Mkutano Mkuu
Kujenga Maisha Yanayohimili Adui
mkutano mkuu wa Oktoba 2022


10:32

Kujenga Maisha Yanayohimili Adui

Ninaomba kwamba tuweze kuendelea kujenga maisha yetu kwa kufuata mipango na maelekezo ya kiufundi ya usanifu wa kiungu yaliyoandikwa na Baba yetu wa Mbinguni.

Kwa miaka mingi kutoka kwenye mimbari hii nzuri katika Kituo cha Mikutano, tumepokea ushauri mzuri, maongozi, maelekezo na ufunuo. Wakati mwingine, wazungumzaji wametumia ulinganisho unaohusishwa na maeneo yao ya ujuzi na uzoefu ili kueleza kwa uwazi na kwa nguvu kanuni ya injili ya Yesu Kristo.

Kwa njia hii, kwa mfano, tumejifunza kuhusu ndege na safari za ndege ambapo kupaa kidogo kwa mwanzo kunaweza kutuongoza hadi mahali pa mbali na tunakoenda.1 Pia kwa njia hii, tumejifunza kutokana na ulinganisho wa kazi ya moyo wetu wa kimwili kwa badiliko kubwa la moyo linalohitajika ili kuitikia mwaliko wa Bwana wa kumfuata Yeye.2

Wakati huu, ningependa kwa unyenyekevu kuongezea ulinganisho uliotokana na maandalizi ya taaluma yangu. Ninamaanisha ulimwengu wa uhandisi wa ujenzi. Tangu mwanzo wa masomo yangu ya chuo kikuu, nilikuwa na ndoto ya wakati ambapo ningekamilisha mahitaji ya kuhitimu kuhudhuria darasa ambalo lingenifundisha jinsi ya kusanifu majengo na miundo mingine ambayo ingeweza kuchukuliwa kuwa “ya kukinzana na matetemeko ya ardhi.”

Hatimaye siku ikafika kwa darasa langu la kwanza kwenye somo hili. Maneno ya kwanza kutoka kwa profesa yalikuwa yafuatayo: “Hakika mna hamu ya kuanza kozi hii na kujifunza jinsi ya kusanifu miundo ya kukinzana na matetemeko,” ambayo wengi wetu tulitikisa vichwa vyetu kwa hamu. Kisha profesa akasema, “Samahani kukuambieni kwamba hili haliwezekani, kwa maana siwezi kuwafundisha jinsi ya kusanifu jengo ambalo ni dhidi ya, ambalo ‘linakinzana na,’ au linalopingana na tetemeko la ardhi. Hii haingii akilini,” alisema “kwa maana matetemeko ya ardhi yatatokea tu, tupende au tusipende.”

Kisha akaongeza, “Ninachoweza kuwafundisheni ni jinsi ya kusanifu miundo inayostahimili tetemeko la ardhi, miundo ambayo inaweza kustahimili nguvu zinazotokana na tetemeko la ardhi, ili jengo hilo libaki limesimama bila kupata madhara yoyote makubwa na kisha kuendelea kutoa huduma ambayo kwayo liliundwa.”

Mhandisi hukokotoa hesabu zinazoonyesha vipimo, ubora na sifa za misingi, nguzo, mihimili, ubamba wa zege na vipengele vingine vya kimuundo vinavyosanifiwa. Matokeo haya yanatafsiriwa katika mipango na vipimo vya kiufundi, ambavyo lazima vifuatwe na mjenzi bila kukiuka ili kazi ifanyike na hivyo kutimiza kusudi ambalo kwalo jengo hilo lilijengwa.

Ingawa zaidi ya miaka 40 imepita tangu darasa hilo la kwanza katika uhandisi wa kustahimili matetemo, nakumbuka kikamilifu wakati nilipoanza kupata ufahamu wa kina na kamili zaidi wa umuhimu mkuu kwamba wazo hili lingekuwepo katika miundo ambayo ningesanifu maisha yangu ya baadaye ya kitaaluma. Si hivyo tu, bali hata muhimu zaidi—kwamba darasa lingekuwepo daima katika uadilishaji wa maisha yangu mwenyewe na kwa wale ambao ningeweza kutumia ushawishi chanya juu yao.

Tumebarikiwa kiasi gani kutegemea ujuzi wa mpango wa wokovu ulioundwa na Baba yetu wa Mbinguni, kuwa na urejesho wa injili ya Yesu Kristo na kutegemea mwongozo wa kiungu wa manabii wanaoishi! Yote hayo huunda “mipango” iliyobuniwa kitakatifu na “maelekezo ya kiufundi” ambayo hutufundisha waziwazi jinsi ya kujenga maisha yenye furaha—maisha yanayohimili dhambi, yanayohimili vishawishi, yanayohimili mashambulizi kutoka kwa Shetani, ambaye kwa bidii anatafuta kuvunja hatima yetu ya milele pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na pamoja na familia zetu pendwa.

Mwokozi Mwenyewe, mwanzoni mwa huduma Yake, “aliachwa ajaribiwe na ibilisi.”3 Lakini Yesu alishinda jaribu hilo kuu. Je, ingekuwaje kama angekuwa na tabia ya kumpinga Shetani au kupinga majaribu? Kilichomfanya Yesu kuibuka mshindi kutoka nyakati hizo ngumu zaidi ni maandalizi Yake ya kiroho, ambayo yalimruhusu kuwa katika hali ya kuhimili vishawishi vya adui.

Je, ni baadhi ya mambo gani ambayo yalimsaidia Mwokozi kuwa tayari kwa ajili ya wakati huo muhimu?

