Nao Wakataka Kumwona Yesu Yeye ni Nani
Ninatoa ushahidi kwamba Yesu yu hai, kwamba anatujua, na kwamba ana uwezo wa kuponya, kubadilisha, na kusamehe.
Akina kaka, akina dada, na marafiki, mnamo 2013 mimi na mke wangu, Laurel, tuliitwa kuhudumu kama viongozi wa misheni katika Misheni ya Czech/Slovak. Watoto wetu wanne walihudumu pamoja nasi.1 Tulibarikiwa kama familia kuwa na wamisionari mahiri na Watakatifu wa ajabu wa Czech na Slovakia. Tunawapenda.
Familia yetu ilipoingia katika uwanja wa misheni, jambo ambalo Mzee Joseph B. Wirthlin alifundisha lilienda nasi. Katika hotuba yenye kichwa cha habari “Amri Kuu” Mzee Wirthlin aliuliza, “Je, unampenda Bwana?” Ushauri wake kwetu sisi ambao tungejibu “ndiyo” ulikuwa rahisi na wa kina: “Tumieni muda pamoja Naye. Tafakarini maneno Yake. Jitieni nira Yake. Tafuteni kuelewa na kutii.”2 Mzee Wirthlin kisha aliahidi baraka za kuleta mabadiliko kwa wale walio tayari kutoa muda na nafasi kwa Yesu Kristo.3
Tulichukua ushauri na ahadi ya Mzee Wirthlin moyoni. Pamoja na wamisionari wetu, tulitumia muda mrefu pamoja na Yesu tukijifunza Mathayo, Marko, Luka, na Yohana kutoka Agano Jipya na 3 Nefi kutoka Kitabu cha Mormoni. Mwishoni mwa kila mkutano wa wamisionari, tulijikuta tumerudi katika kile tulichotaja kama “Injili Tano”4 kusoma, kujadili, kuzingatia na kujifunza kuhusu Yesu.
Kwangu mimi, kwa Laurel, na kwa wamisionari wetu, kutumia muda na Yesu katika maandiko kulibadilisha kila kitu. Tulipata shukrani ya kina ya kile Yeye alichokuwa na kile kilicho muhimu Kwake. Kwa pamoja tulizingatia jinsi Yeye alivyofundisha, kile Alichofundisha, jinsi alivyoonesha upendo, kile alichofanya ili kubariki na kuhudumu, miujiza Yake, jinsi alivyojibu usaliti, kile alichofanya kwenye hisia ngumu za kibinadamu, vyeo na majina Yake, jinsi alivyosikiliza, jinsi Alivyosuluhisha mzozo, ulimwengu Alimoishi, mifano Yake, jinsi Alivyohimiza umoja na ukarimu, uwezo Wake wa kusamehe na kuponya, mahubiri Yake, maombi Yake, dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Ufufuko Wake, injili Yake.
Mara nyingi tulijihisi kama yule mtu “[mfupi] kwa kimo” Zakayo akikimbia kupanda mkuyu Yesu alipokuwa akipitia Yeriko kwa sababu, kama Luka alivyoeleza, ‘tulitafuta kumwona Yesu alikuwa nani.5 Haikuwa Yesu kwa jinsi tulivyotaka au tulivyotamani awe, bali Yesu jinsi alivyokuwa na alivyo.6 Kama vile Mzee Wirthlin alivyoahidi, tulijifunza kwa njia ya kweli kwamba “injili ya Yesu Kristo ni injili ya mabadiliko. Inatuchukulia sisi kama wanaume na wanawake wa dunia na inatusafisha kuwa wanaume na wanawake wa milele.”7
Hizo zilikuwa siku maalum. Tulikuja kuamini kwamba “kwa Mungu hakuna lisilowezekana.”8 Alasiri takatifu huko Prague, Bratislava, au Brno, tukipata uzoefu wa nguvu na uhalisia wa Yesu, huendelea kuvuma katika maisha yetu yote.
