Mkutano Mkuu
Jibu ni Yesu
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


Jibu ni Yesu

Bila kujali jinsi changamoto zilivyo ngumu au za kuchanganya, daima unaweza kukumbuka kwamba jibu ni rahisi; jibu daima ni Yesu.

Ni heshima iliyoje kuzungumza nanyi kwenye kikao hiki cha mkutano mkuu. Leo ninawahutubia ninyi kama marafiki. Katika Injili ya Yohana, Mwokozi alifundisha kwamba sisi ni marafiki Zake kama tunafanya kile anachotuomba sisi tufanye.1

Ni upendo wetu binafsi na wa pamoja kwa Mwokozi, na maagano yetu pamoja Naye, ambayo hutuweka sisi pamoja Naye. Kama Rais Henry B. Eyring alivyofundisha: “Kwenu ningependa kusema jinsi Bwana anavyowapenda na kuwatumaini. Na, hata zaidi, ningependa kuwambia jinsi Yeye anavyowategemea ninyi.”2

Nilipoitwa kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka na Rais Russell M. Nelson, Nilifurikwa na hisia. Ilikuwa hisia ya kuzidiwa. Mke wangu Julie, na mimi tulisubiria kwa hamu kikao cha Jumamosi alasiri cha mkutano mkuu. Ilikuwa inanyenyekeza kukubaliwa. Kwa makini nilitazama hatua zangu kuelekea kwenye kiti nilichopangiwa ili nisianguke katika jukumu langu la kwanza.

Mwishoni mwa kikao hicho, kitu kilitokea ambacho kilikuwa na athari kubwa sana kwangu. Washiriki wa akidi walipanga mstari na kuwasalimia Viongozi Wakuu wenye Mamlaka wapya mmoja mmoja. Kila mmoja alishiriki upendo wao na kutuunga mkono. Kwa moyo mkunjufu walisema, “Usihofu—u mmoja wetu.”

Katika mahusiano yetu na Mwokozi, Yeye hutazama moyo na “hana mapendeleo kwa watu.”3 Fikiria jinsi Yeye alivyowachagua Mitume Wake. Yeye hakuzingatia hadhi wala utajiri. Anatualika tumfuate Yeye, na Anatuhakikishia kwamba sisi ni wa Kwake.

Ujumbe huu ni mahususi kwa vijana wa Kanisa. Ninaona ndani yenu kile Rais Nelson anakiona ndani yenu. Alisema kwamba “kuna kitu maalumu kisichopingwa kuhusu kizazi hiki cha vijana. Baba yenu wa Mbinguni lazima ana imani kubwa ndani yenu kuwatuma ulimwenguni wakati huu. Ninyi mmezaliwa kwa ajili ya makuu!”4

Nina shukrani kwa kile nilichojifunza tokea kwa vijana. Nina shukrani kwa kile watoto wangu hunifunza, kwa kile wamisionari wetu hunifunza, na kile wapwa wangu wa kiume na kike hunifunza.

Siyo kitambo sana, nilikuwa nikifanya kazi shambani kwetu pamoja na mpwa wangu Nash. Ana miaka sita na ana moyo safi. Nash ni mpwa wangu mpendwa, na ninaamini mimi ni mjomba wake mpendwa nikizungumza katika mkutano leo.

Aliponisaidia kupata suluhisho kwa ajili ya mradi wetu, nilisema, “Nash, hilo ni wazo zuri sana Je, ni kwa jinsi ulipata kuwa mwerevu hivi? Alinitazama kwa onyesho katika macho yake ambayo yalisema, “Mjomba Ryan, kwa nini hukuja jibu la swali hili?”

Aliinua mabega yake na kushusha, akatabasamu na kwa kujiamini akasema, “Yesu.”

Nash alinikumbusha katika siku hiyo juu ya fundisho hili rahisi na muhimu. Jibu la maswali rahisi sana na matatizo magumu sana daima ni sawa. Jibu ni Yesu Kristo. Kila suluhisho linapatikana Kwake.

Katika Injili ya Yohana, Mwokozi aliwaambia wanafunzi Wake kwamba Yeye angeandaa mahali kwa ajili yao. Tomaso hakuelewa na alimwambia Mwokozi:

“Bwana, sisi hatujui uendako; nasi twaijuaje njia?

“Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima: mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”5

Mwokozi aliwafundisha wanafunzi Wake kwamba Yeye ndiye “njia, kweli na uzima.” Yeye ni jibu la swali la jinsi ya kuja kwa Baba wa Mbinguni. Kupata ushuhuda wa kazi Yake ya kiungu katika maisha yetu ilikuwa ni jambo nililojifunza kama mvulana.

Nilipokuwa nikitumikia kama mmisionari, Rais Howard W. Hunter alitualika kufanya kitu kilichokuwa na athari kubwa katika maisha yangu. Alisema: “Ni lazima tumjue Kristo vyema kuliko tunavyomjua; lazima tumkumbuke Yeye zaidi kila mara kuliko tunavyomkumbuka; ni lazima tumtumikie Yeye kwa kwa bidii kuliko tunavyomtumikia.”6

Wakati huo, nilikuwa nikiwaza kuhusu jinsi ya kuwa mmisionari bora. Hili lilikuwa ndilo jibu: kumjua Kristo, kumkumbuka Yeye na kumtumikia. Wamisionari kote duniani wameungana katika kusudi hili: “kuwaalika wengine kuja kwa Kristo kwa kuwasaidia kupokea injili ya urejesho kupitia imani katika Yeye na Upatanisho Wake” na kupitia “toba, ubatizo, kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu na kuvumilia hadi mwisho.”7 Kwa marafiki zetu mnaowasikiliza wamisionari, ninaongeza mwaliko wangu wa kuja kwa Kristo. Kwa pamoja tutajitahidi kumjua Yeye, kumkumbuka na kumtumikia.

Kutumikia misheni ilikuwa wakati mtakatifu wa maisha yangu. Katika usaili wangu wa mwisho pamoja naye kama mmisionari, Rais Blair Pincock alizungumza juu ya mabadiliko yanayokuja kwa viongozi wa misheni, yeye na mkewe pia walikuwa wanakaribia kumaliza huduma yao. Sote tulikuwa na huzuni kwa kuacha kitu tulichokipenda sana. Angeweza kuona kwamba nilifadhaishwa na wazo la kutokuwa mmisionari. Alikuwa mtu wa imani kuu na kwa upendo alinifundisha kama alivyokuwa amefanya hapo awali kwa miaka miwili. Alionyesha picha ya Yesu Kristo juu ya dawati lake na kusema, “Mzee Olsen, Yote yatakuwa SAWA kwa sababu hii ni kazi Yake.” Nilihisi kuhakikishiwa kujua kwamba Mwokozi atatusaidia, si tu wakati tunatumikia bali daima, kama sisi tutamruhusu.

Dada Pincock alitufundisha kutoka ndani ya moyo wake kwa virai rahisi vya Kihispania. Wakati aliposema, “Jesucristo vive,” nilijua ilikuwa kweli na kwamba Yeye yu hai. Aliposema, “Elderes y hermanas, les amo,” nilijua kwamba anatupenda na anataka sisi tumfuate Mwokozi daima.

Mke wangu pamoja nami hivi karibuni tulibarikiwa kutumikia kama viongozi wa misheni kufanya kazi na wamisionari wa ajabu huko Uruguay. Ningependa kusema kwamba hawa walikuwa wamisionari bora duniani, na natumaini kwamba kila kiongozi wa misheni anahisi hivyo. Wafuasi hawa walitufunza kila siku kuhusu kumfuata Mwokozi.

Wakati wa usaili wa kila mara mmoja wa akina dada mmisionari wetu wazuri aliingia ofisini. Alikuwa mmisionari mwenye mafanikio, mkufunzi mahiri, na kiongozi aliyejitolea. Alitegemewa na wenzi wake na kupendwa na watu. Alikuwa mtiifu, mnyenyekevu na mwenye kujiamini. Mazungumzo yetu ya awali yalifokasi kwenye eneo lake na watu aliokuwa akiwafundisha. Mazungumzo haya yalikuwa ya tofauti. Nilipomuuliza alikuwa anaendeleaje, ningeweza kuona alikuwa na shida. Alisema, “Rais Olsen, mimi sijui kama ninaweza kufanya hili. Sijui kama nitakuwa mzuri vya kutosha. Sijui ninaweza kuwa mmisionari ambaye Bwana ananihitaji niwe.”