Kwanza, Alikuwa amefunga kwa siku 40 mchana na usiku, mfungo ambao lazima uliambatana na maombi thabiti. Kwa hiyo, ingawa alikuwa dhaifu kimwili, roho Yake ilikuwa imara sana. Hata hivyo, kwa bahati nzuri, hatuombwi kufunga kwa muda kama huo—badala yake ni saa 24 tu na mara moja kwa mwezi—kufunga hutujaza nguvu za kiroho na hututayarisha kuwa wastahimilivu kwa majaribu ya maisha haya.

Kuhusu jambo la pili, katika masimulizi ya majaribu ambayo Mwokozi alikutana nayo, tunaona kwamba daima alimjibu Shetani akiwa na maandiko akilini Mwake, akiyanukuu na kuyatumia kwa wakati ufaao.

Shetani alipomjaribu kugeuza mawe kuwa mkate ili kushibisha njaa Yake kutokana na mfungo Wake wa muda mrefu, Bwana akamwambia, “Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, bali kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.”4 Kisha, Bwana alipokuwa juu ya kinara cha hekalu, ibilisi alijaribu kumjaribu ili aonyeshe uwezo Wake, ambapo Bwana alimjibu kwa mamlaka: “Tena imeandikwa, usimjaribu Bwana, Mungu wako.”5 Na kwa jaribio la tatu la Shetani, Bwana alijibu, “Imeandikwa, Msujudie Bwana, Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.”6

Tukio la tetemeko la ardhi huacha alama yake hata kwenye majengo ambayo yalisanifiwa na kujengwa kwa usahihi—matokeo kama nyufa, samani zilizoanguka au dari na madirisha yaliyovunjika. Lakini jengo hili lililosanifiwa na kujengwa vizuri litatimiza kusudi lake la kuwalinda wakaaji wake, na kwa ukarabati kiasi, litarejea kwenye hali yake ya awali.

Kwa mtindo sawa na huo, mapigo ya adui yanaweza pia kusababisha “nyufa” au uharibifu fulani katika maisha yetu, licha ya juhudi zetu za kujenga maisha yetu kulingana na muundo mkamilifu wa kiungu. “Nyufa” hizi zinaweza kujidhihirisha kupitia hisia za huzuni au majuto kwa sababu ya kufanya makosa fulani na kwa kutokufanya kila kitu kikamilifu, au kwa kuhisi kwamba sisi si wazuri kwa kiasi tunachotaka kuwa.

Lakini kile kilicho cha maana hapa ni kwamba tukiwa tumefuata mpango na vipimo vilivyosanifiwa kiungu , yaani, injili ya Yesu Kristo, sisi bado tunasimama. Muundo wa maisha yetu haujabomolewa kwa sababu ya juhudi za adui au kwa hali ngumu ambazo tumelazimika kukabiliana nazo; badala yake, tuko tayari kusonga mbele.

Shangwe iliyoahidiwa katika maandiko kama kusudi la uwepo wetu7 haipaswi kueleweka kumaanisha kwamba hatutakuwa na shida au huzuni, kwamba hatutakuwa na “nyufa” kama matokeo ya majaribu, dhiki au kutokana na majaribu halisi ya maisha yetu ya duniani.

Shangwe hii inahusiana na mtazamo wa Nefi juu ya maisha aliposema, “Baada ya kuona mateso mengi katika siku zangu, walakini, nikiwa nimependelewa sana na Bwana katika siku zangu zote.”8 Siku zake zote! Hata siku ambazo Nefi aliteseka wakati wa kutoelewana na kukataliwa na kaka zake mwenyewe, hata walipomfunga ndani ya merikebu, hata siku ambayo baba yake, Lehi, alipofariki, hata wakati Lamani na Lemueli walipokuwa maadui wakuu wa watu wake. Hata katika siku hizo ngumu, Nefi alihisi kupendelewa sana na Bwana.

Tunaweza kuwa na amani ya kujua kwamba Bwana hataruhusu kamwe tujaribiwe kupita uwezo wetu wa kuhimili. Alma anatualika “kukesha na kusali daima, ili [sisi] tusijaribiwe zaidi ya yale ambayo [tunaweza] kuvumilia, na hivyo kuongozwa na Roho Mtakatifu, katika kuwa wanyenyekevu, wapole, watiifu, wenye subira, wenye upendo na wenye uvumilivu.”9

Haya yanaweza kutumika pia kwa majaribu ya maisha. Amoni anatukumbusha juu ya maneno ya Bwana: “Nendeni … na mvumilie mateso yenu kwa subira, na nitawapa mafanikio.”10

Bwana daima hutoa msaada tunapokabiliana na dhiki, majaribu, kutoelewana, udhaifu na hata kifo. Yeye amesema, “Na sasa, amini ninawaambia, na lile nisemalo kwa mmoja nasema kwa wote, muwe na furaha, watoto wadogo; kwani mimi nipo katikati yenu, na sijawasahau.”11 Yeye kamwe hatatuacha!

Ninaomba kwamba tuweze kuendelea kujenga maisha yetu kwa kufuata mipango na maelekezo ya kiufundi ya usanifu wa kiungu iliyoandikwa na Baba yetu na kufanikishwa kupitia Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Hivyo, kwa sababu ya neema inayotufikia kupitia kwa Upatanisho wa Mwokozi wetu, tutafaulu katika kujenga maisha yanayohimili dhambi, yenye kuhimili majaribu na kuimarishwa kuhimili nyakati ngumu na za huzuni maishani mwetu. Na zaidi ya hayo, tutakuwa katika hali ya kupata baraka zote zilizoahidiwa kupitia upendo wa Baba yetu na Mwokozi wetu. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.