Mara nyingi tulisoma Marko 2:1–12. Hadithi hapo inavutia. Ninataka kusoma sehemu yake moja kwa moja kutoka kwa Marko, na kisha nishiriki jinsi nilivyoielewa baada ya kujifunza kwa kina na majadiliano na wamisionari wetu na wengine.9
“[Yesu] akaingia Kapernaumu tena baada ya siku kadha wa kadha; na ikasikika kwamba yumo nyumbani.
“Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni, akawa akisema nao neno lake.
“Wakaja watu wakimleta mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne.
“Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo: na wakiisha kuivunja wakaliteremsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza.
“Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”
Baada ya mazungumzo na baadhi ya watu katika umati,10 Yesu anamtazama mtu aliyepooza na kumponya kimwili, akisema:
“Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako uende nyumbani kwako.
“Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, namna hii hatujapata kuiona kamwe.”11
Sasa hadithi kama nilivyokuja kuielewa: mapema katika huduma Yake, Yesu alirudi Kapernaumu, kijiji kidogo cha wavuvi kilichoko kwenye ufuko wa kaskazini wa Bahari ya Galilaya.12 Yeye hivi karibuni alikuwa amefanya mfululizo wa miujiza kwa kuponya wagonjwa na kutoa pepo wabaya.13 Wakiwa na shauku ya kumsikia na kumwona mtu anayeitwa Yesu, wanakijiji walikusanyika kwenye nyumba ambayo ilisemekana kuwa anakaa.14 Walipofanya hivyo, Yesu alianza kufundisha.15
Nyumba za wakati huo katika Kapernaumu zilikuwa na paa tambarare, za orofa moja, zikiwa zimepangwa pamoja.16 Paa na kuta zilikuwa mchanganyiko wa mawe, mbao, udongo, na nyasi, zilizofikiwa kwa seti ya hatua rahisi kando ya nyumba.17 Umati wa watu ukaongezeka upesi katika ile nyumba, wakajaza chumba ambacho Yesu alikuwa akifundisha, wakaenea hata njiani.18
Hadithi hiyo inamlenga mtu “mgonjwa wa kupooza” na marafiki zake wanne.19 Kupooza ni aina ya kiharusi, mara nyingi huambatana na udhaifu na kutetemeka.20 Ninawaza kwamba mmoja wa wale wanne akiwaambia wengine, “Yesu yuko kijijini kwetu. Sote tunajua miujiza aliyofanya na wale aliowaponya. Ikiwa tunaweza kumfikisha tu rafiki yetu kwa Yesu, pengine na yeye pia anaweza kuponywa.”
Kwa hiyo, kila mmoja wao anachukua kona ya mkeka au kitanda ambacho rafiki yao amelazwa na kuanza kumbeba kupitia njia za vichochoroni, nyembamba, zisizo na lami za Kapernaumu.21 Misuli ikiwa inauma wanapinda kona ya mwisho na kugundua kwamba umati au, kama maandiko yanavyouita, “msongamano” wa watu waliokusanyika kusikiliza ni mkubwa sana kiasi kwamba haiwezekani kufika kwa Yesu.22 Kwa upendo na imani, wanne hawa hawakati tamaa. Badala yake, wanapanda ngazi hadi juu ya paa tambarare, kwa uangalifu wakimwinua rafiki yao na kitanda chake, wanavunja dari ya chumba ambamo Yesu anafundisha, na kumshusha rafiki yao.23
Fikiria kwamba katikati ya kile ambacho lazima kilikuwa kipindi kigumu cha kufundisha, Yesu anasikia kelele ya kukwaruza, anatazama juu, na kuona shimo linaloongezeka kwenye dari huku vumbi na nyasi zikianguka ndani ya chumba. Mtu aliyepooza kitandani kisha anashushwa chini. Inashangaza kwamba Yesu anatambua kwamba huku si kukatiza bali badala yake ni jambo muhimu. Anamtazama mtu yule kitandani, anamsamehe dhambi zake hadharani, na kumponya kimwili.24
Kwa maelezo hayo ya Marko 2 akilini, kweli kadhaa muhimu zinakuwa wazi kuhusu Yesu kama Kristo. Kwanza, tunapojaribu kumsaidia mtu tunayempenda kuja kwa Kristo, tunaweza kufanya hivyo kwa kujiamini kwamba Yeye anao uwezo wa kuinua mzigo wa dhambi na kusamehe. Pili, tunapoleta magonjwa ya kimwili, kihisia, au mengine kwa Kristo, tunaweza kufanya hivyo tukijua kwamba anao uwezo wa kuponya na kufariji. Tatu, tunapofanya bidii kama wale wanne kuwaleta wengine kwa Kristo, tunaweza kufanya hivyo kwa uhakika kwamba Yeye huona nia zetu za kweli na ataziheshimu ipasavyo.