Alikuwa mmisionari wa mzuri sana. Bora katika kila njia. Ndoto ya rais wa misheni. Kamwe sikuwahi kuwa na wasiwasi kuhusu uwezo wake kama mmisionari.

Nilipokuwa ninamsikiliza, nilisumbuka kujua cha kusema. Kimya kimya niliomba: “Baba wa Mbinguni huyu ni mmisionari bora. Ni Wako. Anafanya kila kitu sawa sawa. Sitaki kuharibu sasa. Tafadhali nisaidie kujua cha kusema.”

Maneno yalinijia. Nilisema, “Hermana, nasikitika sana unahisi hivi. Acha nikuulize swali. Kama ungekuwa na rafiki unayemfundisha ambaye anahisi hivi, ungesema nini?”

Alinitazama na kutabasamu. Kwa roho hiyo ya mmisionari isiyokosea na kwa uthibitisho, alisema, “Rais, hiyo ni rahisi. Ningemwambia kwamba Mwokozi anakujua vyema. Ningemwambia kwamba Yeye yu hai. Yeye anakupenda. Wewe ni mzuri vya kutosha, na unaweza!”

Kwa kicheko kidogo alisema, “Nadhani kama hii inatumika kwa marafiki zetu, basi inaweza pia kutumika kwangu.”

Tunapokuwa na maswali au mashaka, tunaweza kuhisi kwamba suluhisho ni gumu sana au kupata majibu kunachanganya sana. Na tukumbuke kwamba adui, hata baba wa uongo wote, ni msanifu wa mkanganyiko.8

Mwokozi ni Bwana wa urahisi.

Rais Nelson amesema:

“Adui ni mjanja. Kwa milenia amekuwa akifanya jema lionekane baya na baya lionekane jema. Ujumbe wake huwa wa kelele, kishujaa na wa kujisifu.

“Hata hivyo, ujumbe kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni ni tofauti kabisa. Yeye anawasiliana kwa njia rahisi, kwa utulivu na uwazi mzuri sana kwamba hatuwezi kukosa kumuelewa Yeye.”9

Tuna shukrani kiasi gani kwamba Mungu anatupenda sana kwamba Yeye alimtuma Mwanawe. Yeye ni jibu.

Rais Nelson hivi karibuni alisema:

“Injili ya Yesu Kristo kamwe haijawahi kuhitajika zaidi kama ilivyo leo. …

“… Hii inasisitiza haja ya haraka kwetu ya kufuata maelekezo ya Bwana kwa wanafunzi Wake ya ‘kwenda … ulimwenguni mwote, na kuhubiri injili kwa kila kiumbe.’”10

Kwa wale ambao watachagua kutumikia, ninaweza kushuhudia baraka ambazo zitakuja kama unafuata mwito wa nabii. Kutumikia si kuhusu wewe; ni kuhusu Mwokozi. Utaitwa mahali fulani, lakini cha muhimu sana utaitwa kwa watu fulani. Utakuwa na jukumu kubwa na baraka ya kuwasaidia marafiki wapya kuelewa kwamba jibu ni Yesu.

Hili ni Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, na hapa ndipo kwetu sote. Kila kitu ambacho Rais Nelson kwa upendo anatuhimiza kufanya kitatuongoza karibu na Mwokozi.

Kwa vijana wetu wa wazuri—ikijumuisha mpwa wangu Nash—katika maisha yenu yote, bila kujali jinsi changamoto zilivyo ngumu au za kuchanganya, daima mnaweza kukumbuka kwamba jibu ni rahisi; jibu daima ni Yesu.

Kama ambavyo nimekuwa nikisikia wale walioidhinishwa kama manabii, waonaji na wafunuzi wakisema mara nyingi, mimi pia ninasema kwamba tunawapenda, tunawashukuru na tunawahitaji. Ninyi ni wa hapa.

Ninampenda Mwokozi. Ninatoa ushahidi wa jina Lake, hata Yesu Kristo. Nashuhudia kwamba Yeye ndiye “mwanzilishi na mkamilishaji wa imani yetu,”11 na ni Bwana wa urahisi. Jibu ni Yesu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha