Mfumo kwa ajili ya Ufunuo Binafsi
Tunahitaji kuelewa mfumo ambao ndani yake Roho Mtakatifu hufanya kazi. Tunapofanya kazi ndani ya mfumo, Roho Mtakatifu anaweza kufungua umaizi wa kushangaza.
Kama wengi wenu, nimekuwa nikishawishiwa sana na Mzee Dieter F. Uchtdorf kwa miaka mingi. Hiyo inaelezea, angalau kwa sehemu kile ninachotaka kusema.1 Kwa hiyo, nikiomba radhi kwake …
Marubani mahiri wa ndege huruka katika viwango vya ndege zao na hufuata maelekezo ya waongoza ndenge juu ya matumizi ya njia ya kurukia na njia ya ndege. Kwa ufupi ni kwamba, marubani hufanya kazi ndani ya mfumo. Bila kujali wana akili kiasi gani au vipaji kiasi gani, ni kwa kuruka tu ndani ya mfumo huu ndipo marubani wanaweza kwa usalama kufungua uwezo mkubwa wa ndege ili kukamilisha malengo yake ya kimuujiza.
Katika njia sawa na hii, tunapata ufunuo binafsi ndani ya mfumo. Baada ya ubatizo, tunapewa zawadi kuu inayotenda kazi, kipawa cha Roho Mtakatifu.2 Tunapojitahidi kubaki katika njia ya agano,3 ni “Roho Mtakatifu … [ambaye] atatuonyesha [sisi] mambo yote [ambayo sisi] tunapaswa kufanya.”4 Tunapokuwa hatuna uhakika au kukosa amani, tunaweza kuomba usaidizi wa Mungu.5 Ahadi ya Mwokozi isingekuwa wazi zaidi: “Ombeni, nanyi mtapewa; … kwa maana kila aombaye hupokea.”6 Kwa usaidizi wa Roho Mtakatifu, tunaweza kubadilisha asili yetu ya kiungu kuwa hatma yetu ya milele.7
Ahadi ya ufunuo binafsi kupitia Roho Mtakatifu ni ya kustaajabisha, ikifanana sana na ndege katika kuruka. Na kama marubani wa ndege, tunahitaji kuelewa mfumo ambao ndani yake Roho Mtakatifu hufanya kazi kutoa ufunuo binafsi. Tunapofanya kazi ndani ya mfumo, Roho Mtakatifu anaweza kufungua umaizi, mwongozo na faraja ya kushangaza. Nje ya mfumo huo, bila kujali akili au vipawa vyetu, tunaweza kudanganywa na kuanguka na kuungua.
Maandiko huunda kipengele cha kwanza cha mfumo huu kwa ajili ya ufunuo binafsi.8 Kusherehekea katika maneno ya Kristo, kama yanavyopatikana katika maandiko, huchochea ufunuo binafsi. Mzee Robert D. Hales alisema:“Tunapotaka kuzungumza na Mungu, tunasali. Na wakati tunapotaka Yeye azungumze nasi, tunayapekua maandiko.”9
Maandiko pia hutufundisha jinsi ya kupokea ufunuo binafsi.10 Na tunaomba kile kilicho cha haki na kizuri11 na si kile kilicho kinyume na mapenzi ya Mungu.12 Sisi “hatuombi vibaya,” tukiwa na malengo yasiyofaa kuinua ajenda yetu au kutimiza tamaa zetu.13 Zaidi ya yote, tunapaswa kumuomba Baba wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo,14 tukiamini kwamba tutapokea.15
Kipengele cha pili cha mfumo ni kwamba tunapokea ufunuo binafsi kulingana na utambuzi wetu pekee na si katika ridhaa za wengine. Kwa maneno mengine, tunaruka na kutua katika njia tuliyopangiwa. Umuhimu wa njia maalumu iliyopangwa ulifunzwa zamani katika histroria ya Urejesho. Hiram Page, mmoja wa Mashahidi Wanane wa Kitabu cha Mormoni, alidai kuwa alikuwa akipokea ufunuo kwa ajili ya Kanisa zima. Waumini wengi walidanganyika na kushawishika kimakosa.
Katika kujibu, Bwana alifunua wazi kwamba “hakuna mtu atakayeteuliwa kupokea amri na mafunuo katika kanisa hili isipokuwa mtumishi wangu Joseph Smith … mpaka nitakapoteua … mwingine badala yake.”16 Mafundisho, amri na mafunuo kwa ajili ya Kanisa ni haki ya nabii aliye hai, anayeyapokea kutoka kwa Bwana Yesu Kristo.17 Hiyo ndiyo njia ya nabii.
