Mkutano Mkuu
Mkamilishwe ndani Yake
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


10:54

Mkamilishwe ndani Yake

Ukamilifu wetu unawezekana tu kwa neema ya Mungu.

Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, wana nguvu ya kutuokoa na kutubadilisha. Wanaweza kutusaidia kuwa kama Walivyo.

Miaka michache iliyopita, mmoja wa wajukuu wetu wadogo, Aaron, alianza kuwa na matatizo ya kiafya. Alichoka sana, alikuwa na michubuko kidogo na hakuonekana kuwa mwenye afya. Baada ya uchunguzi wa kimatibabu, iligunduliwa kuwa ana ugonjwa wa upungufu wa damu, ugonjwa ambao uboho wake uliacha kuzalisha chembe nyekundu za damu, chembe nyeupe za damu na chembe sahani. Bila matibabu na uponyaji, damu yake haingeganda vizuri au kupambana na maambukizo, hivyo kuanguka kidogo, majeraha au magonjwa vingeweza kuhatarisha uhai.

Kwa muda fulani, Aaron alipokea chembe sahani na kuongezewa damu ili kumuepusha na hatari. Madaktari walieleza kuwa tiba pekee ya ugonjwa huo itakuwa ni upandikizaji wa uboho, na nafasi nzuri ya kufaulu kwa hili ingekuwa kupata ndugu kama mtoaji. Ikiwa mmoja wa ndugu zake angekuwa anaendana sawa, matokeo ya upandikizaji yangeweza kuokoa maisha. Kaka zake wadogo wanne walipimwa, na mmoja, Maxwell, alionekana kuwa anaendana sawa kabisa.

Hata kwa mlingano kamili wa mtoaji, upandikizaji wa uboho bado unaleta hatari kubwa ya matatizo. Mchakato huo ulihitaji kwamba chembechembe za Aaron mwenyewe kwenye uboho wake wenye ugonjwa ziharibiwe kwa mchanganyiko wa tibakemikali na mnururisho kabla ya kupokea chembe chembe kutoka kwenye uboho wa kaka yake Maxwell. Kisha kwa sababu ya mfumo mdhaifu wa kinga wa Aaron, alihitaji kutengwa hospitalini kwa majuma kadhaa na kisha nyumbani kwa miezi kadhaa kwa kufuata sheria maalum, vizuizi na dawa.

Tokeo lililotumainiwa kutokana na upandikizaji huo lilikuwa kwamba mwili wa Aaron haungekataa chembe za mtoaji na kwamba chembe za Maxwell taratibu zingezalisha chembe nyekundu na nyeupe za damu na chembe sahani katika mwili wa Aaron. Upandikizaji wenye mafanikio ulisababisha mabadiliko ya kweli ya kisaikolojia. La kushangaza, daktari alieleza kwamba ikiwa Aaron angefanya uhalifu na kuacha damu kwenye eneo la uhalifu, polisi wangeweza kumkamata kaka yake Maxwell. Hii ni kwa sababu damu ya Aaron ingetoka kwenye seli zilizopandikizwa za Maxwell na kuwa na vinasaba vya Maxwell, na ndivyo ingekuwa hivyo kwa maisha yake yote.

Aaron kuokolewa kwa damu ya kaka yake kumechochea mawazo mengi kuhusu damu ya upatanisho ya Yesu Kristo na athari ya Upatanisho Wake kwetu. Ningependa kuangazia leo juu ya mabadiliko ya kudumu, yaletayo uzima yanayotokea tunapomruhusu Bwana kutenda miujiza ndani yetu.1

Aaron hakuwa na uwezo ndani yake mwenyewe kushinda ugonjwa huo. Mwili wake haungeweza kutengeneza chembe za damu zilizohitajika kuendeleza uhai wake. Bila kujali yeye binafsi angefanya nini, hangeweza kuponya uboho wake. Kama vile Aaron hangeweza kujiponya mwenyewe, sisi hatuwezi kujiokoa wenyewe. Bila kujali uwezo tulionao, elimu, kipaji au nguvu, hatuwezi kujisafisha wenyewe kutokana na dhambi zetu, kubadilisha miili yetu kuwa isiyokufa au kujiinua wenyewe. Inawezekana tu kupitia kwa Mwokozi Yesu Kristo na Upatanisho Wake usio na mwisho. “Na hakuna njia nyingine wala jina lililotolewa chini ya mbingu ambalo mwanadamu anaweza kuokolewa katika ufalme wa Mungu.”2 Ni damu yake ya upatanisho ndiyo inayotusafisha na kututakasa.