Kumbuka, mafundisho ya Yesu yalivurugwa na kutokea kwa shimo kwenye paa. Badala ya kuwaadhibu au kuwafukuza wale wanne waliotoboa shimo darini kwa kuvuruga somo, maandiko yanatuambia kwamba “Yesu aliiona imani yao.”25 Wale walioshuhudia muujiza kisha “wakastaajabu, wakamtukuza Mungu, ambaye amewapa wanadamu uwezo wa namna hii.”26
Akina kaka na akina dada, wacha nimalizie kwa mambo mawili ya ziada. Iwe kama wamisionari, watumishi, marais wa Muungano wa Usaidizi, maaskofu, walimu, wazazi, ndugu, au marafiki, sisi sote tunahusika kama wanafunzi Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kazi ya kuwaleta wengine kwa Kristo. Hivyo, sifa zilizoonyeshwa na marafiki wanne zafaa kuzingatiwa na kuigwa.27 Wao ni wajasiri, wenye kubadilika, wastahimilivu, wabunifu, wenye uwezo mwingi, wenye matumaini, wenye kudhamiria, waaminifu, wenye matumaini, wanyenyekevu, na wenye kuvumilia.
Zaidi ya hayo, marafiki wanne wanasisitiza umuhimu wa kiroho wa kuwa na jumuiya na ushirika.28 Ili kumleta rafiki yao kwa Kristo, kila mmoja wa wanne lazima ashikilie kona yake. Kama mmoja ataachia, mambo yanakuwa magumu zaidi. Ikiwa wawili watakata tamaa, kazi hiyo inakuwa haiwezekani kabisa. Kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya katika ufalme wa Mungu.29 Tunapotimiza jukumu hilo na kufanya sehemu yetu, tunabeba kona yetu. Iwe huko Argentina au Vietnam, Accra au Brisbane, tawi au kata, familia au wenzi wa mmisionari, kila mmoja wetu anayo kona ya kubeba. Tunapofanya hivyo, na iwapo tutafanya, Bwana hutubariki sote. Jinsi alivyoona imani yao, ndivyo atakavyoiona imani yetu na kutubariki sisi kama watu.
Kwa nyakati tofauti nimeshikilia kona ya kitanda na nyakati zingine nimekuwa mtu niliyebebwa. Sehemu ya nguvu ya hadithi hii ya ajabu ya Yesu ni kwamba inatukumbusha tu jinsi tunavyohitajiana, kama kaka na dada, ili kuja kwa Kristo na kubadilishwa.
Haya ni baadhi ya mambo machache niliyojifunza kwa kutumia muda pamoja na Yesu katika Marko 2.
“Mungu na atujalie tuwe na uwezo wa [kubeba kona yetu], ili tusikwepe, tusiogope, bali tuwe na nguvu katika imani yetu, na kudhamiria katika kazi yetu, ili kutimiza makusudio ya Bwana.”28
Ninatoa ushahidi kwamba Yesu yu hai, kwamba anatujua, na kwamba ana uwezo wa kuponya, kubadilisha, na kusamehe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.