Na Tufanye Kutenda Mema Kuwe Kawaida Yetu
Kama tukiwa imara na tusiotingishika katika kutenda mema, mila zetu zitatusaidia kubakia kwenye njia ya agano.
Daima nitakuwa mwenye shukrani kwa ajili ya majukumu yangu ndani ya Kanisa ambayo yamenifanya niishi katika nchi tofauti. Tumepata kwenye kila moja ya nchi hizi utofauti mkubwa na watu maridadi wenye mila na desturi tofauti.
Sote tunazo mila na desturi ambazo ni binafsi, kutoka kwenye familia zetu, au zinazotokea kwenye jamii tunamoishi na tunatumaini kutunza zile ambazo huendana na kanuni za injili. Mila na desturi zenye kuadilisha ni za msingi kwenye juhudi zetu za kubakia kwenye njia ya agano, na zile ambazo ni kikwazo, tunapaswa kuzikataa.
Mila ni mazoea au jinsi iliyozoeleka na ya kitabia ya kufikiri kwa mtu, utamaduni au desturi. Mara nyingi, vitu tunavyofikiri na kufanya katika hali ya mazoea huonekana kawaida.
Niruhusuni nionyeshe hili: Patricia, mke wangu kipenzi, anapenda kunywa maji ya nazi na kisha huila nazi. Wakati wa matembezi yetu ya kwanza huko Puebla, Mexico, tulitembelea mahali ambako tulinunua nazi. Baada ya kunywa maji, mke wangu aliwaomba wapasue nazi na wamletee nazi aile. Na ilipokuja, ilikuwa na wekundu. Walikuwa wameiwekea pilipili! Nazi tamu kwa pilipili! Hilo lilionekana kuwa geni kwetu. Lakini baadaye tulitambua kwamba wageni kwenye hili ni mimi na mke wangu, ambao hatukula nazi kwa pilipili. Huko Mexico, hata hivyo, siyo jambo geni, ni la kawaida kabisa.
Katika tukio jingine tulikuwa tunakula huko Brazil pamoja na marafiki, na wakatuletea parachichi. Na mara tu tulipotaka kuliwekea chumvi, marafiki zetu walitwambia, “Mnafanya nini!? Tumekwishaweka sukari kwenye parachichi!” Parachichi kwa sukari! Hilo lilionekana geni kwetu. Lakini tulijifunza kwamba wageni walikuwa mimi na mke wangu, ambao hatukula parachichi kwa sukari. Huko Brazil, parachichi iliyowekewa sukari ni kitu cha kawaida.
Kilicho kawaida kwa baadhi ni kigeni kwa wengine, kutegemeana na mila na desturi zao.
Je, mila na desturi gani ni za kawaida katika maisha yetu?
Rais Russell M. Nelson amesema: “Leo mara nyingi tunasikia kuhusu ‘mwelekeo mpya.’ Ikiwa kweli unataka kukumbatia mwelekeo mpya, ninakualika kugeuza moyo wako, akili na nafsi kwa kiasi kikubwa kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Acha huo uwe mwelekeo wako mpya” (“Mwelekeo Mpya,” Liahona, Nov. 2020, 118).
Mwaliko huu ni kwa wote. Haijalishi tu maskini au matajiri, walio elimika au wasio na elimu, wazee au vijana, wagonjwa au wenye afya. Anatualika turuhusu mambo ya kawaida katika maisha yetu yawe yale yanayotusaidia kuwa kwenye njia ya agano.
Hakuna nchi ambayo ina vyote vilivyo vizuri au kupendeza. Hivyo, kama Paulo na Nabii Joseph Smith walivyofundisha:
“Kama kuna kitu chochote kilicho chema, chenye kupendeza, au chenye taarifa njema au chenye kustahili sifa, tunayatafuta mambo haya” (Makala za Imani 1:13).
“Ikiwapo sifa nzuri yoyote, yatafakarini hayo” (Wafilipi 4:8).
Tambua ya kwamba hili ni ombi, sio tu nukuu.
