubwa ya maadili ya wakati wetu.

Familia Zinaweza Kufanya Nini Nyumbani ili Kujenga juu ya Nguvu Iliyoanzishwa kwenye Shughuli za Kanisa?

Wakati mmoja nilitumikia kama mume wa rais wa kigingi wa Wasichana. Usiku mmoja nilipatiwa kazi ya kupanga biskuti sebuleni wakati mke wangu akiendesha mkutano ndani ya kanisa kwa ajili ya wazazi na mabinti zao wakijiandaa kuhudhuria kambi ya Wasichana wiki iliyofuata. Baada ya kuelezea mahali pa kuwa na nini cha kuleta, alisema, “Sasa, Jumanne asubuhi mnapowalete wasichana wenu wazuri kwenye basi, muwakumbatie sana. Na muwaage kwa kuwabusu—kwa sababu hawatarudi.”

Nilisikia mtu akitweta, kisha nikatambua ilikuwa ni mimi. “Hawatarudi?”

Lakini kisha akaendelea: “Mtakapowaleta hao wasichana wa Jumanne-asubuhi, wataacha vivuta mawazo vya mambo ya chini na watatumia wiki pamoja wakijifunza na kukua na kumtumaini Bwana. Tutaomba pamoja na kuimba na kupika na kutumikia pamoja na kushiriki shuhuda pamoja na kufanya mambo ambayo yanaturuhusu kumhisi Roho wa Baba wa Mbinguni, wiki nzima, mpaka yaingie hata kwenye mifupa yetu. Na Jumamosi, wasichana ambao mtawaona wakishuka kutoka kwenye basi hilo hawatakuwa wale mliowaleta Jumanne. Watakuwa viumbe wapya. Na kama mtaendelea kuwasaidia wakiwa katika uwanda huo wa juu, watawashangaza. Wataendelea kubadilika na kukua. Na vivyo hivyo kwa familia yenu.”

Jumamosi hiyo, ilikuwa kama vile alivyotabiri. Nilipokuwa nikipakia mahema, nilisikia sauti ya mke wangu katika ule ukumbi ambao wasichana walikuwa wamekusanyika kabla ya kwenda nyumbani. Nilimsikia akisema, “Ee, tazama. Tumekuwa tukiwatazama wiki nzima. Wasichana wetu wa Jumamosi.”

Vijana hodari wa Sayuni wanasafiri kupitia nyakati nzuri mno. Kupata furaha katika dunia hii ya vurugu iliyotabiriwa bila kuwa sehemu ya dunia hiyo, ikiwa na giza kuelekea utukufu, ni agizo lao hasa. Takriban miaka mia moja iliyopita, G. K Chesterton alizungumza kana kwamba aliona hitaji hili kama kiini chake kikiwa kimelenga nyumbani na kikisaidiwa na Kanisa wakati aliposema, “Tunahitaji kuuhisi ulimwengu mara moja kama kasri ya zimwi, itakayoharibiwa na bado kama nyumba yetu wenyewe, ambayo tunaweza kurudi kwayo jioni” (Orthodoxy [1909], 130).

Kwa shukrani, hawaendi nje kupigana peke yao. Wana mmoja na mwingine. Na ninyi mpo nao. Na wanamfuata nabii aliye hai, Rais Russell M. Nelson, ambaye anaongoza kwa ujasiri wa uelewa wa mwonaji katika kutangaza kwamba kazi kuu ya nyakati hizi—kukusanya Israeli—itakuwa kuu na ya muujiza (ona “Hope of Israel” [worldwide youth devotional, June 3, 2018], HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org).

Majira haya ya joto, mimi na mke wangu, Kalleen, tulikuwa tunabadili ndege huko Amsterdam ambapo, miaka mingi iliyopita, nilikuwa mmisionari mpya. Baada ya miezi mingi ya kusumbuka kujifunza Kidachi, ndege yetu ya KLM ilikuwa inatua na rubani alitoa matangazo yasioeleweka kwenye kipaza sauti. Baada ya dakika za ukimya, mwenza wangu alinong’ona, “Nadhani hicho kilikuwa Kidachi.” Tulitazama juu, tukisoma mawazo ya kila mmoja: “Yote yalikuwa yamepotea.”

Lakini yote hayakupotea. Nilipostaajabu juu ya hatua za imani tulizokuwa tumechukua wakati tulipotembea katika uwanja huu wa ndege kuelekea njia yetu ya miujiza ambayo ingetiririka juu yetu kama wamisionari, ghafla nilirudishwa katika hali yangu ya sasa na mmisionari hai, anayevuta pumzi ambaye alikuwa anapanda ndege kurudi nyumbani. Alijitambulisha na kuuliza, “Rais Lund, napaswa kufanya nini sasa? Nifanye nini ili nibaki imara?”

Hali kadhalika, hili ni swali lile lile ambalo liko ndani ya akili za vijana wetu wakati wanapotoka kwenye mikutano ya KNV, kambi za vijana, safari za hekaluni na wakati wowote wanapohisi nguvu za mbinguni: “Ni kwa jinsi gani kumpenda Mungu kunaweza kugeuka kuwa ufuasi wa kudumu?”

Nilihisi mafuriko ya upendo kwa ajili ya mmisionari huyu akitumikia saa zake za mwisho za misheni yake na katika wasaa ule wa utulivu wa Roho, nilisikia sauti yangu ikipasuka pale niliposema kwa urahisi, “Hauhitaji kuvalia beji ili kushuhudia jina Lake.”

Nilitaka kuweka mikono yangu kwenye mabega yake na kusema, “Hivi ndivyo unavyofanya. Unaenda nyumbani na unakuwa hivi. Wewe ni mzuri sana unakaribia kung’aa gizani. Nidhamu na dhabihu yako ya misheni imekufanya wewe kuwa mwana wa kupendeza wa Mungu. Endelea kufanya nyumbani kile ambacho kimekuwa na nguvu sana hapa. Umejifunza kuomba na nani wa kumuomba na lugha ya maombi. Umejifunza maneno Yake na kuja kumpenda Mwokozi kwa kujaribu kuwa kama Yeye. Umempenda Mwokozi jinsi Yeye alivyompenda Baba Yake, umewatumikia wengine jinsi Yeye alivyowatumikia na umeishi amri jinsi Yeye alivyoziishi—na ulipokosa kufanya hivyo, ulitubu. Ufuasi wako si tu wito kwenye T-sheti—umekuwa sehemu ya maisha yako uliyoyaishi kimamilifu kwa ajili ya wengine. Kwa hiyo nenda nyumbani na ufanye hivyo. Kuwa hivyo. Beba nguvu hii ya kiroho katika maisha yako yote.”

Ninajua kwamba kupitia kumtumaini Bwana Yesu Kristo na njia Yake ya agano, tunaweza kupata kujiamini na amani ya kiroho tunapokuza tabia za utakatifu na desturi za haki ambazo zinaweza kuendeleza na kuchochoea moto wa imani yetu. Na kila mmoja wetu asogee karibu na ule moto wenye kuleta joto na, lolote liwalo, tubakie. Katika jina la Yesu Kristo, amina.