Miaka mingi iliyopita, nilipokea simu kutoka kwa mtu mmoja aliyekuwa amekamatwa kwa makosa ya uvamizi. Aliniambia kwamba ilifunuliwa kwake kwamba maandiko ya ziada yalikuwa yamefukiwa chini ya sakafu ya jengo alilotaka kuingia. Alidai kuwa mara baada ya kupata maandiko ya ziada, alijua kwamba angeweza kupokea kipawa cha kutafsiri, angeleta maandiko mapya na kurekebisha mafundisho na mwelekeo wa Kanisa. Nilimwambia kuwa alikuwa amedanganyika na alinitaka mimi nisali juu ya hilo. Nilimwambia nisingefanya hivyo. Alitoa lugha ya matusi na kukata simu.18
Sikuhitaji kusali juu ya ombi lake kwa sababu moja rahisi lakini ya msingi: ni nabii pekee hupokea ufunuo kwa ajili ya Kanisa. Itakuwa ni “kinyume na mapenzi ya Mungu”19 kwa wengine kupokea ufunuo kama huo, ambao unapatikana katika njia ya nabii.
Ufunuo binafsi hakika ni wa watu binafsi. Unaweza kupokea ufunuo, kwa mfano, kuhusu wapi pa kuishi, kazi ipi ya kufanya au nani wa kufunga naye ndoa.20 Viongozi wa Kanisa wanaweza kutoa mafundisho na kushiriki ushauri wa kiroho, ila jukumu la maamuzi haya hubaki kwako mwenyewe. Huo ni ufunuo wako kupokea; hiyo ndio njia yako.
Kipengele cha tatu cha mfumo ni kwamba ufunuo binafsi utaenda sambamba na amri za Mungu na maagano tuliyofanya na Yeye. Fikiria sala inayoenda kama hivi: “Baba wa Mbinguni, huduma za Kanisa zinakera. Naweza kukuabudu siku ya Sabato katika milima au ufukweni? Naweza kusamehewa kwenda kanisani na kupokea Sakramenti ila niendelee kuwa na baraka zilizoahidiwa kwa kuitakasa siku ya Sabato?”21 Katika kujibu sala kama hii, tunaweza kutarajia jibu la Mungu: “Mwanangu, tayari nimefunua mapenzi yangu kuhusiana na siku ya Sabato.”
Tunapoomba ufunuo kuhusu kitu fulani ambacho Mungu tayari ameshakitolea mwongozo wa wazi, tunajiingiza katika kutafsiri hisia zetu kimakosa na kusikia yale tunayotaka kusikia. Mtu mmoja aliwahi kuniambia kuhusu jitihada zake za kuimarisha hali ya kifedha ya familia yake. Alikuwa na wazo la kufanya ubadhirifu wa pesa kama suluhisho, alisali juu ya hilo na akahisi kwamba amepata ufunuo thabiti wa kufanya hivyo. Nilijua kwamba alikuwa amedanganywa kwa sababu alitafuta ufunuo kinyume na amri ya Mungu. Nabii Joseph Smith alionya, “Hakuna maumivu makali kwa watoto wa watu zaidi ya yale ya kuwa chini ya ushawishi wa roho ya uongo, wakati wanapofikiri wana Roho wa Mungu.”22
Wengine wanaweza kuonyesha kuwa Nefi alivunja amri alipomuua Labani. Hata hivyo, angalizo hili halipingani na sheria—sheria kwamba ufunuo binafsi utaendana na amri za Mungu. Hakuna maelezo rahisi ya tulio hili yanayojitosheleza kabisa, ila nitaangazia baadhi ya vipengele hivyo. Swala halikuanza na Nefi kuuliza kama angeweza kumuua Labani. Hakikuwa kitu alichotaka kufanya. Kumuua Labani haikuwa kwa ajili ya manufaa binafsi ya Nefi bali kwa ajili ya kutoa maandiko kwa taifa lijalo na watu wa agano. Na Nefi alikuwa na uhakika kuwa huo ulikuwa ufunuo—hakika, katika hali hii, ilikuwa ni amri kutoka kwa Mungu.23
Kipengele cha nne cha mfumo ni kutambua kile ambacho Mungu tayari amekifunua kwako binafsi, wakati ukiwa tayari kwa ufunuo zaidi kutoka Kwake. Kama Mungu amejibu swali na hali hazikubadilika, kwa nini tutegemee jibu kuwa tofauti? Joseph Smith, alihangaika katika mazingira haya ya kutatiza mwaka 1828. Sehemu ya kwanza ya Kitabu cha Mormoni ilikuwa imetafsiriwa, wakati Martin Harris, mfadhili na mwandishi wa mwanzo, alipomuomba Joseph ruhusa kuchukua kurasa zilizotafsiriwa na kumuonyesha mke wake. Pasipo kuwa na uhakika wa nini cha kufanya, Joseph alisali kuomba mwongozo. Bwana alimwambia kutomruhusu Martin kuchukua kurasa.