Ningependa kila mmoja wetu kutenga muda kutafakari mila zetu na jinsi zinavyoathiri familia zetu.
Miongoni mwa tabia njema ambazo zinapaswa kuwa za kawaida kwa waumini wa Kanisa ni hizi nne:
-
Kusoma maandiko kibinafsi na kama familia. Ili kuwa waongofu kwa Bwana Yesu Kristo, kila mtu anawajibika kujifunza injili. Wazazi wanawajibika kufundisha injili kwa watoto wao (ona Mafundisho na Maagano 68:25; 93:40).
-
Sala binafsi na kama familia. Mwokozi anatuamuru kuomba daima (ona Mafundisho na Maagano 19:38). Sala huturuhusu kuwasiliana kibinafsi na Baba yetu wa Mbinguni kupitia jina la Mwanawe, Yesu Kristo.
-
Kuhudhuria mkutano wa sakramenti kila wiki (ona 3 Nefi 18:1–12; Moroni 6:5–6). Tunafanya hivyo kumkumbuka Yesu Kristo pale tunapochukua sakramenti. Katika ibada hii waumini wa Kanisa hufanya upya agano lao la kujichukulia juu yao jina la Mwokozi, daima kumkumbuka na kushika amri Zake (ona Mafundisho na Maagano 20:77, 79).
-
Kushiriki katika kazi ya hekaluni na historia ya familia. Kazi hii ndiyo njia ya kuunganisha na kufunga familia kwa milele zote (ona Mafundisho na Maagano 128:15).
Je, tunahisi vipi tunaposikia mambo haya manne? Je, haya ni sehemu ya maisha yetu ya kawaida?
Kuna desturi nyingine nyingi ambazo zingeweza kuwa sehemu ya ukawaida tuliouasili, hivyo kumfanya Mungu atawale katika maisha yetu.
Je, tunawezaje kutambua vile vilivyo kawaida katika maisha yetu na ya familia zetu? Katika maandiko tunao mfano mzuri; katika Mosia 5:15 inasema, “Nataka muwe imara na msiotingishika, daima mkitenda matendo mema.”
Ninayapenda maneno haya kwa sababu tunajua kwamba vitu ambavyo huwa vya kawaida katika maisha yetu ni vile tunavyovirudia mara ka mara. Kama tukiwa imara na tusiotingishika katika kutenda mema, mila zetu zitakuwa kulingana na kanuni za injili na zitatusaidia kubaki kwenye njia ya agano.
Rais Nelson ametushauri: “Kumbatia mwelekeo wako mpya kwa kutubu kila siku. Tafuta kuwa na ongezeko la usafi katika mawazo, maneno na matendo. Wahudumie wengine. Tunza mtazamo wa milele. Kuza wito wako. Na licha ya changamoto zako, wapendwa akina kaka na dada zangu, ishi kila siku ili kwamba uwe umejitayarisha zaidi kukutana na Muumba wako” (“Mwelekeo Mpya,” 118).
Sasa sio jambo geni kwangu na mke wangu, Patricia, au kwangu mimi kula nazi kwa pilipili na parachichi kwa sukari—Kusema kweli, tunapenda. Hata hivyo, kuinuliwa ni jambo ambalo hupita zaidi ya hamu za ladha; ni mada ihusianayo na umilele.
Ninaomba kwamba ukawaida wetu uturuhusu kuonja ladha hiyo ya “furaha isiyo na mwisho” (Mosia 2:41) ambayo imeahidiwa kwa wale wanaoshika amri za Mungu na kwamba, kwa kufanya hivyo, tuweze kusema, “Na ikawa kwamba tuliishi kwa furaha” (2 Nefi 5:27).
Kaka na dada zangu, ninashuhudia juu ya wanaume 15 ambao tunawaidhinisha kama manabii, waonaji na wafunuzi, ikiwemo nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson. Ninashuhudia kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni la kweli. Ninashuhudia hasa juu ya Yesu Kristo, Mwokozi na Mkombozi wetu, katika jina la Yesu Kristo, amina.