Ingawa Aaron hakuweza kujitibu mwenyewe, ili upandikzaji ufanye kazi alihitaji kuwa radhi kufanya kile madaktari walichokiomba—hata vitu vigumu sana, vyenye changamoto. Ingawa hatuwezi kujiokoa, tunapojinyenyekeza kwenye mapenzi ya Bwana na kushika maagano yetu, njia iko wazi kwa ajili ya ukombozi wetu.4 Kama mchakato wa ajabu wa vinasaba vya chembe za damu za Aaron kubadilika, tunaweza kubadilisha mioyo yetu,5 kuwa na sura yake katika nyuso zetu,6 na kuwa viumbe vipya katika Kristo.7

Alma aliwakumbusha watu wa Zarahemla juu ya kizazi kilichopita ambacho kilikuwa kimeongoka. Akimzungumzia baba yake, Alma alieleza kwamba “na kulingana na imani yake badiliko kuu likafanyika katika moyo wake.”8 Kisha akauliza, “Mmeshuhudia mabadiliko haya makuu katika mioyo yenu?”9 Sio watu ambao walibadilisha mioyo yao wenyewe. Bwana alifanya mabadiliko halisi. Alma alikuwa bayana sana kuhusu hili. Alisema, “Tazama, aliibadilisha mioyo yao.”10 “Walijinyenyekeza na kuweka tumaini lao kwa Mungu wa kweli na aliye hai … [na] walikuwa waaminifu hadi mwisho … [na] waliokolewa.”11 Watu walikuwa tayari kufungua mioyo yao na kutumia imani, na kisha Bwana akabadilisha mioyo yao. Na, lilikuwa badiliko kubwa lililoje! Fikiria tofauti katika maisha ya watu hawa wawili walioitwa Alma kabla na baada ya mioyo yao kubadilishwa.12

Sisi ni watoto wa Mungu wenye hatima kuu. Tunaweza kubadilishwa kuwa kama Yeye na kupokea “ujalivu wa shangwe.”13 Shetani, kwa upande mwingine, angependa tuwe na huzuni kama yeye.14 Tuna uwezo wa kuchagua yule tutakayemfuata.15 Tunapomfuata Shetani, tunampa nguvu.16 Tunapomfuata Mungu, Yeye anatupa nguvu.

Mwokozi alifundisha kwamba “tunapaswa kuwa wakamilifu.”17 Hili linaweza kuwa la kutatiza. Kwa dhahiri naweza kuona mapungufu yangu na kwa uchungu natambua umbali uliopo kati yangu na ukamilifu. Tunaweza kuwa na mwelekeo wa kufikiri kwamba tunapaswa kujikamilisha wenyewe, lakini hilo haliwezekani. Kufuata kila pendekezo katika kila kitabu cha msaada binafsi hapa duniani hakutauleta ukamilifu. Kuna njia moja tu na jina moja ambapo ukamilifu huja. “Tunakamilishwa kwa njia ya Yesu aliye mpatanishi wa agano jipya, aliyekamilisha upatanisho huu mkamilifu kwa njia ya umwagikaji wa damu yake yeye mwenyewe.”18 Ukamilifu wetu unawezekana tu kwa neema ya Mungu.

Je, unaweza kufikiria jinsi ambavyo ingekuwa vigumu kwa mjukuu wetu mdogo Aaron kudhani alipaswa kuelewa na kufanya taratibu zote za matibabu zinazohusiana na upandikizaji wake mwenyewe? Hatupaswi kudhania kwamba tunahitajika kufanya kile ambacho Mwokozi pekee anaweza kufanya katika mchakato wa kimiujiza wa ukamilifu.

Kama Moroni alivyohitimisha rekodi yake, alifundisha: “Mje kwa Kristo, na Mkamilishwe ndani Yake, … Na ikiwa mtajinyima ubaya wote, na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi neema yake inawatosha, kwamba kwa neema yake mngekamilishwa kwa Kristo.”19 Ukweli wa kufariji na wa nguvu ulioje! Neema yake yatosha kwangu. Neema yake yatosha kwako. Neema yake inatosha kwa ajili ya wale “wasumbukao na kulemewa na mizigo.”20

Kwa matibabu kama ya Aaron, daima kuna kutokuwa na uhakika wa matokeo. Kwa kweli, Aaron alihitaji upandikizaji wa pili wakati ule wa kwanza ulipokuwa na matatizo. Kwa shukrani, pamoja na mabadiliko ya kiroho ya moyo, hatuhitaji kujiuliza ikiwa yatatokea. Tunapoishi kulingana na mapenzi Yake, “tukitegemea kabisa fadhili zake yeye aliye hodari kuokoa;”21 kuna hakikisho la asilimia 100 la kutakaswa na damu ya Mwokozi na hatimaye kukamilishwa ndani Yake. Yeye ni “Mungu wa ukweli, na [hawezi] kusema uwongo.”22

Hapana swali kwamba mchakato huu wa mabadiliko unachukua muda na hautakamilika hadi baada ya maisha haya, lakini ahadi ni ya kweli. Wakati kutimizwa kwa ahadi za Mungu kunaonekana kuwa mbali, bado tunakumbatia ahadi hizo, tukijua zitatimizwa.23

Badiliko la kimuujiza katika afya ya Aaron limeleta shangwe kubwa kwa familia yetu. Fikiria juu ya shangwe kuu mbinguni wakati mabadiliko makubwa yakitokea katika nafsi zetu.

Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, wanatupenda na wamejitolea kwa neema kutubadilisha na kutukamilisha. Wanataka kufanya hili. Ni kiini cha kazi Yao na utukufu.24 Ninashuhudia Wana uwezo wa kufanya hili tunapokaribia Kwao kwa imani. Katika jina la Yesu Kristo, amina.