Martin alimtaka Joseph kumuuliza tena Mungu. Joseph alifanya hivyo, na jibu lilikuwa, bila kushangaza, lile lile. Lakini Martin alimbembeleza Joseph aulize kwa mara ya tatu, na Joseph alifanya hivyo. Mara hii Mungu hakusema hapana. Badala yake, ilikuwa kama vile Mungu alisema, “Joseph, unajua ninavyohisi kuhusu hili, lakini unayo haki yako ya kujiamulia.” Akihisi ahueni kutokana na msongo, Joseph aliamua kumruhusu Martin achukue kurasa 116 za muswada na azioneshe kwa wanafamilia wachache. Kurasa zilizotafsiriwa zilipotea na hazikupatikana tena. Kwa ukali Bwana alimkemea Joseph.24
Joseph alijifunza, kama nabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo alivyofundisha: “Msijaribu kumshauri Bwana, lakini mpokee ushauri kutoka mkono wake. Kwani … anatoa ushauri kwa hekima.”25 Yakobo alitahadharisha kwamba vitu vibaya hutokea wakati tunapoomba vitu tusivyopaswa kuomba. Alitabiri kwamba watu katika Yerusalemu wangetafuta “vitu ambavyo [wasingeweza] kuvielewa,” wangetizama “nje ya alama,” na kutomzingatia kabisa Mwokozi wa ulimwengu.26 Walijikwaa kwa sababu waliomba vitu ambavyo hawakuweza na wasingeweza kuvielewa.
Ikiwa tumepokea ufunuo binafsi kwa ajili ya hali yetu na mazingira hayakubadilika, Mungu amekwisha jibu swali letu.27 Kwa mfano, wakati mwingine tunaomba kwa kurudia rudia kwa ajili ya hakikisho kwamba tumesamehewa. Ikiwa tumetubu, tumejawa na shangwe na amani ya nafsi, na kupokea ondoleo la dhambi zetu, hatuna haja ya kuomba tena bali tunaweza kutumainia jibu ambalo Mungu ametoa tayari.28
Hata tunapotumainia majibu ya Mungu ya kwanza, tunahitaji kuwa tayari kwa ufunuo binafsi utakaokuja. Hata hivyo, miisho michache ya safari za maisha hufikiwa kwa usafiri wa bila kusimama. Tunapaswa kutambua kwamba ufunuo binafsi unaweza kupokelewa “mstari juu ya mstari na kanuni juu ya kanuni,”29 mwongozo huo uliofunuliwa unaweza kuwa na kuongezeka mara kwa mara.30
Vipengele vya mfumo kwa ajili ya ufunuo binafsi huingiliana na kwa pamoja huimarishana. Lakini ndani ya mfumo huo, Roho Mtakatifu anaweza na atafunua kila kitu tunachohitaji ili kuingia ndani na kudumisha kasi katika njia ya agano. Kwa hivyo tunaweza kubarikiwa na nguvu za Yesu Kristo ili kuwa kile Baba wa Mbinguni anachotaka sisi tuwe. Ninawaalika muwe na ujasiri wa kudai ufunuo binafsi kwa ajili yako mwenyewe, kuelewa kile Mungu alichofunua, kilicho sambamba na maandiko na amri alizotupatia kupitia manabii Wake walioteuliwa na kupitia utambuzi wako mwenyewe na haki ya kujiamulia. Ninajua kwamba Roho Mtakatifu anaweza na atakuonyesha mambo yote unayopaswa kufanya.31 Katika jina la Yesu Kristo, amina.